Maisha ya mfanyakazi wa nyumbani katika familia za kifalme na tajiri nchini Qatar

Wakati Kombe la Dunia la FIFA la 2022 likifanyika huko Doha, rekodi ya haki za binadamu ya Qatar imeshutumiwa.
Mengi yameandikwa kuhusu jinsi Qatar inavyowatendea wafanyakazi wahamiaji waliojenga viwanja na hoteli kwa ajili ya mashindano hayo, lakini nani anaandika kuhusu wafanyakazi wa ndani wa kigeni wanaofanya kazi kwa wasomi wa nchi hiyo?
Megha Mohan, mwandishi wa jinsia na utambulisho wa BBC, alizungumza na wafanyakazi wawili wa nyumbani ambao wamelazimika kugharamika kwa maisha marefu ya kufanya kazi bila mapumziko yoyote.
Nilifaulu kuwasiliana na Gladys (si jina lake halisi) baada ya waajiri wake wasomi wa Qatar kwenda kulala usiku.
Aliniambia kupitia ujumbe mfupi wa mtandaoni kwamba anafanya kazi kila siku kuanzia saa mbili asubuhi hadi tano usiku.
Anafanya usafi, kupika, na kulea watoto. Anakula mabaki kutoka kwa milo ya familia na akasema hajapata likizo tangu aanze kazi miezi 18 iliyopita.
Mwajiri wangu mwanamke ni wazimu," Gladys, mwanamke wa Ufilipino katika miaka yake ya 40, anaelezea waajiri wake walivyo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Ananifokea kila wakati."
Kabla ya Qatar kushinda zabuni ya kuandaa Kombe la Dunia la 2022, wafanyikazi wa kigeni hawakuruhusiwa kubadilisha kazi au kuondoka nchini bila idhini ya mwajiri wao.
Hata sasa, hiyo ndiyo hali inayoshuhudiwa katika nchi nyingi za Ghuba.
Lakini kutokana na ukosoaji wa dunia, Qatar imeanza kuleta mageuzi kwa lengo hili, ila si mara zote yanatekelezwa kivitendo.
Kwa mfano, pasipoti ya Gladys iko mikononi mwa waajiri wake.
Hata kama ataomba tena kuacha kazi, hana hakikisho kuwa hilo litakubalika.
Na licha ya hayo yote ambayo Gladys anapitia, yeye anadhani ni mwenye bahati.
Anasema kuwa tofauti na baadhi ya wafanyakazi wa nyumbani, anaruhusiwa kubaki na simu yake.
Pia, yeye hayuko katika hatari ya kuteswa kimwili.
Anasema kuwa wafanyakazi wa nyumbani nchini Qatar mara nyingi hudhulumiwa kimwili.
Ana sababu zingine za kusalia katika kazi yake ya sasa - kwa sababu umri wake umesonga, anadhani hatapata kazi bora zaidi.
Anapata rial 1,500 (zaidi ya Rupia 151,000) kwa mwezi, ambayo anaweza kutuma nyumbani kusaidia familia.
Haki za wafanyakazi wa nyumbani
Kulingana na data ya 2021 kutoka Mamlaka ya Mipango na Takwimu ya Qatar, kuna wastani wa wafanyikazi 160,000 wa nyumbani nchini Qatar.
Mnamo 2017, Qatar ilianzisha Sheria ya Wafanyakazi wa Ndani, ambayo kinadharia inaweka kikomo cha saa za kazi hadi saa 10 kwa siku.
Kwa hivyo, mapumziko ya kila siku, likizo ya kila wiki na likizo ya kulipwa ni muhimu.
Pia ilianzisha kima cha chini cha mshahara mwaka wa 2020 na kuwapa wafanyakazi haki iliyoandikwa ya kubadilisha kazi au kuondoka nchini bila ruhusa.
Hata hivyo, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International linasema sheria hizi hazifuatwi kila mara, na wafanyakazi wa majumbani wanaendelea kufanyishwa kazi kupita kiasi, kutopewa mapumziko, na kutendewa unyanyasaji na udhalilishaji.
Joanna Concepcion wa Migrant International, shiŕika la msingi ambalo linasaidia wafanyakazi wahamiaji nchini Ufilipino, anasema wafanyakazi wengi wahamiaji hunyamaza kimya kuhusu hali duni ya kazi wanayokumbana nayo kwa sababu kipaumbele chao ni kupata pesa kwa ajili ya familia zao.
Lakini, anasema, wafanyakazi katika maeneo ya Ghuba wanaripoti unyanyasaji mkubwa wanapojisikia kujiamini kuongea.
Mwanamke mmoja alisema mwajiri wake aliweka kichwa chake kwenye shimo la choo na kumnyima chakula na maji anapokasirika.

Althea (sio jina lake halisi) anatoa picha tofauti sana ya maisha yake kama yaya nchini Qatar.
Yeye, ambaye anafanya kazi katika familia ya kifalme ya Al Thani, alipiga simu ya video kwa BBC kutoka ghorofa ya chini ya makao ya kifalme.
Alieleza kwa tabasamu na ishara kwamba waajiri wake walimpa iPhone, nguo, vito na viatu vya bei ghali ambavyo hangeweza kamwe kuvinunua Ufilipino.
Kama ilivyokuwa kwa Gladys, Althea analetwa hapa na ugumu wa kupata mshahara kuweza kujikimu kimaisha.
Hata tulipokuwa tukipiga soga naye, wahudumu wengine wa nyumbani wa Ufilipino wanaotumia chumba kimoja kikubwa katika makazi ya Althea walijiunga na simu na kusalimia.
Wanapewa vyumba vyao vya kulala na sehemu yao ya jikoni.
Wasio na bahati ni wafanyikazi wa nyumbani ambao huwa kwenye mitandao ya TikTok na Facebook wakiombwa kuokolewa.
‘’Mara nyingi mimi huona video kama hizo kwenye mtandao, kwa hivyo ninajihisi mwenye bahati sana’’, anasema.
‘’Kila siku ni kama simulizi kwangu’’.
Hata hivyo, pia ni vigumu kutumika katika kile ambacho Althea anakielezea kama ‘’majumba ya Cinderella,’’ yamepambwa kwa dari za juu na vinara vilivyounganishwa, samani za kale zilizopambwa, meza za mapambo zilizopambwa kwa lulu na maua yenye harufu za kuvutia.
Siku ya kawaida ya kazi huanza na wafanyakazi kuandaa kifungua kinywa kwa familia ya kifalme saa 06:30 asubuhi.
Althea anakula baada ya familia ya mwajiri kula.
Baada ya kuondoa mayai yaliyobaki wakati wa kifungua kinywa, wanaanza kusafisha vyumba, kisha kuandaa chakula cha mchana.
‘’Tunaofanya kazi ni wengi kwa hivyo ni rahisi kwetu,’’ anasema Althea.
Kati ya saa tisa na kumi na mbili jioni wahudumu wa nyumbani huenda kwenye makazi yao na kupumzika, kisha kujiandaa kwa chakula cha jioni.
Baada ya chakula cha jioni, huduma za kila siku za Althea huisha, na anaruhusiwa kuondoka kwenye jumba ikiwa anataka.
Familia ya kifalme haijachukua pasipoti ya Althea.
Lakini Althea lazima afanye kazi siku saba kwa wiki - hata wikendi.
Hapati mapumziko ya wiki ambayo ‘yamehakikishwa’ na sheria za Qatar.
Hiyo ndiyo gharama anayolipa ili kuipatia familia yake usaidizi muhimu wa kifedha.
Mary Grace Morales mwenye makazi yake Manila, mwajiri ambaye huwapa wafanyikazi wa Ufilipino kazi chini ya utawala wa kifalme, anasema kuwa kufanya kazi katika jumba la kifahari ni kazi ambayo ‘inaonewa wivu’ na wengi.
‘’Kufanya kazi kama hiyo kuna faida nyingi. Familia ya mwajiri ni wakarimu,’’ anasema.
Akizungumzia matatizo yanayowakabili wafanyakazi wengine wa nyumbani, alisema: ‘’Wasichana wote wanakulia katika jumba la kifalme. Familia huwapa chakula na vinywaji vizuri.’’

Lakini anafafanua kuwa kuna mahitaji maalum ambayo familia za kifalme zinatarajia.
"Wasichana wote waliotumwa kufanya kazi kwa familia ya kifalme ya Qatar ni kati ya umri wa miaka 24 na 35, warembo sana," Morales alisema.
Alitazama skrini kwa muda ili kunitazama vizuri, ambaye alikuwa akimpigia simu kutoka makao makuu ya BBC London.
"Mrembo kuliko wewe," aliniambia huku akitabasamu.
Baadaye alinitumia ujumbe wa WhatsApp kuniomba msamaha.
Watoto wake walikuwa wamesikia maneno yake, na walimwambia kwamba alikuwa amesema jambo lisilofaa.
Nilimhakikishia kwamba sikuchukizwa na hilo - lakini sikumwambia kwamba kuajiri watu kwa kuzingatia mwonekano ni kinyume cha sheria katika nchi nyingi.
"Lazima wawe vijana, kwa sababu familia ya kifalme ya Qatar inahitaji wafanyakazi wenye nguvu na afya ambao wanaweza kufanya kazi vizuri katika mazingira yenye shughuli nyingi ya ikulu."
"Na waombaji wanapaswa kuwa warembo - warembo sana," anasisitiza.
Joanna Concepcion wa shirika la Migrant International anasema madai ya Althea kuhusu kutumikia kama mjakazi wa familia ya kifalme ni ya kweli, lakini Joanna Concepcion wa Migrant International aliongeza: ‘’Hakuna njia ambayo tutajua ikiwa yuko sawa kama bado yuko Qatar, akihudumia familia yenye nguvu. Hapana.’’
Baadhi ya wafanyikazi waliohudumia familia ya kifalme na baadaye kuondoka nchini wamewasilisha malalamiko.
Mnamo mwaka wa 2019, wafanyikazi watatu wa Uingereza na Marekani - mlinzi wa kibinafsi, mkufunzi wa kibinafsi na mwalimu wa kibinafsi - walifungua kesi dhidi ya dadake amiri, Sheikha Al Mayasa bin Hamad bin Khalifa Al Thani, na mumewe.
Alisema alifanya kazi kwa muda mrefu bila kulipwa saa za ziada.
Familia ya kifalme ilikanusha madai hayo na kudai kinga ya kidiplomasia kwa kuwa wito huo ulitolewa New York, Marekani.
‘’Kuripoti na kushughulikia matukio ya vurugu na unyanyasaji, ukosefu wa usalama na afya kazini, na ukosefu wa makao inaweza kuwa changamoto,’’ anasema Dk. Ruba Jaredat, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa Nchi za Kiarabu.
ILO inasema inashirikiana na serikali ya Qatar kuandaa sheria inayohakikisha kiwango cha chini cha mshahara, siku moja ya kupumzika kwa wiki, likizo ya ugonjwa na malipo ya ziada, lakini bado ‘’changamoto’’.
Ingawa analazimika kufanya kazi kwa saa nyingi, ana furaha, asema Althea, anayeishi katika jumba la kifalme.
Kabla ya kwenda kulala, yeye hutuma ujumbe kwa mmoja wa ndugu au wazazi wake nchini Ufilipino.
Mara nyingi anahisi wasiwasi wa kuwa mbali na nyumbani.
Lakini bado ni chanzo muhimu sana cha mapato.
‘’Bila kazi hii, singeweza kupata riziki,’’ anasema.
BBC ilitafuta maoni kutoka kwa familia ya kifalme ya Qatar na ubalozi wa Qatar huko London lakini haikupokea jibu.
Michoro na Martha Clough Reche.












