Urusi ilivyopoteza wanajeshi 100,000 vitani Ukraine

    • Author, Olga Ivshina
    • Nafasi, BBC News Russia
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Mwaka uliopita ulikuwa wa maangamizi makubwa kwa Jeshi la Urusi tangu vita kamili vilipozuka Ukraine: Takriban watu 45,287 waliuawa.

Mwaka wa 2024 uliandikishwa kama mwaka ulioshuhudia vifo vingi zaidi kwa wanajeshi wa Urusi tangu kuanza kwa uvamizi kamili wa Ukraine mwaka 2022.

Kwa mujibu wa takwimu, takriban watu 45,287 waliuawa – karibu mara tatu zaidi ya vifo vilivyorekodiwa katika mwaka wa kwanza wa uvamizi huo, na zaidi ya vifo vya mwaka 2023, ambavyo vilifikia kilele wakati wa vita vya muda mrefu na vya kutisha huko Bakhmut.

Katika hatua za mwanzo za vita, vifo vilitokea wakati wa mapambano katika maeneo muhimu, lakini mwaka wa 2024 ilishuhudiwa idadi ya vifo ikiongezeka mwezi baada ya mwezi, huku mashambulizi yakisonga mbele taratibu.

Kwa msingi wa data, imethibitishwa kuwa Urusi ilipoteza wastani wa wanajeshi 27 kwa kila kilomita moja ya ardhi ya Ukraine waliyofanikiwa kuteka.

Takwimu hizi zilikusanywa na Shirika la utangazaji BBC Urusi, kwa kushirikiana na vyombo huru vya habari Mediazona kupitia uchambuzi wa vyanzo vya wazi kama vile makaburi ya kijeshi, kumbukumbu, na taarifa za vifo.

Mpaka sasa, wametambua majina ya wanajeshi wa Urusi 106,745 waliouawa tangu kuanza kwa uvamizi huo.

Hata hivyo, wataalamu wa kijeshi wanaamini idadi halisi ni kubwa zaidi – na huenda takwimu hizi zinaonesha kati ya asilimia 45 hadi 65 ya vifo vyote. Hii inaashiria kuwa idadi halisi ya waliopoteza maisha huenda iko kati ya 164,223 hadi 237,211.

Tarehe 20 Februari 2024 itakumbukwa kama siku iliyoshuhudia maafa makubwa zaidi kwa wanajeshi wa Urusi katika mwaka huo wa vita dhidi ya Ukraine.

Miongoni mwa waliouawa walikuwa Aldar Bairov, Igor Babych, na Okhunjon Rustamov, ambao walikuwa sehemu ya Brigedi ya 36 ya Washambuliaji wanaotumia pikipiki(Motorised Rifle Brigade) wakati ambapo makombora manne ya masafa marefu aina ya HIMARS kutoka Ukraine yalipiga eneo la mafunzo karibu na mji wa Volnovakha, katika eneo lililokaliwa kimabavu la Donetsk.

Wanajeshi hao walikuwa wameamriwa kupanga mstari kwa ajili ya sherehe ya kutunukiwa medali wakati shambulio hilo lilipotokea.

Wanajeshi 65 waliuawa papo hapo, akiwemo kamanda wao Kanali Musaev, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya.

Aldar Bairov, mwenye umri wa miaka 22 kutoka Buryatia mashariki mwa Siberia, alikuwa amesomea utaalamu wa usalama wa chakula, lakini aliajiriwa kwa amri ya kijeshi na baadaye akasaini mkataba wa kuwa askari mkufunzi.

Mnamo Februari 2022, alitumwa kupigana Ukraine na alihusika katika vita vya Borodyanka, wakati kikosi chake kilipokuwa kikielekea Kyiv mnamo Machi 2022.

Mji huo uliteketezwa karibu kabisa, na vyanzo vya Ukraine viliripoti kuwa baadhi ya wanajeshi wa Urusi walihusika katika mauaji ya raia wakati huo.

Okhunjon Rustamov, mwenye umri wa miaka 31 kutoka Chita, Siberia, alikuwa mfua chuma (welder) kabla ya kurejea jeshini baada ya kutumikia muda wake kwa amri ya jeshi kupitia vikosi maalum (special forces).

Alijikuta vitani tena kupitia msako wa lazima wa kijeshi wa sehemu uliofanyika mwezi Oktoba 2022.

Tofauti na Rustamov, Igor Babych, mwenye umri wa miaka 32, alijitolea mwenyewe kwenda vitani. Kabla ya hapo, alikuwa akifanya kazi na watu wazima na watoto wenye ugonjwa wa kupooza ubongo (cerebral palsy), akiwasaidia kwa matibabu ya mazoezi ya mwili, hadi mwezi Aprili 2023.

Kwa ujumla, wanajeshi wa Urusi 201 walikufa siku hiyo kwa mujibu wa taarifa iliyokusanywa — ikiwa ni miongoni mwa siku za vifo vingi zaidi tangu vita kuanza.

Baada ya saa chache tu kufuatia shambulizi hilo la makombora katika eneo la mafunzo, Waziri wa Ulinzi wa Urusi wa wakati huo, Sergei Shoigu, alikutana na Vladimir Putin kumpa taarifa kuhusu "mafanikio ya kijeshi" kutoka mstari wa mbele.

Hakuna hata kauli moja iliyotolewa kuhusu shambulio hilo, na Wizara ya Ulinzi haikulitaja katika taarifa zake za kila siku kwa umma.

Ndugu wa Rustamov alielezea uchungu wake, akisema:

"Desemba 2022, mume wangu alikufa. Tarehe 10 Februari 2024, baba wa ubatizo wangu. Halafu tarehe 20 Februari, kaka yangu. Kutoka mazishi ya mmoja hadi mwingine."

Maisha ya watu wa kawaida waliovutwa vitani yanaendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa, huku taarifa rasmi zikificha uhalisia wa madhara ya vita hivyo.

Unaweza pia kusoma

Katika uchambuzi wetu, tulikagua tarehe halisi za kifo cha askari. Ikiwa hiyo haikuwepo, tulitumia tarehe ya mazishi au tarehe ambayo kifo kiliripotiwa.

Katika miaka miwili ya kwanza ya vita, 2022 na 2023, hasara kwa upande wa Urusi zilifuatana: mapigano makali na vifo vingi vilipishana na vipindi vya utulivu.

Mnamo 2023, kwa mfano, majeruhi wengi walitokea kati ya Januari na Machi, wakati majeshi ya Urusi yalipojaribu kuteka miji ya Vuhledar na Bakhmut katika mkoa wa Donesk.

Katika mwaka wa kwanza wa uvamizi, kwa mujibu wa takwimu zetu, Urusi ilipoteza takriban askari 17,890. Idadi hii haijumuishi hasara katika vikosi viwili vya jeshi la Urusi katika Eneo la mashariki mwa Ukraine.

Mnamo 2023, idadi iliongezeka hadi 37,633.

Mnamo 2024, hakukuwa na kipindi kinachoonyesha kupungua kwa majeruhi. Vita vya umwagaji damu kwa Avdiivka na Robotyne vilifuatiwa na mashambulizi makali kuelekea Pokrovsk na Toretsk.

Mnamo Agosti 2024, wanajeshi wa Urusi waliuawa wakati vikosi vya Ukraine vilipovuka mpaka na kuingia eneo la Kursk. Kuanzia Agosti 6 hadi 13 pekee, takriban wanajeshi 1,226 wa Urusi walikufa.

Hata hivyo, hasara kubwa zaidi ya jumla ilitokea wakati wa mafanikio ya kasi ndogo kwa upande wa Urusi katika Eneo la mashariki kati ya Septemba na Novemba 2024, kwa mujibu wa mchambuzi mkuu wa kijeshi wa Marekani Michael Kofman.

"Mbinu zilizotumika ni mashambulizi ya mara kwa mara na vikundi vya uvamizi vilivyotawanywa, kwa kutumia vikosi vidogo ambavyo,viliongeza majeruhi kwa ujumla kuhusiana na ardhi iliyopatikana," alielezea.

Baada ya karibu miaka miwili ya mapigano makali, vikosi vya Urusi viliteka ghala la vifaa vya Vuhledar huko Donetsk mnamo 1 Oktoba 2024.

Kwa mujibu wa makadirio ya Taasisi ya Marekani ya Utafiti wa Vita (ISW), kuanzia Septemba hadi Novemba 2024, vikosi vya Urusi viliteka kilomita za mraba 2,356 za Ukraine.

Hata wakati huo, vikosi vya Ukraine vilivyokuwa mbele havikudhoofishwa..

Hasara hii y awali ilikuwa takriban vifo 11,678 kwa jeshi la Urusi.

Idadi halisi ya hasara inaweza kuwa kubwa zaidi. Tumewahesabu askari na maafisa ambao majina yao yalijitokeza katika kumbukumbu zinazopatikana kwa umma na ambao tarehe zao za kifo au mazishi ziliangukia katika kipindi hiki.

Kwa jumla mnamo 2024, kulingana na ISW, Urusi iliteka kilomita za mraba 4,168 za ardhi. Hii ina maana kwamba kwa kila kilomita ya mraba iliyokamatwa, askari 27 wa Urusi waliuawa, na hii haijumuishi waliojeruhiwa.

Hasara ilivyobadili namna ya kuajiri

Urusi imepata mbinu ya kujiimarisha pale ilipodhoofishwa kinguvu.

"Idadi ya walioajiriwa iliongezeka kwa upande wa Urusi katika nusu ya pili ya 2024 na kuzidi majeruhi, ikiruhusu Moscow kutoa fomu za ziada," anasema Michael Kofman.

Malipo ya mara moja kwa askari wanaosaini mikataba mipya yaliongezwa katika mikoa mitatu ya Urusi. Mishahara ya askari wa kujitolea ni mara tano hadi saba zaidi ya wastani wa mshahara katika mikoa mingi.

Pia tunaweka kama watu wa kujitolea wale waliojiandikisha ili kuepuka mashtaka ya jinai, ambayo yaliruhusiwa kisheria mwaka wa 2024.

Wapiganaji wa kujitolea wamekuwa aina inayokua kwa kasi zaidi ya majeruhi katika hesabu zetu, na kufanya robo ya wale tuliowatambua.

Mnamo 2023-2024, maelfu ya wapiganaji wa kujitolea ambao walitia saini mikataba na Wizara ya Ulinzi walitumwa mstari wa mbele siku 10-14 tu baadaye.

Uhaba wa mafunzo umechangia kuwapunguzia nafasi ya kunusurika kifo katika uwanja wa mapambano, wataalam wanasema.

Jamhuri moja ya Urusi, Bashkortostan, imeshuhudia idadi kubwa zaidi ya majeruhi, na vifo 4,836 vilivyothibitishwa. Wengi walikuwa wanatoka vijijini na 38% walikuwa wameenda kupigana bila uzoefu wa kijeshi.

Malipo ya mara moja ya kusaini kandarasi ya jeshi la Urusi huko Ufa ni mara 34 ya wastani wa mshahara wa kiasi cha paundi 600.

Kuhesabu vifo kutoka kwenye data huria hakutakuwa kamili kila wakati.

Hii ni kwa sababu miili ya idadi kubwa ya wanajeshi waliouawa katika miezi iliyopita bado inaweza kuwa kwenye uwanja wa vita na kuirejesha ni hatari.

Idadi ya kweli ya vifo kwa vikosi vya Urusi inaongezeka sana, ikiwa unajumuisha wale waliopigana dhidi ya Ukraine kama sehemu ya nchi zinazojiita Jamuhuri ya watu wa Donetsk na Luhansk.

Tathmini ya miili na ripoti za utafutaji wa wapiganaji ambao wamepoteza mawasiliano inaonyesha kuwa kati ya watu 21,000 na 23,500 wanaweza kuwa wameuawa kufikia Septemba 2024.

Hiyo inaweza kufanya jumla ya vifo kufikia 185,000 hadi wanajeshi 260,700.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi