Faida na hatari za virutubisho vya protini

Chanzo cha picha, Getty Images
Kufichuka ukweli kuhusiana na kifo cha kijana mmoja mwenye asili ya Kihindi kulikotokana na kunywa virutubisho vya protini nchini Uingereza kumezua mjadala. Maswali yanazuka ikiwa virutubisho hivyo vinapaswa kuwekewa alama ya onyo.
Kesi hiyo ya Agosti 15, 2020, inamuhusu Rohan mwenye umri wa miaka 16 ambaye afya yake ilidhoofika ghafla na akafa hospitalini siku tatu baadaye.
Baada ya uchunguzi wa miaka mitatu na nusu, wachunguzi wamefikia hitimisho - kifo cha Rohan kilisababishwa na virutubisho vya protini alivyopewa na baba yake ili kuongeza uzito. Kulingana na wachunguzi, Rohan alikuwa na tatizo la kuzaliwa la amonia .
Mpelelezi aliiambia mahakama - kwa maoni yake, onyo linapaswa kuchapishwa kwenye lebo ya virutubisho vya protini. "Kunywa protini nyingi kunaweza kuwa hatari kwa watu ambao wana ugonjwa wa amonia."
Baada ya habari hii, sio tu nchini Uingereza bali duniani kote, wasiwasi unaonyeshwa kuhusu virutubisho vya protini - kwa sababu ni maarufu sana kwa vijana, hasa wale wanaokwenda kwenye mazoezi ya kuinua vitu vizito.
Kwa nini protini ni muhimu?

Chanzo cha picha, Getty Images
Protini ni virutubisho muhimu. Ina jukumu muhimu katika kujenga na kutengeneza misuli. Protini hufanya moyo, ubongo na ngozi kuwa na afya, pamoja na kuimarisha mifupa na kinga ya mwili.
Kulingana na Baraza la Utafiti wa Kimatibabu – India, gramu 0.8 hadi 1 ya protini kwa kila kilo moja ya uzito wa mwili wa binaadamu kwa siku inatosha. Na robo ya mlo wako inapaswa kuwa protini. Hicho ni kiwango cha kawaida cha protini kinachohitajika mwilini.
Mahitaji ya kila mtu ya protini ni tofauti kulingana na umri, afya, shughuli za kimwili na kiwango cha mazoezi, lakini watu wengi hawajui kiasi halisi wanachohitaji kulingana na afya zao.
Mayai, maziwa, siagi, samaki, kunde, nyama, soya n.k. vina protini nyingi na watu wengi hupata kiasi cha kutosha cha protini kutoka kwenye milo yao.
Vidonge vya protini hutumiwa kutengeneza protini inayokosekana katika vyakula. Vidonge vingi vya protini vinapatikana katika mfumo wa unga, ambao hutumiwa kama kimiminika kizito. Unga huu wa protini unatokana na mimea kama vile viazi, soya, mchele, njegere na mayai au maziwa.
Je, virutubisho vya protini vina hatari gani?

Chanzo cha picha, Getty Images
Dkt. Sameer Jamwal, wa Idara ya Biokemia katika Chuo cha Matibabu cha Dk. Rajendra Prasad, Kangra, Himachal Pradesh anasema, ‘’kama una uzito wa kilo 50, hakuna tatizo ukitumia gramu 50 za protini kwa siku.”
Kulingana na yeye, mwili hubadilisha amonia ya ziada inayozalishwa baada ya usagaji wa protini kuwa urea, ambayo hutolewa kupitia mkojo. Lakini watu wengi hawana vimeng'enya vinavyobadilisha amonia kuwa urea, kumaanisha kuwa wana tatizo la mzunguko wa urea.
Dk. Sameer anaeleza, kiwango cha amonia huongezeka mwilini, jambo ambalo ni hatari sana kwa ubongo. Kuna aina tofauti za matatizo haya ya urea na kwa watu ambao wana aina hii ya tatizo, utumiaji wa protini nyingi unaweza kuwa hatari.
Vrutubisho vya protini miongoni mwa vijana

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Imeonekana kuwa mwelekeo wa kuchukua virutubisho umeongezeka kwa kiasi kikubwa miongoni mwa vijana, hasa wale wanaoshiriki katika kujenga mwili na michezo.
Mmoja wa vijana hao ni Uday, ambaye anasoma katika taasisi binafsi huko Noida. Alikuwa amekonda sana tangu utotoni. Lakini akiwa chuo kikuu, alianza kujisikia aibu kuhusu uzito wake, baada ya hapo alianza kutumia protini ili kuongeza uzito. Uzito wake uliongezeka lakini matatizo pia yalianza.
Manish Singh, daktari mkuu kutoka Kituo cha Matibabu cha Pushpanjali cha Delhi, anasema - amekutana na visa vingi ambapo vijana walianza kutumia virutubisho vya protini bila kufikiria na kisha kuugua.
"Tunaepuka sharubati ya protini kwa sababu wakati mwingine huathiri seli na kupunguza kinga ya mwili," anafafanua.
Dkt. Manish anasema, “nimeona visa vingi vya vijana wenye matatizo ya maini. Hupata nimonia. Halafu nagundua kuwa wanatumia protini hiyo kwa ajili ya kujenga mwili."
Dkt. Manish anaeleza, kuna watu wengi wanaoanza kutumia virutubisho bila kujua faida na madhara yake.
Aanasema, “unajengaje mwili wakati huna afya. Nimeona watu wengi wanaokwenda kwenye jimu na wamepata matatizo ya moyo. Mwili mzuri sio kipimo cha afya njema. Jambo muhimu zaidi ni kuwa na chakula bora."
Soko la virutubisho vya protini

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahitaji ya protini na virutubisho vingine yanakua kwa kasi nchini India. Kulingana na IMRC, soko la virutubisho hivyo nchini India lilikuwa karibu Rupia bilioni 436 - 2022, itakua karibu Rupia bilioni 958 ifikapo 2028.
Biashara ya virutubisho vya protini bandia pia imeanza kupata faida.
Aman Chauhan, anayendesha maonyesho ya virutubisho na bidhaa za afya huko Delhi Magharibi, anasema ni muhimu kuepuka bidhaa mbovu na ghushi.
Anasema, "virutubisho vinapaswa kununuliwa tu kutoka katika maduka yaliyoidhinishwa na makampuni yaliyoidhinishwa. Hakikisha umeangalia muhuri kwenye kifurushi cha bidhaa na lebo ya muagizaji."
Huko Uingereza bado haijaamuliwa ikiwa virutubisho vya protini vinapaswa kuwa na onyo kwenye lebo yao. Lakini je, onyo litatosha?
Madaktari wanasema, watu wanapaswa kutunza lishe zao na kuchukua lishe bora badala ya kutumia virutubisho. Kuwa na onyo lililoandikwa kwenye lebo kunaweza kusiwe na ufanisi sana.












