Senegal: Uchaguzi umetoa matumaini kwa vijana wa Kiafrika waliokata tamaa

    • Author, Leonard Mbulle-Nziege & Nic Cheeseman
    • Nafasi, Wachambuzi

Zaidi ya wiki mbili zilizopita, Bassirou Diomaye Faye alikuwa kiongozi wa upinzani asiyejulikana sana akiteseka gerezani nchini Senegal, akizuiliwa bila kufunguliwa mashitaka – kwa shutuma za kuchochea uasi.

Wiki moja iliyopita, alimshinda mgombea wa chama tawala, Amadou Ba, katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo, na kushinda 54% katika kura za duru ya kwanza.

Siku ya Jumanne, Faye mwenye umri wa miaka 44 anatazamiwa kuapishwa kama rais wa tano wa Senegal na kuwa rais mwenye umri mdogo zaidi barani Afrika kuchaguliwa.

Katika eneo ambalo idadi kubwa ya watu ni chini ya miaka 30, ushindi wake unatoa matumaini kwa vijana hao waliokatishwa tamaa na ukosefu wa fursa za kiuchumi, huku wazee wasomi wakionekana kung'ang'ania madaraka.

Ushindi wake umeimarisha taasisi za kidemokrasia nchini humo na kurejesha imani kwa wananchi juu ya demokrasia wakati ambapo mapinduzi katika mataifa mengine ya Afrika Magharibi yakitokea.

Pia unaweza kusoma

Kazi haikuwa rahisi

Kiongozi wa muda mrefu wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, ambaye amekuwa akifanya kazi na mwenzake Bobi Wine nchini mwake, anasema "mchakato wa uchaguzi wa Senegal umedhihirisha kwamba inawezekana kufikia bila vurugu mageuzi ya kidemokrasia yanayotarajiwa barani Afrika."

Kabla ya uchaguzi serikali ya Rais Macky Sall ilichukua hatua zisizo za kidemokrasia katika kile kilichoonekana kama jaribio la kujaribu kushikilia mamlaka.

Nyingi za hatua hizi zililenga kudhoofisha kasi ya chama maarufu cha upinzani, African Patriots of Senegal for Work, Ethics and Fraternity (Pastef).

Hatu zenyewe ni pamoja na kuwazuilia viongozi maarufu wa chama hicho Ousmane Sonko na Faye, ambaye alikuwa katibu mkuu wa Pastef. Pia kulikuwa na vitisho vilivyoenea kwa wafuasi wa Pastef.

Kufungwa kwa Sonko - kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, kuliibua maandamano makubwa. Na mwitikio wa vikosi vya usalama ulisababisha vifo vingi.

Sonko alitaja mashtaka hayo kuwa ya uwongo na yanalenga kumzuia kuwania urais. Pastef yenyewe ilivunjwa na serikali mwaka jana baada ya kushutumiwa kuchochea ghasia nchini - lakini uongozi wake uliendelea kufanya kazi.

Ilihitaji ushujaa wa ajabu na kazi ngumu kutoka kwa viongozi wa upinzani, mashirika ya kiraia, waandishi wa habari na wale wanaofanya kazi katika baadhi ya taasisi za kidemokrasia ili kuhakikisha hali hii mbaya inaisha katika uchaguzi.

Ni wajumbe wa Baraza la Katiba, mahakama kuu ya Senegal, waliohakikisha uchaguzi utaendelea kama ilivyopangwa – walipoamua kuwa jaribio la rais la kubadilisha tarehe ya uchaguzi lilikuwa kinyume cha sheria.

Sonko pia alionyesha kuwa tayari kubadilika na kumpa mwenzake nafasi kubwa ya kufaulu. Bila hivyo Faye asingewa na uwezo wa kushinda.

Sonko alitarajia kuzuiwa kushiriki uchaguzi huo kutokana na kutiwa hatiani, na ombi lake la kuwa mgombea lilikataliwa na Baraza la Kikatiba kwa msingi kwamba "halikuwa kamilifu."

Licha ya juhudi za kumrejesha, viongozi wa Pastef walifikia hitimisho kwamba hakuna uwezekano wa kugombea urais. Kumuunga mkono Faye, ambaye hakuwahi kushtakiwa, lilikuwa chaguo bora - ingawa ilimaanisha Sonko, kinara wa chama, atakuwa msaidizi wa Faye.

Mashirika ya kiraia na waandishi wa habari pia walifanya kazi kubwa, kuripoti juu ya ukandamizaji wa serikali na ukiukwaji wa haki za binadamu, licha ya kushambuliwa, kuzuiliwa na kupigwa mabomu ya machozi.

Kupitia kazi yao, walihakikisha raia wa Senegal na dunia nzima wanajua kinachoendelea nchini mwao, na hivyo kuongeza shinikizo kwa Rais Sall kuondoka.

Mwishowe, juhudi hizi zilisababisha Sall kuwaachilia Faye na Sonko kutoka jela.

Bado safari ni ndefu

Kama Dkt. Besigye alivyosema, matukio nchini Senegal yalikuwa ukumbusho muhimu kwamba mabadiliko ya kidemokrasia yananufaisha nchi nzima, wakati mapinduzi huunda tu aina mpya ya uongozi wa kidikteta."

Katika nchi kama vile Uganda na Zimbabwe, hali ni ngumu kwa sababu tume za uchaguzi hazina uhuru, mahakama haiko huru, na vikosi vya usalama vinafanya ukandamizaji.

Ni rahisi kusahau kuwa Rais Sall alipoingia madarakani mwaka 2012 ushindi wake pia ulitangazwa kuwa mafanikio ya kidemokrasia.

Lakini kwa kukengeuka misingi na ahadi zilizowafanya watu wamuunge mkono, rais aliyemaliza muda wake sasa atakumbukwa kwa kuwa kiongozi mwingine aliyetumia vibaya nguvu zake.

Ili kuepusha hatima kama hiyo, Faye na Bw Sonko wanafaa kuzingatia ujenzi mpya wa nchi na kuunganisha watu wao.

Hili litafanyika ikiwa wataepuka kupumbazwa na maslahi yao ya kibinafsi, na kuyumbisha serikali kwa kushindana kati yao wenyewe kwa wenyewe.

Jambo la ufanisi zaidi ambalo vyama vya upinzani vinaweza kufanya ili kukuza demokrasia ni kutawala kwa umoja na kuonyesha - kuheshimu haki za kisiasa na uhuru wa kiraia ndiyo njia bora ya kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi na utulivu wa kisiasa.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah