Je, muswada wa mabadiliko ya sheria ya habari umeondoa kero zote Tanzania?

Na Rashid Abdallah

w

Chanzo cha picha, Habarileo

Maelezo ya picha, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Januari 2021, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilikifungia kituo cha utangazaji cha Wasafi TV kwa muda wa miezi sita kuanzia Januari 06 mpaka Juni 2021 kwa kukiuka taratibu za utangazaji .

Maamuzi hayo yalikuja baada ya televisheni hiyo kurusha matangazo ya moja kwa moja ya tamasha na kumuonesha mwanamuziki maarufu nchini humo akiwa amevaa vazi linalomuonesha kuwa kama mtupu bila nguo.

Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa mamlaka ya mawasiliano nchini humo kufungia kituo hicho, mwezi Septemba Wasafi FM ilifungiwa kwa siku saba kuanzia Septemba 12 hadi Septemba 18 mwaka huu.

Huku makosa yakiwa ni kukiuka kanuni za Mawasiliano ya kielektroniki na posta katika utangazaji wa radio na televisheni za mwaka 2018 ambazo zinamtaka maudhui ya staha.

Kwa wadau wa vyombo vya habari matukio ya namna hii ndio yanaakisi uwepo wa sheria zinazotoa mamlaka makubwa kwa taasisi zinazosimamia vyombo vya habari. Wakati mwingine zikitoa adhabu kubwa ukilinganisha na lile linalo tafsiriwa kuwa ni kosa.

Oktoba 2022, akizungumza na chombo kimoja cha habari, Waziri Kivuli wa ACT-Wazalendo anayesimamia Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Uchukuzi, Filberth Macheyeki, akikosoa sheria za namna hiyo alisema;

“Ukiangalia sheria iliyotumika kufunga vyombo ya habari ni kandamizi, hawezi kufanya kosa mwandishi mmoja ukafungia taasisi nzima. Ina maana unakwenda kupoteza ajira za watu wengi. Lakini pia unakwenda kuumiza, kuminya uhuru wa watu kupata habari.”

.

Kipi kimerekebishwa?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Wiki hii Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali ambao ndani yake una sheria nane, ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambao umekuwa ukipigiwa kelele na wadau wakitaka baadhi ya vifungu vibadilishwe.

Wadau waliwasilisha mapendekezo katika vifungu 21, marekebisho nane hayakuwa ya lazima na mapendekezo tisa ndiyo yaliyorekebishwa, mengine ikiwa ni kuondolewa. Hayo ni kwa mujibu wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Kifungu cha 5 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 kinapendekeza kufanya marekebisho kwa lengo la kumwondolea Mkurugenzi wa Idara ya Habari jukumu la uratibu wa matangazo yote ya Serikali.

Kwa kuzingatia hilo marekebisho hayo yataruhusu Serikali kuwa na uhuru wa kuchagua chombo cha habari itakachokitumia kwa ajili ya matangazo kwa kuzingatia nguvu ya ushindani katika soko.

Katika kongamano la Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Wadau wa Haki ya Kupata Habari (CoRI), jijini Dodoma, mwezi Novemba 2022, Mwenyekiti mstaafu wa TEF, Theophil Makunga, alieleza;

“Kifungu cha 50 hata huko nyuma kwenye Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kosa la (defamation) kashfa unapelekwa mahakamani ulipe fidia. Sasa kulifanya jinai ni kama kitisho kwa waandishi wa habari.”

Yaonekana kilio kuhusu jinai hatimaye kimesikika. Kipengele cha kosa la jinai kimeondolewa. Kutoka katika sheria ambayo awali ilipitishwa Septemba 7, 2016 na kuidhinishwa na hayati Rais John Magufuli, Septemba 23, 2016.

Pia, marekebisho hayo yanalenga kupunguza adhabu. Kifungu kinachotaka kifungo cha kati ya miaka 5 hadi 10, sasa itakuwa ni miaka 2 hadi 5. Wakati faini inashuka hadi milioni 3 na ukomo milioni 10, katika adhabu zilizoruhusu hadi faini ya milioni 20.

Mapendekezo na marekebisho ya vifungu hivyo yanakusudia kuondoa adhabu kwa wamiliki wa mitambo ya uchapishaji ambao katika hali ya kawaida hawana uwezo wa kudhibiti maudhui yanayochapishwa katika mitambo.

w

Chanzo cha picha, AFP

Bado kuna tatizo?

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji (TEF), Neville Meena, akihojiwa na Azam TV anasema, “kuna mambo mengi tulitamani yawepo kwenye marekebisho, ambayo tunaamini yana manufaa kwa sekta ya habari kukua na kustawi, hayapo.”

Kwa hakika marekebisho hayo hayakuondoa kero zote ambazo waandishi wa habari na wadau wa habari wamekuwa wakizilalamikia. Kuna mambo ambayo muswada huo haujaonesha kwamba yameguswa ili kurekebishwa.

Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 imeipa mamlaka serikali kufungia magazeti. Pia, kuna kero kuhusu vyombo vya habari kutakiwa kulipia kila mwaka leseni ya kuendesha shughuli zao.

Kingine kinacholalamikiwa ni Kanuni za Mawasiliano za Kielektroniki na Posta, Maudhui ya Mtandaoni za 2020 ambazo pamoja na kuipa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kufungia redio, runinga na vyombo vya habari vya mtandaoni kwa kukiuka yale yaitwayo maadili ya taifa.

James Marenga, Makamu Mwenyekiti wa Media Institute of Southern Africa, Tanzania, anasema, “kuna kipengele ambacho ni kifungu cha saba katika sheria hii, kinaingilia uhuru wa uhariri na uhuru wa vyombo vya habari, kinasema utaandika taarifa zinazohusiana na maslahi ya nchi kwa maelekezo ya serikali. Vipengele hivyo haipaswi kuwepo kabisa.”