Kuna umuhimu gani wa kununua toleo jipya la simu za kisasa?

Chanzo cha picha, Getty Images
Heri ya msimu wa matoleo mapya ya simu za smartphone kwa wote wanaosherehekea. Ni wakati mwingine tena wa mwaka, ambapo kampuni kubwa za teknolojia zinafanya kila wawezalo kukushawishi kununua simu mpya iliyoboreshwa zaidi.
Hivi majuzi tumeona Google ikizindua simu mpya zaidi za Pixel 9, ikifuatwa na Apple ikizindua iPhone 16.
Mnamo mwezi Julai, Samsung ilitoa matoleo mapya zaidi ya simu zake zinazoweza kukunjwa, Z Flip6 na Z Fold6 huku Huawei ikiwa haijaachwa nyuma katika hilo kwa kuzindua simu inayoitwa Mate XT, nchini Uchina, ambayo inajikunjika mara mbili.
Huku mauzo ya simu za smartphone yakipungua duniani kote, ujumbe wa kuvutia wa mauzo unaotolewa unazidi kushangaza.
Mkuu wa Apple Tim Cook aliahidi kwamba iPhone16 "itafafanua upya uwezo wa simu ya smartphone", chochote kitakachojitokeza kumaanisha.
Makamu wa rais wa usimamizi wa bidhaa za Google, Brian Rakowski aliandika maneno mengi mazuri kuhusu muundo "wa kustaajabisha" wa Pixel 9 (sema hili kwa kunong’ona: kwangu bado inaonekana kama iliyo mstatili na nyeusi).
Huawei sasa ina wimbo wake inaomiliki kwa watumiaji, inasema katika vyombo vyake vya habari, "ikielezea kwa nguvu yake yote kufikia ndoto fulani, ikionyesha kwamba kila mafanikio na hatua ambayo kampuni imepata yanatokana na imani katika ndoto zake".
Naam, bado tunazungumza juu ya simu.
Apple na Google kwa kiasi kikubwa zimetumia vipengele vya akili mnemba yaani AI.
Simu mpya ya Google inaweza kuongeza maudhui yaliyotengenezwa kutokana na AI kwenye picha zilizopo, na pia kuondoa zile usizozitaka (kwa viwango tofauti vya mafanikio, kulingana na tajriba yangu).
Akili mnemba katika simu ya Apple ya iPhone16 ina teknolojia ya ChatGPT iliyojumuishwa kwenye msaidizi wa kidijitali Siri - ambayo wengi wanabisha kwamba imekuwa ikihitaji sasisho kwa muda mrefu.
Lakini kuna mtu yeyote aliyesema kwamba wanataka vitu hivi vyote viwepo katika simu zao?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mtaalamu wa simu za mkononi Ben Wood, kutoka kampuni ya utafiti ya CCS Insight, alisema kuwa ingawa vipengele vya AI vinalenga kurahisisha maisha ya kidijitali, haviko katika orodha ya vile ambavyo ni lazima kwa kila mtu.
"Nadhani watu wengi sasa wanajua wanachotaka kutoka kwa simu, na moja ya mambo muhimu zaidi ni kamera," anasema.
Wabunifu wa simu pia wanajua hili. Kipengele cha teknolojia kwa simu mpya kwenye kamera, kawaida ni uboreshaji wa kizazi cha simu kilichopita.
Lakini hata hii sio tena hakikisho la mauzo.
"Kinachotokea ni kwamba watu wanakuwa na simu zao kwa muda mrefu. Huko nyuma mwaka wa 2013 kulikuwa na simu milioni 30 zinazouzwa kila mwaka,” anaongeza Bw Wood. "Mwaka huu itakuwa karibu milioni 13.5."
Bila shaka kuna tatizo la kuongezeka kwa gharama ya maisha linaloathiri maamuzi ya manunuzi.
Na pia kuna bei ya kila simu, ambayo yote yanajumuisha vitu adimu.
Kuongezea, pia kuna mwelekeo unaoenea, hasa kati ya wazazi na vijana, kujaribu kuondokana kabisa na matumizi ya smartphones.
Kuna matukio ambayo yamekuwa yakishuhudiwa huko Uingereza ambapo shule zinakagua sera zao za watoto kuwa na simu ya smartphone shuleni, na chache tayari zimechagua kupiga marufuku hilo moja kwa moja.
Mtandao wa simu za mkononi wa EE unapendekeza kwamba watoto walio chini ya umri wa miaka 11 wasiruhusiwe kuwa na simu za smartphone.
Nova East inaongoza tawi la kaskazini na magharibi la London katika kampeni ya Smartphone Free Childhood, ambayo inawahimiza wazazi na shule kutoa ushirikiano ili kuchelewesha umri ambao watoto wanapewa simu.
"Sio kwamba sisi tunapinga teknolojia, tunataka mema kwa watoto," anasema. "Tungependa kuona makampuni za teknolojia zikitengeneza simu zinazofaa watoto, zinazotoa vipengele muhimu pekee kama vile kupiga simu, kutuma ujumbe, muziki na ramani, bila vipengele vingine vya ziada."

Chanzo cha picha, Getty Images
Dk Sasha Luccioni, mwanasayansi wa utafiti katika kampuni ya AI ya Hugging Face, anasema kuwa hadi sasa, ujumbe huu hauonekani kupokelewa vizuri.
"Kuna mazungumzo mengi ya kupunguza 'matumizi ya vifaa vya kidijitali' katika jinsi tunavyotengeneza na kutumia teknolojia - lakini inaonekana kama wabunifu wa simu za smartphone wanaenda kinyume kabisa na hilo," anasema.
Kwa watumiaji wa simu zingine, alisema, "Watumiaji wa Samsung wanaweza kuchagua jinsi wanavyotumia simu zao za Galaxy zinazolingana vyema na mahitaji yao. Kwa mfano, vipengele vya ustawi kidijitali huruhusu watumiaji kuchagua vipengele wanavyotumia, kwa muda gani, kama vile kuweka muda wa ukomo wa skrini kwenye programu mahususi wanazotaka kujizuia kuzitumia."
Kampuni moja ambayo inasikiliza wito wa kupunguza vipengele vya kwenye simu ni ya Ufilipino ya HMD - ambayo bado inatengeneza simu za kawaida za Nokia.
Mwezi uliopita ilizindua simu yenye mandhari ya Barbie kwa ushirikiano na mtengenezaji wa vifaa vya watoto kuchezea Mattel, na niliijaribu kuitumia.
Kama vile simu nyingi, haina programu, haina duka la programu, haina kamera ya kujipiga picha, na mchezo ni mmoja pekee yaani ‘game’. Ukitaka kusikiliza muziki kuna redio ya FM.
Simu yangu ndio ninayotumia kazini kama kitendea kazi, pia ndio ninayoitumia kama benki, kufanya manunuzi, maelekezo ya mahali, ufuatiliaji wa afya na mipango ya familia, na pia, ndio yenye kipengele cha michezo na inaniwezesha kuingia kwenye mitandao ya kijamii.
"Nadhani jambo tunalosahau kila wakati ni kwamba kuna faida nyingi sana kutokana na kutumia simu za smartphone," anasema Pete Etchells, profesa wa saikolojia na mawasiliano ya sayansi katika chuo kikuu cha Bath Spa, ambaye ameandika sana kuhusu suala la muda wa kutumia skrini.
"Tunaangazia zaidi juu ya mabaya yake. Ni vizuri kila wakati kujua kuwa hizi ni teknolojia zinazorahisisha mambo. Zinatusaidia. Pia, zina mambo mazuri."
Imetafsiriwa na Asha Juma








