Mbivu na mbichi ya Profesa Janabi katika uchaguzi wa Mkurugenzi wa WHO Afrika

Uchaguzi wa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unafanyika Mei 18 huko Geneva Uswisi.
Mataifa wanachama wanapiga kura katika kikao cha pili maalum cha kamati ya kikanda ya shirika hilo, kumchagua mkurugenzi mpya wa WHO Afrika .
Mshindi anakuja kuiziba nafasi ya aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa Kanda hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, waziri wa wa zamani wa afya Tanzania, aliyefariki ghafla Novemba 2024.
Janabi ni mmoja wa wataalamu wakubwa wa afya nchini Tanzania, akiwa pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
Mkurugenzi wa Kanda anachaguliwa kwa kura ya siri katika kikao cha ndani cha Kamati ya Kanda ya WHO kwa Afrika, ambayo ilikutana Januari 14, 2025, na kuamua kutumia utaratibu wa haraka, kumpata Mkurugenzi wa Kanda badala ya mchakato wa kawaida ambayo huchukua muda mrefu.
Mkurugenzi huyo anatarajiwa kuhudumu kwa kipindi cha miaka mitano na ana fursa ya kuchaguliwa tena upya mara moja pekee baada ya kuhudumu awamu ya kwanza.
Kwa mgombea atakayechaguliwa katika wadhifa huo, atakuwa na jukumu muhimu la kuunda sera za afya, kuratibu huduma za dharura na kushinikiza suluhu mpya za afya kote barani Afrika.
Ujumbe wa serikali ya Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Afya Jenista Mhagama, unaendeleza kampeni za kumnadi Prof Janabi, huko Uswisi.
Wapinzani wa Prof. Janabi wanaowania Ukurugenzi WHO
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wagombea nafasi hiyo ni pamoja na Moustafa Mijiyawa (Togo), Dk. N'Da Konan Michel Yao, (Ivory Coast), Mohamed Lamine Dramé, (Guinea) na Prof. Mohamed Janabi (Tanzania).
Moustafa Mijiyawa kutoka Togo alikuwa Waziri wa Afya wa Togo, ambaye anaonekana tishio zaidi kwa Prof Janadi kwenye nafasi hiyo ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Mijiyawa alikuwa Waziri kuanzia 2015 hadi 2024 na amekuwa daktari wa magonjwa ya baridi yabisi kwa zaidi ya miaka 30, akifanya kazi nchini kwake Togo na nje ya nchi. Kazi yake ni pamoja na majukumu katika elimu ya matibabu, physiotherapy na orthosis.
Dk. N'Da Konan Michel Yao, kutoka Ivory Coast ni mtafiti mashuhuri na msomi anayejulikana kwa mchango wake mkubwa kwenye afya ya umma, haswa katika muktadha wa magonjwa ya kuambukiza barani Afrika. Utaalam wake unatiliwa mkazo na ushirikiano wake kwenye shughuli za mashirika mashuhuri, likiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), ambako alihudumu katika makao makuu nchini Uswizi na Ofisi ya Kanda ya Afrika nchini Kongo.
Mohamed Lamine Dramé, kutoka Guinea ana uzoefu mkubwa wa kliniki na uzoefu wa muda mrefu wa usimamizi na afya ya umma iliyoandaliwa kwanza katika nchi yake (Jamhuri ya Guinea). Kisha alifanya kazi na kukusanya uzoefu wa miaka ishirini na moja kama mtaalam mkuu katika ushirikiano wa maendeleo ya kimataifa na taasisi za kimataifa (WHO/Geneva) na mashirika ya nchi mbili (Ushirikiano wa Ujerumani - GIZ & Ushirikiano wa Ubelgiji - Wezesha). Alishirikiana na wachezaji wakuu wa Global Health kama GAVI, GFAMT na WB.














