Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Marekani na Israel zimeshindwa kudhibiti oparesheni za kijeshi na serikali ya Iran?
Gazeti la Uingereza la the Guardian katika uchambuzi wake wa vita vya Marekani na Israel dhidi Iran, linasema kuwa mkakati wa vita wa Marekani dhidi ya Iran umefeli, na sasa wanatafuta mpango mbadala wa kupigana vita hivyo.
Taarifa hiyo inachambua kuwa "Marekani na Israel zimefeli kabisa kudhoofisha mamlaka za Iran" kwani mpango wao ulikuwa kumuua kiongozi mkuu na viongozi wengine wa kidini na makamanda wa kijeshi, ili kuleta mapinduzi katika utawala wa Iran.
Ila sasa utawala wa Iran una kiongozi mpya, na labda kuna wengine wapo ambao watateuliwa iwapo Mojtaba Khamenei atauawa.
Vita hivi huenda vikailemeza Iran, lakini utawala wake utasalia na huenda wakajiandaa Zaidi kurejelea mpango wao wa kutengeneza silaha za nyuklia na kuzitumia siku za usoni.
Uchambuzi wa Guardian unaongeza kuwa "ili kuzuia hilo kutotokea Israel na Marekani lazima waidhibiti Iran kikamilifu, ili waweze kufika maeneo yote ya taifa hilo. Na huenda ni vigumu kufanya hivyo"
Chapisho hilo la the Guradian linaongezea kuwa lazima kuwa na "mpango mbadala" utakaojumuisha kushirikiana na makundi madogo kama Wakurdi na kuwashinikiza kufanya mashambulizi na mpango wa pili ni "Imani ya Dahiya" ambayo inatumika kuiharibu Iran.
Inasemakana kwa sasa jeshi la anga la Marekani linatumia mkakati huo kwa kulenga miundo mbinu ya Iran.
Mwandishi wa uchambuzi huo anasema mkakati huo ulitumika nchini Lebanon, ambapo Israel ilianza kwa kuharibu ngome kuu ya Hezbollah kusini mwa Lebanon, na pia dhidi ya Hamas eneo la Gaza, katika vita ambavyo vimedumu zaidi ya miezi thelathini.
Uchambuzi huo pia unasema kuwa licha ya kutumia "kanuni za Dahiya" bado Hamas inaonekana kuwa na nguvu eneo la Gaza na "huenda mkakati huu usifanye kazi Iran"
Mashambulio makali yanafaa kufanyika ili athari kubwa ya vita hivyo vionekane Iran, na iwapo hili litafanyika jeshi la Revolutionary Guard litaongeza mashambulizi yake katika vituo vya mafuta katika mataifa ya Ghuba na hili litaathiri uchumi wa kitaifa.
Kutokana na hali ya sasa, huenda mashambulizi kutoka pande zote yakapungua badala ya kuongezeka.
Mlango wa bahari wa Hormuz lazima usalie wazi
Gazeti la Uingereza la The Times linasema kuwa mlango wa Bahari wa Hormuz lazima usalie wazi, na lazima Iran isitishwe kushambulia meli za mafuta zinazopitia eneo hilo.
Gazeti hilo linasema athari itakuwa kubwa sana iwapo Iran, itazamisha meli zinazopitia mlango wa bahari wa Hormuz kwani italemaza uchumi wa mataifa yanayo agizia mafuta kutoka nchi za ghuba.
Tayari Iran imelenga meli 14, ambazo zilikuwa zinajaribu kupitia eneo hilo. Na sasa bei ya mafuta imepanda, huku uchumi wa dunia ukiathirika, mataifa yanayokuwa tayari yameanza kurekodi mfumuko wa bei za bidhaa.
The Times inasema kuwa baada ya maeneo ya kurusha makombora ya Iran kuharibiwa , taifa hilo sasa linataka kuharibu uchumi wa dunia kama njia moja ya kukabiliana na Washington.
Bila kuwa na wanajeshi wa ardhini inakuwa vigumu kwa Marekani kuzuia mashambulizi ya meli pwani ya Iran.
Kukidhibiti kisiwa cha mafuta cha Kharg kunahitaji wanajeshi wa ardhini, na Marekani kuwatuma wanajeshi wake, kutasababisha maafa mengi na kuwaghadhabisha raia wa Marekani.
Iran inajihami katika vita hivi kwa kushambulia Jirani zake na kulenga vituo vyao vya mafuta na gesi.
Iwapo Iran itazidi kushambuliwa, basi mataifa ya ghuba yatahitaji ulinzi zaidi kutoka mataifa ya magharibi.
Viwango vitatu vya kurithi
Gazeti la Marekani la The Washington, linaelezea ushindi kwa Iran utakaa vipi.
Kwanza vita vya Iran vinaweza kuisha "mapema" kutokana na jinsi pande zote zinafafanua ushindi.
Vita hivyo vina viwango vitatu, ya kwanza ni kuondoa utawala wa Iran, kuwaondoa viongozi wamajeshi, kulemaza vituo vya oparesheni ya kijeshi, na kuharibu maghala ya kuhifadhi silaha na makombora, ili kuilemeza Iran kijeshi.
Ufanisi wa pili utatokea iwapo utawala wa Iran utaporomoka kabisa, na kutengenezwa kwa utawala mpya utakaokuwa unawajibikia Marekani, "hii ni baada ya viongozi wote kulengwa."
Kulingana na gazeti hilo, iwapo viongozi wengi watalengwa na kuuawa, mfumo wa uongozi wa Iran utaanza kuyumbayumba, na baadhi ya viongozi watakubali kushirikiana na Marekani kama kiongozi wa sasa wa Venezuela baada ya kukamatwa kwa Maduro.
Ufanisi wa tatu utatokea iwapi raia wa Iran wataingia barabarani na kuanza kugoma wakitaka hali ya kawaida kurejeshwa na serikali ya mpito kuundwa kulingana na matakwa ya raia.
Ila iwapo vita hivyo vitamalizwa "mapema" kabla ya kuanguka kwa utawala wa Iran, hii itakuwa ushindi kwa Iran na itaendelea na kampeni yake ya kupinga ushawishi wa mataifa ya magharibi.