Iron Dome: Fahamu jinsi mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel unavyofanya kazi

Iran ilirusha mamia ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Israel, kujibu mashambulizi ya Israel yaliyolenga ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria Aprili 1, na kusababisha mauaji ya wanachama 7 wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi, akiwemo kamanda mkuu.

Israel ilisema kuwa ulinzi wake wa anga ulifanikiwa kukabiliana na mashambulizi mengi, nje ya anga ya Israel, kwa usaidizi wa Marekani na Uingereza.

CNN iliripoti kwamba Rais Joe Biden alitoa wito kwa Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu, katika simu, kuzingatia huo kama "ushindi," kwa sababu tathmini ya Marekani ni kwamba mashambulizi ya Iran "hayakufaulu" na yalionyesha "uwezo wa juu wa kijeshi kwa Israel kwa msaada wa Marekani.”

Mbali na usaidizi wa kijeshi wa Uingereza na Marekani, Israel ilitumia mfumo wa kujilinda dhidi ya makombora unaojulikana kama Iron Dome, ambao umeonyesha ufanisi mkubwa.

Asili ya Iron Dome

Mfumo huu wa ulinzi ulikuja baada ya vita ambavyo Israel ilipigana na Hezbollah ya Lebanon mwaka 2006, maelfu ya makombora yalirushwa Israel, na kusababisha uharibifu mkubwa, uhamishaji wa watu wengi, na watu kadhaa waliuwawa.

Israel kisha ikasema itatengeneza ngao mpya ya ulinzi wa makombora.

Kampuni ya Israel ya Rafael Advanced Defence Systems na Israel Aerospace Industries zilianzishwa kwa usaidizi wa Marekani.

Mwezi Aprili 2010, kampuni ya serikali ya Israel ya Rafael Advanced Defence Systems Ltd. Ilifichua kuwa imeunda mfumo iliouita "Iron Dome" ambao unaweza kunasa makombora ya masafa mafupi za Katyusha, ambayo Hezbollah ya Lebanon iliifyatulia Israel wakati wa vita vya 2006.

Mfumo wa Iron Dome uliwekwa katika majira ya joto ya 2011 karibu na Ukanda wa Gaza, ambapo Hamas ilirusha makumi ya makombora ya Katyusha kwenda Israel.

Baadaye, mfumo huo uliwekwa karibu na miji ya Ashkeloni na Ashdodi, kusini mwa Tel Aviv na karibu na jiji la Netivot, lililoko kilomita 20 kutoka mpaka wa Gaza.

Iron Dome hufanya kazi ya kutoa makadirio kwa kutumia rada wapi kombora lililorushwa litaanguka, kisha ndipo hutoa tathmini ikiwa kombora la kuzuia litumwe au la.

Februari 2019, Jeshi la Marekani lilitangaza mipango ya kununua na kujaribu mfumo wa Iron Dome wa Israel.

Marekani imetoa msaada mkubwa kwa ajili ya maendeleo na uzalishaji wa mfumo huo, na baadhi ya nyenzo vifaa vya mfumo huo vinatoka katika makampuni ya Marekani.

Iron Dome inaelezwa kuwa ni mifumo wa hali ya juu zaidi wa ulinzi duniani, hutumia rada kutambua vitisho na kuviharibu kabla ya kusababisha uharibifu wowote.

2014, maafisa wa Israeli walionya juu ya kile walichokiita "utalii wa Iron Dome," wakimaanisha uhakikisho kuhusu utendakazi wa mfumo huo unawafanya Waisraeli wafuatilie makombora badala ya kutafuta pakujificha.

Mfumo huo unapenyeka?

Gazeti la Uingereza The Telegraph lilichapisha ripoti Mei 2021 yenye kichwa: "Jinsi Hamas walivyoupenya ulinzi wa Iron Dome wa Israel," iliyoandikwa na mwandishi wake wa Mashariki ya Kati, Campbell MacDiarmid, na mwandishi, James Rothwell, kutoka Tel Aviv.

Gazeti hilo lilitaja maswali ya ikiwa jeshi la Israel inapaswa kuuboresha mfumo huo, baada ya raia watano wa Israel kuuawa katika mashambulizi ya makombora.

Gazeti lilidokeza kuwa mfumo huo, ambao maafisa wa Israel wanasema una kiwango cha ufanisi cha asilimia 90, tayari umeiokoa Israel na vifo vingi.

Gazeti hilo lilimnukuu mchambuzi wa masuala ya kijasusi wa gazeti la Jerusalem Post, Yona Jeremy Pope, akisema, "Iron Dome ina udhaifu wake. Lakini alisisitiza haimaanishi kuwa Iron Dome haifai tena."

Brigedia Jenerali Mstaafu wa Israel, Amir Avivi alisema Iron Dome inafanya kazi kama ilivyokusudiwa: "Iron Dome inaweza kutungua kiasi kikubwa cha makombora."

Msemaji wa zamani wa jeshi la Israel Jonathan Conricus anasema, "idadi ya vifo na majeruhi ingekuwa kubwa zaidi kama si mfumo wa Iron Dome."

Stephen Wagner, mhadhiri wa usalama wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Brunel huko London, anasema, "ingawa utendaji wa Iron Dome ni wa kushangaza. Silaha za Hamas ni rahisi na za bei nafuu na zinaweza kupenya mfumo wa ulinzi ambao mamilioni ya dola yalitumiwa kuunda, kwa ufadhili wa Marekani."

Udukuzi wa Iron Dome

Julai 2014, BBC ilipitia ushahidi uliothibitisha kwamba wadukuzi waliweza kunasa nyaraka kadhaa za siri za kijeshi kutoka makampuni mawili ya serikali ya Israel ambayo yalitengeneza Iron Dome.

Udukuzi huu uliripotiwa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya usalama ya Brian Krebs, lakini kampuni zote mbili zilikanusha kuwa mitandao yao ilidukuliwa.

Hata hivyo, timu iliyogundua udukuzi huo iliwezesha BBC kupitia ripoti ya kijasusi iliyoonyesha kuwa mamia ya mafaili yalikuwa yamenakiliwa.

Cyber Engineering ESI ilifuatilia shughuli za wadukuzi katika kipindi cha miezi minane kati ya 2011 na 2012. Ilieleza kuwa taarifa ambazo wadukuzi walikuwa wakizifuata zinahusiana na Iron Dome.

Ripoti ya Cyber Engineering ESI, iliyotayarishwa mwaka 2013, ilionyesha kuwa mashambulizi hayo yalitokea kwa kutumia zana kama zile zinazotumiwa na wadukuzi wa China kupenya makampuni ya ulinzi ya Marekani, madai ambayo serikali ya China ilikana kuhusika.