Jinsi kanisa la Kiambaa linavyojikwamua kutoka makovu ya ghasia za 2007

Na Robert Kiptoo

BBC Swahili

Huku Wakenya wakijitayarisha kupiga kura Jumanne wiki ijayo ili kuwachagua viongozi wapya serikali imechukua hatua zaidi ili kudumisha usalama na amani wakati huo ili kuepuka kilichotokea mwaka wa 2007 ambapo ghasia zilizuka na kusababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine kulazimika kuhama .

Tayari washukiwa kadhaaa wamekamatwa na polisi kwa madai ya kusambaza vijikaratasi vya uchochezi katika kaunti ya Uasin Gishu hali ambayo inawapa waathiriwa wa ghasia za mwaka wa 2007 hali ya wasi wasi.

Hata hivyo hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwa katika maeneo mengi ya Bonde la Ufa, eneo ambalo liliathirika pakubwa na machafuko hayo.

Jukumu la kudumisha amani halijaachiwa tu asasi za serikali bali pia watu binafsi na mashirika ya kidini zinajihusisha makubwa na jitihada hizo .Kasisi wa kanisa la PAG Kiambaa mjini Eldoret Paul Karanja amekuwa akiongoza ibada za kuombea amani wakati wa kipindi hiki .

Miaka kumi na mitano iliyopita makumi ya waumini wa kanisa hili waliteketezwa ndani ya kanisa hili, baada ya ghasia za uchaguzi kuibuka.

Akina mama ,watoto,vijana na wazee ambao ambao walikimbilia kanisa hilo kupata hifadhi baada ya ghasia kuzuka waliuawa baada ya kanisa hilo kuchomwa .

Tangu wakati huo waumini wengi waliondoka na kwa wachache waliobaki, waliendelea kuabudu katika kanisa dogo lililojengwa kutumia mabati.

Paul Karanja ndiye kasisi mkuu wa kanisa hili kwa sasa na anasema walilazimika kubadili jina la kanisa kama njia moja ya kusahau maovu yaliyotokea ndani ya kanisa hilo

Bi Hellen Wangui ni miongoni mwa walionusurika kifo wakati wa ghasia hizo za uchaguzi na anasema licha ya maisha kuendelea makovu ya tukio hilo bado yanawapa matatizo.

Mji wa Eldoret ni miongoni mwa sehemu zilizoathirika pakubwa na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007. Kinyume na ilivyokuwa, wakati huu hali ni tofuati.

Hadi sasa hakuna tukio lolote ambalo limetokea na Moses Ndichu ambaye ni mkaazi wa eneo hili la Kiambaa anasema amani ipo.

Huku shughuli za kampeini zikiendelea makundi mbali mbali yameimarisha juhudi za kuwahimiza wakaazi wa maeneo yote ya mkoa wa bonde la ufa kudumisha amani kabla ya baada ya uchaguzi mkuu. Naomi Njeri ni kiongozi wa kina mama katika kanisa la Kiamba.

Ikiwa imesalia siku sita pekee kabla ya uchaguzi mkuu, watu wengi katika eneo la Bonde la Ufa wana maratajio makubwa kuwa uchaguzi huu utakuwa wa amani. Kasisi Paul Karanja anasema viongozi na wananchi wote wana jukumu la kuhakikisa kuwepo kwa amani.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i amewahakikishia Wakenya kuwa patakuwa na usalama wa kutosha kote nchini wakati n ahata baada ya uchaguzi siku ya Jumanne wiki ijayo.

Kwa waumini wa kanisa la Kiambaa na Wakenya wengi,Imani yao ni kuwepo kwa utulivu na uendeshaji kwa utulivu mchakato mzima wa kura ili wanedelee na Maisha yao kama kawaida.