Taiwan yaongeza muda wa kuhudumu katika jeshi kwa lazima hadi mwaka mmoja

th

Chanzo cha picha, Getty Images

Taiwan itaongeza huduma ya lazima ya kijeshi kutoka miezi minne hadi mwaka mmoja, Rais Tsai Ing-wen amesema.

Uamuzi huo unakuja huku kukiwa na mvutano unaoongezeka na China, ambayo inadai kisiwa hicho kinachojitawala kama eneo lake.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumanne, Rais Tsai alitangaza mipango mipya ya kuimarisha ulinzi wa Taiwan iwapo kutatokea shambulio kutoka Beijing.

"Amani haitashuka kutoka angani... Taiwan iko mstari wa mbele kupinga upanuzi wa kimabavu," alisema. 

Rais Tsai alisema walioandikishwa kujiunga na jeshi pia watapitia mafunzo makali zaidi, wakichukua baadhi ya vipengele kutoka Marekani na wanajeshi wengine wa hali ya juu. Aliongeza kuwa mfumo wa ulinzi wa sasa wa kisiwa hicho hautoshi kukabiliana na uchokozi kutoka kwa China, ambayo ina moja ya idadi kubwa ya wanajeshi na wenye uwezo wa hali ya juu zaidi duniani. 

Jeshi la Taiwan limepungua tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakati wanaume wote wenye umri wa zaidi ya miaka 18 walitakiwa kuhudumu katika jeshi kwa hadi miaka mitatu. Katika miongo michache iliyofuata, huduma ilifupishwa hadi mwaka mmoja na miezi 10 kabla ya kupunguzwa zaidi hadi miezi minne. Sheria hiyo mpya itaanza kutumika Januari 2024 - mwezi huo huo Taiwan itamchagua rais wake mpya 

"Huu ni uamuzi mgumu sana, lakini kama rais, kama mkuu wa vikosi vya kijeshi, ni jukumu langu lisiloweza kuepukika kutetea masilahi ya kitaifa na mfumo wetu wa maisha wa kidemokrasia," Rais Tsai alisema.

"Hakuna mtu anayetaka vita, watu wa Taiwan na Taiwan ni sawa, na jumuiya ya kimataifa ni sawa," alisema, na kuongeza "uchokozi wa kijeshi wa China umezidi kuwa wazi baada ya mazoezi yake ya kivita mwezi Agosti."

th

Chanzo cha picha, Reuters

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mvutano kati ya Taipei na Beijing uliongezeka mwezi Agosti kufuatia ziara ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.

Beijing ilijibu kwa kufanya mazoezi yake makubwa zaidi ya kijeshi katika bahari karibu na Taiwan. Taipei aliita mazoezi hayo "ya uchochezi sana".

Mwezi Oktoba, Rais Xi Jinping wa China hakukataza matumizi ya nguvu kuungana na Taiwan katika hotuba yake ya ufunguzi katika Kongamano la chama cha Kikomunisti mjini Beijing. Baadaye wiki hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alisema China inafuatilia kuungana na Taiwan "kwa muda wa kasi zaidi" kuliko ilivyotarajiwa hapo awali.

Taiwan pia imekuwa katikati ya uhusiano wa Marekani na China kutokana na uhusiano wa karibu wa kisiwa hicho na Washington.

Iliaminika kuwa jambo kuu la mjadala wakati Bw Xi alipokutana na Rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano wa kilele wa G20 mwezi Novemba. Kufuatia mkutano huo, Bw Biden alisema haamini kwamba China ingeivamia Taiwan.

Lakini hali ya wasiwasi iliongezeka tena siku ya Jumatatu wakati Taiwan iliporipoti mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya Wachina kuzunguka kisiwa hicho, huku ndege 71 za jeshi la anga za China, zikiwemo ndege za kivita na ndege zisizo na rubani, zikiingia katika eneo linalojulikana kama kitambulisho cha ulinzi wa anga.