Uchaguzi wa Nigeria 2023: Je madai yanatolewa na wagombea ni ya kweli?

Chanzo cha picha, Getty Images
Huku uchaguzi wa urais nchini Nigeria ukikaribia, wagombea wanaotaka kuchukua nafasi ya Rais Muhammadu Buhari wamekuwa wakitoa madai kuhusu masuala muhimu.
Tumeangazia na kutathmini kauli za Bola Ahmed Tinubu kutoka chama tawala cha All Progressive Congress (APC), pamoja na wanasiasa wa upinzani Atiku Abubakar kutoka chama cha Peoples
Peter Obi: 'Wakati kiwango cha umaskini nchini India ni karibu 16%, kile cha Nigeria ni takriban 63%... kinaainishwa kama maskini wa pande nyingi'

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Obi amechukua data kutoka kwa vyanzo viwili tofauti wakati akitoa dai hili.
Idadi ya India (16.4%) imechukuliwa kutoka Global Multidimensional Poverty Index, iliyotolewa mwaka wa 2022 kwa kuungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Mpango wa Oxford Poverty and Human Development Initiative (OPHI).
Inatathmini umaskini katika zaidi ya nchi 100 zinazoendelea, ikiangalia viashiria 10 vinavyohusu afya, elimu na viwango vya maisha.
Ingawa takwimu za India ni sahihi, katika ripoti hii idadi iliyotolewa kwa Nigeria ni 46.4% - sio 63% iliyotajwa na Bw Obi.
Idadi hiyo imetokana na utafiti tofauti - utafiti wa kitaifa unaojulikana kama Utafiti wa Umaskini wa Multidimensional Nigeria (pia ulitolewa mwaka jana).
Licha ya jina sawa na hilo, si sawa na utafiti wa kimataifa, na itakuwa ni kupotosha kutumia taarifa kutoka kwa tafiti hizo mbili pamoja, kulingana na Prof Sabina Alkire, mkuu wa Oxford Poverty and Human Development Initiative (OPHI).

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kipimo cha kitaifa ni mahususi kwa kuangazia umaskini katika nchi na mara nyingi hufikiwa kulingana na hali ya kila nchi na kwa Nigeria, ina viashirio vya ziada ambavyo havijajumuishwa katika utafiti wa kimataifa, anaongeza Prof Alkire.
Na pia tunahitaji kufahamu kuwa data kutoka kwa utafiti wa kimataifa ni ya miaka tofauti - takwimu za Nigeria ni za 2018 na za India kutoka 2019-21.
Hii inazua maswali zaidi kuhusu kama ni ulinganisho halali, kwa kuwa data ya Nigeria inatanguliza janga la Covid.
Watafiti wa Benki ya Dunia wanaeleza kuwa kutathmini mwelekeo wa umaskini nchini Nigeria kwa muda mrefu imekuwa vigumu kutokana na kubadilika kwa mbinu za kupima kipimo hicho.
Bw Obi pia amedai Nigeria "imeipiku India kama makao ya kundi kubwa la watu maskini kabisa duniani".
Kipicho cha Umaskini Duniani, ambacho inafuatilia maendeleo yaliyofanywa na nchi katika kumaliza umaskini uliokithiri, ilionyesha kwa mara ya kwanza Nigeria ilikuwa mbele ya India kwa watu wanaoishi katika umaskini uliokithiri mwaka 2018.
Makadirio ya hivi punde ni kwamba Nigeria ina watu milioni 71 katika umaskini uliokithiri (wanaoishi chini ya dola 1.90 kwa siku) ikilinganishwa na watu milioni 44 kutoka nchini India.
Atiku Abubakar: 'Katika miaka mitano tu kati ya 2015 na 2020, idadi ya watu walioajiriwa kikamilifu ilipungua kwa 54% - kutoka milioni 68 hadi watu milioni 31'

Chanzo cha picha, Getty Images
Bw Atiku Abubakar wa chama cha upinzani cha PDP, ambaye alikuwa makamu wa rais kutoka 1999 hadi 2007, alisema hayo mwezi Januari.
Yuko sahihi kuhusu idadi ya wale walioainishwa kama walioajiriwa kikamilifu mnamo 2020, kulingana na data rasmi.
Lakini takwimu yake ya 2015 pia inajumuisha wale waliofafanuliwa kama wasio na ajira - ambao wanafanya kazi kwa saa chache kuliko ambavyo wangependa, au kufanya kazi bila kutumia ujuzi wao kikamilifu.
Mnamo mwaka wa 2015, kulikuwa na watu milioni 55 walioajiriwa kikamilifu kulingana na Ripoti ya Serikali ya Ukosefu wa Ajira/ Kufanya kazi Zisizotosheleza”, ambayo ingemaanisha kuwa takwimu sahihi za kushuka kwa ajira ni 44%.
Bola Tinubu: '[Ukosefu wa usalama] kwa kweli umepungua... [tulikuwa] na bendera za wanajihadi wa kigeni nchini Nigeria, hilo halipo tena'

Chanzo cha picha, Getty Images
Ukosefu wa usalama umekuwa suala kuu uchaguzi huu, haswa vita dhidi ya vikundi vya wapiganaji wa Kiislamu kama Boko Haram.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na BBC, Bw Tinubu, wa chama tawala cha All Progressive Congress (APC), alitaka kutetea rekodi ya rais wa sasa, Muhammadu Buhari, ambaye ni kiongozi wa chama chake.
Alidai wanajihadi wa kigeni wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika majimbo manne wakati Bw Buhari alipochukua hatamu mwaka wa 2015 na kwamba sio hivyo tena.
"Hilo limepita kitambo," alisema.
Kundi la Boko Haram kwa hakika limedhoofishwa na limesukumwa nje ya eneo mengi lililokuwa likidhibiti hapo awali, lakini makundi mengine yameimarika zaidi katika kipindi hiki, miongoni mwao ni Islamic State West Africa Province (Iswap), ambalo lilijitenga na Boko Haram.
David Malet, kutoka Chuo Kikuu cha Marekani huko Washington DC, ambaye amekuwa akitafiti wapiganaji wa kigeni tangu mwaka 2005, anasema ni vigumu kusema ni makundi mangapi yaliopo nchini Nigeria, lakini anasema bado ni tatizo.
"Pamoja na usajili uliofanywa na Islamic State, kwa hakika kuna makundi mengi zaidi leo katika nchi jirani katika kanda, hivyo kuna uwezekano kuna wengi zaidi nchini Nigeria pia," aliiambia BBC.
Serikali pia inakabiliwa na changamoto nyingine zinazohusiana na usalama - miongoni mwao ujambazi, utekaji nyara na migogoro inayohusisha wafugaji na jamii za wakulima, pamoja na waasi waliojitenga kusini-mashariki.
"Kwa ujumla, Nigeria ilisalia kuwa moja ya nchi zenye vurugu zaidi barani Afrika mwaka jana," kulingana na Armed Conflict Location & Event Data Project (ACLED) .















