Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Marekani inapendelea uwepo wa taifa huru la Palestina?
Kura ya turufu ya Marekani ya kukataa kupitisha muswada wa azimio katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo inapendekeza Baraza Kuu kukubali Palestina kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa, limelileta suala la uzito wa Washington katika kuunga mkono suluhisho la kuwa na serikali mbili.
Rasimu ya azimio hilo, ambayo ilizuiwa na utawala wa Biden siku ya Ijumaa usiku, iliidhinishwa na idadi kubwa ya nchi 15 wanachama wa Baraza la Usalama, zikiwemo nchi zinazoshirikiana na Marekani kama vile Ufaransa, Korea Kusini na Japan, kuwa nchi 12. walipiga kura ya kuidhinisha, huku Uingereza na Uswizi zikisusia kupiga kura.
Palestina ni nchi isiyo mwanachama ambayo ina hadhi ya mwangalizi katika Umoja wa Mataifa kwa azimio lililopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo 2012.
Marekani ina uhalali wake wa kukataa kupitisha azimio hilo, kwani Naibu Balozi wa Marekani Robert Wood alisema kuwa kura ya turufu ya Marekani “haioneshi upinzani dhidi ya taifa la Palestina, lakini ni kukiri kwamba taifa la Palestina haliwezi kuanzishwa isipokuwa kwa mazungumzo ya moja kwa moja. kati ya pande mbili (Wapalestina na Israel).”
Miongoni mwa wale wanaoona kwamba Marekani inataka kufikia suluhu ya mataifa mawili na wale wanaoona kinyume chake, Khattar Abu Diab, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Paris, aliiambia BBC Arabic kwamba wanazungumza kuhusu taifa la Palestina, au mataifa mawili, suluhisho la serikali, lilianza kuangaziwa hasa tangu Makubaliano ya Oslo, ambayo pia yanataja hatua za mpito.
"Kila mtu anajua kwamba njia hii, ambayo Marekani ilikuwa inasimamia, haikufikia matokeo kwa sababu Marekani ilikuwa na upendeleo kwa Israel," Alisema.
Wakati huo huo, mwanadiplomasia wa Marekani ambaye anaongoza Baraza la Sera za Mashariki ya Kati, Gina Winstanley, anasema kuwa nchi yake "inaunga mkono kwa nguvu suluhisho la serikali mbili."
Kwa nini Washington haikukubaliana na rasimu ya azimio hilo?
Tangu kuanza kwa vita vya Gaza tarehe 7 Oktoba, maafisa katika utawala wa Rais wa Marekani Joe Biden walizungumza mara kwa mara juu ya ulazima wa kusonga mbele kwa suluhisho la mataifa mawili kama njia ya kufikia amani kati ya Wapalestina na Israel.
Washington, mshirika mashuhuri zaidi wa Israel, inahalalisha, kupitia maafisa wake, kukataa kwake kukubali uanachama kamili wa taifa la Palestina bila ya kibali cha Israel kwa kusema kwamba hilo lazima lifanyike "kupitia diplomasia na si kwa kulazimisha," kulingana na kile Waziri wa mambo ya Nje , Anthony Blinken, alisema katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mkutano wa G7 huko Capri.
Blinken alisema, "Tunaendelea kuunga mkono taifa la Palestina kwa kuhakikisha usalama wa Israel."
Marekani ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Israel kama taifa huru mnamo Mei 14, 1948.
Winstanley aliiambia Idhaa ya Kiarabu ya BBC kwamba Marekani imekuwa ikipinga kuruhusu "Palestina kuwa mwanachama kamili bila muundo wa taifa kuwa wazi, na kwa idhini ya Israel."
Ni vyema kutambua kwamba ingawa zaidi ya miaka 75 imepita tangu Israel itangaze kuanzishwa kwa taifa hilo, mipaka yake bado haijaamuliwa kikamilifu.
Khattar Abu Diab, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Paris, anaeleza kwamba tatizo kuu ni kupata kibali cha Israel, kwa kuwa “tangu kuuawa kwa Waziri Mkuu wa Israeli Yitzhak Rabin, ndoto ya amani imezima kwa njia moja au nyingine, na mazingira ya kisiasa ya Israel yanazidi kuwa magumu."
Kuhusu mazingira ya kisiasa ya Wapalestina, Abu Diab anasema kwamba, kuna tatizo pia kwa Marekani, ambayo inataka yeyote anayeelekea katika taifa la Palestina awe na udhibiti wa ardhi na kutumia mamlaka ipasavyo.
Kuna tatizo la makazi, ukuta wa utengano ambao Israel iliuanzisha katika Ukingo wa Magharibi, na ukosefu wa umoja wa Wapalestina. "Bila shaka kutakuwa na matatizo ya mipaka, makazi na kuamua ukubwa wa eneo hilo, lakini haya ni masuala ambayo Marekani inayaona kama aina ya uhalali wa msimamo wake wa kuegemea Israel," Khattar anaongeza.
Israel, pamoja na serikali yake kwa sasa inayoongozwa na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, inakataa kuanzishwa kwa taifa la Palestina, na kukaribisha kura ya turufu ya Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz, alieleza pendekezo lililotolewa na Algeria kuwa la “aibu,” na akasema, “Pendekezo hilo la aibu lilikataliwa, na ugaidi hautalipwa,” kulingana na kile kilichoripotiwa na gazeti la Kiebrania Haaretz. .
Balozi wa Israel Gilad Erdan alimshukuru Rais wa Marekani Joe Biden kwa kile alichokiita "kusimama na ukweli na maadili mbele ya unafiki na siasa" katika kutumia kura yake ya turufu dhidi ya rasimu ya azimio hilo.
Alizingatia kwamba kupiga kura kuunga mkono azimio hilo "kutahimiza tu Wapalestina kukataa 'suluhu' na kufanya amani iwe jambo lisilowezekana kufikiwa."
Netanyahu pia alisema mapema kwamba "Mapatano ya Oslo yalikuwa kosa kubwa ambalo halipaswi kurudiwa," na alizingatia kuwa kuwapa Wapalestina mamlaka kamili ni tishio kwa maisha ya Waisraeli.
Kwa upande mwingine, Mamlaka ya Palestina, inayoongozwa na Mahmoud Abbas, imelaani uamuzi huo wa Marekani na kusema katika taarifa yake kwamba kura ya turufu ya Marekani haikuwa ya haki, isiyo ya kimaadili, na haina haki, na inapingana na matakwa ya jumuiya ya kimataifa, ambayo inaunga mkono kwa dhati serikali. ya Palestina kupata uanachama kamili katika Umoja wa Mataifa...”
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Sera hii ya kichokozi ya Marekani dhidi ya Palestina, watu wake, na haki zake halali inawakilisha uchokozi wa wazi dhidi ya sheria za kimataifa, na inahimiza kuendelea kwa vita vya Israel vya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wetu katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Hamas pia ililaani kura ya turufu ya Marekani na kusema katika taarifa yake kwamba Marekani "imesisitiza msimamo wake dhidi ya watu wetu wa Palestina na haki yao ya kujitawala na kuanzishwa kwa taifa lao huru la Palestina.
Je, ingekuwaje iwapo Marekani isingetumia kura yake ya turufu?
Blinken alisema azimio lililopigiwa kura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa "halitakuwa na athari yoyote katika maendeleo ya mambo na kufikia taifa la Palestina."
Winstanley anaona kuwa wakati Marekani inaunga mkono suluhu ya mataifa mawili, "ina wasiwasi kuwa bila ya kibali cha Israel, uanachama wa Umoja wa Mataifa hautakuwa na maana halisi na huenda ukasababisha kuongezeka kwa mivutano ya kikanda."
Anaashiria kile kinachotokea katika Ukanda wa Gaza kwa kusema, "Bila idhini ya Israel, ushirikiano wa pande mbili unaohitajika ili kuhakikisha uendelevu wa taifa la Palestina hautawezekana. Bila idhini ya Israel, ni jinsi gani mipaka inaweza kuamuliwa au kulindwa? Hali ya sasa katika Ukanda wa Gaza inaonesha jinsi gani utambulisho na uungwaji mkono wa Israel ni muhimu,” anasema Winstanley.
Wakati Mamlaka ya Palestina inaamini kwamba ilikuwa ni lazima kupitisha rasimu ya azimio la kutambua uanachama kamili wa Palestina katika Umoja wa Mataifa, ilisema katika taarifa yake kwamba "kupatikana kwa amani, usalama na utulivu katika eneo letu na dunia kunategemea utekelezaji wa uhalali wa kimataifa.
Maazimio, kukomesha uvamizi wa Israel katika ardhi ya Palestina, na kutambua haki halali za watu wa Palestina, kwanza kabisa." Haki yake ya kujitawala na kuanzishwa kwa nchi yake huru na Jerusalem Mashariki kama mji mkuu wake.”
Khattar anasema kwamba kuidhinisha rasimu ya azimio inaweza kuwa jambo la kiishara, "lakini ni muhimu ili kusajili nafasi kwa siku zijazo. Hii ni hatua ambayo lazima ikamilishwe sasa.”
Anaongeza kuwa hata kama Baraza la Usalama halitakubali, "ikiwa nchi za Ulaya zitaanza, kama Uhispania na Ireland ... kutambua taifa la Palestina kwa upande mmoja, itakuwa na maana kubwa. Itamaanisha kuweka msingi wa siku zijazo na kwamba kuna utashi wa kisiasa wa kimataifa kutafuta suluhisho na njia ya kutoka kwenye mzozo huu sugu.
Baada ya kumalizika kwa kura hiyo, Mwakilishi wa Kudumu wa Taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa, Balozi Riyad Mansour, alisema, “Uanachama wa Taifa la Palestina katika Umoja wa Mataifa si jambo la kiishara, bali ni suala la umuhimu kwa Wapalestina na watu wa eneo hili katika hatua hii nyeti.”
Mansour aliongeza, "Hii ni hatua ambayo imekuwa ikisubiriwa tangu mwaka 1947. Ni hatua ya lazima ya kukomesha dhulma ya kihistoria ambayo imekuwa ikitendewa watu wa Palestina tangu uamuzi wa mgawanyiko, kupitia Nakba, na hadi leo. ili imani irejeshwe katika uhalali wa kimataifa na sheria za kimataifa, na katika shirika hili na katiba yake."
Balozi wa Algeria Ammar Ben Jama alisema kwamba kukubali uanachama kamili wa Palestina ni hatua madhubuti "kuelekea kurekebisha dhuluma ya muda mrefu... Udhalimu huu wa kihistoria lazima ushughulikiwe na mizani ya haki kusawazishwa."
Umoja wa Mataifa unasema kwamba “makubaliano kati ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama ni muhimu ili kukubali nchi yoyote mpya mwanachama. Maombi ya uanachama katika Umoja wa Mataifa yanatumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kisha kupelekwa kwa Baraza la Usalama na Baraza Kuu.
Baraza la wanachama 15 ndilo linaloamua kama litakubali serikali au la baada ya hapo. Kamati ya Kuandikishwa kwa Wanachama Wapya hujadili suala hili, kisha hutuma uamuzi wake kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama 193.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anaamini kwamba "kushindwa kupiga hatua kuelekea suluhu la serikali mbili kunaongeza hali tete na hatari kwa mamia ya mamilioni katika eneo zima, kwani wataendelea kuishi chini ya tishio la mara kwa mara la ghasia."
Licha ya azimio nambari 242 la Umoja wa Mataifa, ambalo linasisitiza kujiondoa kwa Israel katika ardhi ilizozikalia mwaka 1967, Wapalestina hawajapata dola yenye mamlaka kamili juu ya ardhi hizi hadi leo.
Imetafsiriwa na Lizzy masinga n kuhaririwa na Seif Abdalla