Pandashuka za kiuchumi katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais William Ruto
Na Abdalla Seif Dzungu
BBC Swahili

Saa 12:44 siku kama hii mwaka mmoja uliopita, Rais William Ruto aliweka mkono wake juu ya Biblia na kula kiapo cha rais wa tano wa jamhuri ya Kenya.
Chini ya joto kali lililochochewa na ukame uliokuwa ukiendelea wakati huo, Rais mpya aliweka wazi orodha ya ahadi zake kwa maelfu ya Wakenya waliomiminika katika uwanja wa Kimataifa wa Kasarani , mbali na wale waliokuwa wakitazama hafla hiyo katika simu na runinga kwamba angepunguza gharama na kuunda nafasi za kazi kwa mamilioni ya raia wasio na kazi na kushughulikia masuala mengine yanayoathiri "Mahasla".
Wakati akitoa ahadi hizo taifa lilikuwa na matarajio mengi licha ya ongezeko la joto la kisiasa baada ya mahakama kutupilia mbali ombi la upinzani kwamba uchaguzi wa 2022 ulikuwa umekumbwa na udanganyifu.
Lakini licha ya joto hilo la kisiasa lililofuatiwa na maandamano ya mara kwa mara yalioandaliwa na upinzani kupinga utawala wake na hali mbaya ya kiuchumi , mwaka mmoja baadaye Rais Ruto anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuunganisha nchi pamoja na kuwapunguzia ugumu wa maisha Wakenya wa kawaida ambao wanatatizika kupata riziki huku bei za bidhaa za kimsingi zikiendelea kupanda.
Kiongozi huyo vilevile amekosolewa jinsi ameshughulikia sekta za uchumi, afya na elimu ambapo sera zake zimekuwa haziwiani na ahadi zake.
Hatahivyo serikali imekuwa ikijitetea na kusema kwamba ililazimika kuchukua hatua ilizochukua katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kusafisha uchafu ulioachwa na utawala uliopita. Licha ya kwamba wamezidisha hali ngumu inayowakabili Wakenya.
Madeni
Ruto aliapa kupiga breki za kuendelea kukopa baada ya kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, ambaye mara kwa mara wakati wa kmapeni za uchaguzi uliopita alimtuhumu kwa kukopa zaidi.
Hata hivyo, alikopa kiasi kikubwa zaidi kwa mwaka mmoja kwani deni la Kenya lilizidi KSh 10 trilioni. Katika mwaka wa kifedha uliomalizika Juni, deni la jumla la Kenya lilipanda kwa KSh 1.56 trilioni hadi kufikia KSh 10.19 trilioni, kutoka KSh 8.63 trilioni katika kipindi kama hicho mwaka wa 2022.
Ushuru wa Juu

Chanzo cha picha, AFP
Katika manifesto yake, Rais Ruto aliahidi kukomesha ulipaji kodi wa kiwango cha juu, ili Kuwalinda wafanyabiashara na kodi hiyo ya kupita kiasi, ahadi ambayo inaonekana alipuuza alipoongeza VAT kutoka asilimia nane hadi kumi na sita.
Rais pia aliweka utaratibu mpya wa kutoza ushuru unaowaacha baadhi ya wafanyakazi kusalimisha takriban asilimia 40 ya mishahara yao kwa serikali ikiwa ni kodi ya asilimia 35 ya mapato kwa watu wanaopata kipato cha juu, ushuru wa nyumba wa asilimia 1.5, kuongeza bima ya afya ya NHIF kwa asilimia 2.7. mbali na kodi ya asilimia 2.5 kwa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Jamii (NSSF).
Hali hiyo ilizua maandamano kote nchini yalioandaliwa na viongozi wa upinzani kupinga hatua hiyo ya serikali.

Chanzo cha picha, Afisi ya naibu wa rais Kenya
Kiwango cha Juu cha Ukosefu wa Ajira
Uhaba mkubwa wa ajira ni changamoto nyingine inayokabili serikali ya Ruto. Mnamo Machi, Ofisi ya Kitaifa ya Takwimu (KNBS) ilitoa ripoti iliyoonyesha kwamba idadi ya Wakenya wasio na ajira iliongezeka hadi milioni 2.97.
Takriban nusu, au milioni 1.33, ya Wakenya wasio na kazi hawakuonyesha nia ya kutafuta kazi au kuanzisha biashara. Shirikisho la Waajiri nchini (FKE) lilibaini kuwa makampuni yalikuwa yanakabiliana na mfumuko wa bei.
Baadhi yao yamelazimika kuwafuta wafanyakazi ili kukimu mahitaji ya kodi ya juu iliowekwa na serikali huku baadhi ya wawekezaji wakiamua kufungasha na kuelekea katika mataifa yenye viwango vya chini vya kodi.
Elimu

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka mmoja tangu William Ruto achaguliwe kuwa rais, sekta ya elimu imeshuhudia mtikisiko katika shughuli zitakazoathiri shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Mabadiliko hayo yanaanzia kwenye marekebisho ya muundo wa ufadhili wa chuo kikuu hadi marekebisho ya Mtaala unaozingatia Umahiri (CBC).
Kabla ya utawala wake, Dkt Ruto alikuwa ameeleza nia yake ya kutumia elimu kuendesha mtindo wake wa kiuchumi wa chini kwenda juu. Yani {Bottom up}.
Mfano, kuondolewa kwa ulifadhili wa wanafunzi kulingana na kozi walizochukua huku serikali ikipaswa kutunza asilimia 70 ya ada hiyo huku mikopo na ada za moja kwa moja zinazolipwa na wazazi zikikidhi asilimia 30 iliyobaki ya ada.
Hata hivyo, kutokana na changamoto za ufadhili serikali haikuwa ikituma fedha hizo kwa kila mwanafunzi.
Matokeo yake yameziweka taasisi nyingi kwenye madeni; wakati Uhuru Kenyatta akiondoka, taasisi hizo zilikuwa na deni la takriban Sh61 bilioni.
Hatahivyo serikali ya Kenya Kwanza ilijizatiti na kuwaajiri walimu 35,790 Ili kukabiliana na changamoto sugu ya uhaba wa walimu nchini.
Kati ya hao 1000 waliajiriwa katika shule za msingi kwa masharti ya kudumu na pensheni, walimu 3,986 katika shule za msingi, 9,000 waliajiriwa katika shule za sekondari za chini kwa masharti ya kudumu na pensheni.
Wengine 21,365 waliweka kandarasi za mafunzo kwa shule za msingi na 439 kama wahitimu kwa shule za sekondari chini ya 8-4-4.
Mfuko wa Husler
Wakenya wamekuwa wakipata hazina ya Hustler Fund tangu uzindulzi wake mwezi Novemba mwaka uliopoita. Ilikuwa mojawapo ya ahadi zilizotolewa na Ruto wakati wa kampeni za 2022.
Mkopo huo hutolewa kwa riba ya 8% kwa mwaka (0.002% kwa siku).
Ilizinduliwa kwa awamu, huku ya kwanza ikiwa ni mkopo wa kibinafsi unaotoa kati ya KSh 500 na KSh 50,000.
Awamu ya pili inalenga biashara ndogo na za kati na vikundi (chamas), ambavyo vinapata kati ya ksh 20,000 hadi KSh 1 milioni.
Mbolea ya ruzuku
Utawala wa Kenya Kwanza Alliance ulianzisha ruzuku ya mbolea ili kuwawezesha wakulima kununua pembejeo kwa bei ya chini na kuimarisha uzalishaji wao.
Hatahivyo katika siku za hivi karibuni kumekuwa na pingamizi kutoka kwa Upinzani kuhusu mbolea hiyo ambapo kiongozi wa Upinzani Raila Odinga amenukuliwa akisema kwamba mbolea hiyo ilitolewa bure na serikali ya Urusi hivyobasi serikali haikufaa kuiuzia wakulima

Chanzo cha picha, Getty Images
Bei ya juu ya mafuta na unga
Wakati huo huo, rais alikaidi ahadi zake za kupunguza gharama ya mafuta.
Badala yake, wabunge washirika wa Muungano wa Kenya Kwanza walipiga kura ya kuongeza maradufu kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye mafuta kutoka 8% hadi 16%.
Kwa hivyo, gharama ya petroli iliongezwa hadi KSh 194.68, dizeli hadi KSh 179.67 na mafuta taa hadi KSh 169.48.
Hali hiyo ilichochea kuongezeka kwa bei za bidhaa muhimu kote nchini.












