Vurugu zinaathiri vipi uchumi wa Kenya?

Na Rashid Abdallah

BBC Swahili

tdrgrt

Chanzo cha picha, Getty Images

Tangazo la Urusi la kujitoa katika mkataba wa nafaka kati yake na Ukraine limepokelewa kwa huzuni kubwa katika nchi zinazotegemea uingizwaji wa nafaka hizo ili kulisha raia wake. Nchi ya Kenya ni moja kati ya zilizoeleza masikitiko yake wazi wazi.

Imeitaja hatua hiyo ni, ‘kusalitiwa kwa watu ambao nchi zao zinakabiliwa na ukame.’ Nchi nyingi barani Afrika zinapitia kipindi kigumu cha mfumuko wa bei, ikichangiwa na mambo makubwa matatu. Mosi, janga la uviko 19, ambalo limeathiri chumi za nchi nyingi duniani.

Pili, vita vya Urusi na Ukraine - vimepelekea kupanda kwa bei ya bidhaa na nishati. Tatu, katika baadhi ya mataifa barani Afrika (Kenya ikiwemo), ukame umechangia uzalishaji wa ndani hasa katika eno la kilimo kuathirika.

Lakini nchini Kenya kuna jambo la nne ambalo ni nyongeza kati ya yale yanayoumiza uchumi wa nchi hiyo; nalo ni maandamano ya muungano wa Azimio unaongozwa na mwanasiasa wa upinzani, Raila Amolo Odinga.

Kufuatia maandamano yaliyoambatana na vurugua, Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, anasema, ‘hata asiyesikia anajua kuna hasara kwa biashara ndogo ndogo, zile zilizofungwa na zilizoporwa.’

Kenya ina historia ya maandamano yanayosababisha majeruhi na vifo. Na sasa maandamano yamerudi tena. Swali ambalo makala hii itajaribu kulijibu, ni maeneo gani yataathirika zaidi ikiwa maandamano haya yatadumu?

Utalii

eeweew

Mapato ya sekta ya utalii nchini Kenya yaliongezeka kwa asilimia 83 mwaka 2022 kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Utalii iliyotolewa mwezi Februari mwaka huu. Ongezeke hili ni zaidi ya ile asilimia 72 kabla ya janga la uviko 2019.

Taarifa ilieleza pia, idadi ya watalii wa kimataifa iliongezeka na kufikia milioni 1.4, ukilinganisha na mwaka 2021 ambapo watalii walikuwa ni 870,00 tu. Wageni wanaongoza kutembelea nchi hiyo ni kutoka Marekani, Uganda, Uingereza na Tanzania.

Maandamano dhidi ya kupanda kwa gharama ya maisha, yanatokea katika kipindi ambacho shughuli za kitalii ni nyingi. Vuta nikuvute inayotokea, inaweza kuathiri shughuli za hoteli, nyumba za wageni, mikahawa na waongoza watalii.

Takribani watu milioni 3.1 wameajiriwa katika sekta hiyo, kwa mujibu wa mtandao wa Bloomberg. Utalii ni chanzo cha tatu cha fedha za kigeni, huku utalii wa kutembelea mbuga za wanyama na fukwe za bahari ya Hindi vikiwa ndio vivutio vikuu.

Uwekezaji kutoka nje

Amani na usalama ni moja ya kipaumbele cha mwekezaji yeyote, nchi zote zenye usalama mdogo, uwekezaji nao ni mdogo. Vurugu ama fujo na uwekezaji ni mambo yasiyokaa meza moja asilani.

Katika juhudi za kuvutia wawekezaji, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya katika tovuti yake inaeleza, nchi hiyo inatoa mazingira salama (kwa uwekezaji), ikijumuisha utulivu wa kisiasa, kuyataja kwa uchache. Hali ya sasa ikiendelea kama ilivyo, ahadi hii ya Kenya kwa wawekezaji itakuwa mashakani.

Akizungumza mwezi uliopita pembeni ya mkutano wa New Global Financing Pact, nchini Ufaransa, Rais wa Kenya, William Ruto, alieleza kwa vyombo vya habari mazingira ya sasa ya uwekezaji nchii kwake:

‘Tumefanya mabadiliko katika mazingira ya kuvutia wawekezaji wa moja kwa moja katika bajeti yetu ya sasa. Na tumeweka katika gazeti la serikali baadhi ya mabadiliko hayo, na wawekezaji binafsi wanaweza kuwa na mitaji yao bila ya kukatwa kodi.’

Shughuli za ndani za kiuchumi

e4rt

Chanzo cha picha, AFP

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Maandamano ya kisiasa yanaweza kuwa na athari mbaya za muda mfupi na muda mrefu; kutatizika kwa shughuli za ndani za kiuchumi, kutapelekea kupungua kwa uzalishaji, kuvurugika kwa myororo wa usambazaji wa chakula na kusababisha kupungua kwa mauzo ya nje na watu kupoteza kazi.

Gazeti la the Standard la nchini huo linaandika, maandamano ya kila wiki ya mwaka 2016, wakati viongozi wa upinzani walipodai mageuzi ya tume ya uchaguzi, kila biashara nane kati ya kumi ziliathirika, makadirio ya mapato yaliyopotea katika kila biashara kwa kila siku ya maandamano ni shilingi za kikenya 48,304.

Ripoti ya Agosti 2016, ya Muungano wa Sekta Binafsi nchini Kenya (KEPSA), ilionesha -mapato yaliyopotea kutokana na uhaba wa wateja, kufungwa kwa biashara, waajiriwa kutofika kazini, uharibifu wa mali na uporaji.

Vurugu za kisiasa zitokeapo na kutatiza shughuli za kila siku za uchumi, huathiri pia ukusanyaji wa mapato kwa serikali. Katika hali kama hii, Mamlaka ya Mapato nchini Kenya (KRA), inaweza kushindwa kufikia lengo lake la ukusanyaji.

‘Kipaumbele chetu ni kuhakikisha tunapambana na changamoto ya gharama za maisha. Kwa sababu ya vita vya Urusi na Ukraine na swala la mabadiliko ya tabia nchi ambalo limefanya mvua kutotabirika, tutatumia malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa chakula na kutengeneza mazingira ya ajira,’ rais Ruto akiwa Ufaransa.

Ahadi yake haikufanikiwa kuushawishi upinzani kuachana na maandamano. Ikiwa maandamano yatazidi kuendelea uchumi wa nchi utazidi kuumia. Bilashaka, mazungumzo ya kisiasa ndio njia pekee ya kutafuta suluhu ya patashika hii.