Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maisha ya ajabu ya wapenzi waliomuua binti yao bila kukusudia
- Author, Daniel Sandford & Sarah McDermott,
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Jioni ya tarehe 5 Januari 2023, polisi waliitwa baada ya gari lililotelekezwa kuonekana linawaka moto karibu na Bolton, Uingereza. Ndani ya mabaki ya gari, maafisa waligundua pesa taslimu pauni 2,000, simu 34 za bei nafuu, na pasipoti ya mwanamke.
Kondo la nyuma lililofungwa kwenye taulo lilipatikana kwenye kiti cha nyuma. Kuashiria kuwa kuna mtoto mchanga alizaliwa.
Mmiliki wa pasipoti na mpenzi wake, walikuwa wanajulikana sana na vyombo vya usalama. Utafutaji wa nchi nzima ulianza.
Lakini kwa muda wa miezi miwili iliyofuata, wakati wa majira ya baridi kali, wapenzi hao walijitahidi sana kuepuka kukamatwa. Waliishi kwa shida katika hema la bei rahisi na kuchakura mapipa.
Walipokamatwa mwishoni mwa Februari, mtoto wao hawakuwa naye tena - na walikataa kuwaambia polisi aliko mtoto huyo.
Wawili hao walijaribu sana kukimbia vyombo vya usalama, kwa sababu huyu hakuwa mtoto wao wa kwanza. Walikuwa na wengine wanne - wote wako katika vituo vya matunzo.
Ndani ya siku chache, polisi waligundua maiti katika kibanda huko Brighton, karibu na eneo ambalo wawili hao walikamatwa. Ndani ya mfuko uliofunikwa kwa udongo na takataka, mwili wa msichana mchanga - mwenye umri wa wiki chache tu ulipatikana, ukiwa ufungwa katika shuka la pinki.
Uchunguzi wa BBC
BBC imekuwa ikichunguza maisha ya Constance Marten na Mark Gordon, na matukio yaliyosababisha kifo cha mtoto wao wa tano, Victoria.
Constance anatoka katika familia tajiri iliyo na uhusiano wa karibu na familia ya kifalme ya Uingereza - aliwaambia marafiki zake kuwa alicheza na Mwana mfalme William na Harry wakiwa watoto. Naye Gordon ni mtoto wa muuguzi ambaye alihamia Uingereza kutoka Caribbean.
Wakiwa vijana, mmoja wao alisafiri hadi Nigeria kujiunga na kanisa la siri la kiinjilisti, huku mwingine akipelekwa katika gereza la Florida kwa sababu ya ubakaji.
Baba yake Constance, Napier alimwoa msoshalaiti anayeitwa Virginie Camu mwaka 1986, na baadaye wakazaa watoto watatu. Mkubwa ni huyo Constance, alizaliwa Mei 1987 – ambaye sasa anajulikana kwa jina la utani "Toots."
Mama yake Mark Gordon, Sylvia, alikuja Uingereza na aliolewa na Luckel Satchell, pia kutoka Jamaica, alizaa naye watoto wanne. Lakini ndoa yake iliishaisha alipokuwa na ujauzito wa Gordon, mtoto wake wa tano, ambaye alimzaa mwaka 1974.
Gordon alipokuwa bado mdogo, Sylvia aliacha kazi yake kama muuguzi katika kiwanda cha magari cha Chrysler huko Midlands, na kuhamia Marekani, hatimaye akaishi Florida.
Akiwa na umri wa miaka 14, katika jiji la Miami, Gordon alifanya uhalifu wa kikatili.
Nyaraka za mahakama ya Marekani zinaonyesha, mapema asubuhi ya Aprili mwaka 1989, alivunja nyumba ya jirani yake mwenye umri wa miaka 30, akiwa na mkasi wa kukatia bustani na kisu cha jikoni.
Akiwa amevalia mavazi meusi, huku uso wake ukiwa ameufunika kinyago, Gordon alimwambia mwanamke huyo asipige kelele la sivyo atamuua mwanawe na bintiye, waliokuwa wamelala katika chumba jirani. Kwa saa nne na nusu zilizofuata, alimbaka akiwa amemuwekea kisu.
Baada ya shambulio hilo, polisi aliyekuwa akishika doria katika kitongoji hicho alipata nailoni yenye matundu ya macho na pua nje ya nyumba ya Gordon na akakamatwa ili kuhojiwa.
Gordon awali alikiri makosa, lakini baadaye alikana na kesi ikaenda mahakamani.
Katika kusikilizwa kwa hukumu yake mwaka 1990, mwanamke ambaye alimbaka alimwomba hakimu atoe adhabu kali kwa Gordon, wakati huo akiwa na umri wa miaka 15.
Mark Gordon alihukumiwa kifungo cha miaka 40 jela.
Wakati Gordon akiwa gerezani huko Florida, Constance – mdogo kwa miaka 13 kuliko Gordon - alikuwa akilelewa Dorset, Uingereza.
Alisoma St Mary's, Shaftesbury, shule binafsi ya wasichana ambapo alikuwa na sifa ya kuwa mkaidi kidogo. Akiwa na umri wa miaka saba, wazazi wake walitengana.
Baba yake aliripotiwa kuiacha familia yake kwa safari ya kiroho kwenda Australia, wakati mama yake alikuwa na ujauzito wa mtoto wake wa nne. Baadaye aliolewa tena.
Baada ya kumaliza shule mwaka 2006, Constance na mamake walisafiri kwa ndege hadi Nigeria, kutembelea kanisa liitwalo Synagogue, Church of All Nations (Scoan) mjini Lagos.
Mama ambaye wakati huo akijulikana kama Virginie De Selliers, kisha akarudi Uingereza, huku binti yake akibaki kuwa mfuasi wa kanisa hilo.
Uchunguzi wa BBC Africa Eye ulipata ushahidi wa unyanyasaji na mateso mengi yaliyofanyika Scoan chini ya uongozi wa TB Joshua, ikiwa ni pamoja na madai ya ubakaji uliofanywa na Joshua mwenyewe na kulazimishwa kutoa mimba, unyanyasaji uliochukua karibu miaka 20. Mhubiri huyo alifariki 2021.
Lakini BBC haina sababu ya kuamini kwamba Constance - ambaye alikuwa na umri wa miaka 19 wakati huo - alifanyiwa unyanyasaji wowote huko.
BBC ilimtafuta Virginie de Selliers kwa maoni yake, lakini hakujibu
Baada ya miezi minne, Constance alifukuzwa Scoan na kurudi Uingereza, ambako alijiunga na Masomo ya Kiarabu na Mashariki ya Kati katika Chuo Kikuu cha Leeds na kukaa mwaka mmoja huko Cairo.
Akiwa bado mwanafunzi, jarida la Tatler lilichapisha ripoti kuhusu Constance mwenye umri wa miaka 21 kama "mtoto wake wa mwezi, katika makala ya Januari 2009.
Baada ya chuo kikuu, Constance alifanya kazi kama mtafiti katika kituo cha habari cha Al Jazeera na kujaribu kutengeneza filamu kuhusu TB Joshua. Lakini kufikia 2015, aliacha uandishi wa habari na akaamua kufanya mazoezi ya kuwa mwigizaji.
Constance atoweka
Lakini mapema 2016, Constance alitoweka. Hakwenda tena darasani, hakujibu simu, na hakuna mtu aliyeweza kumpata kwenye mitandao ya kijamii.
Gordon aliachiliwa kutoka gerezani mapema 2010 baada ya kutumikia kifungo miaka 20. Alirudishwa nchini Uingereza, ambako aliwekwa kwenye sajili ya wahalifu wa ngono.
Constance anasema mara ya kwanza kukutana na Gordon ni kwenye duka la udi huko Tottenham, kaskazini mwa London. Familia ya binti huyo ilikutana naye, na walikuwa na wasiwasi sana kuhusu uhusiano huo.
Lakini kufikia mwaka 2017 Constance na Gordon walikuwa Amerika Kusini, na waliporudi Uingereza, Constance - ambaye wakati huo alikuwa na umri wa miaka 30 - alikuwa na mimba ya mtoto wake wa kwanza.
Kulikuwa na wasiwasi juu ya mtoto hata kabla ya kuzaliwa.
Constance hakuhudhuria kliniki ya ujauzito hadi ujauzito ukiwa wa miezi sita na aliwaambia wakunga kuwa anaishi kwenye gari la kempu. Alipoacha kuhudhuria kliniki, wafanyakazi wa matibabu waliokuwa na wasiwasi walitoa tahadhari ya kitaifa - wakiziomba hospitali zingine kumtafuta yeye na Gordon. Lakini tayari walikuwa wameondoka London.
Baadaye Constance alisema walihamia Wales ili kujiepusha na familia yake, ambao anasema waliajiri wapelelezi binafsi kumfuatilia kwa vile hawakumkubali Gordon.
Tarehe ya Constance ya kujifungua ilipokaribia, yeye na Gordon walikuwa wakiishi katika hema karibu na maegesho ya magari ya duka kubwa huko Carmarthen.
Kufika hospitalini, Constance alionyesha dalili za hofu. Alitoa jina la uwongo na alizungumza kwa lafudhi ya uwongo ya Ki Irish - akiwaambia wafanyakazi kuwa anatoka jumuiya ya wasafiri.
Lakini wafanyakazi hawakushawishika, wakikumbuka tahadhari ya kitaifa iliyotolewa London, waliita polisi.
Kulikuwa na mapambano na maafisa, wakisaidiwa na akina baba wengine kwenye wodi ya uzazi, ilibidi kutumia dawa ya kuwasha kumkabili Gordon.
Alikamatwa na baadaye kuhukumiwa kifungo cha wiki 20 gerezani kwa kuwashambulia maafisa wawili wa kike. Na hivyo alikosa wiki za kwanza za maisha ya mtoto wake mpya.
Huku Constance alikwenda kukaa katika sehemu ya akina mama na watoto wanaohitaji usaidizi. Lakini kulikuwa na maswali kuhusu uwezo wake wa kumtunza mtoto wake kwa usalama.
Wafanyakazi wa kijamii walipata chupa za divai kwenye chumba chake na kumuonya Constance juu ya hatari ya kupitiwa na usingizi akiwa na ananyonyesha mtoto.
Ndani ya miezi sita amri ya usimamizi ilitolewa, ili kuruhusu maafisa wa huduma za kijamii kufuatilia hali ya mtoto. Kesi ndefu katika mahakama ya familia ikaanza.
Hukumu zilizopatikana na BBC zinaonyesha Constance na Gordon mara nyingi walijiwakilisha wenyewe badala ya kutumia mawakili, walizungumza uwongo, wakati mwingine hawakufika kusikiliza kesi, na walionekana kukwepa kwa makusudi kutoa ushahidi.
Kurudi London
Kufikia mwishoni mwa 2018 wawili hao walirudi London. Waliishi katika maeneo mbalimbali, wakiondoka bila kulipa kodi zaidi ya mara moja, kulingana na wamiliki wa nyumba.
Majirani wa zamani wanasema Constance na Gordon hawakuonekana kuwa na kazi, mara chache walitoka nje, na wakati mwingine walikuwa wakigombana.
Baada ya kuzaliwa kwa mtoto wao wa pili, watu wa huduma za kijamii walihusika tena.
Wakati wa ujauzito wa tatu, mahakama ya kifamilia ilitilia uzito kesi yao baada ya Constance kuanguka kutoka kwenye dirisha la ghorofa ya kwanza, huku akiwa na ujauzito wa wiki 14 wa mtoto wake wa tatu. Wafanyakazi wa ambulensi walipowasili, Gordon awali alikataa kuwaruhusu kuingia ndani, ndipo polisi wakaitwa.
Constance aliwaambia polisi kwamba alikuwa akijaribu kurekebisha antena ya TV alipoanguka kutoka dirishani, lakini hakimu baadaye alisema kuna uwezekano, ni Gordon ndiye "alimsababishia" kuanguka.
Constance alikaa hospitalini kwa siku nane, mtoto wake ambaye hajazaliwa hakudhurika.
Alipotoka hospitalini, Constance alikimbilia Ireland na watoto wake wawili, lakini walichukuliwa na kupelekwa katika vituo vya matunzo mara tu aliporudi London. Constance na Gordon hawajawahi kuwapata tena watoto hao.
“Wawili hao waliweka uhusiano wao mbele kuliko mambo mengine yote," hakimu wa mahakama ya familia aliandika Februari 2021, na “waliona usaidizi wowote ule ni kama chuki".
"Kauli kali zinazotolewa na wazazi hawa, zinaashiria ni ya watu wawili ambao wameungana barabara katika mapambano yasiyokoma dhidi ya mpinzani asiyekuwepo," taarifa hiyo ilieleza.
Majirani wanakumbuka maafisa wa polisi walipiga simu mara kadhaa kabla ya kuzaliwa mtoto wa tatu na kuwaambia "tufahamisheni ikiwa mtasikia sauti ya mtoto."
Wiki mbili baada ya kuzaliwa, mtoto huyu pia alichukuliwa.
Constance na Gordon waliweza kuwatembelea watoto wao katika kituo cha malezi na kuleta muziki wa kucheza au zawadi. Waliwafariji watoto ikiwa wamekasirika, na kuimba na kucheza nao.
Kiisha yeye na Constance walianza kukosa kuhudhuria kuona watoto wao. Hawakutoa maelezo kwa watoto hao kwa nini hawakuhudhuria na mwishowe wakaacha kuhudhuria kabisa.
Kufikia Mei 2021, Constance alijifungua mtoto wa nne ambaye alichukuliwa baada ya wiki moja.
Miezi minane baadaye, Januari 2022, hakimu wa mahakama ya familia aliamua kwamba watoto wote wanne, wote wenye umri wa chini ya miaka 10 - wanapaswa kuchukuliwa moja kwa moja.
Katika dakika za mwisho Constance alisema atajitenga na Gordon ili kupata kuwalea watoto wake - lakini hakimu hakuamini angefanya hivyo.
Samantha Yelland, mwendesha mashtaka mkuu aliyeshughulikia kesi hiyo, anasema. “Wako kwenye mapenzi - kwa kiwango ambacho wanajipa kipaumbele wao kwanza kuliko watoto wao."
Septemba 2022, Constance alikuwa mjamzito tena. Kwa kuhofia mtoto huyu atachukuliwa, yeye na Gordon waliondoka nyumbani kwao kusini-mashariki mwa London - tena bila kulipa kodi - na kufanya maandalizi ya kutoweka.
Constance alikuwa akikusanya pesa, na kwa muda wa miezi minne iliyofuata yeye na Gordon waliishi katika nyumba mbalimbali, wakiondoka mara kwa mara ili kuepuka kutambuliwa.
Alificha ujauzito wake kwa uangalifu sana, na kama sio gari lao kuteketea kwa moto kwenye barabara kuu Januari 2023, mtoto wao mpya angebaki kuwa siri.
Bila pasipoti ya Constance, ambayo ilikuwa imeachwa kwenye gari, hawakuweza kuondoka nchini. Badala yake yeye na Gordon walielekea kusini, hatimaye wakafika pwani karibu na Brighton, ambako waliishi kwa shida katika hema dogo, dhaifu wakati majira ya baridi.
Wakati msako wa kuwatafuta ukiendelea na vyombo vya habari vikitangaza habari yao, Constance na Gordon wakiwa na mtoto wao mchanga, walinaswa kwenye CCTV.
Mtoto Victoria alionekana hajavaa vya kutosha kwa hali ya hewa ya baridi - wakati mwingine bila soksi, kofia na bila blanketi. Wazazi wake walinunua kigari ambacho hakikufaa kwa mtoto mchanga, kisha wakakitupa siku hiyo hiyo na kumbeba ndani ya zipu ndani ya koti la Constance.
Constance anasema alilala kwenye hema huku akimnyonyesha Victoria ndani ya koti lake. Anadai aliamka akiwa amelala juu ya mtoto huyo. Victoria alikuwa hatikisiki tena.
"Alikuwa amelegea" na midomo yake ikawa ya bluu,” Constance aliwaambia wapelelezi.
Yeye na Gordon walijaribu kumzindua mtoto wao kwa kumpuliza mdomoni na kusukuma kifua chake. Lakini hakuzinduka.
Wenzi hao waliubeba mwili wake kwenye begi la kubebea mizigo - na wakaupeleka ufukweni huko Brighton. Walisema walitaka kumzika lakini walikuwa wamekula kidogo sana wakati wote wa kukimbia kwao na hawakuwa na nguvu ya kuchimba shimo.
Constance alifikiria kuuchoma maiti Victoria na alikuwa amenunua chupa ya petroli - lakini akabadili wazo.
Baada ya siku 54, maafisa wa polisi waliwasaka Constance na Gordon na wakakamatwa. Mwili wa Victoria ulipatikana siku mbili baadaye.
Mtaalamu wa kuchunguza maiti alihitimisha kuwa haikuwezekana kubaini sababu ya kifo chake, lakini alisema mtoto huyo anaweza kuwa amekufa kutokana na baridi au kulaliwa.
Constance Marten, 38, na Mark Gordon, 51, walikana kumdhuru Victoria na kuficha kifo chake, lakini wamepatikana na hatia ya kuua bila kukusudia kwa uzembe.
Katika kesi yao ya kwanza walipatikana na hatia ya ukatili wa watoto, kuficha kuzaliwa kwa mtoto Victoria na kuizuia mahakama isitoe haki.
Wawili hao wanatarajiwa kuhukumiwa mwezi Septemba, mwaka huu.
Mwandisi wa BBC Helena Wilkinson, anasema nimeripoti kesi nyingi za uhalifu, lakini sijawahi kuona kesi kama ya Constance Marten na Mark Gordon. Kesi yao ilikuwa ya ajabu.
Wawili hao wakiwa mahakamani juu ya kifo cha mtoto wao, walionekana bado wanapendana kwa dhati na bado walikuwa na umoja thabiti. Na walikuwa na dharau kubwa kwa mchakato wa mahakama.