Majimbo tisa ya Marekani ambayo yanaamini Trump 'alitumwa na Mungu' kuwa rais

Muda wa kusoma: Dakika 7

Dakika chache kabla ya ibada ya Jumapili katika Kanisa la Grace Reformed Baptist Church huko Elgin, mji wa takribani watu 2,000 katika jimbo la kusini la Oklahoma, Mchungaji Dusty Deevers, 36, aliyevalia vizuri na kwa tabasamu la kung'aa, anawasalimia waumini mia moja.

Katika ukumbi wa hekalu na kuta zake nyeupe kuna baadhi ya vijitabu vyenye mchoro wa kile kinachoonekana kuwa mtoto asiye na uhai.

“Unaposoma aya hii, watoto watatu wanachinjwa isivyo haki nchini Marekani,” inasomeka, ikirejelea utoaji mimba kuwa “maangamizi makubwa” ya nyakati zetu, suala lenye utata na muhimu katika kampeni kabla ya uchaguzi ujao wa Novemba 5.

Vipeperushi hivi ni kiungo cha wazi kati ya dini na siasa, ambazo zinazidi kuhusishwa kwa sehemu ya wapiga kura nchini Marekani.

Saa 10:45 ibada huanza, huku Deevers akipiga gitaa na kuimba pamoja na waumini, ikifuatiwa na mahubiri yanayotegemea kifungu cha Biblia kutoka katika Injili ya Yohana.

Deevers, seneta mzaliwa wa Elgin na watoto sita, shahada ya uzamili katika dini na biashara ya mali isiyohamishika, anahubiri kutoka kwenye membari siku ya Jumapili na kupendekeza sheria Jumatatu kama seneta katika Capitol ya Oklahoma, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya wabunge wako Republican.

Anawakilisha mambo mawili, kisiasa na kidini ambapo vinawatambulisha viongozi wengi wa eneo hilo.

Mambo mawili kwa pamoja katika ule unaoitwa Ukanda wa Biblia wa Marekani, ambapo Elgin ni mali yake: sehemu kubwa ya nchi yenye imani kali za kidini na kihafidhina ambapo mijadala michache ni nani atashinda kati ya Donald Trump wa Republican, ambaye anajionesha kama kiongozi.

Mprotestanti, na Mwanademokrasia Kamala Harris, mwanamke ambaye alikulia katika nyumba yenye mila ya Kiprotestanti na Kihindu na ambaye ameolewa na Myahudi.

Uko kusini mwa Marekani, Ukanda wa Biblia ni eneo kubwa ambalo linajumuisha takribani majimbo tisa yenye Waprotestanti wengi ambayo Trump alishinda katika uchaguzi uliopita wa urais.

Na kwa hivyo inatarajiwa kutokea tena mnamo Novemba 5.

"Hakuna namna ya kutenganisha Ukristo na siasa"

"Umeionaje ibada?" Deevers ananiuliza, katika jaribio lake la kwanza la kutaka kujua mimi ni nani tunapoketi kuzunguka meza katika ofisi ya kanisa na washiriki wengine.

"Naweza kukuuliza maswali machache kabla ya kuanza mahojiano?" Anasema. “Bila shaka,” ninajibu.

Baada ya mazungumzo marefu kuhusu masuala ya kidini, ananiambia kuwa kwa muda mfupi ajenda yake ya kisiasa inalenga kukomesha uavyaji mimba, kuondoa ponografia na kukomesha ukusanyaji wa kodi ya mapato na mali.

Haya ni mawazo ya kihafidhina ya kidini zaidi, inayozidi kuwa na ushawishi ndani ya Chama cha Republican kinachoongozwa na Trump.

Lakini baada ya muda mrefu, lengo lake ni kubwa zaidi: kugeuza Marekani, ambayo inachukuliwa kuwa nchi ya kwanza isiyo ya kidini katika historia, kuwa taifa la Kikristo.

Na ili kutekeleza dhamira hii, sehemu muhimu ya mkakati ni kushika nyadhifa za kisiasa katika ngazi za juu.

"Je, unataka kugeuza Ikulu kuwa ufalme wa Mungu?" nauliza. "Kila kitu Duniani ni ufalme wa Mungu," anasema.

Maono yake ya kisiasa ni kwamba "miundo ya kiutawala lazima ibadilishwe."

“Tumaini kuu zaidi kwa taifa hili, na mtu bora zaidi wa kujaza pengo la uongozi, ni Kristo,” anaeleza.

Aaron Hoffman, baba wa watoto watano mwenye umri wa miaka 37, anaamini hivyo. Anajitayarisha kuwa mchungaji wa kanisa jipya la Kibaptisti.

Kutenganisha kanisa na serikali, kutoka kwa mtazamo wake, hakuna maana. "Hakuna namna ya kutenganisha Ukristo na siasa," anasema.

Mada hiyo inamgusa sana kiasi machozi yanatiririka mashavuni mwake anapoeleza kwamba Wamarekani wamemwasi Kristo kwa muda mrefu sana, lakini anaonya kwamba bado wanaweza kutubu. Maono yake kwa siku zijazo ni kwamba sheria za nchi zifuate zile za Biblia.

Nikitembea kwenye uwanja wa kanisa Jumapili mnamo mwezi Julai, mmoja wa waumini waliohudhuria ibada, Gina Desmarais, ananiambia kwamba amebarikiwa watoto wanne.

Badala ya kuwapeleka shuleni, anapendelea kuwasomesha nyumbani, ili wafuate maadili ya Kikristo. Na ikiwezekana, angependa kuishi katika nchi inayoongozwa kulingana na mafundisho ya Biblia.

"Huwezi kuwalazimisha watu kuwa Wakristo, huwezi kulazimisha mioyo yao. Lakini sera na sheria zinazofungamana na Maandiko ni nzuri kwa kila mtu, hata wasioamini," anasema kwa sauti ya utulivu sana.

"Trump alitumwa na Mungu"

Kuanzisha makanisa madogo katika jumuiya maskini zaidi, wachungaji wa Bible Belt wana ushawishi mkubwa miongoni mwa waumini, na wengi wanauelekeza kuelekea mrengo wa kihafidhina zaidi wa Chama cha Republican.

Na Trump imekuwa chombo bora kwa kundi hili kufanya maendeleo katika miaka ya hivi karibuni.

Mchungaji na Seneta Dusty Deevers, hata hivyo, anaamini kwamba Trump haendi vile angependa. "Anakielekeza Chama cha Republican," anahoji. Kwa hiyo nikimuuliza atampigia nani kura anasema bado hana uhakika.

Wachungaji wengine wa Oklahoma, kama vile Jackson Lahmeyer na Paul Blair, wanamuunga mkono mgombea wa Republican kwa moyo wote, kama vile idadi kubwa ya watu huko Oklahoma.

"Trump alitumwa na Mungu kutawala nchi hii," anaeleza Lahmeyer, mwanzilishi wa kundi la Pastors4Trump, ambalo lengo lake ni "kuhamasisha kambi ya kupiga kura ya kiinjilisti."

Lahmeyer anaamini kwamba ilikuwa "muujiza wa Kimungu" kwamba rais wa zamani alinusurika jaribio la mauaji katika mkutano wa kisiasa katikati ya Julai. "Tulikuwa hatua moja mbali na vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi yetu."

Aliyekuwa mgombea wa Seneti ya Marekani kutoka Oklahoma (alishindwa katika kinyang'anyiro cha mgombea mwingine wa Republican), Lahmeyer anakataa kutambuliwa kama mzalendo wa Kikristo.

"Hiyo si kitu zaidi ya nembo ambayo vyombo vya habari vimetupa ili kutuonesha kama tishio kwa demokrasia," anasema. "Siyo kweli."

Wala Mchungaji Paul Blair, kiongozi wa Kanisa la Fairview Baptist Church huko Edmond, kitongoji cha Oklahoma City, hajielezei hivyo.

“Samahani kwa mavazi ninayovaa,” anasema Blair aliyevalia kimichezo tunapoelekea ofisini kwake ndani ya kanisa.

Akiwa ameketi kwenye meza yake, mchungaji ananionesha picha za wakati wake kama mchezaji wa kulipwa wa kandanda kwenye safu ya ushambuliaji ya Chicago Bears mwishoni mwa miaka ya 1980.

Leo, Blair hupanga Kambi za Mafunzo ya Wachungaji wa Uhuru, ambapo wanasoma maada kama vile ushawishi wa Kikristo serikalini au utetezi wa uhuru wa raia, ili viongozi wa kidini "wafikirie kibiblia katika nyanja zote za maisha, pamoja na maeneo ya serikali ya kiraia, uchumi, jinsia, kibinadamu, upendo na familia."

Anajipambanua kama "mchungaji mzalendo" na anafikiria kwamba nchi yake inapaswa kurudi kwenye maadili ya wakati wake wa kuanzishwa, wakati Azimio la Uhuru lilitiwa saini mnamo 1776.

“Serikali haiwezi kudhibiti kanisa,” anasema kasisi huyo, ambaye alikuwa mgombea wa useneta Oklahoma.

"Hata hivyo, Wakristo daima wameathiri serikali," anaongeza.

Blair anaamini kwamba Trump alikuwa mshindi halali wa uchaguzi wa 2020 na kwamba wale waliofungwa kwa kuhusuka na shambulio la Capitol mnamo Januari 2021 ni "wafungwa wa kisiasa."

Sasa anatumai kuwa, Novemba 5, Trump, ambaye alishinda Oklahoma kwa 65% ya kura (moja ya kura nyingi zaidi nchini), atakuwa rais wa Marekani kwa mara ya pili.

Trump na uavyaji mimba

Wafuasi wa rais huyo wa zamani wanamshukuru, miongoni mwa mambo mengine, kwa uteuzi wa kihistoria wa majaji watatu katika Mahakama ya Juu katika kipindi chake cha uongozi, na kuhakikisha kuwepo kwa wingi wa wahafidhina katika chombo hicho cha juu zaidi cha mahakama kwa miongo kadhaa.

Kutokana na wingi huu wa wahafidhina, Mahakama Kuu iliondoa mwaka wa 2022 haki ya kutoa mimba ambayo ilikuwa imehakikishwa nchini kwa karibu nusu karne.

Na hilo lilisababisha majimbo ya Bible Belt kama vile Oklahoma na Arkansas kuwa na sheria kali kuhusu uavyaji mimba: Unaweza tu kufanywa ikiwa maisha ya mama yako hatarini.

Katika majimbo mengine, sheria inajumuisha vizuizi vingine, kama vile wakati kijusi hakitarajiwi kuishi, katika kesi ya ubakaji, au ikiwa ujauzito hauzidi wiki sita.

North Carolina ndiyo jimbo pekee katika Beltway linaloruhusu uavyaji mimba hadi miezi mitatu ya ujauzito, ubaguzi ambao Waprotestanti wahafidhina wanaona kuwa haukubaliki.

Utoaji mimba kwa hakika ni moja ya masuala makubwa katika uchaguzi huu, kwa kuwa mrengo wa kihafidhina zaidi wa Chama cha Republican, chenye nguvu zaidi katika Ukanda huo, hauridhiki na kile ambacho kimefikiwa na hata unatetea sheria inayokataza kutolewa kwa mimba kote nchini, jambo ambalo huenda likawezekana iwapo Trump atarejea madarakani.

Licha ya tofauti anazoweza kuwa nazo na Trump, ambaye wengi wanamwona kama mwana uhuru wa New York asiye na maadili ya kidini, tajiri huyo alifungua milango ya Ikulu ya White House kwa viongozi maarufu wa Kiprotestanti wakati wa utawala wake na anaendelea kushiriki katika hafla kubwa na wachungaji wa kiinjili ambao wamempa msaada wao.

Huku karibu 40% ya wakazi wa Marekani wakijitangaza kuwa Waprotestanti, kwa mujibu wa Kituo cha Utafiti cha Pew, Republican wanajaribu kwa bidii kushinda kura za wale ambao hawawezi kuwasamehe Wanademokrasia kwa kuunga mkono kwao uchaguzi huru wa wanawake kuavya mimba, miongoni mwa mambo mengine.

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga