Ugonjwa wa kisukari unaweza kutibika na kuzuiwa kirahisi - Daktari anaeleza

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Dr. Jason Fung
- Nafasi, BBC Science Focus
Fikiria mwili wako kama bakuli kubwa la sukari. Wakati wa kuzaliwa, bakuli ni tupu. Baada ya miongo kadhaa, unakula sukari na wanga na bakuli linajaa polepole.
Na unapokula tena, sukari inamwagika juu ya kingo za bakuli kwa sababu bakuli tayari limejaa.
Hali hiyo hiyo ipo katika mwili wako. Unapokula sukari, mwili wako hutoa homoni ya insulini kusaidia kuipeleka sukari kwenye ya seli zako za mwili, ambapo hutumiwa kukupa nguvu.
Ikiwa hutachoma sukari hiyo vya kutosha, baada ya miongo kadhaa seli zako hujaa na haziwezi kushughulikia sukari hiyo tena.
Na unapokula sukari tena, insulini haiwezi kuzipeleka tena kwenye seli zako zinazofurika, kwa hivyo sukari inamwagika ndani ya damu.
Sukari husafiri katika damu yako katika mfumo unaoitwa glukozi na kuwa nayo nyingi – inakuwa ndio dalili ya kisukari cha aina ya 2.
Sukari nyingi inapokuwa kwenye damu, insulini haifanyi kazi yake ya kawaida ya kuhamisha sukari kwenye seli. Ndipo tunasema mwili umekuwa sugu kwa insulini, lakini sio kosa la insulini. Shida kuu ni kwamba seli zimejaa sukari.
Ili kukabiliana na glukozi ya ziada katika damu, mwili hutoa insulini zaidi ili kuondokana na hali hiyo. Hilo hupelekea glukozi zaidi kwenda kwenye seli zinazofurika ili kuweka kiwango cha damu kuwa cha kawaida.
Lakini hilo ni suluhisho la muda tu kwa sababu tatizo la sukari nyingi halijashughulikiwa; imehamisha tu sukari ya ziada kutoka kwenye damu hadi kwenye seli. Wakati fulani, hata mwili hauwezi kulazimisha sukari zaidi kwenda kwenye seli.
Nini hutokea ikiwa sukari ya ziada haitaondoka?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwanza, mwili unaendelea kuongeza kiwango cha insulini inachozalisha ili kujaribu kulazimisha glukozi zaidi kwenda kwenye seli. Lakini hii hupelekea tu upinzani zaidi wa insulin.
Wakati viwango vya insulini haviwezi tena kuendana na upinzani unaoongezeka, viwango vya sukari ya damu huongezeka. Hapo ndipo daktari wako ana uwezekano wa kugundua ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2.
Daktari wako anaweza kukuandikia dawa kama vile sindano za insulini, au labda dawa inayoitwa metformin, ili kupunguza sukari katika damu, lakini dawa hizi haziondoi glukozi iliyozidi mwilini. Badala yake, huitoa tu glukozi kwenye damu na kuirudisha ndani ya mwili.
Kisha husafirishwa kwenye viungo vingine vya mwili, kama vile figo, mishipa ya fahamu, macho, na moyo, ambapo hatimaye inaweza kusababisha matatizo mengine. Tatizo la msingi, bila shaka, halijatibika.
Dawa zinaweza kuchukua nafasi. Mara ya kwanza, unahitaji dawa moja tu, lakini hatimaye inakuwa mbili na kisha tatu, na dozi inakuwa kubwa.
Ikiwa unatumia dawa zaidi na zaidi ili kuweka glukozi katika kiwango kizuri, ugonjwa wako wa kisukari unazidi kuwa mbaya.
Tumia sukari kidogo

Chanzo cha picha, Getty Images
Mara tu unapoelewa kuwa kisukari cha aina ya 2 ni sukari nyingi sana mwilini, suluhisho linakuwa lipo wazi. Achana na sukari. Achana nayo. Kuna njia mbili tu za kufanikisha hilo. Tumia sukari kidogo na Choma sukari iliyobaki mwilini.
Hayo tu ndiyo unayohitajika kufanya. Huhitaji kutumia dawa, hakuna upasuaji na hakuna gharama.
Usitumie vyakula vilivyoongezwa sukari. Usitumie vyakula vya wanga na wanga uliosafishwa sana kama vile unga kwani humeng'enywa haraka kuwa glukozi.
Mbinu bora ni kupunguza au kuacha kula mikate na pasta zilizotengenezwa kutokana na unga mweupe, pamoja na mchele mweupe na viazi.
Unapaswa kula protini kiasi sio sana. Inapomeng'enywa, protini ya chakula, kama vile nyama, hugawanyika kuwa asidi ya amino. Protini inahitajika kwa afya njema, lakini asidi ya amino ikizidi haiwezi kuhifadhiwa katika mwili na hivyo hubadilishwa kuwa glukozi.
Kwa hiyo, kula protini nyingi huongeza sukari katika mwili. Kwa hivyo unapaswa kuepuka vyakula vya protini vilivyochakatwa sana, vilivyokolezwa kama vile unga wa protini.
Mafuta asilia, kama vile yale yanayopatikana kwenye parachichi, karanga na mafuta ya mizeituni - yana athari ndogo kwenye sukari ya damu au insulini na yanajuulikana kuwa ni mazuri kiafya kwa ugonjwa wa moyo na kisukari. Mayai na siagi pia ni vyanzo bora vya mafuta asilia.
Kula mafuta asilia hakuongezi ugonjwa wa kisukari cha aina ya 2 au ugonjwa wa moyo. Kwa kweli, yana manufaa kwa sababu husaidia kujisikia vizuri mwilini bila kuongeza sukari.
Ili kuweka sukari kidogo ndani ya mwili wako, tumia vyakula vya asili, ambavyo havijachakatwa. Kula vyakula visivyo na wanga uliosafishwa, kula protini kidogo, na mafuta mengi ya asili.
Choma sukari iliyobaki

Chanzo cha picha, Getty Images
Mazoezi - yanaweza kuwa na manufaa kwa mgonjwa wa kisukari cha aina ya 2, lakini mazoezi hayana nguvu sana katika kupunguza ugonjwa kuliko kuzingatia vyakula.
Kufunga ni njia rahisi na ya uhakika ya kuulazimisha mwili wako kuchoma sukari. Ikiwa huli, unafunga. Unapokula, mwili wako huhifadhi nishati ya chakula; unapofunga, mwili wako huchoma nishati ya chakula.
Na glukozi ndio chanzo cha nishati ya chakula. Kwa hivyo, ikiwa unaongeza vipindi vyako vya kufunga, unaweza kuchoma sukari iliyohifadhiwa.
Kufunga ni tiba ya zamani zaidi inayojulikana na imekuwa ikitekelezwa katika historia ya mwanadamu bila shida. Lakini ikiwa unatumia dawa, unapaswa kutafuta ushauri wa daktari kabla kuanza kufunga.
Je, ikiwa hutokula, sukari yako ya damu itashuka? Ndio. Usipokula, utapunguza uzito? Ndio. Kwa hiyo, tatizo ni nini? Hakuna tatizo.
Ili kuchoma sukari, njia bora ni kufunga kwa masaa 24, mara mbili hadi tatu kwa wiki. Njia nyingine maarufu ni kufunga kwa saa 16, mara tano hadi sita kwa wiki.
Uwezo wa kutibu kisukari cha aina ya 2 uko ndani ya uwezo wako. Kinachohitajika ni kuwa na nia na ujasiri wa kupingana na mazoea.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi












