Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Siku ya Utoaji Mimba Salama: Wanawake wakieleza waliyoyapitia walipoavya mimba
Utoaji mimba uhalalishwe? Ni swali ambalo limeendela kuibua mijadala duniani kote
Katika jimbo la Texas Marekani, sheria inayokataza utoaji mimba iliyofikisha wiki sita (mwezi mmoja na wiki mbili) imeanza kutumika au kufanya kazi mwezi huu. Kwa upande mwingine, Mexico hivi karibuni imeondoa kwenye makosa ya uhalifu huko kaskazini mwa jimbo la Coahuila.
"Ukweli ni kwamba suala la utoaji mimba wakati wote limekuwa tata," anasema Anu Kumar, rais na mtendaji mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu lililopo Marekani la Ipas.
Lakini anaamini kwamba mambo yanaenda katika muelekeo sahihi. "Tangu mwaka 1994, zaidi ya nchi 40 zimefanyia marekebisho sheria zao kuhusu utoaji mimba," aliongeza.
Siku ya kimataifa utoaji mimba salama, tumewauliza wanawake watano kueleza mikasa yao ya kuavya mimba. Wanatokea maeneo mbalimbali duniani, baadhi wametaka tufiche utambulisho wao.
'Nilitoa nilipogundua aliyenipa ujauzito simuhitaji awe baba wa mtoto wangu' - Sandra, kutoka Bangkok
Sandra alianza kugundua mabadiliko katika mwili wake wiki nane baada ya kupata mimba. Alipima na kugundulika ana mimba.
"Nilipogundua tu simuhitaji mtu huyu awe baba wa watoto wangu," Sandra aliiambia BBC. "Alikua 'mpenda ngono', na nilikuwa bado sijafikia ndoto yangu."
Alikuwa anajua kuhusu kikundi cha Tamtang huko Thailand, ambacho kilikuwa kinaelimisha jamii kuhusu utoaji salama wa mimba, akawafuata kuomba msaada.
Wakati huo utoaji mimba Thailand ilikuwa kosa kisheria isipokuwa kama imetokana na kitendo cha ubakaji au tatizo la kiafya la mama. Sandra aliamua kutoa mimba mwaka 2019 wakati huo bado sheria hiyo inafanya kazi.
"Nilikuwa njia panda- je niwaambie kwamba nilinyanyaswa kingono, au ningeonekana kituko kusema siwezi kumudu? Nilikuwa na mawazo lukuki kichwani kwangu, anasema.
"Nilijiambia mwenyewe kwamba kila kitu kilikuwa sawa mpaka siku moja nilipoota ujumbe wa matusi katika mitandao ya kijamii kupinga utoaji mimba ."
Anamatumaini siku moja wanawake wataweza kurejeshewa uhuru wa miili yao. "Kwa sababu hata sheria ziweje, bado kuna unyanyapaa mwingi unaodhibiti uhuru wetu"
'Tunavyozidi kujitokeza kuzungumza kuhusu utoaji mimba, ndivyo jamii itakavyokuwa imara' - Erin, Marekani
Erin alitoa mimba kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 28, na mimba ya hivi karibuni kutoa alitoa akiwa na miaka 36. "Nimekuwa nikiwaza kwamba nilikuwa nakengeuka kwa kutoa mimba mara nyingi," ameiambia BBC.
"Hata hivyo, katika majukumu yangu ya sasa kama mwanaharakati kuhusu utoaji wa mimba, nimejifunza kwamba utoaji mimba ni jambo la kawaida."
Lakini utoaji mimba mara nyingi hakujapunguza aibu ya uamuzi wake wa kutoa mimba "Natumai hili litabadilika muda mfupi ujao."
Kampeni za Erin kuhusu haki za uzazi anafanya akiwa na shirika linaloitwa Shout Your Abortion. Inamsaidia kupaza zaidi sauti kuhusu uzoefu wake wa utoaji mimba.
"Imekuwa hatua kubwa, tangu nianze kufanya kazi hii, ilikuwa inanipa shida hata kutamka tu kwa sauti neno utoaji mimba," Anasema. "Leo imekuwa kawaida na rahisi kwangu kuzungumzia wazi kuhusu utoaji mimba."
'Aibu ilinifanya nihisi kutengwa na jamii' - Indu, India
"Nilikuwa na umri wa miaka 31 na nilikuwa nimepoteza simu yangu," Indu anaiambia BBC. "Nilienda kununua simu mpya, nilianza kusikia kichefuchefu. Mpenzi wangu akashauri nikapime ujauzito".
Alipopimwa alikutwa na mimba, na alitaka kuitoa. "Ndio kwanza nilikua naanza kazi, mpenzi wangu pia aliniunga mkono."
Alienda kwa mtaalamu wa masuala ya uzazi akafanikiwa kutoa kirahisi mimba hiyo kwa kutumia vidonge, lakini baada ya zoezi hilo kasheshe likaanza.
"Nilitokwa damu sana na kujisikia kichefuchefu zaidi, niliogopa. Nililia sana kama roho inataka kutoka."
Nchini India utoaji mimba ni jambo lisilozungumzwa huku wanawake wakisikika kwa uchache kupigia kelele suala hilo', kama ilivyoripotiwa na IndiaSpend mwezi Septemba 2020.
"Nilishikwa na hasira kupitia masahibu yale kimwili na kiakili, ingawa ilituhusu watu wawili," Anasema Indu. "Chini ya kipindi cha mwaka mmoja baadae nilianza kutumia dawa za kuondoa msongo wa mawazo."
Anasema iliathiri uhusiano wake, na kwa muda mrefu aliogopa kushiri mapenzi. Ilinifanya nigundue kuwa kuna umuhimu wa mtu kupata msaada wa kihisia.
"Nikifikiria huko nyuma, nahisi kama ningekuwa na nafasi ya kuzungumzia utoaji mimba kwa uwazi zaidi, nadhani mambo yangekuwa tofauti."
'Utoaji mimba unachukuliwa kama dhambi katika jamii' - Jocelyne, DRC
Jocelyne alijifungua mtoto wake wa pili miezi minne iliyopita. "Nilianza kuonyesha dalili za maziwa kuvimba, kukosa hamu ya kula na uchovu," anasema.
Muda mfupi baadaye akagundua kwamba ana mimba na aliamua kuitoa. "Wakati wa kuanza mchakato huu afya ya mtoto wangu ni kipaumbele cha kwanza. Kulikuwa kuna hofu kuhusu madhila ya dawa za utoaji mimba , lakini nilivuka kwa msaada wa mume wangu."
Anasema hakuwahi kumsikia mtu akizungumzia utoaji mimba katika jamii. "Kutoa mimba hapa ni jambo la siri mno na linachukuliwa kama dhambi kwenye jamii," anasema. "Mtu anayetoa mimba atafungiwa ndani kama watu watajua kuhusu alichofanya."
'Ndoto yangu ni kuona siku moja wanawake wanakuwa huru' - Maria, Mexico
Maria akiwa na miaka 35 alikuwa anataka kutoa mimba, lakini alikulia katika mazingira ambayo kutoa mimba kunaonekana kama uuaji, kilikuwa kitu cha hatari sana'.
Lakini mambo yalikuwa tofauti alipokutana na daktari. Daktari alimfahamisha na kumuelekeza kuhusu mchakato wa kutoa mimbaulivyo," anasema.
"Kamwe hakuwahi kunihoji, kunikaripia, ama kunichukulia kama mtu ninayekwepa wajibu au majukumu. Hapo ndipo nilipoelewa uzito wa unyanyapaa kuzunguka suala hili la utoaji mimba."
Anasema huduma za utoaji mimba salama ni ngumu kupatikana, licha ya ukweli kwamba ni halali kisheria katika mji wa Mexico City.
"Ni kitu kinachochukua kama dakika 30 au pengine chini ya hapo," anasema.
"Ilikuwa ngumu kwa mimi kuamini kwamba katika kipindi cha muda mfupi, kila kitu kimekuwa sawa."
Akiwa na miaka sasa 38, anasema asingependa kuzaa. "
"Natamani siku moja wanawake wawe huru kabisa kuchagua na kuamua kuhusu maisha yetu, hasa yanayohusu masuala ya miili yetu. Natumaini siku moja, ndoto hii itageuka kuwa kweli, na itavuka mipaka."