Kwa nini China inataka kushiriki utatuzi wa mgogoro wa Israel na Palestina?

    • Author, Dima Odeh
    • Nafasi, BBC

Mfalme wa Bahrain, Hamad bin Isa Al Khalifa, Rais wa Misri, Abdel Fattah Al-Sisi, Rais wa Tunisia, Kais Saied, na Rais wa UAE, Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, wataelekea China siku ya Jumanne kufuatia mwaliko wa Rais Xi Jinping, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema, viongozi wa nchi za Kiarabu watahudhuria sherehe za ufunguzi wa Mkutano wa kumi wa jukwaa la Ushirikiano kati ya China na nchi za Kiarabu, kulingana na shirika la habari la China, Xinhua.

Wakati wa mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ding Li alisema Rais Xi Jinping "atafanya mazungumzo na wakuu wa nchi hizo nne ili kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande hizo mbili na masuala ya kikanda na kimataifa."

Li aliongeza, kutakuwa na msimamo wa pamoja kati ya China na nchi nne za Kiarabu kuhusu suala la Palestina.

China siku zote imeeleza kuunga mkono suala la Palestina na suluhu ya mataifa mawili ili kusuluhisha mzozo wa Israel na Palestina, huku Rais wa China akitoa wito wa kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa amani kwa lengo la kusuluhisha mzozo huo.

Mwezi Novemba mwaka jana, Beijing ilikaribisha wajumbe kutoka nchi za Kiarabu na Kiislamu kujadili hali ya Ukanda huo na kujaribu kuzishawishi nchi za Magharibi kutafuta usitishaji vita, operesheni za kijeshi na kuruhusu kuingia misaada ya kibinadamu.

Ukanda wa Gaza ulikumbwa na mashambulizi makali ya Israel kujibu shambulio lililoanzishwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba.

Mwishoni mwa mwezi wa Aprili, Beijing pia ilikuwa mwenyeji wa ujumbe kutoka harakati ya Hamas na ujumbe wa harakati ya Fatah kujadili juhudi za ndani za maridhiano.

Lakini swali kuu: Kwa nini China inataka kuwa mpatanishi katika mzozo wa Palestina na Israel? Je, jitihada zake zinaweza kufanikiwa?

Maslahi ya pande zote mbili

Beijing ina maslahi na pande zote mbili za mzozo. China siku zote imeunga mkono suluhisho la serikali mbili, na huko nyuma, haswa katika miaka ya 1960 na 1970, ilitoa silaha kwa Harakati ya Ukombozi wa Palestina.

Lakini leo hii ina uhusiano mkubwa wa kiuchumi na Israel. China ni mshirika wake wa pili wa kibiashara.

Hussein Ismail, naibu mhariri wa toleo la Kiarabu la jarida la China Today, anaamini Beijing ina sifa ya kuwa mpatanishi katika mzozo huu, licha ya kuwepo mambo yanayoweza kuifanya kazi hii kuwa ngumu kwake.

Ismail anaongeza: “China ina uhusiano mzuri sana na nchi za Kiarabu, na wakati huo huo ina uhusiano mzuri na Israel, lakini inafahamu fika kwamba suala la mzozo wa Palestina na Israel lina uhusiano wa karibu na Marekani.”

“Inafahamu vyema kuwa Washington ndiye mhusika mkuu, haswa kwa Israel. Kwani ndiyo pekee inayoweza kuweka shinikizo kwa Israel, wakati China haina uwezo kama huo."

Uhusiano mzuri kati ya Israel na Marekani unaiweka China katika hali ngumu kuweza kupatanisha Israel na Wapalestina.

Profesa Kerry Brown, wa Masomo juu ya China katika Chuo Kikuu cha King's College London, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Lao China, anasema; "sidhani kuwa China inatafuta kuwa mpatanishi tu, ila pia inataka utulivu Mashariki ya Kati ili kulinda maslahi yake ya kiuchumi na rasilimali inazopata kutoka kanda hiyo”.

"China imeweza kujenga uhusiano wa kirafiki na washirika wote wakuu Mashariki ya Kati, hilo ni tofauti na Mrekani.”

Mtarajio ya kimkakati

China ni nchi ya pili yenye nguvu kubwa kiuchumi duniani, na ina jeshi la tatu kwa nguvu duniani, na imekuwa na mipango mingi inayoiwezesha kuwa mdau na mshirika mkuu katika uongozi wa dunia.

Kwa mujibu wa Hussein Ismail, “Beijing inaamini mizozo lazima isuluhishwe kwa amani. Hapana shaka tunazungumzia nchi ambayo ina malengo ya kimkakati, na maslahi yake katika eneo la Mashariki ya Kati.”

Eneo la Mashariki ya Kati lina umuhimu mkubwa kwa China. Mbali na kuwa ndio chanzo kikuu cha usambazaji wa nishati, eneo hilo ni nyumbani kwa makampuni makubwa ya Kichina ya ukandarasi na uwekezaji nje ya China.

Ismail anatuambia, "Kanda ya Mashariki ya Kati ni muhimu kwa China katika mpango wake wa kutandaza miundombinu, ambapo Beijing inategemea kwa kiasi kikubwa kubadilisha sura ya uhusiano wa kimataifa, iwe katika siasa, uchumi na hata usalama."

China ilizindua Mpango wa "Belt and Road Initiative" mwaka 2013, mradi mkubwa wa miundombinu ambao unalenga kupanua uhusiano wake wa kibiashara kwa kujenga bandari, reli, viwanja vya ndege na majengo ya viwanda.

Wakati Beijing, ikiendelea na juhudi zake za kuimarisha ushawishi huu, itaendelea kutafuta nafasi ya kupatanisha migogoro ili kuleta utulivu, hasa Mashariki ya Kati, kwa sababu ya shughuli zake za kiuchumi huko Misri, Saudi Arabia, Iran, na kwengineko.

Imetafsiriwa na Rashid Abdalla na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi