Vifahamu vyuo vikuu kumi bora duniani 2025

.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Asha juma
    • Nafasi, BBC, Nairobi
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Data inayoonyesha vyuo vikuu bora duniani 2025 ya jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education imeshatoka na bila shaka kuna wengi wenye uwezo walio na ndoto ya kusoma katika vyuo vikuu vya nje ya bara la Afrika.

Lakini wakati shauku na hamu inazidi kushika kasi, dunia bado inaendelea kutafakari hatua ya Marekani ya kusitisha kwa muda utoaji wa viza ya elimu kwa wanafunzi wa kigeni.

Zaidi ya wanafunzi milioni 1.1 wa kimataifa kutoka zaidi ya nchi 210 walijiunga na vyuo vya Marekani katika mwaka wa 2023-24, kulingana na Open Doors, shirika linalokusanya data za wanafunzi wa kigeni.

Wakati wanafunzi wanaendelea kulitafakari hilo, nikufahamishe vyuo vikuu 10 bora duniani, kulingana na jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education.

1. Chuo Kikuu cha Oxford

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chuo Kikuu cha Oxford cha Uingereza kimeendelea kuchukua uongozi katika orodha ya vyuo vikuu bora duniani kulingana na jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education.

Utendaji wa taasisi hiyo umekuwa ukiimarika pakubwa katika mapato yake, idadi ya wale wanaonukuu utafiti unaofanywa na taasisi hiyo pamoja na alama inazopata katika ufundishaji wake.

Chuo Kikuu cha Oxford ni kikongwe zaidi katika ulimwengu unaozungumza Kiingereza na cha pili cha zamani zaidi ulimwenguni. Wakati tarehe halisi ya kuanzishwa kwake haijulikani, kuna ushahidi kwamba kilikuwa tayari kinatoa mfunzo kwa wanafunzi mnamo mwaka 1096.

Oxford ina mtandao wa waliohitimu wa watu zaidi ya 250,000 ambapo wengine ni washindi wa medali zaidi ya 120 za Olimpiki, washindi wa tuzo zaidi ya 20 za Nobel, na viongozi zaidi ya 30 duniani kama vile Bill Clinton, Aung San Suu Kyi, Indira Gandhi na mawaziri wakuu wa Uingereza 26, miongoni mwao wengine.

2. Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT)

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Massachusetts Institute of Technology (MIT) sasa ni chuo kikuu kinachoongoza nchini Marekani na kimeshika nafasi ya pili ulimwenguni kwa utendaji wake bora zaidi, kulingana na jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education.

Kikianzishwa mnamo mwaka 1861, chuo cha MIT kilikuwa jamii ndogo tu ya wanaotafuta utatuzi wa changamoto wanazokumbana nazo na wapenzi wa sayansi walio na hamu ya kuleta maarifa yao pamoja, leo hii, MIT imeibuka kuwa chuo kikubwa cha elimu kikiwa na zaidi ya wanafunzi 11,000 wa shahada ya kwanza na wahitimu.

Watafiti wa MIT wako mstari wa mbele katika uvumbuzi wa masuala kadhaa kama akili mnemba, utafutaji suluhu katika mabadiliko ya hali ya hewa, VVU, saratani, na kupunguza umasikini huku utafiti wa zamani wa MIT ukichochea mafanikio ya kisayansi kama vile uvumbuzi wa rada na mengineo.

Miongoni mwa waliowahi kusomea chuo hichi ni pamoja na Buzz Aldrin, mwanaanga wa zamani, mhandisi na rubani wa ndege ya kivita. Alikuwa mmoja wa watu wawili wa kwanza kutua kwenye Mwezi mnamo mwaka 1969.

Kofi Atta Annan alikuwa mwanadiplomasia wa Ghania ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Saba wa Umoja wa Mataifa kutoka 1997-2006. Annan na UN walipokea Tuzo la Amani la Nobel la 2001.

3. Chuo Kikuu cha Harvard

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chuo Kikuu cha Harvard mwaka 2025 kimepanda juu hadi nambari tatu kutoka nafasi ya nne 2024.

Kikiwa kilianzishwa 1636, Chuo Kikuu cha Harvard ndio kikongwe zaidi nchini Marekani na kinachukuliwa kuwa moja ya vya kifahari zaidi ulimwenguni.

Chimbuko la jina la chuo hichi ni mfadhili wake wa kwanza, John Harvard, ambaye aliacha maktaba yake na nusu ya mali yake kwa taasisi hiyo wakati alipoaga dunia mnamo 1638.

Pia ni kimoja ya vyenye kupokea ufadhili mkubwa zaidi wa kifedha.

Taasisi hii imezalisha zaidi ya washindi wa Tuzo za Nobel 45, zaidi ya viongozi wa dunia 30 na zaidi ya washindi wa Tuzo ya Pulitzer 40.

Marais kumi na tatu wa Marekani wana digrii za heshima kutoka kwa taasisi hiyo; wa hivi karibuni zaidi akiwa John F. Kennedy mnamo 1956.

4. Chuo Kikuu cha Princeton

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kulingana na jarida la elimu kutoka Uingereza la Times Higher Education, chuo kikuu cha Princeton kimefanya vizuri na kupanda juu kutoka nambari sita hadi nafasi ya nne.

kilianzishwa mnamo 1746 kama Chuo cha New Jersey, na kupewa jina jipya Chuo Kikuu cha Princeton mnamo 1896 kwa heshima ya eneo ambako chuo hicho kiko.

Kikiwa kimetoa washindi wa Tuzo ya Nobel zaidi ya 40, wa miaka ya hivi karibuni ni pamoja na wataalamu wa dawa Tomas Lindahl na Osamu Shimomura, wachumi Paul Krugman na Angus Deaton na wataalamu wa fizikia Arthur McDonald na David Gross.

Chuo cha Princeton pia kimefundisha marais wawili wa Marekani, James Madison na Woodrow Wilson, ambaye pia alikuwa rais wa chuo kikuu kabla ya kuingia Ikulu.

Wahitimu wengine wanaotambulika ni pamoja na Michelle Obama, waigizaji Jimmy Stewart na Brooke Shields, mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos na mwanaanga Pete Conrad.

MIT na Princeton vimejitokeza kuwa vyuo vilivyoboreka zaidi katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

5. Chuo Kikuu cha Cambridge

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kilianzishwa mnamo mwaka 1209, Chuo Kikuu cha Cambridge cha Uingereza ni taasisi ya utafiti wa umma. Historia yake ya miaka 800 hufanya kiwe miongoni mwa vyuo vya zamani zaidi ulimwenguni.

Chuo cha Cambridge kina wanafunzi zaidi ya 18,000 kutoka tamaduni mbalimbali za dunia. Karibu 4,000 ya wanafunzi wake ni wa kimataifa kutoka nchi 120 tofauti.

Shule sita zipo katika katika chuo kikuu hichi, chenye takriban vitivo 150 na taasisi zingine. Shule hizo sita ni: Arts and Humanities, Biological Sciences, Clinical Medicine, Humanities and Social Sciences, Physical Sciences and Technology.

Chuo hiki kinakadiriwa kuwa na thamani ya karibu £ bilioni 6.

6. Chuo Kikuu cha Stanford

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Chuo Kikuu cha Stanford kimechukua nafasi ya pili. Kilianzishwa mnamo 1885 na Seneta wa California Leland Stanford na mkewe, Jane, "kuendeleza ustawi wa umma".

Mtoto wa pekee wa wanandoa hao alikuwa amefariki dunia kwa homa ya matumbo au 'typhoid', na uamuzi wao wa kujenga chuo kikuu kwenye shamba lao ulikusudiwa kama ukumbusho.

Michezo ni maarufu chuoni humo huku wanafunzi, kitivo na wafanyakazi wakifurahia sanaa, vituo vya burudani na programu za ustawi.

7. Taasisi ya Teknolojia ya California

California Institute of Technology (Caltech) ni taasisi maarufu ya sayansi na uhandisi na taasisi ya elimu, ambapo kitivo cha kipekee na wanafunzi hutafuta majibu ya maswali magumu, kugundua maarifa mapya, kuongoza katika uvumbuzi na kujitahidi kubadilisha siku za usoni kuwa bora zaidi.

Wahitimu na kitivo cha Caltech wamepata tuzo 39 za Nobel, medali 71 za kitaifa za Sayansi au Teknolojia za Marekani na nyingi nyinginezo. Wanasayansi wakuu wanne wa Jeshi la Anga la Marekani pia wamesoma katika taasisi hiyo.

Wanafunzi wa Caltech pia wanajulikana sana kwa kujitosa kwenye uigizaji wa vichekesho.

8. Chuo Kikuu cha California, Berkeley

.

Chanzo cha picha, Reuters

Chuo Kikuu cha California, Berkeley cha utafiti wa umma, kinachukuliwa kuwa moja ya vyuo vikuu vya kifahari nchini Marekani.

Kitivo cha Berkeley kimeshinda tuzo 19 za Nobel, zaidi katika fizikia, kemia na uchumi. Washindi wa hivi karibuni ni pamoja na Sauli Perlmutter, ambaye alishinda Tuzo la Nobel la 2011 kwa Fizikia.

Berkeley ina utamaduni kama kitovu cha harakati za kisiasa. Wakati wa miaka ya 1960 na 1970, kilikuwa kitovu cha maandamano ya wanafunzi dhidi ya Vita vya Vietnam.

9. Imperial College London

Imperial College London, taasisi ya kisayansi iliyo katikati mwa mji mkuu, inachukuliwa kuwa moja ya taasisi zinazoongoza nchini Uingereza.

Imperial ilipewa cheti chake mnamo 1907.

Taasisi hiyo ina washindi 14 wa Tuzo la Nobel, akiwemo Sir Alexander Fleming, mgunduzi wa penicillin.

Wahitimu mashuhuri ni pamoja na mwandishi wa hadithi za kisayansi HG Wells, mpiga gitaa maarufu Brian May, waziri mkuu wa zamani wa India Rajiv Gandhi na wengineo.

10. Chuo Kikuu cha Yale

.

Chanzo cha picha, EPA

Chuo Kikuu cha Yale ni cha utafiti na taasisi ya tatu kongwe ya elimu ya juu nchini Marekani.

Historia ya Yale inaanzia mwaka 1701.

Mnamo mwaka 1718 ilipewa jina la Chuo cha Yale, kwa heshima ya mfadhili wa Wales Elihu Yale, na ilikuwa chuo kikuu cha kwanza nchini Marekani kutoa PhD, mnamo 1861.

Karibu mwanafunzi mmoja kati ya watano ni wa kutoka nje ya nchi, na zaidi ya nusu ya wahitimu wote wanapokea ufadhili kutoka chuo hicho.

Miongoni mwa wahitimu wa chuo hicho ni marais watano wa Marekani: William Howard Taft, Gerald Ford, George HW Bush, Bill Clinton na George W. Bush.

Wengine maarufu ni pamoja na waliokuwa mawaziri wa Marekani Hillary Clinton na John Kerry, na mwigizaji Meryl Streep