Waandishi bila mipaka: Israel bado inaongoza kusababisha vifo vya waandishi wa habari

Chanzo cha picha, RSF
Shirika la uangalizi wa vyombo vya habari la Reporters Without Borders (RSF)linasema mwaka 2025 umekuwa mmoja wa miaka hatari zaidi kwa waandishi wa habari, likibainisha kuwa jeshi la Israel kwa kuwaua waandishi 29 katika Ukanda wa Gaza linawajibika kwa zaidi ya nusu ya vifo vya waandishi duniani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Katika ripoti yake ya kila mwaka, RSF pia imetaja nchi zinazowafunga waandishi wengi zaidi duniani, China na Urusi zikiwa juu ya orodha hiyo, zikifuatiwa na Azerbaijan, Iran, Misri, Israel na Saudi Arabia.
Ripoti hiyo, iliyotolewa Disemba 12, 2025, inachunguza matukio kati ya Desemba 1, 2024 na Desemba 1, 2025.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi ya waandishi wa habari waliouawa mwaka wa 2025 imefikia 67, mmoja zaidi ya mwaka uliotangulia. Nusu ya waandishi hao waliuawa katika eneo la Mashariki ya Kati.
RSF imezitaja Israel, magenge ya uhalifu, na jeshi la Urusi kuwa sababu kuu za vifo hivyo vya wanahabari.
- Asilimia 43 ya waandishi waliuawa na jeshi la Israel katika maeneo ya Palestina;
- Asilimia 24 waliuawa na magenge ya kihalifu na mitandao ya biashara ya dawa za kulevya, huku asilimia 13 ya mauaji haya yakitokea Mexico;
- Asilimia 4 ya vifo inadaiwa kusababishwa na jeshi la Urusi.
RSF inaielezea Israel kama "adui mkuu wa waandishi wa habari", ikisema kuwa tangu Oktoba 2023, takriban waandishi 220 wameuawa na jeshi la nchi hiyo, angalau 65 kati yao wakiwa wameuawa wakitekeleza majukumu yao.
Huu ni mwaka wa tatu mfululizo Israel inatajwa katika ripoti ya RSF kama chanzo kikuu cha vifo vya waandishi wa habari.
Mexico inatajwa kuwa eneo hatari zaidi kwa waandishi baada ya Palestina, huku ongezeko la mauaji ya waandishi mwaka 2025 likihusishwa na ongezeko la uhalifu wa magenge.
Waandishi tisa wameuawa barani Afrika mwaka huu.
RSF inasema kwamba licha ya mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Claudia Sheinbaum na ahadi zake za mageuzi, 2025 umekuwa mwaka mbaya zaidi kwa wanahabari nchini Mexico katika kipindi cha miaka mitatu.
Kati ya waandishi waliouawa mwaka huu, wawili waliuawa wakiwa katika majukumu nje ya nchi zao mpiga picha wa Ufaransa nchini Ukraine na mwandishi kutoka El Salvador nchini Honduras.
Waandishi wengine wote waliuawa katika nchi zao walipokuwa kazini.
Iran yawa nafasi ya saba kwa kuwaweka waandishi gerezani

Chanzo cha picha, Reuters
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kwa mujibu wa RSF, waandishi 503 wanashikiliwa gerezani katika nchi 47.
China inaongoza kwa kuwafunga wanahabari 121, ikifuatiwa na Urusi yenye wanahabari 48 gerezani.
Iran inashika nafasi ya saba ikiwa na waandishi 21 gerezani, nyuma ya Azerbaijan yenye 25.
Misri, Israel na Saudi Arabia pia zinatajwa katika nafasi ya saba hadi ya kumi mfululizo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa zaidi ya nusu ya waandishi waliotafuta msaada wa dharura kutoka RSF mwaka 2025 walilazimika kukimbia mataifa yao na kuishi uhamishoni.
Waandishi wa Iran ni miongoni mwa makundi makubwa zaidi yaliyotuma maombi ya msaada huo kutoka nchi 44 tofauti.
Nchi iliyotoa maombi mengi zaidi ya kutaka msaada ni Afghanistan, yenye maombi mapya 134, ikifuatiwa na Urusi yenye maombi 48. Iran inashika nafasi ya nne katika orodha hiyo.
RSF pia imeripoti tukio moja la mwandishi kupotea nchini Iran mwaka 2025.
Mkurugenzi Mkuu wa RSF, Thibaut Bruton, amesema: "Waandishi hawafi tu; wanauawa. Idadi yao inaendelea kuongezeka kutokana na vitendo vya makundi yenye silaha, majeshi rasmi, vikosi visivyo rasmi na mitandao ya uhalifu."
Amesema kwamba mwaka mmoja tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria, bado waandishi wengi waliokamatwa au kutekwa wakati wa utawala wake hawajulikani walipo, na kufanya Syria kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya waandishi waliopotea, zaidi ya robo ya waliopotea duniani.
RSF imeongeza kuwa Urusi chini ya Vladimir Putin inawashikilia waandishi wa kigeni wengi zaidi kuliko taifa lolote, ikiwa na 26, ikifuatiwa na Israel yenye wanahabari wa kigeni 20.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa waandishi 20 wa Palestina wako gerezani Israel, 16 kati yao wakiwa wamekamatwa Gaza na Ukingoni katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Je, wanahabari wa Afrika wako katika hali gani?
Huku zikiwa zimesalia zaidi ya wiki tatu kabla ya mwisho wa mwaka, idadi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa vyombo vya habari waliouawa barani Afrika imeongezeka.
Kwa mfano nchini Sudan, waandishi wa habari tisa waliuawa, na kupelekea jumla ya waliouawa kufikia 15 katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili ambapo waandishi wa habari wametekwa nyara, kubakwa na kulazimishwa kukimbia na Jeshi la Wanajeshi wa Msaada wa Haraka. Haya ni kwa mujibu wa Kamati ya kulinda wanahabari (CPJ).
Kwingineko, IFJ pia ilirekodi mauaji ya mwanahabari mmoja nchini Msumbiji, Somalia na Zimbabwe.
Waandishi wa habari wa Kiafrika waliendelea kufungwa kwa mashtaka yasiyo wazi na ya uzushi.
Waandishi wa habari 27 bado wamefungwa barani Afrika. Eritrea (7) ndiye mlinzi mkuu wa wanahabari barani Afrika, ambao baadhi yao wamekuwa gerezani kwa zaidi ya muongo mmoja.
Rais wa IFJ Dominique Pradalié alisema: "Mauaji na kufungwa kwa waandishi wa habari yanaongezeka mwaka wa 2025, na inatia aibu sana kuona jinsi serikali ndogo duniani kote zinavyofanya kuwalinda au kuzingatia kanuni za msingi za uhuru wa vyombo vya habari. Badala yake, tunashuhudia ulengaji wa moja kwa moja, majaribio ya wazi ya kunyamazisha sauti muhimu, na juhudi za kudhibiti vitendo hivi vya kimataifa vinavyohusu maslahi ya umma.
Nchi nyingi za Kiafrika zinaendelea kutumia sheria zao za kitaifa kwa kutumia sheria hiyo kuwanyamazisha waandishi wa habari, kulingana na IFJ.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid












