Kwa nini hamu ya vyakula vitamu huongezeka wakati wa Ramadhani?

rfd

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 3

Watu wengi wanaofunga huwa na tabia ya kula vyakula vitamu kupita kiasi, wakati wa mwezi wa Ramadhani, jambo ambalo mtaalamu wa lishe Reem Al-Abdallata anasema:

"Tatizo liko katika jinsi tunavyokula chakula. Wakati mfungaji anapokula kiasi kikubwa cha tende, ambayo ni sukari - mwanzoni mwa kifungua kinywa...

“Huchochea na kuongeza kiwango cha insulini katika damu, ambayo hupelekea mtu kutaka kula na hasa vyakula vitamu.”

Anaongeza: “Kosa wanalofanya baadhi ya ni kuanza kifungua kinywa kwa kula kati ya tende (3-5) na kisha kunywa juisi, hasa zile juisi za mwezi wa Ramadhani ambazo zina sukari nyingi.”

Mtaalamu anataja sababu za watu kupenda kula vyakula vya sukari kupita kiasi katika mwezi wa Ramadhani, hutokana na kuongezeka kwa hisia za kuhitaji sukari, baada ya kiwango cha sukari kwenye mwili kupungua wakati wa mfungo.

Reem Al-Abdallat anaeleza: “Inapendeza zaidi kwa mfungaji kufuturu kwa tende moja na kisha kula kitu chenye protini, kama vile kuku, samaki, nyama, au hata glasi ya maziwa.

Wataalamu wanapendekeza kunywa maji wakati wa kifungua kinywa, ambayo huchangia kupunguza hamu ya kutaka kula vitu vitamu.

Wataalamu wa masuala ya lishe pia wanasema unywaji wa maji ya kutosha husaidia kuupa mwili unyevu na kuulinda dhidi ya upungufu wa maji mwilini.

Mtaalamu wa masuala ya lishe Reem Al-Abdallat anasisitiza umuhimu wa utumiaji wa juisi na vinywaji ambavyo havina utamu wa kutiwa na vya sukari ya asili, kwa lengo la kuhifadhi afya ya binadamu na kuepuka kuongezeka uzito.

Vyakula na Hisia Zetu

sx

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwanasaikolojia Rasha Bouana amesema wakati wa mahojiano yake na BBC: "Kadiri kiwango cha sukari kwenye damu kinavyopungua, mtu aliyefunga hujikuta na hamu ya kutaka kula vitu vitamu, kwa sababu vinaongeza nguvu katika mwili.”

Anaongeza: "Lakini hiyo sio sababu pekee. Tamaa hii inaweza pia kuhusishwa na sababu za kisaikolojia, kwani kula vyakula vitamu kunahusishwa na hisia zetu za furaha. Kula vitu vitamu hutoa homoni ya serotonin, ambayo inawajibika kwa hisia za kuridhika na furaha."

"Kilicho muhimu kwetu ni kuelewa uhusiano kati ya vyakula tunavyokula na hisia zetu, kwani hii inaweza kutusaidia kula lishe bora na yenye manufaa."

Mwanasaikolojia huyo anashauri kupata ushauri wa daktari ikiwa jitihada zako za kujizuia hazifaulu, kwa kuwa kutamani vitu vitamu mara kwa mara ni kiashiria cha tatizo la kiafya.

Kudhibiti hamu ya vyakula vitamu

FV

Chanzo cha picha, EPA

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wataalamu wa lishe wanasema kudhibiti hamu ya vyakula vitamu wakati wa mwezi wa Ramadhani huanza na kifungua kinywa hadi mlo wa daku.

Amua wakati maalumu wa kula vyakula vitamu wakati wa Ramadhani, kwani watu waliofunga hawapaswi kula vitu vitamu mwanzoni mwa mlo mkuu wa futari.

Kufanya hivyo itasababisha kula kwa kiasi kikubwa kwa sababu ya njaa ya kutaka kula na huenda ikaleta mkorogeko wa tumbo.

Kwa hiyo, wakati mzuri wa kula vitu vitamu ni saa mbili au tatu baada ya kifungua kinywa, na unapaswa kula kwa kiasi kidogo na si kwa kila siku.

Usile vitu vitamu pekee, ni afadhali kula na kitu chenye ladha chungu, kama vile kikombe cha kahawa, ili kupunguza hisia za kuhitaji kula vitu vitamu zaidi.

Baada ya kula kitu kitamu, kunywa maji, maziwa, mtindi, au karanga chache ili kudhibiti kiwango cha insulini katika mwili wako.

Pika vyakula vitamu mwenyewe nyumbani ili kudhibiti idadi na ubora, na kupunguza idadi ya kalori kw akadiri uwezavyo.

Hakikisha vitu vitamu hazipatikani kila wakati nyumbani kwako, kwani uwepo wao huongeza hamu ya kula.

.

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi