Je, Kenya inahitaji ‘handshake’ nyingine?

Chanzo cha picha, AFP
- Author, Abdallah Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
Siku chache baada ya viongozi , wanadiplomasia na Wakenya kushinikiza kusitishwa kwa maandamano dhidi ya serikali nchini Kenya yaliosababisha mauaji ya Zaidi ya watu 30, fununu zinazoenea katika taifa hilo ni kwamba kuna mpango wa viongozi wakuu kufanya kazi Pamoja.
Hatua hii inajiri baada ya rais William Ruto na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kudaiwa kukutana mjini Mombasa , ambapo pande kinzani ziliamua majadiliano ndio suluhu ya hali ngumu ya kiuchumi iliopo nchini humo.
Mkutano huo pia ulijiri siku chache tu baada ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kudaiwa kuzuru nchini Kenya ili kuwakutanisha viongozi hao, ziara ambayo haijathibitishwa na utawala wa rais huyo hadi kufikia sasa.
Wakati huo, maandamano dhidi ya seriikali yaliotishwa na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kupinga muswada wa fedha wa 2023 yalikuwa yamealika maua huku thamani kubwa ya mali ikiharibiwa na biashara zikisitishwa.
Na hayo yakijiri pande kinzani zilizidi kujipiga kifua huku zikirushiana kidole cha lawama kwa yaliojiri.
Hatahivyo ujio wa aliyekuiwa rais wa Niger Olesegum Obasanjo ulipoza hali na viongozi wawili wa pande kinnzani Rais William Ruto na mwenzake Raila odinga wakakubaliana kuketi katika meza ya majadiliano.
Ni kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi kama hizo ndiposa katika serikali zilizopita, upinzani umefanikiwa kushirikiana na serikali kwa lengo la kusitisha maandamano na kurejesha utulivu nchini.
Lakini je iwapo viongozi hao wanahitaji kufanya kazi pamoja ni mfumo gani watakaofuata?
Serikali ya Mseto
Hii ni serikali ambayo inajumuisha upinzani ndani yake ambapo baadhi ya viongozi wa upinzani hupatiwa nyadhfa za uwaziri kama vile ilivyokuwa baada ya uchaguzi wa 2007 katika ya Rais Mwai Kibaki na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga.
Vilevile kuna serikali ambayo upinzani unashirikiana na serikali na kuunga mkono mipango ya serikali bila kujiunga moja kwa moja na serikali, ijapokuwa kiongozi wa upinzani anaweza kupigania baadhi ya viongozi wake wajumuishwe katika nyadhfa ndogo ndogo za serikali kama vile makatibu wa kudumu katika wizara na mabalozi.
Ila viongozi wakuu wa upinzani hawatachukua nyadhfa zozote katika serikali hiyo kama ilivyokuwa wakati wa handshake kati ya rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu Raila Odinga.
Katika ushirikiano huu Upinzani uliunga mkono serikali na ulipiga kura pamoja na serikali bungeni.

Je ni aina ipi ya serikali ya ‘Handshake’ inayohitajika Kenya?
Mwaka 2018, taifa la Kenya lilijipata katika msukosuko wa kisiasa na kiuchumi kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi hivyobasi ‘handshake’ kati ya serikali na upinzani iliondoa wasiwasi uliokuwepo na kuleta utulivu na uthabiti.
Mwaka 2022, Wakenya walishuhudia ghasia nyengine za baada ya uchaguzi zilizosababishwa na maandamano ya kupinga serikali ambapo baadhi ya raia walipoteza maisha yao , mali yenye thamani kubwa kuharibiwa huku biashara zikipata hasara kubwa na azma ya kuwekeza ikipungua.
Kulingana na Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa nchini Kenya david Burare , Handshake kwa sasa italeta utulivu amani na biashara zitaendelea kama kawaida na wawekezaji watakuwa na hamu ya kuwekeza tena.
Lakini Je, mpango wa handshake utaendelezwaje?

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Viongozi wakuu wa muungano wa upinzani wa Azimio wamenukuliwa wakisema kwamba hawataki kuingia katika serikali, lakini ukweli ni kwamba kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wafuasi wao ambao wanawataka kuingia serikalini.
Kulingana na hitaji moja la muungano huo katika meza ya mazungumzo ni ushirikishwaji wa Wakenya wote bila ya kujali wanakotoka katika masuala ya kitaifa – hii inaweza kumaanisha kwamba wanapaswa kushirikishwa katika uendeshaji wa serikali .
Lakini kwa upande wa pili utawala wa Kenya kwanza unasisitiza kwamba uko huru kujadiliana kuhusu masuala yoyote yale isipokuwa ugawaji wa mamlaka serikalini.
Hii ndio sababu rais William Ruto amenukuliwa akisema kwamba ‘’tuwache serikali ifanye kazi yake na upinzani nao ufanye kazi yake’’.
Ni kutokana na msimamo wake huo ndiposa amependekeza kuundwa kwa wadhfa wa kiongozi wa upinzani – Wadhfa ambao utafadhiliwa na serikali huku wakikubaliana kushirikiana katika uundaji wa tume huru ya IEBC, utekelezaji wa sheria ya jinsia ya thuluthi mbili mbali na uwekejai wa waziri mwandamizi.
Je Wakenya wamejifunza nini kutoka kwa Handshake?
Wakati wa enzi ya Kibaki wakati timu ya Raila ilipoingia katika serikali mipango mingi ilitekelezwa, katika sekta zote za serikali.
Ndiyo maana watu wamekuwa wakisema kwamba Kibaki na Raila walifanya kazi nyingi kwa nchi hii.
Tatizo pekee ambalo lilishuhudiwa wakati huo kulikuwa na ugomvi mkubwa, kati ya pande hizo mbili za muungano, baadhi ya viongozi kutoka upande wa Kibaki walimkatisha tamaa Raila kwa sababu walidhani anapata sifa kupita kiasi kuliko Kibaki.
Baadhi ya mawaziri hawakuridhika kuripoti kwa Raila Odinga na wakati fulani kumkosoa hadharani.
Upinzani ambao ungewakilishwa na Raila na wenzake ulidhoofika hivyo ilikuwa vigumu kuikosoa au kuiweka katika mizani serikali ya muungano.
Chini ya mpangilio wa handshake kati ya Raila na Uhuru ilikuwa vigumu kusema ulikuwa ni mpangilio wa aina gani. Kilichobainika wakati mwingine makatibu wa baraza la mawaziri walionekana wakiripoti kwa Raila Odinga bila kujulikana walikuwa wanaripoti kwake kama nani?
Vilevile Manifesto ya chama tawala cha Jubilee haikufuatwa waziwazi na badala yake Mswada wa BBI ulichukua sehemu kubwa ya utawala wa rais Uhuru na kusababisha tofauti zisizoweza kusuluhishwa kati yake na naibu wake William Ruto.
Kilichowakasirisha wengi ni kwamba Upinzani ulidhoofika kabisa. Kinaya cha mpango mzima - ni kwamba wanachama wa upinzani walitetea vikali mipango ya serikali na wabunge katika upande tawala walikosoa programu za serikali.
Naibu rais alikua kiongozi wa upinzani na hatimaye mgombea wa upinzani, wakati kiongozi wa upinzani alikuwa katika mduara wa ndani wa serikali na hatimaye kuwa mgombea urais wa serikali.
Je upi muongozo? Na mchambuzi David Burare
Kulingana na mchanganuzi wa masuala ya kisiasa David Burare, Wakenya wamekuwa wakionesha mfano mbaya baada ya kila uchaguzi kwasababu anayeshindwa katika uchaguzi wa urais amekuwa akimshika mateka anayetangazwa mshindi hadi wanapoingia katika makubaliano ya kugawana mamlaka {Handshake}.
‘’ Ni Kwanini basi tufanye uchaguzi ilhali tunajua kwamba Mshindi na aliyeshinda watashirikiana katika serikali mpya, hatua hiyo inaondoa mafanikio ya Kidemokrasia tuliyopata’’, alisema bwana Burare
Hatahivyo mchangunzi huyo amesema kwamba kuna haja ya kuangazia suala la mshindi kuzawadiwa kila kitu hususan katika taifa ambalo mshindi na aliyeshindwa wamepata karibia kura sawa za jumla ya kura za waliosajiliwa kushiriki katika shughuli hiyo.
Vilevile mchanganuzi huyo amesisitiza kuundwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani ambayo itafadhiliwa na serikali ili kuuwezesha upinzani kufanya kazi yake kwa ufanisi.
‘’ Kiongozi huyo wa upinzani na naibu wake watakuwa wanachama wa bunge , kwasababu handshake kati ya Raila na Kibaki Pamoja na ile kati ya Uhuru na Raila hazikuisaidia nchi hii pakubwa isipokuwa kuleta utulivu pekee’’, alisema Burare.
Aliongezea kwamba badala yake Miungano hiyo miwili iliuwa upinzani ambao ni muhimu katika kuikosoa serikali na kuhakikisha kuwa inatekeleza ahadi zake zote.
‘’Kwa hali tuliyopo kwa sasa bila upinzani ulioimarika , tutaendelea kupoteza raslimali na kukuza ufisadi serikalini, huku ushindani ukiwa kuhusu ni nani aliyefuja fedha nyingi badala y ani wizara gani iliotoa huduma bora kwa raia’’, alihitimisha bwana Burare.












