Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwanamume asiye makazi na mjane tajiri: Haya ni mapenzi au kuna hila?
Na Sue Mitchell
BBC News
Mwanamume asiye na makazi anahamia kwa mwanamke tajiri zaidi - ni hadithi ya mapenzi ya kweli, au au kuna jambo lililojificha?
Carolyn Holland alikuwa mjane tajiri mwenye umri wa miaka 80, akiishi katika eneo la mapumziko la pwani la Cayucos la California, alipokutana na David Foute, mwanamume ambaye Carolyn alimshinda kwa miaka 23 .
Alikuja kumfanyia kazi ndogo ndogo. Wiki chache baadaye, walikuwa wanandoa, wakitangaza upendo wao usio na mwisho.
Carolyn alisema hangeweza kutarajia kupenda sana mtu asiyemfahamu au kuwa na uhusiano wa kimapenzi, katika umri wake: "Amenipa kitu maalum, kwa sababu ya roho yake ya kujali. Tunashiriki mengi. Napenda utu wake na ninachukia anapoondoka."
"Nitaenda kumtunza kadri niwezavyo hadi wakati ambapo sitaweza," Dave aliniambia. "Wanaume wote wanajua kuwa Carolyn ni msichana wangu na hatusubuani. Sikawii nje kwa sababu nina mtu wa kwenda nyumbani kwake. Nitabaki naye hadi mwisho ."
Hata hivyo, binti zake waliona mambo kwa njia tofauti.
Waliamini kuwa Dave alikuwa anataka kumdanganya mama yao na baadaye angemuacha na majonzi .
Nilifahamu kuhusu hadithi ya Dave na Carolyn kwa sababu ninaishi mtaani kwao. Kasi ya maisha ni ya polepole huko Cayucos, na watu huchukua muda kuketi pamoja na kuzungumza.
Kuna gati ya ufuoni inayonyoosha karibu futi elfu moja ndani ya bahari na jioni mwanga unapofifia, unaweza kuwaona wapiga mbizi walioainishwa dhidi ya jua linalotua. Ni taswira nzuri ya hadithi ya mapenzi na nilitaka kumwamini Dave - lakini kama familia ya Carolyn, pia nilikuwa na shaka.
Je, Carolyn alikuwa karibu kuathiriwa na matumizi mabaya ya fedha, ambayo huathiri karibu mtu mmoja kati ya watano walio na umri wa zaidi ya miaka 60?
Mpenzi wa Dola Milioni moja
Sue Mitchell anasimulia hadithi ya kweli, iliyorekodiwa katika muda halisi, kuhusu ukosefu wa makazi na utajiri unavyogongana wakati mjane milionea alipompenda mfanyakazi wake.
"Tofauti ya umri ilinisumbua sana - hiyo ilikuwa onyo," mpwa wa Carolyn, Kim, aliniambia. "Kwa nini mtu wa umri huo ajifanye kama anampenda, isipokuwa kutaka mahali pa kukaa?"
Nilikuwa katika nafasi ya pekee ya kutazama hadithi hiyo ikiendelea. Kila mtu aliyehusika alitaka kuzungumza - binti za Carolyn walikuwa na hamu ya kutoa sauti kuhusu wasiwasi wao. Dave na Carolyn walifikiri walikuwa wakihukumiwa vibaya na walitaka kusimulia hadithi yao.
Nilipokutana na Dave kwa mara ya kwanza, nilimchangamkia sana. Alikuwa amependekezwa kunifanyia kazi ya ukarabati na jirani, kupitia kanisa la mtaa ambako alikuwa mshiriki wa kawaida . Dave aliwavutia wafanyakazi wengine wote kazini. Alicheza ala ya harmonica na gitaa, alikuwa mcheshi na alionekana wazi sana juu ya maisha yake ya zamani.
Hata hivyo, kadiri nilivyosikia ndivyo nilivyozidi kuelewa kwa nini familia ya Carolyn ilikuwa na wasiwasi. Dave alikuwa amefika Cayucos bila makao na alikuwa akiishi kwa shida, akilala nje kando ya gati, alipokuja kwa mara ya kwanza nyumbani kwa Carolyn kufanya kazi fulani.
Alikubali kwa urahisi kuwa alikuwa mraibu wa dawa ya kulevya ya crystal meth. Ilikuwa imempeleka kwenye biashara ya dawa za kulevya na hatimaye kumfanya awe mbishi sana hivi kwamba alifungwa jela kwa kutengeneza mabomu ya bomba ambayo polisi waliamini yalihusishwa na uwezekano wa shambulio la Walmart. Dave alikuwa - na bado anashawishika kuwa duka hilo lilikuwa na njama ya kutuwekea chipu maalum za kompyuta .
Dave alidai kuwa ameacha dawa za kulevya, lakini niliona alikuwa akinywa pombe kidogo, na alivuta bangi pia.
Binti za Carolyn, Susan na Sally, walishtushwa na mabadiliko ya utu wa mama yao baada ya kukutana na Dave. "Ni kama ulimwengu wa ndoto, ni wa ajabu sana," Sally alisema. "Alikuwa kama kijana alipokuja. Alikuwa akifanya haya yote ya ajabu akicheka .
Mabinti hawakuamini hata kidogo kuwa wanachoshuhudia ni mapenzi. Walichoona ni mwanamke mzee mpweke aliyehitaji mwenza, na mgeni mjanja mwenye hila .
Pia kulikuwa na suala la urithi. Akiwa na marehemu mume wake, Joe, Carolyn alikuwa ameunda mali lenye thamani ya dola milioni chache.
"Ni pesa za familia yetu, wazazi wangu walifanya kazi kwa bidii kwa pesa hizo. Je, tunapaswa kuwa sawa, tu kumpa mtu kama huyu asiyejijua?" Aliniuliza.
Binti za Carolyn waliamini kuwa tayari alikuwa amepoteza uwezo wake wa kiakili alipokutana na Dave. Walijaribu kumfanya atangazwe kuwa hafai kiakili kusimamia mambo yake mwenyewe.
"Wanadhani nina Alzheimers," Carolyn aliniambia. "Ndio, nasahau mambo mengi, lakini nina msongo wa mawazo sana. Ninaweza kufanya maamuzi yangu mwenyewe."
Uhusiano wake na Dave ulikuwa ukimsukuma Carolyn mbali na binti zake, lakini alihisi alikuwa na haki ya kuwa na mwenzi wa chaguo lake. Carolyn alisema hawakuwa wamempa usaidizi aliohitaji baada ya kifo cha baba yao: "Hawakuwahi kuja kuniona kabla ya Dave, kwa kweli hawakuja."
Binti zake walipinga kauli hiyo yake kuhusu kilichotokea . Susan, ambaye anaishi saa tano kutoka hapo, alisema alitamani angekuwa karibu zaidi, lakini yeye na Sally walikuwa wakilea watoto na kufanya kazi wakati wote. "Tulijaribu kumjumuisha katika kila kitu," alisema na kuongeza kuwa mama yake alisita kujihusisha.
Kabla ya Dave kuja, Sally - ambaye aliishi karibu - alikuwa amemsaidia mama yake na akaunti zake na marejesho ya kodi. Walakini, mpasuko huo ulimsukuma Carolyn kuchukua udhibiti wa fedha zake.
Muda mfupi baadaye, Carolyn alisaini makubaliano ya mkopo na Dave, na kumruhusu kununua gari la $40,000. Nilimuuliza nini kingetokea ikiwa Dave angetoweka, na kumuacha alipe gharama kamili ya mkopo. Alisema hakujali, na hakujali binti zake walifikiria nini.
"Ndio, wanadhani wananilinda kutoka kwa David, lakini David ndiye jambo bora zaidi lililonipata."
Je, ukweli ulikuwa upi kuhusu Dave? Nilimwona akirudi kwa Carolyn baada ya kazi ya siku moja, akimpikia chakula cha jioni na kumkumbusha kumeza dawa zake. Ni nyakati kama hizi ambazo zilinifanya niamini kwamba alimpenda na kumjali kwa dhati.
Lakini pia nilimshuhudia mjini, akijigamba kwa marafiki zake kwamba hivi karibuni hatolazimika kufanya kazi tena.
Niliamua kuchunguza maisha yake ya nyuma. Nilichogundua ni historia mbaya ya unyanyasaji wa nyumbani na kutelekezwa kwa watoto.
Uhusiano mmoja ulikuwa umeisha aliposhuku kuwa mwenzi wake hakuwa mwaminifu, naye akampiga. Katika ndoa ya awali, kulikuwa na mtoto wa kike ambaye alikuwa karibu kufa kutokana na kutelekezwa. Mtoto huyu alikuwa ameuzwa na Dave kwa wanandoa ambao hatimaye walimchukua kisheria.
Nilipozungumza naye, Dave alisema haya yote yalikuwa zamani - sasa alikuwa mshiriki wa kanisa, na alikuwa amefanya mapatano na Mungu ili kuishi maisha bora. Alikuwa amekuja Cayucos bila chochote, na aliona uhusiano wake na Carolyn kama ishara kwamba uhusiano wao ulikusudiwa kuwa.
"Angalia kile Yesu alinibariki nacho," alisema. "Siwezi kumuacha, kwa sababu natakiwa kuwa naye hapa."
Lakini hadithi yao ilikuwa imefika kilele cha wakati mchungu.
Moja ya mali ya Carolyn ilikuwa shamba moja lenye nyumba mbili katika mji wa karibu. Dave alimshawishi aweke nyumba hizo sokoni, ingawa nyumba moja ilikodishwa kwa mjukuu wake mwenyewe na familia yake.
Mabinti wa Carolyn walikasirika, wakiamini kwamba alikuwa akitumia fursa ya udhaifu wa akili wa mama yao. Walinionyesha picha kutoka kwa kamera ya usalama, ya mama yao akionekana kuchanganyikiwa huku Dave akiwaonyesha mawakala wa mali isiyohamishika karibu.
Carolyn alikuwa ameahidi kutoa baadhi ya $600,000 (£480,000) kutokana na mauzo ya mali hiyo kwa Dave, ili kuandalia maisha yake ya baadaye.
Uuzaji ulipita haraka na hundi iliyotumwa kwa Carolyn ilikuwa ikingoja kukusanywa kutoka kwa mawakala wanaoshughulikia uuzaji. Lakini wakati huo huo, alilazwa hospitalini na Covid.
Carolyn alikuwa amekataa kuchanjwa kwa ushauri wa Dave - alimshawishi kuwa mpango wa chanjo ulikuwa mchakato wa udhibiti wa serikali.
Kufikia wakati aliporudishwa nyumbani, hali mbaya ya kimwili na kiakili ya Caroline ilikuwa imewaruhusu binti zake kupata hadhi ya kuwa wakili, na kuwapa udhibiti wa mambo yake ya kifedha.
Carolyn alikufa hivi karibuni. " Hakufa kwa ajili ya Covid ," anasema Susan, "lakini hakika haikusaidia kwa sababu tayari hali yake ya kiafya ilikuwa ikidorora'
Mabinti hao hawakumruhusu Dave kumtembelea Carolyn katika siku zake za mwisho, na hawakumpigia simu kumwambia amekufa. Hakukuwa na mazishi pia, kwa sababu mabinti hao walikasirishwa na ukosefu wa usaidizi ambao walifikiri kuwa kanisa la mtaa lilikuwa limewapa.
Susan na Sally bado wanahisi kwamba mama yao alitumiwa vibaya, na kwamba hakuna mtu - madaktari, polisi au huduma za utunzaji - aliwasaidia. "Mikono ya kila mtu ilikuwa imefungwa," anasema. "Hawakuwa wanaona tulichokuwa tunakiona."
Kuna watu milioni moja nchini Uingereza wenye shida ya akili, theluthi moja yao hawajatambuliwa. Inawatia hatarini sana. Baada ya kusikia Susan na Sally wakieleza wasiwasi huu kuhusu mama yao, nilizungumza na madaktari bingwa kuhusu walichosema, na suala la matumizi mabaya ya fedha, ambalo ni tatizo linaloongezeka nchini Uingereza na Marekani likajitokeza
Kwa mujibu wa Dk Mark Lachs, wa kampuni ya Weill Cornell Medicine na mwenzake, Dk Jason Karlawish, kutoka Penn Memory Centre, uwezo wa kifedha unaweza kuwa mojawapo ya mambo ya kwanza kushuka wakati ubongo unaharibiwa na magonjwa au umri.
Wanataka mchakato huu kutambuliwa kama hali wanayoiita Age Associated Financial Vulnerability - mtindo wa tabia hatari ambayo haiendani na maamuzi ambayo wangefanywa hapo awali.
Dk Karlawish anasema: "Uamuzi wa kifedha ni changamoto sana kiakili. Hata ukiwa na upungufu mdogo wa utambuzi, unaweza kufanya makosa na fedha, ingawa kwa ujumla unafanya sawa katika maisha yako ya kila siku." Madaktari wananiambia kwamba nusu ya wagonjwa wanaokuja katika kliniki yao ya kumbukumbu huko New York wamezuiliwa.
Veronica Gray ni mkurugenzi wa sera katika shirika la misaada la Uingereza Hourglass, ambalo huendesha simu ya msaada kwa wazee ambao wamenyanyaswa. Anasema kwamba £19.5m ziliripotiwa kwa Hourglass kama fedha ambazo ziliibwa , kulaghaiwa au kulazimishwa kutoka kwa waathiriwa wakubwa mnamo 2022 - ongezeko la 50% katika kipindi cha 2017-2019.
Katika 70% ya kesi hizi, mwana au binti mzima anahusika. Wengine ni marafiki, walezi, wapenzi wapya na hata wajukuu. Kesi nyingi haziripotiwi kwa polisi na waathiriwa wanalazimika kuishi na athari mbaya ya unyanyasaji huu wa kifedha.
Bi Gray anauita uhalifu uliofichwa: "Wengi hupoteza kiasi kikubwa cha fedha, hupoteza mali ambayo wameishi kwa miaka mingi na hupata madeni makubwa."
Kwa familia kama za Carolyn, kuna eneo hatari inalozunguka uwezo wa kiakili na haki ya kujiamulia katika maisha ya baadaye. Sio hadithi isiyo ya kawaida pia - madaktari wanasema kwamba wanasikia hadithi zinazofanana kila wakati.
Huko Cayucos, Dave hana makao tena, ingawa ana gari ambalo Carolyn alimsaidia kununua. Ameegesha eneo lile lile alilokuwemo alipowasili mjini kwa mara ya kwanza, akijaribu kujitafutia riziki kwa kuuza vito na kazi za sanaa zilizotengenezwa kwa vitu vilivyosindikwa.
Mara ya mwisho nilipomwona, alikuwa katika hali ya mawazo na kujiambia mara kwa mara kwamba anampenda Carolyn: "Alipopiga simu nilikuja, nimemkosa Carolyn, nilimpenda Carolyn," aliniambia. "Nilikuwa kwenye misheni yangu ndogo kujaribu kumfanya awe na fahari'
Ripoti ya ziada ya Ben Milne
Sue Mitchell yuko kwenye X, zamani Twitter
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah