Hali ya upashaji habari ilivyo baada ya kufungwa kwa baadhi ya vyombo vya habari Burundi

Vipaza sauti

Changamoto ya kupata taarifa nchini Burundi baada ya kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza kilichotokea Juni 8, kinaendelea kudidimiza mazingira ya vyombo vya habari baada ya kukandamizwa kwa miaka kadhaa.

Vyombo vingi vya habari vilipigwa marufuku na kufukuzwa nchini humo 2015, wakati Nkurunziza na wafuasi wake walipoanza kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. Kupata taarifa za kuaminika kuhusiana na shughuli za nchi kwa sasa hivi ni changamoto kubwa.

Nkurunziza, ambaye anasemekana alikufa kwa mshtuko wa moyo, amekuwa madarakani tangu kuanza kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe 2005. Alitakiwa kukabidhi madaraka kwa Rais mteule Evariste Ndayishimiye Agosti 20.

________________________________________

Kutangazwakwa kifo cha Nkurunziza

Juni 8, kupitia akaunti moja ya Twitter nchini Burundi, @iBurundi Twitter account, inayoendeshwa na wanahabari na wanaharakati waliokimbilia nchi za nje, waliandika kwamba Nkurunziza amelazwa katika hospitali ya Karuzi Mashariki mwa nchi hiyo kupata matibabu ya ugonjwa wa Covid-19.

Siku moja baadae, akaunti rasmi ya serikali ya Twitter ikathibitisha kwamba Nkurunziza, 55, amekufa kwa mshtuko wa moyo katika hospitali ya Karuzi na kukanusha taarifa kuwa amekufa kwa virusi vya corona.

Vyombo vya habari vilisema kuwa mke wake, Denise, alikuwa mjini Nairobi kuanzia Mei 28, akipata matibabu ya virusi vya corona.

Kifo cha Nkurunziza kimezua maswali mengi ya ikiwa madai ya serikali ya kukanusha taarifa hizo ni ya kweli na kujua hisia za watu nchini humo, upokezaji wa madaraka na hali ilivyo kwa ugonjwa wa Covid-19. Kulikuwa na taarifa za uhakika tena kwa haraka kutoka kwa vyombo vya habari lakini maswali hayo pia yalipeleka uvumi mwingi kwenye mitandao ya kijamii.

Katika matangazo ya chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali cha RTNB Channel 1 na baadhi wa vyombo vya habari mitandaoni, muziki wa dini ya kikiristo ulitawala kwa muda mwingi huku taarifa kidogo tu zikitolewa kuhusiana na hali ilivyo.

________________________________________

Burundi

Ukandamizaji wa vyombo vya habari

Nkurunziza kuwania muhula wa tatu madarakani 2015 kulisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa. Maandamano ya kupinga serikali ambayo hayakuwahi kushuhudiwa hapo kabla yalitawala pamoja na jaribio la mapinduzi ambalo halikufanikiwa, watu mashuhuri nchini humo wakapoteza maisha na kukandamizwa kwa vyombo vya habari, mashirika ya kijamii na upinzani.

Wakati wa au baada tu ya jaribio la mapinduzi Mei, majengo ya kituo cha habari kinachojitegemea cha African Public Radio (RPA), Radio Bonesha, Radio Isanganiro na Radio-Tele Renaissance vilivamiwa na kuchomwa moto. Kampuni ya gazeti maarufu nchini humo la Iwacu pia ikavamiwa

Baadae, serikali ikafunga vyombo vya habari kadhaa vinavyojitegemea vyenye makao yake katika mji wa Bujumbura, na kuvishtumu baadhi yao kwa kutangaza jaribio la mapinduzi ya kijeshi ambalo halikufaulu.

Watu wengi zaidi wakaanza kutegemea taarifa za vyombo vya habari vya kimataifa kama Radio Ufaransa, Televisheni ya France24, idhaa ya BBC ya Kinyarwanda/Kirundi na Sauti ya Amerika (VOA).

Lakini pia vilivamiwa wakati mgogoro wa kisiasa ulipopamba moto.

Mwanahabari wa RFI na AFP Esdras Ndikumana alikimbilia uhamishoni nchini Kenya baada ya kupigwa akiwa kizuizini Agosti 2015.

Kamati ya kulinda wanahabari ilisema kwamba karibU wanahabari 100 wamelazimika kukimbilia nchi za nje baada ya kuanza kwa kamata kamata ya wanahabari Aprili na mwisho wa 2015.

Wale waliosalia nchini Burundi kwa sasa hivi wanafanyakazi kwa hofu na hawawezi kufanya kazi yao ya uanahabari kwa uhuru. Wanahabari wanne nchini nchini humo wa gazeti la kibinafsi la Iwacu na madereva wao walikamatwa mwaka jana wakiwa wanaangazia mapigano kati ya makundi ya waasi na vikosi vya serikali.

Machi 2019, serikali ilipiga marufuku shirika la habari la BBC upeperushaji wa matangazo yake nchini humo baada ya kulishtumu kwa kupeperusha makala ambayo haikuwa na taarifa za kweli iliyoangazia unyanyasaji wa haki za binadamu. Aidha marufuku hiyo pia ilielekezwa kwa shirika la habari la VOA kwa kuajiri mwanahabari aliyekuwa anaipinga serikali.

________________________________________

Studio

Mazingira ya hofu

Baadhi ya vyombo vya habari vilivyopigwa marufuku kwa sasa hivi vimeanza kupeperusha matangazo yake mtandaoni na kukosoa vikali serikali, ingawa kuna wasiwasi kuhusu usawa wa baadhi ya taarifa wanazotoa. Kwasababu maafisa wa serikali hawako tayari kuzungumza nao, mara nyingi taarifa zao huegemea upande mmoja. Hilo limepunguza uaminifu kwa taarifa zao.

Gazeti la Iwacu linatoa taarifa za kila siku kwenye tovuti na mtandao wake wa Twitter. Lakini pia limeshutumiwa kwa kuwa na upendeleo na Baraza la Taifa la Mawasiliano nchini Burundi.

Idhaa ya Kinyarwanda/Kirundi ya VOA pia linapeperusha matagazo yake kila siku kupitia masafa mafupi na kuweka taarifa kila zinapotokea kwenye tovuti yake.

BBC pia inatoa taarifa ya habari kwa nchi hiyo na Rwanda.

Vyombo vingi vya habari vinashirikisha wengine taarifa ya habari wanazopeperusha kupitia mtandao wa WhatsApp.

SOS Medias Burundi, inayoendeshwa na wanahabari wanaounga mkono uhuru wa habari imekuwa chombo kikuu cha taarifa nchini humo.

Chombo cha habari kinachomilikiwa na serikali, RTNB TV, Radio 1 na Channel 2, bado vimeshikiliwa haswa na serikali na chama tawala cha CNDD-FDD. Chombo cha RTNB kinaendeshwa na Eric Nshimirimana, aliyekuwa kiongozi wa waasi wa kundi la Imbonerakure linaloshtumiwa kwa unyanyasaji mkubwa wa haki za binadamu na uvamizi wa vyombo vya habari.

Kanisa Katoliki linaendesha vyombo vya habari ambavyo vimejikita zaidi katika masuala ya kidini lakini pia navyo vimekuwa vikinyanyaswa.