Recep Tayyip Erdogan: Muuza malimau aliyebadilisha hatima ya Uturuki

Erdogan

Chanzo cha picha, Reuters

Kutoka katika maisha ya kawaida, Recep Tayyip Erdogan ameibuka na kuwa gwiji wa kisiasa ambaye ameiongoza Uturuki kwa miaka 20 na ameweka alama yake nchini humo pengine kuliko kiongozi yeyote tangu Mustafa Kemal Ataturk, baba wa taifa na rais wa kwanza wa taifa hilo.

Jumapili hii alifanikiwa kurejesha mamlaka yake kwa miaka mitano zaidi kwa kumshinda mgombea wa upinzani Kemal Kilicdaroglu katika duru ya pili ya uchaguzi uliokuwa na ushindani wa karibu ambao mtawala huyo amelazimika kugombea katika miongo miwili.

Katika asilimia 99.85% ya kura zilizohesabiwa, Erdogan alipata asilimia 52.16% ya kura huku mgombea wa upinzani akipata asilimia 47.84%, kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka za Uchaguzi za Uturuki.

Saa chache kabla ya matokeo rasmi kutangazwa, Erdogan alikuwa amejitangazia mshindi, huku mpinzani wake - bila kukubali ushindi - alielezea mchakato huo kuwa "usio wa haki".

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, na mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, wamempongeza Erdogan kwa kuchaguliwa tena.

Erdogan

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Wafuasi wa Erdogan wakifurahia hotuba yake baada ya uchaguzi, Ilikuwa Mei 28, 2023.

Kilicdaroglu, ambaye aliweza kuunganisha vyama vyote vya upinzani nchini humo, na kutoa upinzani mkubwa zaidi dhidi ya Erdogan tangu aingie madarakani mwaka 2003.

Lakini Recep Tayyip Erdogan ni nani, mtu ambaye ameiongoza Uturuki kwa miongo miwili iliyopita?

Kutoka kuuza malimau na ndimu hadi kuwa Rais

Erdogan alizaliwa mwaka wa 1954 na kukulia katika eneo karibu na Bahari Nyeusi, kaskazini mwa Uturuki.

Erdogan

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Erdogan ndiye mwanasiasa mwenye nguvu zaidi Uturuki tangu Ataturk.

Alipokuwa na umri wa miaka 13, baba yake aliamua kuhamia Istanbul, akiwa na wazo la kuwapa watoto wake fursa bora zaidi.

Erdogan kisha alianza kuuza malimau na mikate inayojulikana kama "simit" ili kupata pesa za ziada.

Alisoma shule ya Kiislamu kabla ya kuingia chuo kikuu na kupata shahada ya utawala wa biashara.

Shahada hii imekuwa suala la utata kwa upande wa upinzani, ambao unaonyesha kuwa hakuwahi kupata shahada hiyo, tuhuma ambayo Erdogan amekuwa akiikana.

Rais wa sasa wa Uturuki alikuwa akipenda sana soka na alikuwa sehemu ya timu mbalimbali hadi miaka ya 1980.

Lakini shauku yake kuu ilikuwa siasa. Katika miaka ya 70 na 80 alikuwa sehemu hai ya duru za Kiislam, na alikua mwanachama wa chama cha Kiislam ambacho kiliongozwa na Necmettin Erbakan.

Chama hicho kilipozidi kupata umaarufu katika miaka ya 1990, Erdogan aligombea umeya wa Istanbul katika uchaguzi wa 1994 na kulitawala jiji hilo kwa miaka minne iliyofuata.

Erdogan

Chanzo cha picha, EPA-EFE

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Erbakan, ambaye alikuwa waziri mkuu wa kwanza wa Kiislamu nchini Uturuki, alihudumu kwa mwaka mmoja tu kabla ya mapinduzi yaliyofanywa na jeshi mwaka 1997.

Kwa sababu hii, Erdogan alijikuta katika msuguano na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Mwaka huo huo, alishtakiwa na kuhukumiwa kwa tuhuma za kuchochea chuki kwa kusoma katika uwanja wa umma shairi ambalo lilikuwa likisema: "Misikiti ni vizuizi vyetu, huweka kofia zetu, na minara ya 'bayonets' na imani ya askari wetu."

Baada ya kukaa gerezani kwa miezi minne, alirudi kwenye siasa. Lakini mnamo mwaka 1998, chama chake kilipigwa marufuku kwa kukiuka kanuni za siasa za Uturuki.

Mnamo Agosti 2001, Erdogan alianzisha chama kipya chenye misingi ya Kiislamu na Abdullah Gul: Chama cha Haki na Maendeleo (AKP, kwa kifupi chake kwa Kituruki).

Umaarufu wa Erdogan ulikua, haswa kati ya vikundi viwili: Waturuki wenye misimamo ya kidini ambao walihisi kutengwa na wasomi wa kidini, na kundi la pili ni wale ambao walikuwa wameteseka kiuchumi wakati wa machafuko yaliyoikumba nchi hiyo mwishoni mwa miaka ya 1990.

Mnamo 2002, AKP ilishinda uchaguzi wa bunge, na mwaka uliofuata Erdogan aliteuliwa kuwa waziri mkuu.Na amebaki kuwa kiongozi wa chama chake hadi leo.

Amekuwa Waziri Mkuu mara tatu

Tangu 2003, Erdogan amehudumu kama waziri mkuu kwa mihula mitatu. Kuanzia hapo, aliongoza nchi hiyo kuelekea kwenye ukuaji wa uchumi na alionekana kama mwanamageuzi.

Erdogan

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu wa tabaka la kati waliongezeka nchini Uturuki na mamilioni ya watu walitoka kwenye umaskini huku Erdogan akifanikisha mipango mikubwa ya miundombinu.

Pia alifanikiwa kuwashawishi wapiga kura wachache wa Kikurdi katika miaka yake ya kwanza madarakani.

Haki za Wakurdi zilipewa mkazo na baada ya miongo mitatu ya migogoro, mchakato wa amani ulianza Machi 2013, na kusababisha Chama cha Wafanyakazi wa Kurdistan (PKK) kutangaza kusitisha mapigano. .

Lakini makubaliano hayo yalidumu kwa miaka miwili pekee na mzozo ukarejea nchini.

Kufikia 2013, wakosoaji wengi walianza kuonya kwamba Erdogan alikuwa anakuwa kiongozi wa kiimra. Kukaanza kutokea maandamano ya hapa na pale na kupinga mipango ya Serikali.

Erdogan aliamuru kufurushwa kwa waandamanaji kutoka eneo maarufu la Gezi Park na matumizi ya nguvu kupita kiasi ya vikosi vyake yalisababisha wimbi kubwa la hamasa kubwa nchini kote.

Hili liliashiria mabadiliko katika utawala wake. Kulingana na wakosoaji wake, rais alikuwa anaongoza kama sultani wa Dola ya Ottoman kuliko mwanademokrasia.

Kujijenga zaidi na kutengeneza nguvu zake kiutawala

Baada ya muhula wa tatu, Erdogan alilazimika kuachia ngazi kama waziri mkuu kwa sababu hangeweza kuwania muhula mwingine.

Kwa hivyo, alichukua chaguo la kugombea urais katika uchaguzi ambao haujawahi kufanywa.

Kisha akarekebisha katiba na kuiingiza nafasi hiyo mpya ambayo haikuwepo kikatiba, ambayo wakosoaji walikosoa wakisema ingezuiam kuanzishwa kwa nchi isiyo ya kidini.

Lakini mapema katika urais wake, ilibidi akabiliane na matatizo mawili: chama chake kilipoteza wingi wa wabunge kwa miezi kadhaa mwaka 2015, na mwaka uliofuata, Julai 15, nchi hiyo ilishuhudia jaribio lake la kwanza la mapinduzi katika miongo kadhaa.

Takriban watu 300 walipoteza maisha huku kukiwa na majaribio ya kumuondoa Erdogan madarakani.

Erdogan

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan akiwasalimia wafuasi wake wakati wa mkutano wa uchaguzi mjini Manisa nchini Uturuki.

Majaribio hayo ya vuguvugu la Gulen, yaliongozwa na Fethullah Gulen, mhubiri wa Kiislamu anayeishi uhamishoni nchini Marekani.

Wakati huo, historia ya nchi ilibadilika.

Kufuatia jaribio la mapinduzi ya 2016, karibu watumishi wa umma 150,000 walifutwa kazi na watu wengine 50,000 walishikiliwa, wakiwemo wanajeshi wa Kikurdi, wanahabari, wanasheria, maafisa wa polisi na wanasiasa.

Mateso haya ya upinzani au watu walioonekana kupinga utawala wake na mwenendo wake yalisababisha kelele nje ya mipaka ya Uturuki, ambayo ilisababisha kufungiwa kwa uhusiano wake na Umoja wa Ulaya, hivyo kwamba matarajio ya Uturuki kuwa mshirika wa umoja huo haijafanikiwa kwa miaka mingi. .

Na madai ya kuongezeka kwa wahamiaji kupitia Ugiriki yamezidisha hali ya wasiwasi Ulaya dhidi ya nchi hiyo.

Mnamo 2017, Erdogan alishinda kura ya maoni ambayo ilimpa mamlaka makubwa zaidi kama rais, ikiwa ni pamoja na haki ya kuweka hali ya hatari, kuwateua maafisa wa umma na kuingilia kati mfumo wa mahakama.

Siasa za Kimataifa

Wakati wa miongo yake miwili madarakani, Erdogan pia alijijengea jina katika siasa za kimataifa. Alionyesha ushawishi wa Uturuki kama nguvu ya kikanda na diplomasia yake yenye nguvu iliwakasirisha washirika wake huko Ulaya na nchi zingine.

Erdogan

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Erdogan amekuwa na uhusiano mzuri na nchi za Urusi na Iran.

Ingawa alikuwa kiongozi wa nchi ya NATO, Erdogan amedumisha uhusiano wa karibu na Vladimir Putin wa Urusi na amejiweka kama msuluhishi katika vita vya Urusi nchini Ukraine.

Erdogan alisaidia makubaliano ambayo yalifungua njia salama kwa mauzo ya nafaka ya Ukraine katika Bahari Nyeusi na kuzuia kusambaratika kwake wakati Urusi ilipoamua kusitisha mpango huo.

Pia ilizisubirisha Sweden na Finland na matakwa yao ya kujiunga na NATO.

Hatimaye aliidhinisha kuthibitishwa kwa Finland lakini akaizuia Sweden isiingie, akiitaja nchi hiyo kuwa inawahifadhi Wakurdi wanaotaka kujitenga na wapinzani wengine aliowaona kama "magaidi".

Vikwazo vya uchaguzi

Wakosoaji wengi waliona uchaguzi wa serikali za mitaa wa 2019 kama "pigo la kwanza" kwa utawala wa muda mrefu wa Erdogan, chama chake kilishindwa katika miji mitatu mikubwa ya Uturuki: Istanbul; mji mkuu, Ankara; na Izmir.

Erdogan

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, "Uhuru kwa waandishi wa habari waliofungwa": Zaidi ya waandishi wa habari 100 wanashikiliwa na mamlaka

Kupoteza umeya wa Istanbul kwa tofauti kidogo ya kura na Ekrem Imamoglu wa chama cha upinzani cha Republican People's Party (CHP) kulileta pigo kubwa kwa Erdogan, ambaye alikuwa meya wa jiji hilo katika miaka ya 1990.

Imamoglu alitaka kuongeza mafanikio haya kitaifa, kwa kufanya kampeni pamoja na Kemal Kilicdaroglu, mgombea urais wa upinzani aliunganisha vyama vya upinzani dhidi ya Erdogan.

Mojawapo ya changamoto nyingi alizokabiliana nazo Erdogan wakati wa kampeni ni ukosoaji wa serikali kutojitayarisha lakini pia kushughulikia kwa mwendo wa kobe tetemeko la ardhi lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 50,000 Februari mwaka huu na kuwaacha mamilioni ya watu bila makazi nchini Uturuki.

Kingine ni hali mbaya ya kiuchumi, huku mamilioni ya watu wakiteseka kutokana na mzozo wa kupanda kwa gharama za maisha.

Sasa Erdogan ana miaka mitano zaidi mingine ya kujaribu kurekebisha matatizo haya na mengine.