Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, shambulizi la Iran dhidi ya Israel linampa Netanyahu fursa mpya?
Haikuwa siku nyingi zilizopita ambapo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa chini ya shinikizo kubwa.
Baada ya wafanyakazi saba wa kutoa misaada kutoka shirika la World Central Kitchen kuuawa na jeshi la Israel huko Gaza tarehe 1 Aprili, Rais wa Marekani Joe Biden alionekana kukosa subira na mshirika wake.
Siku hiyo hiyo, Israel ilishambulia makao ya wanadiplomasia wa Iran mjini Damascus, na kumuua jenerali mkuu, na maafisa wengine wasiopungua sita, na kukiuka mikataba ya kisheria inayokataza mashambulizi dhidi ya balozi.
Israel ilidai kwamba Iran ilipoteza ulinzi huo kwa kugeuza jengo la kibalozi lililoharibiwa kuwa kituo cha kijeshi. Iran iliahidi kulipiza kisasi, lakini mashambulizi ya hapo awali dhidi ya makamanda wakuu yalisababisha maneno mengi kuliko vitendo.
Nje ya Iran, shambulio la Damascus lilifunikwa na ghadhabu iliyosababishwa na mauaji ya timu hiyo kutoka kwa World Central Kitchen, shirika la kutoa misaada lenye makao yake makuu nchini Marekani.
Ikulu ya White House ilitoa taarifa ya hasira kutoka kwa Rais Biden. Alikasirika na kuvunjika moyo. Israel haikufanya vya kutosha kuwalinda wafanyakazi wa shirika la kutoa misaada au raia wa Palestina.
Katika mazungumzo ya simu ya hasira na waziri mkuu, alidai matakwa makubwa. Gaza inapaswa kufurika na misaada ya kibinadamu. Israel lazima ifungue vivuko zaidi vya mpaka, pamoja na bandari ya kuingiza kontena huko Ashdodi, umbali wa chini ya saa moja kwa gari kutoka kwa watoto wanaofariki kwa njaa kaskazini mwa Gaza.
Waziri Mkuu Netanyahu aliahidi kuwa mambo yatabadilika lakini Israel, ilikuwa inachelewa kuchukua hatua.
Kando na msukumo kutoka Ikulu ya White House, Bw Netanyahu pia alikuwa chini ya shinikizo kutoka kwa watu wenye msimamo mkali ambao uungwaji mkono wao katika bunge la Israel unaweka muungano wake madarakani.
Sio tu kwamba wanapinga msaada kuingia Gaza. Wanaamini kuwa vita hivyo vimeipatia Israel fursa ya kuwaweka upya walowezi wa kiyahudi huko Gaza. Makaazi ya Wayahudi huko yalihamishwa na kubomolewa na Israel mnamo 2005 kama sehemu ya kujiondoa kwa upande mmoja kutoka kwa eneo hilo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Marekani ilikuwa ikiongeza shinikizo. Siku ya Alhamisi, Samantha Power, afisa wa ngazi ya juu wa masuala ya kibinadamu wa Marekani, alisema ni Habari "ya kuaminika" kwamba njaa tayari inaathiri sehemu za Gaza.
Ilikuwa dhahiri kwa marafiki wa Israel pamoja na maadui zake kwamba kuzingira kwake Gaza kwa miezi sita kulikuwa kumezua hali ya dharura ya chakula duniani. Kulikuwa na uvumi mwingine kwamba Marekani ingeweka masharti ya matumizi ya silaha inazotoa kwa Israeli.
Siku ya Jumamosi asubuhi, saa chache kabla ya shambulio la Iran dhidi ya Israel, gazeti la New York Times liliandika juu ya hasira kali, hasa miongoni mwa Wanademokrasia mashuhuri katika Bunge la Marekani. Iliomba kusitishwa kwa usambazaji wa silaha kwa Israel.
Chini ya kichwa cha habari, Misaada ya Kijeshi kwa Israeli Haiwezi Kuwa Bila Masharti, bodi ya wahariri wa gazeti hilo ilimkashifu Bw Netanyahu na watu wenye msimamo mkali katika serikali yake kwa kuvunja "kifungo cha uaminifu" na Marekani. Kujitolea kwa Marekani kwa Israel, na haki yake ya kujilinda, hakumaanisha kwamba Rais Biden "amruhusu Bw. Netanyahu kuendelea kucheza michezo yake ya isiyofaa", ilisema.
Kisha shambulio la kwanza kabisa la Iran dhidi ya Israel lilimpa waziri mkuu njia ya kujinusuru katika joto hilo.
Katika hatua ya ajabu ya ushirikiano wa kijeshi, Marekani na washirika wengine wa Magharibi waliisaidia Israel kuangusha ndege zisizo na rubani 300 na makombora yaliyorushwa na Iran.
Hakuna kiongozi wa kiarabu ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa vita vya Israel huko Gaza kama mfalme Abdullah wa Jordan. Lakini jeshi la anga la Jordan lilijiunga na operesheni hiyo, na kuangusha makombora kuelekea Israel.
Wito wa kuweka masharti ya usaidizi wa kijeshi kwa Israel ulibadilishwa na maneno ya mshikamano.
Waziri Mkuu Netanyahu amepewa fursa mpya za kisiasa. Gaza sio tena angalizo katika vichwa vya habari, angalau kwa siku moja au mbili.
Lakini shinikizo kwa waziri mkuu limebadilika. Sio kwamba limekwisha. Hatua zinazofuata za Israel zinaweza kuifanya kuongezeka maradufu.
Rais Biden ameweka wazi kile anachofikiria kinapaswa kutokea baadaye. Israeli inapaswa kutangaza ushindi katika kipindi hiki, "kuchukua ushindi", na sio kujibu mashambulizi. Alitangaza tena kwamba uungaji mkono wa Marekani kwa Israel ulikuwa "thabiti".
Hiyo iliendana na sera yake thabiti tangu mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba. Rais na utawala wake wamefanya kazi kwa bidii kukomesha vita zaidi, vya pande zote katika Mashariki ya Kati, hata waliposambaza silaha nyingi kwa Israel ambazo zimetumika kuleta madhara makubwa na kuua huko Gaza.
Tangu Oktoba Israel imekubali silaha na usaidizi wa kidiplomasia ulioandamana nao na kupuuza wito wa Joe Biden unaozidi kukata tamaa na hasira wa kuheshimu sheria za vita na kulinda raia.
Siku chache tu baada ya ushirikiano wa kijeshi ambao haujawahi kushuhudiwa kutoka kwa washirika wake dhidi ya Iran, Israel inaonekana kwa mara nyingine tena kuwa na mwelekeo wa kupuuza sio tu ushauri wa Joe Biden wa kutolipiza kisasi, lakini hisia zinazofanana na hizo kutoka kwa nchi zingine ambazo zilisaidia Jumamosi usiku.
Kama vile Joe Biden, Waziri Mkuu Rishi Sunak wa Uingereza na Rais Emmanuel Macron huko Ufaransa walituma ndege za kivita, wote waliilaani Iran, na wote wameitaka Israel kutojibu shambulizi la Iran.
Haya yanawadia dhidi ya imani za muda mrefu huko Israeli. Moja ni usadikisho wa kina kwamba kwa Israel kunusurika kunategemea kujibu mashambulizi kwa nguvu nyingi sana.
Nyingine ni mtazamo wa Benjamin Netanyahu, alioueleza mara nyingi katika miaka yake ya uongozi, kwamba Iran ni adui hatari zaidi wa Israel, anayeelekea kuangamiza taifa la Kiyahudi. Waisraeli wengi wanakubaliana na maoni hayo.
Sasa, baada ya miaka mingi ya uadui tangu Mapinduzi ya Kiislamu mwaka 1979, Iran kwa mara ya kwanza imeanzisha mashambulizi ya moja kwa moja dhidi ya Israel. Vita vya muda mrefu vya siri vimejitokeza hadharani.
Israel imesema swali sio kama itajibu, lakini ni lini na vipi. Baraza la mawaziri la vita limekuwa likijadili jinsi ya kufanya hivyo bila kuanzisha vita vya kila upande. Mwishowe, hata hivyo, shambulio lolote itakuwa ni kama kamari kwamba Iran haitaki vita vya pande zote pia, itajibu ipasavyo. Hiyo ni dhana hatari. Pande zote mbili tayari zimefikiria vibaya nia ya mwenzake.
Kwa mara nyingine tena, Benjamin Netanyahu na serikali yake wamedhamiria kupuuza matakwa ya washirika ambao wamekwenda hatua ya ziada kuisaidia Israel dhidi ya maadui zake. Washirika wake wasio na msimamo mkali wanadai kufanyike shambulio kali dhidi ya Iran. Mmoja wao alisema Israel inapaswa "kuwa mbaya zaidi".
Wakati huo huo maafa ya kibinadamu yanaendelea huko Gaza. Angalizo la kimataifa katika hili limepungua lakini litarudi. Jeshi la Israel bado linaendesha shughuli zake huko Gaza na bado linaua raia. Ghasia mbaya kati ya Wapalestina na walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi zimeongezeka tena. Vita vya mpaka vya Israel na Hezbollah vinaweza kuongezeka kwa kasi.
Imetafsiriwa na Asha Juma na kuhaririwa na Yusuf Jumah