Iran yafanya shambulizi la anga dhidi ya Israel

Iran imerusha makumi ya ndege zisizo na rubani na makombora huko Israel, kuashiria shambulio la kulipiza kisasi lililokuwa likitarajiwa.

Ni mzozo wa kwanza wa moja kwa moja kati ya maadui hao wawili, ambao wamekuwa katika vita vya nyuma ya pazia kwa miaka mingi, na Iran ikitumia vikosi vya washirika wake.

Jeshi la Israel limesema Israel na nchi nyingine zimenasa makumi ya makombora na ndege zisizo na rubani, nyingi zikiwa nje ya anga ya Israel.

Rais wa Marekani Joe Biden alisema "tuliisaidia Israel kuziangusha karibu zote".

"Iran na washirika wake wanaoendesha shughuli zao nje ya Yemen, Syria na Iraq walianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya kijeshi nchini Israel," alisema, akionyesha kulaani vikali shambulio hilo.

Jeshi la Walinzi la Iran linalojulikana kama Islamic Revolution Guard Corps (IRGC) limesema shambulio hilo lililenga "maeneo mahususi".

Iran ilikuwa imeapa kulipiza kisasi kwa shambulizi la ubalozi mdogo nchini Syria la tarehe 1 Aprili ambapo maafisa saba wa IRGC waliuawa, akiwemo kamanda mkuu. Iliishutumu Israel kwa kufanya shambulizi hilo, lakini Israel haikuthibitisha wala kukanusha taarifa hizo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliitisha kikao cha baraza la mawaziri la vita baada ya kuanza kwa shambulizi la Iran, na baadaye alizungumza na Rais Biden, ambaye alisema alithibitisha "kujitolea kwa dhati kwa Marekani kwa usalama wa Israel".

Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) Admiral Daniel Hagari alisema baadhi ya makombora ya Iran yalishambulia ndani ya Israel, na kusababisha uharibifu mdogo kwa kambi ya kijeshi lakini hakuna majeruhi.

Huduma ya ambulensi ya Israel ilisema msichana wa Bedouin mwenye umri wa miaka saba amejeruhiwa na vifusi vilivyoanguka katika eneo la kusini la Arad.

"Shambulio kubwa la leo usiku la Iran ni baya zaidi," alisema. "Pamoja na washirika wetu, tunafanya kazi kwa nguvu zote kulinda Taifa la Israel na watu wa Israel."

Amesema Iran imerusha "kundi kubwa la zaidi ya ndege 200 za kuua, makombora ya kuongozwa na kujiongoza yenyewe", akiongeza kuwa Israel na "washirika wake katika eneo lote" wamekamata nyingi ya makombora hayo.

Maafisa wawili wa Marekani waliiambia CBS, mshirika wa BBC wa Marekani, kwamba majeshi ya Marekani yalidungua ndege kadhaa zisizo na rubani, lakini hawakubainisha ni wapi na jinsi gani zilinaswa.

Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilisema ndege za RAF zimetumwa nchini Iraq na Syria ili kuzuia "mashambulizi yoyote ya angani ndani ya misheni zetu zilizopo".

Ving'ora vilisikika kote Israel na milipuko mikubwa ikishuhudiwa juu ya anga ya Jerusalem, huku mifumo ya ulinzi wa anga ikirusha vitu kwenye mji huo.

Israel, Lebanon na Iraq zilifunga anga zao, huku Syria na Jordan zikiweka ulinzi wao wa anga katika hali ya tahadhari.

Jeshi la Iran la IRGC - tawi lenye nguvu zaidi la vikosi vyake vyenye silaha - lilisema lilifanya shambulio hilo "ili kulipiza kisasi uhalifu wa mara kwa mara wa utawala wa Kizayuni [Israel], ikiwa ni pamoja na shambulio kwenye ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus".

Muda mfupi kabla ya habari za kuanza kwa shambulizi la Iran, Waziri Mkuu Netanyahu alisema "mifumo ya ulinzi" ya Israel imewekwa.

"Tuko tayari kwa hali yoyote, kwa kujilinda na kushambulia. Taifa la Israel liko imara. IDF ni imara. Umma uko thabiti.

"Tunashukuru kwa Marekani kusimama pamoja na Israel, pamoja na msaada wa Uingereza, Ufaransa na nchi nyingine nyingi."

Rais Biden alikuwa amekatiza safari ya kuelekea Delaware kurejea Ikulu ya White House huku hali ya wasiwasi ikiongezeka siku ya Jumamosi.

Baada ya kuzungumza na Bw Netanyahu baadaye alisema "kesho nitawakutanisha viongozi wenzangu wa G7 ili kuratibu jibu la kidiplomasia kwa mashambulizi ya Iran."

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak alilaani shambulio la "kizembe" la Iran, na kuapa kwamba Uingereza "itaendelea kutetea usalama wa Israel na wa washirika wetu wote wa kikanda".

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa taarifa akisema "analaani vikali ongezeko kubwa linalowakilishwa na mashambulizi makubwa yaliyoanzishwa dhidi ya Israel" na Iran.

Aliongeza kwa kutoa wito wa "kukomeshwa mara moja kwa uhasama huu" na kwa pande zote kujizuia kwa kiwango cha juu.

"Si kanda wala dunia inayoweza kumudu vita vingine," alionya.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana Jumapili kwa mkutano wa dharura kuhusu shambulizi la Iran dhidi ya Israel, rais wake Vanessa Frazier alisema.

Mapema wiki hii, mawaziri wa ulinzi na wa mambo ya nje wa Israel walionya kuwa iwapo Iran itaishambulia Israel, Israel itashambulia tena ndani ya Iran.