Jinsi kituo cha nyuklia cha Zaporizhia kinavyotofautiana na kile cha Chernobyl

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika siku za hivi karibuni, zaidi ya milipuko kumi na mbili imetikisa vituo vya Zaporizhia, kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya, kilichoko kusini mashariki mwa Ukraine na chini ya udhibiti wa Urusi tangu mwanzo wa uvamizi.
Urusi na Ukraine zimeshutumiwa kwa shambulio hilo la bomu.
Shirika la Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) limeeleza mara kwa mara wasiwasi wake kuhusu mashambulizi dhidi ya mtambo huo na kupendekeza kuanzishwa kwa eneo la usalama wa nyuklia kukizunguka.
Kulipua kinu cha nyuklia kumefanywa kama "mchezo wa kuigiza", Olli Heinonen, naibu mkurugenzi mkuu wa zamani wa IAEA, aliiambia BBC.
"Kombora moja katika eneo lisilofaa kwa wakati usiofaa litakuwa na athari kubwa", alionya afisa huyo wa zamani katika shirika la Umoja wa Mataifa la kufuatilia masuala ya nyuklia.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kombora moja haiwezekani kusababisha uharibifu kwenye kinu chenyewe, ambacho kinalindwa kwa kujengewa saruji na chuma umbali wa mita kadhaa.
Hatari, anasema, ni kwamba mlipuko huo wa mabomu ungekata umeme kwa mfumo wa kupoeza, ambayo ingemaanisha kinu au mafuta yaliyotumiwa yangepata moto sana, na kusababisha mafuta kuyeyuka na kutolewa kwa mionzi.
Zaidi ni kwamba wafanyakazi "wanaweza kufanya makosa" kutokana na shinikizo lao, ikiwa wana uwezo wa kuuendesha.
"Ni mchezo hatari na lazima usitishwe," Heinonen aliongeza.
"Habari kutoka kwa timu yetu zinatia wasiwasi sana," alisema Rafael Grossi, mkuu wa IAEA, ambaye wafanyakazi wake walisema kumekuwa na uharibifu wa baadhi ya majengo, mifumo na vifaa kwenye kiwanda hicho.
"Kumekuwa na milipuko kwenye eneo la kinu hiki kikubwa cha nguvu za nyuklia, jambo ambalo halikubaliki kabisa. Yeyote aliye nyuma ya hili lazima aache mara moja. Kama nilivyosema mara nyingi, wanacheza na moto," aliongeza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiwanda kikubwa zaidi barani Ulaya
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kiwanda cha Nguvu za Nyuklia cha Zaporizhia, kilichojengwa kati ya 1984 na 1995, ndio mtambo mkubwa zaidi wa nyuklia barani Ulaya na wa tisa kwa ukubwa duniani.
Kina vinu 6, kila kimoja kikitoa 950MW, na kuzalisha 5,700MW, nguvu ya kutosha kwa baadhi ya nyumba milioni 4.
Kulingana na IAEA, katika nyakati za kawaida mtambo huo huzalisha takriban 20% ya umeme wa Ukraine na karibu nusu ya nishati inayotokana na mitambo ya nyuklia ya nchi hiyo.
Kiwanda hicho kiko kusini mashariki mwa Ukraine, huko Enerhodar, kwenye ukingo wa hifadhi ya Kakhovka, kwenye Mto Dnieper.
Ni takriban kilomita 200 kutoka eneo lenye mgogoro la Donbas na kilomita 550 kusini mashariki mwa Kyiv.
Umuhimu wa mtambo huo ulisababisha Urusi kuuchukua mnamo Machi, mwanzoni mwa vita.
Tangu wakati huo, pande zote mbili zimeshutumu kila mmoja kwa milipuko ya mara kwa mara.
Moscow ilibakisha mafundi wa Ukraine kuendesha kituo hicho.
Mnamo Agosti, mtambo huo ulikatwa kwa muda kutoka kwa gridi ya umeme ya Ukraine kwa mara ya kwanza katika historia yake, wakati ambapo moto uliathiri mara mbili njia yake ya mwisho ya umeme ya kilovolti 750.
Wataalamu wa nyuklia wa Umoja wa Mataifa walifanya ukaguzi wao wa kwanza katika mtambo huo mnamo Septemba, wakifuatana na wanajeshi wa Urusi, na kugundua kwamba uadilifu wa mtambo huo "umekiukwa mara kadhaa".
Tofauti na mtambo wa nyuklia wa Chernobyl
Baadhi ya wachambuzi wanasema mtambo wa Zaporizhia ni tofauti na salama kuliko ule wa Chernobyl ambao ulikuwa angalizo baada ya kutokea kwa ajali mabaya zaidi ya nyuklia duniani mwaka wa 1986.
Vinu sita huko Zaporizhia, tofauti na Chernobyl, ni mitambo ya maji yenye shinikizo (PWRs) na una miundo ya kuzuia maafa karibu nao ili kusitisha kutolewa kwa mionzi.
"Zaporizhia ulijengwa katika miaka ya 1980, hivyo ni ya kisasa," anasema Mark Wenman, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Udaktari katika Mustakabali wa Nishati ya Nyuklia.
"Ina jengo imara kabisa. Unene wa 1.75m, saruji iliyoimarishwa sana yenye uwezo wa kuhimili tetemeko la ardhi na inachukua muda mwingi ndio livunjike".
Anakataa kulinganisha ajali ya Chernobyl mwaka wa 1986 au ile ya Fukushima mwaka wa 2011.
Chernobyl ilikuwa na dosari kubwa za ubunifu wake, anaelezea, wakati huko Fukushima jenereta za dizeli zilijaa sana, kitu ambacho anaamini kuwa hakiwezi kutokea Ukraine, kwa kuwa jenereta ziko ndani ya jengo la kontena.
Mtambo wa Zaporizhia pia hauna grafiti kwenye kinu chake.
Huko Chernobyl, grafiti ilisababisha moto mkubwa na ilikuwa chanzo cha bomba la mionzi iliyosafiri kote Ulaya.
Kwa kuongeza, mitambo ya PWR pia ina mifumo ya ulinzi wa moto iliyojengwa.
Baada ya ajali ya 9/11, vinu vya nguvu za nyuklia vilijaribiwa kwa mashambulio yanayoweza kutokea na ndege kubwa na kupatikana kuwa salama kwa kiasi kikubwa, kwa hivyo uharibifu wa jengo la kontena la kinu hauwezi kuwa hatari kubwa zaidi.

Chanzo cha picha, Reuters
Hatari ya usambazaji wa umeme
Kinachotia wasiwasi zaidi ni kupotea kwa usambazaji wa umeme kwa vinu vya nyuklia.
Hilo likitokea na jenereta za dizeli zilizotayari zikishindwa kufanya kazi, kutakuwa na hasara wa kipozea.
Bila umeme wa kuwasha pampu karibu na msingi wa kiyeyusho cha moto, mafuta yangeanza kuyeyuka.
Kiwanda hicho kilikatwa kwa muda kutoka kwa gridi ya taifa ya Ukraine mnamo Agosti 25, wakati moto ulipotokea mara mbili kwenye njia yake ya mwisho ya umeme ya kilovolti 750.
Vinu vingine vitatu viliondolewa kwa utendaji wake wa kazi.
Katika kesi hiyo, umeme ulisambazwa kupitia laini isio na nguvu kutoka kwa kituo cha karibu cha makaa ya mawe, na kwa mujibu wa mamlaka, jenereta za dizeli pia zilitumiwa.
Hata hivyo, shirika la nyuklia la Ukraine linadai kuwa jenereta si suluhisho la muda mrefu na kwamba ikiwa njia ya mwisho ya umeme katika gridi ya taifa itakatika, mafuta ya nyuklia yanaweza kuanza kuyeyuka, "na kusababisha kutolewa kwa dutu zenye mionzi."
Kushindwa kwa pampu na jenereta kunaweza kusababisha joto kupita kiasi kwa msingi wa kinu na uharibifu wa kiwanda cha umeme.
"Hiyo haitakuwa mbaya kama ajali ya Chernobyl, lakini bado inaweza kusababisha kutolewa kwa mionzi na hiyo inategemea ni njia gani upepo unavuma,” asema Claire Corkhill, profesa wa uharibifu wa nyenzo za nyuklia katika Chuo Kikuu cha Sheffield.
Kwake, hatari ya kutokea kitu kibaya ni halisi, na Urusi ingefichuliwa kama Ulaya ya Kati.
Profesa Iztok Tiselj, wa uhandisi wa nyuklia katika Chuo Kikuu cha Ljubljana (Slovenia), anaamini kwamba hatari ya tukio kubwa la mionzi ni ndogo, kwani ni vinu viwili tu kati ya sita vinavyofanya kazi.
"Kwa mtazamo wa raia wa Ulaya hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi," anasema.
Vinu vingine vinne viko katika hali ya kuzimwa yaani viko baridi, kwa hivyo kiasi cha nishati kinachohitajika kupoza vinu ni kidogo.
Sababu za kibinadamu
Hatari nyingine kubwa ya usalama inaweza kutoka kwa mafuta yaliyotumika katoka mtambo wa Zaporizhia.
Mara baada ya mafuta kuisha, taka hupozwa kwenye madimbwi ya mafuta yaliyotumika na kisha kuhamishiwa kwenye hifadhi kavu.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Ikiwa zitaharibiwa, mionzi ingetoka, lakini madhara yake hayangekuwa makubwa sana kama vipoozeo kushindwa kufanya kazi," anasema Profesa Corkhill.
Katikati ya mgogoro huu ni wafanyakazi wa mtamboni wanaofanya kazi chini ya Urusi na chini ya shida nyingi.
Wafanyakazi wawili wameiambia BBC kuhusu hatari ya kila siku ya kutekwa nyara.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa Urusi kuondoa wanajeshi wake na kufanya eneo hilo kuwa "salama kwa kila mmoja na lisilo na vita".
Hata hivyo, Urusi imekataa ikisema kuwa hii itafanya mtambo huo kuwa hatarini zaidi.
Wafanyikazi wameonywa juu ya maafa ambayo yangetokea ikiwa Urusi itajaribu kuzima mtambo wote ili kukata umeme kutoka Ukraine na kuunganisha tena na rai ya Crimea inayokaliwa na Urusi.
Mark Wenman anaamini kwamba ni sababu ya kibinadamu ambayo inaleta hatari kubwa zaidi ya ajali ya nyuklia, iwe kutokana na uchovu wa kila siku au msongo wa mawazo, "na hiyo inakiuka kanuni zote za usalama".
Katika barua iliyotiwa saini na wafanyakazi kadhaa, wanatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutafakari: onasema, "Tunaweza kudhibiti kitaalamu utengano wa nyuklia lakini hatuna ulinzi dhidi ya kutowajibika na wazimu wa watu."















