Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Gorée: Kisiwa kilichobeba siri ya ukatili wa Utumwa Afrika
Kisiwa cha Gorée, karibu na pwani ya Dakar, Senegal, kinaaminika kuwa kituo kikuu cha maelfu ya kwa maelfu ya watumwa waliokuwa wanasafirishwa kikatili kwenda Amerika katika karne ya 16 mpaka 19.
Kwenye kisiwa hiki kunapatikana nyumba ya makumbusho ya watumwa ambayo ilikuwa inahifadhi kati ya watumwa 150 mpka 200 kwa wakati mmoja kusubiri kusafirishwa na kuuzwa kwenye mataifa ya Amerika.
Ni jumba lenye vyumba kama seli vyenye kuhifadhi watumwa wanaume, wanawake na watoto, waliokuwa wanatunzwa tofauti tofauti.
Mwandishi wa habari na mwanariadha Ade Adepitan ametembelea jumba hilo la makumbusho ya Watumwa kisiwani humo ili kuelewa zaidi hali ambazo watu waliokuwa watumwa walikabiliana nazo kabla ya kuvuka Bahari ya Atlantiki.
Ade anakutana na mwelekezi wake anayejitambulisha kwa ajina la Colonel ambaye anamkaribisha na kwa pamoja wanaingia kwenye jumba hilo kupitia 'korido' nyembamba ambayo watumwa hao walikuwa wakipitishwa kuelekea mwenye bahari kupanda mitumbwi na kusafirishwa.
Kwa mujibu wa Colonel, mtumwa akipanga mstari na kupitishwa hawezi tena kurejea, hakuna kurejea tena, njia inayoitwa kwa kimombo "doorway of no return."
'kile unachokiona mbele yako ni mlango wa kutorejea kwanini umeitwa hivyo kwa sababu yoyote atakayepita njia hii kuelekea kule ni sawa na kusema kwa heri Afrika', alisema.
Kwa mujibu wa wataalamu wengi wanasema kuwa wafanyabiashara ya watumwa kutoka Ulaya walisafirisha watumwa wakiaafrika zaidi ya milioni kumi kupitia bahari ya Atlantiki.
Watumwa hawa wanadaiwa kutoka kwenye jamii mbalimbali barani Afrika, ikiwemo ya jamii ya Yoruba kutoka Nigeria, anakotokea Ade Adepitan ambao wakati wa utumwa walisifika kwa kuwa na nguvu.
'Moja ya kabila bora wakati wa utumwa lilikuwa ni Yoruba, wafanyabiashara ya watumwa waliwataja Yoruba kama watumwa bora au farasi wenye nguvu," anasema Colonel.
Wakati wa kupandishwa kwenye mitumbwi wakitokea kwenye 'korido' la jumba hilo Colonel anaeleza kwamba, kuna wakati watumwa walijaribu kutaka kukimbia kwa kuruka bahari, waliona bora kujitoa uhai kuliko kusafirishwa utumwa.
"Kulikuwa na papa wengi, wengi kila wakati hapa," anasema Colonel. Kwa nini papa walikuwa ni wengi? kwa sababu, mtumwa yeyote aliyekuwa mgonjwa au na uchungu wangemtupa baharini, ndio sababu kuliwa na papa wengi kila wakati."
Kwa sababu hiyo na zingine kwenye maeneo mengine ya kusafirishwa watumwa, inaelezwa zaidi ya waafrika milioni moja wanaaminika kuwa walifariki kabla ya hata kuwasili Amerika.
"Siwezi hata kusema kwa maneno au kuelewa vile hali ilikuwa kwa waafrika wale, waliowekwa hapa katika mazingira ya kutisha! Wengi wao kutoka kabila ambalo…ambalo ninatoka na mbaya zaidi nilichokisia hapa ni mwanzo tu"anasikitika mwandishi Ade Adepitan.
Ade Adepitan, anachunguza asili ya jumba hilo la utumwa na kutembelea mandhari tofauti za Afrika ili kufichua jinsi bara hilo linavyobadilika katika Karne ya 21.