Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Tuliishiwa na mafuta tukakwama katikati ya bahari"
"Kulikuwa na takriban watu 140 ambao walipanda mashua katikati ya usiku, saa nane usiku."
Doudou Diop, Msenegali mwenye umri wa miaka 30, alikuwa akihatarisha kila kitu katika safari ya hatari ya boti kwenda Ulaya, kilomita 1,700 (maili 1,056) kutoka Senegal hadi visiwa vya Canary vya Uhispania.
Njia hii ya kupita Atlantiki iligonga vichwa vya habari baada ya shirika lisilo la kiserikali kusema boti tatu zilizokuwa na watu 300 zilitoweka mwishoni wa Juni.
Nilisafiri hadi katika kijiji cha mbali cha wavuvi kiitwacho Cavontin kusini mwa Senegali, ili kuchunguza. Ni mahali ambapo mamia ya wanaume husafiri kila mwaka kutafuta maisha bora huko Ulaya.
Nilimkuta Doudou Diop akiwa ameketi kwenye roshani ya nyumba yake duni wakati mvua ikinyesha, na wanawake wote katika familia yake walikuwa wamekusanyika kumzunguka.
"Tuliondoka bila matatizo na tukaweza kufika Morocco," alisema.
"Tulikuwa kilomita 500 tu kutoka Visiwa vya Canary wakati injini yetu ilipogoma ghafla. Tuliishiwa na mafuta na tukakwama katikati ya bahari na hatukuweza kuendelea na safari yetu."
Doudou Diop anasema mamlaka ya Morocco iliwakamata wote, na kuwapeleka katika mji wa karibu wa pwani, Nouadhibou, nchini Mauritania.
"Waliandika majina yetu na maelezo binafsi na kutuweka kwenye mabasi yanayoelekea nchi yetu, Senegal."
Doudou Diop alikuwa ametoweka kwa wiki moja, hivyo familia yake ilifarijika kujua kwamba bado yu hai. Haijabainika iwapo boti aliyokuwemo ilitajwa katika taarifa au ripoti zozote za vyombo vya habari.
Wakati huohuo, mzozo ulizuka kati ya serikali ya Senegal na shirika la wakimbizi la Walking Borders, kuhusu idadi ya wahamiaji ambao walipotea baharini.
Mkanganyiko wa taarifa
Helena Maleno, mwanzilishi wa Walking Borders, alianzisha kampeni ya onyo la wahamiaji waliopotea kwenye boti mnamo 9 Julai. Maleno anasema aliwasiliana na mamlaka nchini Senegal, Mauritania, Morocco na Uhispania, akiwataka wajiunge na utafutaji wa boti zilizopotea.
Mamlaka ya Uhispania imewaokoa wahamiaji 86 kutoka katika mashua iliyokuwa ikielea karibu na visiwa vya Canary walipokuwa katika harakati za kutafuta mojawapo ya boti tatu zilizotoweka.
Kisha Wizara ya Mambo ya Nje ya Senegal ilitoa taarifa; "ukaguzi uliofanywa unaonyesha habari hii haina msingi," ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa raia wake 260 waliokolewa katika eneo la maji ya Morocco kati ya Juni 28 na Julai 9.
Walking Borders baadaye ilitoa taarifa nyingine, ikisema imeweza kuthibitisha watu waliookolewa waliotajwa na serikali ya Senegal walikuwa kwenye boti zingine "ambazo pia ziliondoka kwenye pwani ya Senegal lakini sio boti zilizo na watu 300."
Mnamo Julai 13, boti nyingine ilitia nanga kwenye ufuo wa Visiwa vya Canary ikiwa na wahamiaji 41 wakitokea Senegal.
Nilipojaribu kutafuta ukweli, nilimkuta mwanamke mmoja tu huko Kafontin ambaye alisema jamaa yake amepotea. Hakutaka jina lake litajwe na akaniambia amepoteza mawasiliano na mpwa wake mwenye umri wa miaka 17.
Alisema inaonekana alikuwa kwenye moja ya boti hizi tatu, "Ninaogopa. Hatuna habari juu yake. Siku zimepita na bado hatujui chochote kuhusu yeye."
"Kuna mkanganyiko wa kweli kuhusu hatima ya watu 300 waliopotea," mjumbe wa idara ya usalama ya eneo hilo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliniambia.
Afisa huyo aliongeza, "ukiachana na bibi huyu hakuna mtu yeyote hapa mjini ambaye amekwenda katika mamlaka au vyombo vya usalama kusema anatafuta ndugu au jamaa zao."
Lakini bila shaka hii haishangazi, kwa sababu watu wengi wanatoka mikoa mingine au hata kutoka nchi jirani, na hawana uhusiano na kijiji hiki.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, takriban watu 559 walipoteza maisha mwaka jana walipokuwa wakijaribu kufika Visiwa vya Canary kutoka Senegal. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu pekee, Visiwa vya Canary vilipokea zaidi ya wahamiaji 7,000.
Ndoto zilizovunjika
Kutokana na hali ngumu ya uchumi siku zote kuna kundi la vijana wanaotafuta nafasi ya maisha bora.
Doudou ameishi katika eneo la Casamance kusini mwa Senegal maisha yake yote. Baada ya kifo cha babake, anasema alihisi shinikizo la kuchukua jukumu la kutunza familia yake akiwa mtoto wa kwanza.
"Nilitamani hali bora ya maisha na pesa za kutosha ili niweze kumtunza mke wangu, binti yangu, mama yangu na familia nzima," alisema, akiongeza kuwa usafiri wa boti kwa mtu mmoja unagharimu faranga za CFA 400,000 (dola 682).
"Niliondoka bila kusema chochote kwa mtu yeyote, nilikuwa na mipango yangu, nilitaka kufika Ulaya kwa sababu hakuna kitu hapa, hakuna matumaini."
Aliendelea kusema, "nimevunjika moyo sana kwa sababu nilitaka kufika Uhispania. Nina marafiki ambao walifanikiwa kufika huko na walikuwa wakinisubiri."
Gnara Diabang Ba, ni naibu meya na kutoka upinzani.
"Inakera sana," anasema Gnara. "Inasikitisha sana kuona habari nyingi kwa sababu ya wahamiaji kuondoka kwenda Ulaya au kujaribu kuondoka kwenda Ulaya."
"Kama afisa wa mtaa aliyechaguliwa najisikia vibaya. Tukiwaomba vijana kubaki, basi tunapaswa kuwapa ajira na elimu bora. Tusipofanya hivyo, basi tumeshindwa vibaya."
Meya David Diatta, ambaye ni wa chama kimoja, ana maoni sawa na Gnara, ‘harakati za uhamiaji ni eneo la kimkakati la manispaa ya Cavontein," anasema na kuongeza, "asilimia tisini na moja ya jamii yetu inaundwa na visiwa, jeshi la wana maji lina uwezo mdogo sana wa kushughulikia kile kinachoendelea huko.
Kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 40, hata wahitimu wa vyuo vikuu.
"Tunateseka sana, hakuna ajira, na hakuna msaada kutoka kwa mamlaka," anasema Ibrahima, 28, ambaye ana shahada ya kwanza katika sosholojia.
Anaongeza, "rafiki zangu wengi walichukua boti za wavuvi hadi kufika Visiwa vya Canary na kufanikiwa. Tunawaona kwenye mitandao ya kijamii, na inaonekana kuna tofauti kubwa."
"Natamani niende siku moja lakini nahitaji pesa"