Mabaki ya dinosaria mkongwe zaidi barani Afrika yapatikana Zimbabwe

ANDREY ATUCHIN / VIRGINIA TECH

Chanzo cha picha, ANDREY ATUCHIN/VIRGINIA TECH

Maelezo ya picha, Ubunifu mpya wa Mbiresaurus raathi

Wanasayansi nchini Zimbabwe wamefukua mabaki ya dinosaria mkongwe zaidi barani Afrika, ambaye aliishi zaidi ya miaka milioni 230 iliyopita.

Mbiresaurus raathi alikuwa na urefu wa mita moja, alikimbia kwa miguu miwili na alikuwa na shingo ndefu na meno yaliyochongoka.

Wanasayansi wamesema ni aina ya sauropodomorph, jamii ya sauropod, ambayo ilitembea kwa miguu minne.

Mifupa hiyo iligunduliwa wakati wa misafara miwili ya Bonde la Zambezi mwaka 2017 na 2019.

"Tunapozungumza juu ya mabadiliko ya dinosaria wa zamani, mabaki kutoka enzi ya Triassic ni nadra," Darlington Munyikwa, naibu mkurugenzi wa Makumbusho ya Zimbabwe, ambaye ni sehemu ya msafara huo aliiambia BBC.

Alisema kuwa mabaki ya enzi hizo - ambayo yalimalizika zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita - yamefukuliwa Amerika Kusini, India na sasa Zimbabwe.

Ugunduzi huo unatarajiwa kutoa mwanga zaidi juu ya mageuzi nakuhama kwa dinosaria wa awali, nyuma wakati dunia ilikuwa bara moja kubwa na Zimbabwe ilikuwa katika latitudo sawa na nchi hizo, alisema.

Zimbabwe imekuwa ikifahamu kuhusu masalia mengine katika eneo hilo kwa miongo kadhaa na Bw Munyikwa alisema kuna maeneo mengeni ambayo yanahitaji uchunguzi zaidi katika eneo hilo, kulingana na upatikanaji wa fedha"

Inaonyesha kwamba dinosaur hawakuanza duniani kote, kutawala dunia tangu mwanzo kabisa," Christopher Griffin, mwanasayansi mwingine aliyehusika katika msafara huo, aliiambia BBC.

"Wao, na wanyama walioishi nao, wanaonekana kuwa walidhibitiwa na mazingira fulani huko kusini ya mbali ambayo leo ni Amerika Kusini, kusini mwa Afrika na India."

ANDREY ATUCHIN / VIRGINIA TECH

Chanzo cha picha, ANDREY ATUCHIN/VIRGINIA TECH

Maelezo ya picha, Christopher Griffin mwaka 2017, akichimba sehemu ya mifupa ya Mbiresaurus raathi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Aliongeza kuwa utafiti huo ulikuwa "dinosaria wa mwisho mkongwe zaidi kuwahi kupatikana barani Afrika".

Prof Anusuya Chinsamy-Turan, mtaalamu wa elimu ya kale katika Chuo Kikuu cha Cape Town, aliambia BBC kwamba ugunduzi huo ulikuwa muhimu kwa sababu ulikuwa sehemu ya ukoo uliozaa dinosaur sauropod, ambao ni pamoja na diplodocus na brontosaurus.

"Inatuambia kwamba wakati dinosaur walipokuwa wakibadilika, walipatikana katika mabara tofauti, lakini wanaonekana kufuata mazingira ya joto yenye unyevunyevu badala ya maeneo makavu," aliiambia BBC. "Tunatumai kuna wengine zaidi kutoka katika eneo hilo."

Aliongeza kuwa eneo ambalo ugunduzi huo ulifanyika kulikuwa na uchunguzi wa hivi karibuni wa madini ya gesi.

“Natumani kuna sera kali ya kuhakikisha kwamba wakikumbana na mabaki wanakabidhi kwenye makumbusho ili tusipoteze nyenzo hizo,” alisema.

Mifupa iliyokaribia kukamilika ya Mbiresaurus raathi imehifadhiwa kwenye chumba katika jumba la makumbusho katika jiji la kusini mwa Zimbabwe la Bulawayo. Inafikiriwa kuwa ni ya kipindi cha Carnian wakati wa Triassic, wakati Zimbabwe ya leo ilikuwa sehemu ya Pangaea bara kubwa zaidi.

Dinosaria waliaminika kuzoeana vyema na latitudo za juu ambapo Zimbabwe ya leo iko, ambayo ilikuwa na unyevunyevu na yenye uoto wa kutosha.