Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mtandao wa X na harakati za mapambano mtandaoni Tanzania
Katika zama hizi za kasi ya habari na mawasiliano ya kidijitali, mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa kuu la sauti ya wananchi. Miongoni mwa mitandao hiyo, X (zamani ikijulikana kama Twitter) imejipambanua kama uwanja muhimu wa mapambano ya kijamii, kisiasa, na kidemokrasia.
Kuanzia kampeni za mabadiliko hadi harakati za haki za binadamu, X si jukwaa la mijadala tu, bali pia silaha ya harakati, chombo cha mawasiliano ya dharura, na kiunganishi cha makundi mbalimbali ya kijamii.
Hata hivyo, mara kadhaa kumekuwa na jitihada za wazi na za chini kwa chini za kudhibiti au kuzima sauti hiyo, hasa kutokana na namna mtandao huu unavyotazamwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa, wa dini, na taasisi za dola.
Je, ni kwa kiwango gani X imebadilisha mazingira ya kijamii na kisiasa Tanzania? Na kwa nini kila mara huonekana kuwa kwenye hatihati ya kuzimwa?
Mtandao wa X na historia yake Tanzania
X ilianza kupata umaarufu nchini Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2010, hasa miongoni mwa wanahabari, wanaharakati, na watu wa mijini wenye uelewa wa teknolojia.
Kadri muda ulivyosonga, ikawa chombo muhimu kwa makundi mengi kuanzia wanafunzi, wanasiasa, waandishi wa habari, wasanii, wafanyabiashara, na wananchi wa kawaida.
Tofauti na mitandao mingine kama Facebook au Instagram ambayo hutumika zaidi kwa burudani na mawasiliano ya kijamii, X imebeba jukumu la kuendesha mijadala ya kitaifa, kampeni za kisiasa, na kufuatilia utendaji wa serikali.
Watumiaji wake wengi nchini Tanzania ni watu wenye kiwango cha angalau elimu ya sekondari, huku kundi kubwa likiwa na elimu ya chuo.
Katika mazingira haya, X imekuwa mahali pa watu wanaotafuta uwajibikaji wa viongozi, utawala bora, haki za binadamu, na maendeleo ya kidemokrasia, kwa kasi na wepesi ambao haujawahi kushuhudiwa katika vyombo vya kawaida vya habari.
Kutokana na nguvu yake katika kuendesha mijadala mikali, mwandishi Lukelo Francis aliwahi kuandika makala yenye kichwa, "Twitter: Jamhuri Inayoitingisha Jamhuri ya Tanzania?"
Katika makala hiyo, alinukuu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyosema Julai 5, 2022, alipokutana na wachezaji wa Serengeti Girls:
"Huko kwenye mitandao kuna Jamhuri ya Twitter... sasa na sisi tujenge Jamhuri ya wapambanaji."
Kauli hiyo inaonyesha namna X inavyochukuliwa kama nchi ndani ya nchi yenye sauti na nguvu kubwa isiyodhibitika kirahisi. Mtandao wenye nguvu.
Harakati maarufu kupitia X nchini Tanzania
Nguvu ya X nchini Tanzania imeonekana wazi kupitia kampeni mbalimbali zilizoibuliwa au kupelekwa mtandaoni na kupata uungwaji mkono mkubwa. Hashtags zimekuwa zana mpya za mapambano ya kisasa.
Baadhi ya kampeni maarufu ni pamoja na:
#ChangeTanzania; mojawapo ya vuguvugu la kwanza la kuhamasisha mabadiliko ya kijamii na kisiasa.
#FreeZitto, #FreeMbowe, #FreeLissu; ni harakati za kupinga kukamatwa kwa viongozi wa upinzani na kudai haki za kiraia.
#FreeSoka, #FreeMdude; ni kampeni zinazodai kupatikana kwa watu waliopotea au kushikiliwa pasipo taarifa.
#FreeMA; hii ilikuwa kampeni ya kumuunga mkono Maxence Melo, mwanzilishi wa Jamii Forums, katika mapambano dhidi ya kesi zinazohusiana na uhuru wa habari.
#SisiNiTunaumia; hiki kilikuwa kilio cha vijana dhidi ya hali ngumu ya maisha, kilichoenea hadi nchi jirani.
Mijadala hii mara nyingi imevuka mtandao na kuingia kwenye majukwaa mengine: magazeti, bunge, na hata majukwaa ya kimataifa. Lakini si wote wanaoiona kama harakati chanya, wengine huihusisha na uchochezi, matusi kwa viongozi, au uenezi wa maudhui yasiyofaa.
Rais wa awamu ya nne Tanzania, John Magufuli aliwahi kusema: "Natamani siku moja malaika washuke waizime hii mitandao yote," akionesha wazi kutoridhishwa na jinsi mitandao hiyo, hasa X, inavyotumika.
Kuzimika, kuzimwa au kutopatikana kwa mtandao wa X
Kuanzia Mei 21, 2025, X haikupatikana nchini Tanzania hali iliyotokea muda mfupi baada ya taarifa za kudukuliwa kwa akaunti za taasisi kadhaa zikiwemo Jeshi la Polisi, TIC na mtandao wa simu Airtel.
Taarifa za uongo na zenye viashiria vya uchochezi zilianza kusambazwa, na Jeshi la Polisi na Serikali ikatoa onyo kali. Baada ya muda mfupi, upatikanaji wa X ukawa mgumu katika maeneo mengi.
Shirika la uangalizi wa mtandao la NetBlocks limeripoti kuzimwa kwa mtandao wa X nchini Tanzania kuanzia Mei 20, likisema mtandao wa X ulikuwa chini kwa watoa huduma wakuu wa huduma za mtandao Tanzania (ISPs) Halotel, Airtel, Liquid Telecom, Habari Node, na Vodacom.
Lakini hadi sasa hakuna tamko rasmi la serikali kuwa mtandao huo umefungwa, umezimwa, kuna hitilafu au umezimika wenyewe?
Waziri wa Teknolojia, Jerry Slaa, aliliambia Bunge: "Page mbili za taasisi za Serikali zilidukuliwa kutokana na ulinzi dhaifu wa tarakimu... lakini mifumo yetu ipo salama."
Hali hii imewafanya wengi kujiuliza: Je, X imezimwa kwa sababu hizi za kiusalama zinazoelezwa?
Lakini si mara ya kwanza Mtandao huu wa X zamani Twitter kutopatikana nchini Tanzania
Wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, mitandao mingi ikiwemo X haikupatikana, na wananchi walilazimika kutumia VPN kwa mawasiliano. Aprili 2021, X ilirejea baada ya zaidi ya miezi kadhaa ya kutopatikana bila VPN.
Septemba 2021, X haikupatikana kwa siku kadhaa bila maelezo rasmi kama ilivyotokea pia kwa muda mwaka 2024.
Matukio kama haya pia yameshuhudiwa Nigeria (#EndSARS), Kenya, na Burundi, ishara kuwa mitandao ya kijamii inapofikia kiwango cha kuchochea mabadiliko, hutazamwa kama tishio na mamlaka katika nchi hizo.
Mwaka 2024, kulishuhudiwa kampeni kutoka kwa viongozi wa dini na siasa nchini Tanzania wakitaka X ipigwe marufuku nchini humo. Waliidai kuwa chanzo cha mijadala isiyofaa, uvunjaji wa maadili, na uchochezi.
Hadi sasa, bado haijajulikana wazi kama serikali itaendelea na mwelekeo wa kuifungia rasmi X, au itaacha nguvu ya teknolojia itawale mjadala wa kitaifa.