Siku ya Kiswahili: Lugha ya wakati wa amani na vita

.

Chanzo cha picha, Ikulu ya Tanzania

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili

Bila shaka si kosa la lugha, ikiwa lugha fulani itatumika na majambazi, waasi au watu wowote waovu. Lugha ni chombo tu cha mawasiliano, waweza itumia kumbembeleza mke wako asikukimbie, na kinyume chake waweza itumia wakati unawacharanga mapanga wasio na hatia.

Maadhimisho ya lugha ya Kiswahili yalitangazwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Mosi Julai, 2024, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja lilipitisha azimio la kuitambua tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kimataifa Kiswahili.

Tanzania kama nchi zingine zingine katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 07 Julai, 2024, Rais wa nchi hiyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezungumzia Kiswahili kama lugha iliyotumika wakati wa ukombozi wa Uhuru wa Tanganyika, Zanzibar, Kenya na nchi zingine za Afrika.

‘’...Kiswahili ni lugha ya Ukombozi, ni lugha ya Umoja ni lugha ya Amani na ni Lugha ya Biashara,’’ Rais Samia alisema katika hotuba yake ya maadhimisho ya siku hii.

OL

Chanzo cha picha, UN

Historia ya Kiswahili nchini Uganda, imegubikwa na matukio ya kinyama na ya kutisha ya umwagaji damu hasa ya baada ya Uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1962.

Ivan Alvaro, kutoka Kampala, Uganda, anasema, “Waganda hawajawahi kupata mabadiliko ya uongozi kwa njia ya amani, madaraka huchukuliwa kwa mtutu wa bunduki, tangu wakati wa Milton Obote, Idi Amin, Godfrey Binaisa, Yusuf Lule, kisha Obote tena, na huyu wa sasa Yoweri Museveni, wote wamechukua madaraka kwa nguvu.

Anaendelea kusema, “Askari walikuwa wanavamia vijiji huku wakizungumza Kiswahili, wakiwapiga watu, wakila vyakula vyao, wakibaka na kuuwa. Katika maeneo mengi ya Uganda, Kiswahili kimeonekana kama lugha ya wauaji na wabakaji. Kwa hakika, ni historia yenye mtiririko wa matukio ya watu waovu. Ndio maana Waganda wengi wameshindwa kukikumbatia Kiswahili.”

Naam, hiyo ni historia ya kweli, wala haiwezi kufutika, na mapenzi yetu kwa lugha ya Kiswahili hayawezi kuponya moja kwa moja majera ya uovu uliofanyika, lakini simulizi hizo sio historia pekee ya lugha hii.

Mwanasiasa wa upinzani kutoka Afrika Kusini wa chama cha The Economic Freedom Fighters, Julius Sello Malema, alipata kusema kuhusu, njia bora ya kuwaunganisha Waafrika na kuachana na lugha zenye mizizi ya ukoloni:

“Jambo la maana kufanya, ikiwa tunataka kuliunganisha bara la Afrika, ni kukifundisha Kiswahili na kuzihimiza nchi nyingine kufundisha Kiswahili. Jambo la msingi ni mawasiliano.”

Wakati nikiwa Uganda kwa miaka miwili na nusu ya masomo kati ya 2021/23, nilishuhudia muamko mpya wa kizazi kinachopenda kujifunza Kiswahili.

Hiyo ni kusema, ile mitazamo ya hofu iliyopo, imeanza kuondoka polepole, pengine uhamasishaji kama huo wa Malema unasaidia kubadilisha mitazamo hiyo, ingawa bado kuna kazi kubwa inahitajika kufanywa.

Pia unaweza kusoma

Lugha ya Amani

x
Maelezo ya picha, Kuna zaidi ya lugha 100 zinazongumzwa nchini Tanzania lakini Kiswahili kinazungumzwa na asilimia 90 ya idadi ya watu
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka huu Siku ya Kiswahili Duniani, itaadhimishwa Julai 5, 2024, katika makao makuu ya Unesco huko Paris, Ufaransa chini ya kauli mbiu, “Kiswahili: Elimu na Utamaduni wa Amani.”

Utamaduni wa amani, ndipo hasa penye msingi wa makala yenyewe. Katika nchi kama Tanzania, ambapo Kiswahili kinaunganisha makabila zaidi ya mia, kuna hadithi tofauti na ile iliopo Uganda.

Kwa Tanzania, Kiswahili ni mfano wa lugha ambayo ni chanzo cha mshikamano kwenye taifa lenye watu wenye kutofauatiana mambo mengi ya kimila na kitamaduni.

Wazo la Kiswahili kuwa lugha ya Kiafrika lilianzishwa katika miaka ya 1960 na rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, ambaye alitumia lugha hiyo kuunganisha taifa lake baada ya uhuru.

"Nyerere alikuwa na mchango mkubwa sana katika ukuaji wa matumizi ya Kiswahili, alielewa kuwa watu wake walihitaji lugha hiyo kwa ajili ya biashara na kuelewana. Aliikubali kwa dhana ya Uafrika na aliiona kama aina ya ukombozi," anasema Dr. Ida Hadjivayanis, mhadhiri na mtaalamu wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha London.

Fauka ya hayo, Kiswahili kimetambulika katika taasisi kubwa kama Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Leo hii Kiswahili kinatumika kwenye ulinzi wa amani katika nchi kama DR Congo, na wanajeshi kutoka mataifa ya Afrika, yakiwemo ya Afrika Mashariki. Na walinda amani walioko Somalia, Kiswahili pia hutumika katika shughuli zao.

Lugha iliyokua

SD

"Ilianza kama lugha ndogo katika pwani ya Afrika Mashariki, baadaye ilikutana na wafanyabiashara kutoka ulimwengu wa Kiarabu na Kimagharibi na ikatanuka," anasema Dr. Hadjivayanis.

Moja ya sababu za ushindi wake barani Afrika ni kwa sababu ni lugha ya Kibantu, ilikubaliwa haraka na Wabantu, ambao waliweza kuisoma na kuielewa kwa urahisi kwa sababu tayari walikuwa wakizungumza lugha nyingine za familia moja.

Kwa mujibu wa Unesco, Kiswahili kina wazungumzaji takribani milioni 230 duniani kote. Ndio lugha ya Afrika iliyoenea zaidi katika eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, pia iko katika orodha ya lugha kumi zinazozungumzwa katika eneo kubwa kijiografia.

Ni lugha rasmi katika nchi kadhaa, ikiwemo DR Congo, Kenya, Rwanda, Tanzania na Uganda. Na inazidi kuenea kwa sababu baadhi ya serikali za Afrika, zimewekeza katika kuwafundisha watoto wa shule lugha hiyo katika nchi kama Afrika Kusini na Namibia.

Licha ya ukuaji wa Kiswahili, zipo changamoto zake ambazo mdau wa lugha hiyo na mwandishi wa riwaya za Kiswahili, kutoka Tanzania, Maundu Mwingizi anaziona:

“Kwenye kutafsiri lugha na kuyaweka maandishi fulani kwenye Kiswhaili, wapo wanaoharibu. Lugha inakuwa lakini inaharibika. Hasa kwenye kutafsiri habari, mtu anatafsiri kutoka Kingereza kuja Kiswahili lakini inakuwa ni kama google ndio imetafsiri.”

Maundu pia, anagusia changamoto inayozikumba taasisi za kusimamia Kiswahili, akieleza kuwa, kuna wakati hulazimisha kutengeneza misamiati mipya bila kuzingatia wazungumzaji wenyewe hutumiaje meneno yao.

“Ni utamaduni wa kupika maneno mapya yasiyojuulikana hata yametoka wapi,” anasema Mwingizi.

Kauli hiyo haitofautiana na maneno ya mshairi wa Kiswahili na mtangazaji wa muda mrefu, Mohammed Khelef, aliposema, ‘ni maneno yanayopikwa kwenye maabara ya lugha.’

Kwa upande mwingine, Mwingizi anahimiza mamlaka za Kiswahili kusimamia kutotumiwa maneno ambayo si sahihi, hasa kwenye vyombo vya habari. Na pia kuwasimamia waandishi wa Kiswahili katika matumizi sahihi ya maneno wakati wanapoandika.