Kiswahili au Kiingereza?Lugha ya kufundishia inavyoipasua kichwa Tanzania

Na Ezekiel Kamwaga

Mchambuzi,Tanzania

th

Chanzo cha picha, AFP

Miezi michache iliyopita, mmoja wa wahadhiri waandamizi wa Chuo Kikuu cha SOAS nchini Uingereza, Profesa Stephen Chan, alipata kunieleza kwamba miaka 50 iliyopita aliwahi kuwa na ndoto za kuja kusoma masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Raia huyo wa New Zealand aliamini kuna maeneo ya kitaaluma ambako chuo hicho cha Tanzania kilikuwa kinatoa elimu ya kiwango cha dunia.

Ni katika miaka hiyo ambapo Umoja wa Mataifa (UN) ulikuwa ukiitaja na kuipongeza Tanzania kama mojawapo ya nchi za dunia ya tatu zilizofanikiwa kupambana na ujinga kiasi kwamba zaidi ya asilimia 80 ya watu wake walikuwa wanajua kusoma na kuandika.

Miaka 50 baadaye, sifa hiyo ya Tanzania katika kutoa elimu ya kiwango cha dunia katika ngazi ya chuo kikuu haipo tena – vyuo vyake vyote vikiwa havimo hata kwenye orodha ya vyuo vikuu bora 50 barani Afrika.

Katika ngazi ya elimu ya awali, shirika lisilo la kiserikali la HakiElimu, liliwahi kutoa ripoti iliyoonyesha walau nusu ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wanapata shida kwenye kujua kusoma na kuandika.

Takwimu hizo zimezua mjadala mkubwa nchini kuhusu mustakabali wa elimu ya taifa hilo.

Mjadala huo kwa sasa unabebwa zaidi na suala la endapo msingi wa matatizo ya sasa unatokana na utata wa lugha ya kufundishia.

Lugha ya Kufundishia (LYK)

th
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nchini Tanzania, katika shule zote za umma, mfumo ni wa kufundisha masomo yote kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika ngazi ya Shule ya Msingi – huku Kiingereza kikifundishwa kama somo, na kuanzia ngazi ya sekondari na kuendelea, LYK huwa ni Kiingereza.

Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya elimu niliozungumza nao, matarajio ya mfumo huo yalikuwa kwamba miaka saba ya kufundishwa somo la Kiingereza katika ngazi ya msingi, ni maandalizi ya kumfanya mwanafunzi aweze kufundishwa na kuelewa masomo mengine katika lugha ya Kiingereza atakapofika sekondari na vyuoni.

Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kwamba matarajio hayo ya kuelewa Kiingereza katika miaka ya awali hayafikiwi.

Katika kipindi cha walau miaka mitano iliyopita, takwimu za Baraza la Mitihani ya Taifa la Tanzania (NECTA) zinaonyesha kwamba zaidi ya wanafunzi wanaomaliza mitihani ya shule ya msingi huwa hawafaulu somo la Kiingereza.

Hata katika matokeo ya mtihani wa ngazi ya Diploma ya Ualimu nchini Tanzania, mara nyingi ufaulu huwa ni wa kuanzia kiwango cha daraja C kushuka chini- kwa mujibu wa takwimu tofauti zilizotolewa na wasomi na watafiti katika sekta ya elimu nchini Tanzania.

Kama zaidi ya wanafunzi wanaoingia sekondari huwa hawajui Kiingereza, maana yake ni kwamba wanakwenda kufundishwa masomo ambayo watapata taabu kuyaelewa. Na huu ndiyo msingi hoja ya wanaotaka LYK iwe Kiswahili kwa sababu ndiyo ambayo wanafunzi wanaielewa.

Kwao, kufundisha mtu kupitia lugha asiyoelewa ni sawana kutwanga maji kwenye kinu.

Wanaotaka Kiingereza kipewe nafasi zaidi wanafanya hivyo kwa hoja kwamba ndiyo lugha yenye maarifa na taarifa zaidi kwa sasa na kwamba kuifahamu kunampa mwanafunzi wigo mpana zaidi wa kufanikiwa katika maisha yake ya baadaye.

Changamoto kubwa zaidi

th

Hata hivyo, kulinganisha na nchi zilizoendelea kielimu duniani, Tanzania ina changamoto kubwa zaidi za kushughulika nazo kuliko lugha ya kufundishia na kujifunzia.

Kwa mfano, utafiti maarufu wa Smith (1999) ulihitimisha; “elimu bora itatolewa mahali ambapo kuna walimu bora”.

Katika enzi za ukoloni na miaka ya awali ya Uhuru – ualimu ulikuwa ni taaluma inayoheshimika sana nchini Tanzania.

Baba wa Taifa la Tanzania, Julius Nyerere, alikuwa mwalimu na alianza harakati za kudai Uhuru akitokea kufundisha. Walimu walikuwa chanzo cha maarifa kwenye jamii na waliojulikana kwa uwezo wao mkubwa kitaaluma.

Hili linaakisiwa na mafanikio ya taifa kama Singapore kielimu. Katika taifa hilo ambalo linatajwa miongoni mwa yenye elimu bora duniani, sifa ya kwanza ya mtu kuwa mwalimu ni kuwa katika asilimia tano za kwanza za watu waliofaulu zaidi kwenye mitihani. Hivyo walimu ni watu ambao wangetaka wangekuwa madaktari, wahandisi, wanasheria na kadhalika lakini wakaamua kuwa walimu.

Wakiingia kazini wanalipwa mishahara mizuri ambayo ni juu ya wastani wa mishahara ya kawaida kwenye nchi zilizoendelea. Matokeo yake nchi hiyo sasa ina wananchi wenye elimu na maarifa makubwa.

Hali hii ni tofauti na Tanzania ambako ualimu hauonekani kama taaluma kwa watu waliofaulu vizuri zaidi na maslahi yao ni duni kiasi kwamba si ndoto ya wengi kuwa walimu.

Walimu hao wanafundisha katika madarasa yenye wanafunzi wengi – kukiwa na ripoti ya baadhi ya shule ambako wanafunzi takribani 100 wanategemea walimu wawili au watatu ingawa takwimu zinaonyesha mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 70. Kidunia, wastani ni mwalimu mmoja kwa walau wanafunzi 30.

Kwa mujibu wa takwimu rasmi za Ofisi ya Rais (TAMISEMI), mwaka huu idadi ya wanafunzi katika shule za sekondari za umma nchini Tanzania inakadiriwa kufikia wanafunzi milioni tatu lakini idadi ya walimu wa ngazi hiyo haijafika hata elfu 90.

th

Katika miaka ya karibuni, kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, mkazo zaidi unawekwa katika ujenzi wa madarasa na madawati lakini ukosefu wa walimu wenye maarifa ya kutosha, motisha na idadi inayoendana na wanafunzi waliopo, ni changamoto kubwa zaidi kwenye elimu ya Tanzania.

Tatizo lingine kubwa ni kuhusu aina ya elimu inayotolewa katika shule za Tanzania.

Nchini Singapore, mwongozo wa elimu yao unataka kuzalisha wanafunzi wenye uelewa mpana, maadili na uwezo wa kutatua changamoto za sasa na baadaye. Ndiyo sababu, kuanzia ngazi ya awali, watoto huchujwa na kupangwa kutokana na uwezo wao kitaaluma lakini pia kulingana na vipaji tofauti walivyonavyo.

Kwa kiasi kikubwa, mfumo wa elimu wa Tanzania unaangalia zaidi kupitia ufaulu katika mitihani ya mwisho ya kumaliza ngazi ya elimu husika.

Wakati enzi za ukoloni na miaka ya awali ya Uhuru mwanafunzi alikuwa anapata elimu na mambo mengine ya shule – lakini alikuwa pia anafundishwa stadi za kazi.

Ndiyo sababu Nyerere mwenyewe alijenga nyumba yake ya kwanza kijijini kwao Butiama kwa mkono wake kwa sababu walifundishwa ujenzi shuleni.

Mtu mwenye elimu alikuwa si anajua tu fizikia, kemia na bailojia, lakini alikuwa pia fundi mwashi, mkulima, mfugaji na stadi nyingine za maisha.

Nchini Tanzania, mtu anaweza kusoma kuanzia chekechea hadi Chuo Kikuu na akamaliza akiwa hana ujuzi wa stadi za maisha kama ilivyo katika nchi zilizoendelea.

th

Umasikini na utamaduni wa Tanzania unaleta changamoto kubwa mbili katika maendeleo ya elimu.

Mosi, kulinganisha na nchi kama China, Korea, Japan na India ambazo zina utamaduni wa kuandika wenye maelfu ya miaka, Tanzania na nchi nyingi za Afrika zilikuwa na utamaduni wa kurithishana maarifa kwa njia ya mdomo na hivyo hakuna maarifa mengi yaliyoandikwa tayari vitabuni kulinganisha na wenzetu kwingineko.

Kufidia pengo hilo, Tanzania inahitaji kuchapisha vitabu vingi zaidi na namna nyingine za kupasisha maarifa ili wanafunzi wapate elimu na maarifa yanayotakiwa sasa. Hili linahitaji uwezo mkubwa wa kiuchumi.

Kwa mujibu wa utafiti uliowahi kufanywa na taasisi kama UWEZO na HakiElimu, kwa wastani, kitabu kimoja hutumiwa na wanafunzi watatu nchini humo.

Kama hali ya uchumi ya Tanzania itaimarika, kama ilivyo kwa Korea Kusini, China, Japan, Singapore na Ushelisheli, inaweza kuwa na uwezo wa kuajiri walimu zaidi, kutoa motisha zaidi kwa watu kujiunga na taaluma hiyo, kutoa mafunzo yanayotakiwa kujibu changamoto za sasa na baadaye na pia kununua vitabu vingi zaidi.

Walimu wazuri zaidi, wengi zaidi na wenye motisha zaidi watafanya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi wawe na uwezo mzuri zaidi wa kujua lugha ya Kiingereza – na nyingine watakazofundishwa, na pengine hakutakuwa na mjadala kuhusu lugha ipi inafaa kufundishia.