Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kipi kinafuata kwenye vita vya kuavya mimba Marekani?
Idara ya Sheria ya Marekani imekata rufaa dhidi ya uamuzi wa jaji wa Texas wa kusimamisha uidhinishaji wa kidonge cha kutoa mimba cha mifepristone.
Wanasheria wa utawala wa Biden walisema uamuzi wa wiki iliyopita "uliopotoshwa" ulihatarisha afya ya wanawake kwa kuzuia ufikiaji wa kidonge kilichotajwa kwa muda mrefu kama salama.
Jaji wa Texas wiki iliyopita alisitisha uidhinishaji wa dawa hiyo, lakini aliipa serikali siku saba kukata rufaa.
Kikiwa kinatumika katika utoaji mimba mwingi nchini Marekani, kidonge hicho kimeruhusiwa kwa zaidi ya miaka 20.
Vita hivyo huenda vikaelekea katika Mahakama ya Juu, na kuongeza wasi wasi juu ya upatikanaji wa dawa hiyo kwa mamilioni ya wanawake.
Mgogoro huo wa kisheria unaweza kutangaza pigo kubwa zaidi kwa upatikanaji wa utoaji mimba tangu mahakama kuu ya nchi hiyo majira ya joto yaliyopita kuamua kuwa hakuna haki ya kuavya mimba nchini kote.
Kwa sasa, kidonge bado kinapatikana.
Siku ya Jumatatu, idara ya haki iliwasilisha hoja ya dharura, ikitaka kuzuia kwa muda uamuzi wa Ijumaa iliyopita huko Amarillo, Texas.
Mawakili wa utawala wa Biden wameomba uamuzi kufikia tarehe 13 Aprili - siku moja kabla ya uamuzi wa mahakama ya chini kuanza kutekelezwa.
Serikali ilisema uamuzi wa Texas "haufai" kwa sababu ungebadilisha uamuzi wa kisayansi wa Utawala wa Chakula na Dawa (FDA), ambao unaidhinisha dawa nchini Marekani.
Hoja ya serikali, ikiwa itafaulu, itahifadhi idhini ya mifepristone hadi rufaa isikizwe mbele ya Mahakama ya Rufaa ya Mzunguko wa Tano.
Iwapo idara ya haki haitashinda hoja hii ya dharura, mawakili wake watapeleka kesi hiyo kwenye Mahakama Kuu inayotawaliwa na wahafidhina ndani ya saa chache, wataalam wa sheria wanatabiri.
Mifepristone ni sehemu ya dawa mbili zinazosababisha uavyaji mimba.
Kidonge hiki huzuia mimba kwa ufanisi, wakati dawa ya pili, misoprostol, huondoa mfuko wa uzazi.
Alliance Defending Freedom, kikundi cha utetezi wa kisheria cha Kikristo cha kihafidhina ambacho kiliwakilisha walalamikaji katika kesi ya Texas, kilisema kuwa FDA katika mchakato wake wa kuidhinisha wa miaka minne ilipuuza athari zinazoweza kujitokeza za mifepristone kwa miili inayoendelea ya wasichana wanaobalehe.
Wakili wake mkuu, Erin Hawley, alisema Jumatatu: "Kwa kuidhinisha kinyume cha sheria dawa hatari za kuavya mimba za kemikali, na kuweka utaratibu wake wa uavyaji mimba kwa njia ya barua, FDA iliweka wanawake katika hatari, na shirika hilo linapaswa kuwajibika kwa vitendo vyake vya kutojali.
"Mimba sio ugonjwa, na dawa za kutoa mimba kwa kemikali hazitoi faida ya matibabu."
Mashirika makuu ya matibabu kama vile Chuo cha Marekani cha Madaktari wa uzazi na Wanajinakolojia na Shirika la Afya Ulimwenguni wanasema mifepristone ni salama na inafaa.
Uamuzi wa Ijumaa wa Jaji Matthew Kacsmaryk huko Texas ulitangaza idhini ya FDA ya mifepristone mwaka 2000 kuwa batili.
Katika maoni ya kurasa 67, aliyeteuliwa na Trump alisema FDA ilikiuka sheria za shirikisho zinazoruhusu uidhinishaji wa haraka wa dawa fulani.
Lakini dakika 18 tu baada ya uamuzi wa Texas, jaji mwingine wa shirikisho, huyu aliyeteuliwa na Obama katika jimbo la Washington, aliamuru kwamba ufikiaji wa mifepristone uhifadhiwe katika majimbo 17 ya kiliberali.
William Eskridge, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Yale, aliiambia BBC: "Agizo la kesi ya Washington linatumika kwa majimbo 17, na amri ya kesi ya Texas inatumika kwa majimbo 50.
"Hilo linaweka shinikizo kubwa kwa Mahakama ya Juu kufanya mapitio [ya kesi] mapema badala ya baadaye."
Siku ya Jumatatu, zaidi ya wasimamizi 300 wa dawa, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Pfizer Albert Bourla, walitoa wito wa kubatilishwa kwa uamuzi wa Texas, wakisema ni "uamuzi wa kupuuza sayansi".