Uchaguzi wa Nigeria 2023: Unachohitaji kujua

Chanzo cha picha, AFP
Mwezi ujao wapiga kura katika nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, Nigeria, watapiga kura kumchagua rais wao ajaye huku kukiwa na hali ya kutokuwa na furaha nchini humo kutokana na hali mbaya ya usalama na matatizo ya kiuchumi. Je, kuna yeyote kati ya walio mstari wa mbele, ambao wengi wao wamekuwa katika mfumo wa kisiasa kwa miongo kadhaa, atakayebadilisha nchi?
Kuanzia mfumuko mkubwa wa bei hadi mashambulizi mabaya ya watu wenye silaha dhidi ya raia wasio na hatia , utawala wa miaka saba wa Rais anayeondoka Muhammadu Buhari umeifanya Nigeria kukabiliwa na matatizo mbalimbali.
Wafuasi wake wanasema amefanya kila awezalo na kuangazia mafanikio, kama vile kazi yake katika miradi ya miundombinu na majaribio ya kupambana na itikadi kali. Lakini hata mke wake mwenyewe, Aisha Buhari, ameomba msamaha kwa watu wa Nigeria kwa kushindwa kutimiza matarajio yao.
Kwa hiyo atakayeshinda uchaguzi hatakuwa na kazi rahisi.
Uchaguzi ni lini?
Unatarajiwa kufanyika Jumamosi tarehe 25 Februari 2023.
Ikiwa hakuna mshindi dhahiri,duru ya pili itafanyika ndani ya wiki tatu. Pia kutakuwa na uchaguzi wa magavana wa majimbo wenye nguvu nchini humo Jumamosi tarehe 11 Machi.
Mkuu wa tume ya uchaguzi amepuuzilia mbali mapendekezo kwamba kura inaweza kucheleweshwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama.
Nani anagombea urais?
Jumla ya wagombea 18 wanafanya kampeni za kuwania nafasi hiyo ya juu, lakini watatu pekee ndio wana nafasi ya kushinda, kulingana na kura za maoni.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Bola Ahmed Tinubu, 70, anawakilisha chama tawala cha All Progressives Congress (APC). Anajulikana kama 'godfather' wa kisiasa katika eneo la kusini-magharibi, ana ushawishi mkubwa lakini amekuwa akikabiliwa na madai ya rushwa kwa miaka mingi na afya mbaya, ambayo yote anakanusha.
Wengine wanasema kauli mbiu yake ya kampeni Emi Lokan, ambayo ina maana "ni zamu yangu [kuwa rais]" katika lugha ya Kiyoruba, inaonyesha hali ya kustahiki.
Atiku Abubakar, 76, anagombea kwa niaba ya chama kikuu cha upinzani cha People's Democratic Party (PDP). Amewahi kugombea kiti cha urais mara tano kabla - zote ameshindwa. Sehemu kubwa ya kazi yake imekuwa katika ukanda wa madaraka, akiwa amefanya kazi kama mtumishi wa juu wa serikali, makamu wa rais chini ya Olusegun Obasanjo na mfanyabiashara maarufu. Kama vile Bw Tinubu, ameshutumiwa kwa ufisadi na kuweka urafiki mbele jambo ambalo anakanusha.
Peter Obi , mwenye umri wa miaka 61, ana matumaini ya kuvunja mfumo wa vyama viwili ambavyo vimetawala Nigeria tangu mwisho wa utawala wa kijeshi mwaka 1999 na anagombea na chama kidogo kisichojulikana cha Labour.
Ingawa alikuwa katika PDP hadi mwaka jana, anaonekana kama sura mpya na anafurahia kuungwa mkono kwenye mitandao ya kijamii na vijana wa Nigeria. Mfanyabiashara huyo tajiri aliwahi kuwa gavana wa Jimbo la Anambra kusini-mashariki kutoka 2006 hadi 2014. Wafuasi wake, wanaojulikana kama "OBIdients" wanasema yeye ndiye mgombea pekee mwenye uadilifu, lakini wakosoaji wake wanahoji kuwa kura ya Obi ni kuipoteza kwa sababu hana uwezekano wa kushinda.
Nani ana uwezekano wa kushinda?
Mazoea yanapendekeza mgombea kutoka kwa mojawapo ya vyama viwili vikuu atashinda - Bw Atiku au Bw Tinubu. Lakini wafuasi wa Bw Obi wanatumai kuwa anaweza kuwashangaza ikiwa wanaweza kuhamasisha vijana wengi kupiga kura kumuunga mkono.
Je, uchaguzi hufanyika vipi?
Ili kushinda, mgombea anapaswa kupata idadi kubwa zaidi ya kura nchini kote, na zaidi ya robo ya kura zilizopigwa katika angalau theluthi mbili ya majimbo ya Nigeria.Ikiwa hakuna wagombeaji atakayeafikia hili, kutakuwa na duru ya pili, ndani ya siku 21 kati ya wagombeaji wawili wa juu.
Masuala makuu ni yapi?
Kupunguza ukosefu wa usalama ni moja wapo ya maswala muhimu ya wapiga kura, katika nchi ambayo kwa sasa inakabiliwa na mzozo wa utekaji nyara kwa ajili ya fidia na kupambana na wapiganaji wa Kiislamu katika maeneo ya kaskazini.
Matukio mawili ya kushtua zaidi mwaka jana ni shambulio la risasi katika Kanisa Katoliki la Owo na kuvamiwa na watu wenye silaha katika treni ya abiria ambapo makumi ya watu waliuawa au kutekwa nyara.

Chanzo cha picha, AFP
Rais Buhari anasema ametimiza ahadi yake 'kubwa na kwa ujasiri kukabiliana na ugaidi", lakini Wanigeria wengi wanahisi nchi bado haiko salama.Uchumi ni eneo jingine la kuleta wasi wasi. Mnamo 2022 mfumuko wa bei ulipanda kwa miezi 10 mfululizo, ukipungua hadi 21.3% kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizotolewa mwezi huu.
Kupanda huku kwa gharama ya maisha kumeziacha familia nyingi zikihangaika kutafuta riziki, huku vyombo vya habari vya nchini vikielezea hali hiyo kuwa "mbaya".Ukosefu wa ajira pia ni tatizo kubwa, na kuwaacha wahitimu wengi wakiwa na hofu kwamba huenda wasipate kazi hata baada ya miaka mingi ya kusoma chuo kikuu.
Takwimu za hivi punde kutoka Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu nchini humo zinaonyesha kuwa 33% ya watu hawana ajira - na kupanda hadi 42.5% kwa vijana watu wazima
Licha ya kuwa mzalishaji mkuu wa mafuta, Wanigeria wanne kati ya 10 wanaishi chini ya mstari wa umaskini na "wanakosa elimu na upatikanaji wa miundombinu ya kimsingi, kama vile umeme, maji salama ya kunywa, na kuboreshwa kwa vyoo," kulingana na Benki ya Dunia.Wengi wa wagombea wameweka masuala haya katikati ya kampeni zao.
Lakini matatizo haya yamekuwa yakiongezeka kwa miaka kadhaa, na kuwaacha baadhi ya Wanigeria wakiwa na mashaka kuhusu iwapo yeyote atakayeshinda uchaguzi ataweza kuyarekebisha. Licha ya idadi kubwa ya wapiga kura waliojiandikisha - milioni 93.5 - wasiwasi unaendelea kuhusu kutojali na ni watu wangapi watajitokeza siku hiyo kupiga kura .
Huku kukiwa na karibu 40% ya wapiga kura waliojiandikisha chini ya miaka 34, kura hiyo imeitwa "uchaguzi wa vijana" na mkuu wa uchaguzi Mahmood Yakubu.
Je, kura itakuwa huru na ya haki?
Katika chaguzi zilizopita nchini Nigeria kumekuwa na ripoti za kuaminika za wanasiasa kuvuruga uchaguzi, kwa kusababisha vurugu kuwatisha wapiga kura au kunyakua masanduku ya kura na kuyajaza.
Lakini Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (Inic) inasema matumizi ya teknolojia mpya yatasaidia kuhakikisha kuwa kura ni salama na haijakumbwa na udanganyifu au wizi.Pia kumekuwa na visa vya wanasiasa kuwalipa wapiga kura maskini kuwaunga mkono, hata kwenye vituo vya kupigia kura.
Lakini mabadiliko ya hivi majuzi ya noti za naira yamelazimisha uhaba wa fedha ambao utafanya ununuzi wa kura kuwa mgumu, na maajenti wa usalama pia huwakamata washukiwa ambao wanatoa au kupokea pesa.
Inec pia imesema ni kinyume cha sheria kwa wapiga kura kupokea simu kwenye vyumba vya kupigia kura na kupiga picha za karatasi zao za kupigia kura, kwani uthibitisho huu kwa kawaida hutakiwa na wanunuzi wa kura.Baadhi ya ofisi za INEC zimeshambuliwa katika maandalizi ya upigaji kura.
Novemba mwaka jana tume ya uchaguzi lilifanya mkutano wa dharura kuhusu mashambulizi dhidi ya majengo yake, ambayo vyombo vya habari vya ndani vilielezea kama "mwenendo wa kutatanisha" .
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue
Mwisho wa X ujumbe
Pia kumekuwa na malalamiko kuhusu usajili wa wapigakura unaotiliwa shaka . Mwaka jana wachunguzi wa kidijitali waligundua kadi za wapiga kura kwenye rejista ya kidijitali ya uchaguzi ambayo ilionekana kuwa na picha za watoto.
Umri halali wa kupiga kura nchini Nigeria ni miaka 18.Baadhi ya wengine kwenye orodha ya awali walionekana kujiandikisha zaidi ya mara moja, kwa kubadilisha sura zao , nguo au jinsi walivyokuwa wamekaa.Wakati wa ugunduzi huo, INEC ilisema inakaribisha msaada wa Wanigeria kusafisha rejista hiyo.
Mnamo Januari 11, IEC ilitoa rejista mpya , ambayo ilisema wapiga kura 53,264 wasiostahiki wameondolewa. Pia ilisema kuwa wapiga kura wenye umri mdogo na wanunuzi wa kura watachukuliwa hatua.
Uchaguzi gani mwingine unafanyika?
Pamoja na kura ya urais, umma pia utakuwa ukichagua wawakilishi wao kwa bunge - Bunge la Kitaifa.Kuna wabunge 469 wanaojumuisha Maseneta 109 na wajumbe 360 wa Baraza la Wawakilishi.Wiki mbili baadaye tarehe 11 Machi pia kutakuwa na uchaguzi wa kuchagua magavana wa majimbo 28 kati ya majimbo 36 ya Nigeria.
Unahitaji nini kupiga kura?
Ili kupiga kura, unahitaji kuwa na Kadi halali ya Mpiga Kura wa Kudumu (PVC), ambayo inaonyesha kwamba umejiandikisha kupiga kura na kuthibitisha utambulisho wa mpigakura.

Chanzo cha picha, AFP
PVC ina data ya kibayometriki ya mpigakura, inayotumiwa kama uthibitishaji zaidi siku ya uchaguzi.
Data hii imehifadhiwa kwenye kadi .Walakini, kuna muda mdogo, kwani tarehe ya mwisho ya kupata PVC ni 29 Januari.
Ili kupiga kura yako, unahitaji kufika katika kituo chako cha kupigia kura kati ya saa 08:00 na 14:00 na PVC yako. Ilimradi uko kwenye foleni ya kupiga kura kufikia 14:00, utaruhusiwa kupiga kura yako, INEC inasema.Raia wa Nigeria wanaoishi ughaibuni hawaruhusiwi kupiga kura nje ya nchi.
BVAS ni nini?
Uchaguzi huu ni tofauti na ule wa awali kwa sababu mfumo mpya unatumika - Mfumo wa Uidhinishaji wa Wapigakura wa Bimodal (BVAS), ambao ni kifaa kilichoanzishwa na INEC mwaka wa 2021 kwa lengo la kukomesha udanganyifu katika uchaguzi.
BVAS kimsingi ni kisanduku kidogo cha mstatili chenye skrini iliyobobea zaidi kiteknolojia kuliko Visomaji vya Smart Card vilivyotumika hapo awali.Faida kuu ya BVAS ni kwamba ina uwezo wa kuwatambua wapigakura mara mbili siku ya uchaguzi kupitia alama zao za vidole na utambuzi wa uso.
Hii inapaswa kuwazuia watu wasio na PVCs halali kupiga kura, pamoja na wale ambao hawana sifa ya kupiga kura kujaribu kufanya hivyo.
Kipengele kingine cha BVAS ni kwamba inapakia matokeo ya kura moja kwa moja kwenye tovuti ya kuangalia matokeo ya IEC ili watu wote wayaone, ambayo kwa nadharia ina maana kwamba matokeo hayawezi kubadilishwa.
Kumekuwa na wasiwasi kuhusu BVAS baada ya kukumbwa na hitilafu katika chaguzi za majimbo kote mwaka wa 2021 na 2022, lakini INEC inasisitiza kuwa matatizo haya yametatuliwa.
Tutapata lini matokeo?
Katika chaguzi mbili zilizopita za urais mshindi amejulikana siku ya tatu baada ya kupiga kura.
Lakini kura zitahesabiwa punde tu upigaji kura utakapokamilika Jumamosi tarehe 25 Februari.
Wale watakaosalia katika vituo vyao vya kupigia kura watatangaziwa matokeo, lakini ni mchakato mrefu kabla ya matokeo yote kufika Abuja kutoka makumi kwa maelfu ya vitengo vya kupigia kura kote nchini.
BVAS inaweza kuharakisha mchakato mwaka huu, lakini maafisa walioteuliwa na Inec bado watalazimika kusafiri hadi Abuja kutoka majimbo 36 na nakala kusomwa kwa sauti.
Hapo ndipo mwenyekiti wa INEC atatangaza mshindi - au kwamba duru ya pili inahitajika.
Taarifa ya ziada ya Nduka Orjinmo huko Abuja















