Siku 100 za utawala wa Ruto: Uzito kwa rais wa Kenya kuambatanisha maneno na vitendo

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Yusuf Jumah
- Nafasi, Senior Journalist
- Akiripoti kutoka, Nairobi
Siku zina kasi.Na hazina huruma iwapo ndimi za viongozi wa kisiasa zinatoa cheche na ahadi na kusikika kama wimbo mtamu katika masikio ya wapiga kura na wananchi kwa jumla .
Kwa rais wa Kenya William Ruto siku zake 100 akiwa usukani kuiongoza nchi hiyo zimetimia leo tarehe 22 Disemba 2022.
Katikati ya harakati za kampeni alitoa ahadi nyingi mno ambazo kwa wafuasi wake zilipokelewa kama mwanzo wa matumaini ya kurahisisha hali zao.
Hata hivyo sio rahisi kukadiria mafanikio ya utawala wake katika siku 100 bila kuzingatia mambo kadhaa.
Kuna tofauti ya mcheza densi na mpiga gita-mmoja ana utaalamu wa kusuka sauti za nyaya za gita kutoa mlio wa kuvutia kuwa muziki.
Mwingine hana kubwa ila kusikia mlio huo mtamu na kuuainisha na densi ya maungo ya mwili wake kuunda densi.Ndio hali inayoeleza kinachofanyika sasa kuhusiana na matumaini ya wengi wakati wa kampeni na hali halisi wakati huu ambapo Ruto amekuwa uongozini kwa zaidi ya miezi mitatu .
Awali ahadi zake zilikuwa rahisi kuzitoa na zilisikika kama wimbo kwa wafuasi wake.Lakini sasa ,kibarua kimebadilika baada ya muziki kukoma na kazi ngumu ya kutekeleza ahadi hizo kuanza .
Kwa ahadi nyingi alizotoa rais na muungano wake wa Kenya Kwanza ,amepondwa na uhalisia wa mambo baada ya kuchukua usukani .
Kuna ahadi kadhaa alizofaulu kuzitimiza na nyingine huenda amezifanya hadi kufikia katikati lakini kwa wengi,makubwa bado hayajatimizwa ama faida hazijakuwa wazi .
Ruto amefaulu kuzitekeleza vipi baadhi ya ahadi hizo na ni zipi?
Gharama ya Maisha/Bei ya unga .

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Iwapo kuna bidhaa inayowakilisha mahangaiko ya maisha ya kila siku kwa mwananchi wa kawaida Kenya ,basi ni unga wa mahindi .
Rais ,akiwa mgombeaji wa urais miezi mitatu iliyopita aliahidi kuteremesha bei ya unga wa mahidni hadi shilingi 70 kwa pakiti ya kilo mbili.
Hadi sasa ushahidi bado upo wa uzito wa jukumu hilo .
Rais na naibu wake Rigathi Gachagua wamewaambia wananchi kuwa wavumilivu kwani wanahitaji muda zaidi kutimiza hilo.
Kwa wengi,huenda safari hiyo ikakomea hapo na kulea matumaini zaidi ya ahadi hiyo kutimizwa hivi karibuni ni jambo ambalo hawatakubali kulifanya .
Utawala wake uliondoa ruzuku kwa bidhaa kama unga na mafuta,jambo ambalo baadhi ya wadadisi walisema liliharakishwa.
Lakini Serikali mpya ilidai ruzuku haikuwa suluhisho la kudumu .
Bei ya mbolea hata hivyo ilipunguzwa kutoka shilingi 6000 hadi 3500 ili kuhakikisha wakulima wanafanikisha uzalishaji wa mazao.
Afueni ya hatua hiyo itahitaji muda ,na sio siku 100 .
Ruto aliahidi kurekebisha uchumi kwa kupunguza deni la serikali, kupunguza bei ya bidhaa muhimu, na kuunda "hustler fund" kutoa mkopo wa kibinafsi kwa Mkenya yeyote aliye na simu ya rununu ..
Lakini kitendo chake cha kwanza baada ya kushika wadhifa huo ilikuwa kupunguza ruzuku ya chakula na mafuta iliyoletwa na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.
Huku Ruto akisema kuwa afua hizo "hazikuzaa matunda yoyote", kuondolewa kwao kulikuwa ombi kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, mkopeshaji mkuu Kenya.
Benki Kuu ya Kenya ilipandisha viwango vya riba kwa jumla ya asilimia 1.75 mwaka wa 2022, idadi kubwa zaidi katika kipindi cha miaka saba, huku mfumuko wa bei ulipanda hadi kufikia kiwango cha juu cha miaka mitano cha asilimia 9.6 mwezi Oktoba.
Iwapo maamuzi ya utawala mpya yangebadilisha mambo kuwa bora ama kuleta afueni ni jambo litakalohitaji muda kutathmini lakini huo ndio uhalisia wa mambo siku 100 baadaye .
Asilimia 50 ya wanawake katika baraza la mawaziri

Iwapo kuna kundi lililobeba matumaini makubwa ya kushuhudia ufanisi katika uakilishi sawa wa kijisnia katika serikali ya Ruto ni wanawake .
Alitoa ahadi ambayo hata ilitiwa Saini katika mkataba maalum na makundi ya wanawake kwamba nusu ya baraza lake la mawaziri itakuwa na wanawake .
Alipotangaza baraza hilo ,ahadi hiyo ilitupwa kapuni na ni wanawake saba pekee ndio walioteuliwa katika baraza la watu 22.
Mambo hayakuboreka hata wakati makatibu wa kudumu wa wizara walipotangazwa .
Huenda ulikuwa mkosi wa mwanzo wa kuzima matumaini makubwa ya kuwapa wanawake sauti zaidi ili wajiwekee msingi wa kuafikia ubora zaidi wa uwezo wao katika masuala ya uongozi na usimamizi wa masuala ya serikali na nchi yao .
Hazina ya ‘Hustler’

Iwapo kuna ahadi ya Ruto iliyokodolewa macho na kungojewa na wengi hasa wafuasi wake basi ni hii ya kutoa mikopo ya shilingi bilioni 50 kwa mahasla.
Wengi wa wafuasi wake wanaojitambua kama watu wa kipato cha chini waliitegemea ahadi hii kuwa kitovu cha mafanikio yao .
Hata hivyo baada ya hazina hiyo kuanzishwa na rais Ruto,maoni yanayokinzana yamejitokeza ,lakini kikubwa ni iwapo azma ya hazina hii itatimizwa iwapo kiasi cha fedha wanazopewa watu na hali ya sasa ya mfumko wa bei za bidhaa vinawiiana kuleta athari yoyote kubwa katika kufumua nyenzo za kiuchumi .
Kwanza ahadi ilikuwa ya kutoa hela hizo bila riba lakini sasa mkopo huo unakuja na riba ya asilimia 8 na unafaa kulipwa ndani ya siku 14 .
Watu wengi wanaoomba mkopo wanalalama kwamba kiasi wanachopewa hakiwezi kuwakwamua kutoka lindi la mahitaji yao ya kimsingi na dharura kwani wengi wanapewa chini ya shilingi 1000.
Endapo hilo litakuja kutulia na manufa ya hazina hii kudhihirika ni jambo linalohitaji muda na macho kuangalia .
Kunao wanaosema heri nusu shari kuliko kamili na hatua ya rais kuitekeleza ahadi yenyewe licha ya kuibadilisha pakubwa ni nzuri na wameikaribisha .
Makovu ya kisiasa/Juhudi za kuiponya nchi

Hakuna asiyetambua kwamba uchaguzi uliopita nchini Kenya ulizua mgawanyiko mkubwa miongoni mwa watu na taasisi za serikali.
Hakuna mfano mzuri wa mgawanyiko huo kama ilivyodhihirika ndani ya tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.
Licha ya rais Ruto kuapa kuliponya taifa na kumaliza migawanyiko iliyosababishwa na uchaguzi uliopita ,hatua ya serikali kuwatimua afisini makamishna wanne wa tume ya IEBC ambao walipinga ushindi wake imetafsiriwa na wakosoaji wa rais kama hila ya kisiasa ambayo ina hatari ya kuzidisha mpasuko nchini .
Washirika wa rais wanasema uamuzi huo ni wa kuwaajibisha maafisa hao ambao inadaiwa 'walihatarisha nchi’ kwa kupinga ushindi wa Ruto lakini kwa upande mwingine imechukuliwa kama mwanzo wa ajenda ya hila dhidi ya wenye maoni tofauti na ya rais na serikali yake .
Iwapo mkondo utasalia huo na upinzani kulitumia suala hilo kama ajenda ya kuendelea kukoka moto wa kisiasa nchini,huenda utulivu unaohitaji kwa hatua nyingine za ustawishaji wa nchi zikalemazwa na safari isiyofika mwisho ya siasa za uchaguzi mmoja hadi mwingine nchini Kenya .
Ngoma ya kudumisha utawala bora/uhusiano na Idara ya mahakama na Bunge
Rais Ruto tangu mwanzoni aliahidi kuhakikisha kwamba anadumisha uhuru wa idara ya mahakama na kuipa ufadhili inavyohitajika .
Aliwateua majaji sita ambao mtangulizi wake Uhuru Kenyatta alidinda kuwateua .
Hilo Pamoja na kuahidi kutoa ufadhili kwa idara ya mahakama ni mambo ambayo yamepokelewa na hisia mseto kulingana na unayemuuliza kupata jibu .
Kulingana na mtaalam wa masuala ya utawala bora Calvin Muga ,Kwa wafuasi wa Ruto hatua hiyo ni nzuri kufanikisha upatikanaji wa haki lakini kwa wakosoaji wake ,kuna mengi yanayojitokeza .
Kiongozi wa Azimio Raila Odinga amemshtumu Ruto kwa ‘kuiteka’ idara ya mahakama.
Kwanza hakufurahishwa na uamuzi wa mahakama ya juu Zaidi kuidhinisha ushindi wa Ruto na pili upinzani umetafsiri kwa njia tofauti hatua ya mahakama za Kenya kutupilia mbali kesi zilizokuwa zikiwakabili viongozi wanaodaiwa kuwa washirika wa rais William Ruto.
Katika msururu wa kesi hizo -wiki hii ,kesi ya mauaji dhidi ya Waziri wa Utumishi wa Umma Aisha Jumwa ilitupiliwa mbali na mahakama na ile ya ufisadi dhidi ya aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko kufutwa pia .
Muga anasema Upinzani unachukulia ushirikiano huo wa ‘msaada wa kufanikisha Mahakama’ kutoka kwa rais kama wenye matarajio ya ‘maamuzi’ yanayoegemea upande mmoja lakini hilo lipo tu katika ndimi ila hakuna ushahidi wa wazi kuhusu madai hayo kwani kikatiba idara ya mahakama ina uhuru wake unaofaa kuendesha mwongozo wake wa utendakazi na huduma kwa wananchi .

Chanzo cha picha, William Ruto/Twitter
Rais pia ana kibarua cha kudumisha maridhiano katika teuzi za maafisa wa serikali anazofanya ili kutosheleza mahitaji na maslahi ya kimaeneo na kijamii nchini .
Minong’ono ya hapa na pale kuhusu wanaoteuliwa huenda imekuwa ya kimya kimya lakini inaweza kulipuka baadaye na kuunda msingi mbovu wa utawala wake katika siku zijazo .
Uhusiano wake na bunge pia umewekwa katika darubini.
Ameonekana kuwapendelea wabunge chipukizi kushikilia nafasi za uongozi wa bunge na kamati za bunge .
Hili kwa wafuasi wake ni jambo zuri kwani alitoa ahadi kwa vijana kuwapa nafasi na sauti katika utawala wake na pia uhusiano wa akribu na bunge unarahisisha ufanisi wa ajenda za utungaji sheria na sera .
Kwa wakosoaji wake ,rais anawatumia vijana wasio na uzoefu ili aweze kuwashawishi na kupinda maamuzi ya taasisi kama bunge kwa manufaa yake.
Kufahamu athari na ukweli wa madai ya pande zote mbili,ni jambo litakalohitaji muda kuona faida na hasara zake .
Rais Ruto pia ana kibarua cha kuainisha kauli na vitendo vya maafisa wa serikali yake kuhusu masuala muhimu yanayohusu nchi .
Mawaziri wake Mithika Linturi na Moses Kuria kwa mfano ,wameonekana kutoa kauli zinazokinzana kuhusu kuagizwa kwa vyakula vya GMO nchini .
Tofauti kama hizo zinapunguza Imani ya wananchi kwautawala huu ,kulingana na mtaalam wa masuala ya utawala bora Calvin Muga .
Iwapo kuna kibarua kwa utawala huu ili kuanza kufanikisha kikamilifu ahadi ilitoa kwa Wakenya basi jukumu litaanza na kukomesha wimbo wa lawama kwa utawala uliotangulia na kufanya maamuzi na kuchukua hatua za kuleta afueni kwa wananchi wanaolalamikia gharama ya juu ya maisha au kuondoa vikwazo njia ili kuwawezesha wengi wenye uwezo kujitafutia kipato.












