Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Wapalestina waliokimbilia Kusini mwa Gaza wanarudi Kaskazini?
Saa za kwanza za mapatano kati ya Israel na Hamas yalipoanza kutekelezwa siku ya Ijumaa, makombora na ndege za kivita zilinyamaza huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Badala yake kukawa na msongamano wa magari, honi za magari na ving’ora vya gari za kubebea wagonjwa. Huku idadi kubwa ya Wapalestina waliokimbia makazi yao wakijaribu kurejea Kaskazini.
Majira ya saa moja kwa saa za huko siku ya Ijumaa asubuhi, makubaliano yaliyosimamiwa na Qatar yalianza kutekelezwa; yanajumuisha usitishaji vita wa siku nne na kubadilishana mateka na wafungwa wa Kipalestina.
Vilevile kuingia kwa misaada ya kibinadamu na ya matibabu katika Ukanda wa Gaza - ikiwemo mafuta, ambayo Israel ilikuwa imezuia yasiingie.
Idadi ya watu waliokimbia makazi yao katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita kati ya Israel na Hamas Oktoba 7 inazidi milioni moja na laki 700, kwa mujibu wa ripoti ya siku ya Alhamisi ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Kazi kwa ajili ya Wakimbizi (UNRWA).
Milioni moja kati yao wanaishi katika vituo vya shirika hilo - wanajumuisha sehemu kubwa ya wale waliokimbia kutoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza kuelekea Kusini.
Wakati mapatano hayo yakiendelea, Misri iliwafahamisha Wapalestina waliokwama nchini Misri na wanaotaka kurejea kwa hiari Ukanda wa Gaza, kivuko cha Rafah kitafunguliwa kuanzia Ijumaa - hilo liliwafanya wengi wao kurudi Gaza.
Wanaorudi Washambuliwa
Saa 3:30 asubuhi, Yasser Tafesh aliwasili katika eneo lililopo kilomita 5 kutoka katikati ya Gaza, ambako aliishi kabla ya vita, akitokea kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Wakati umati wa watu wakirejea, vifaru vya Israel viliwashambulia na kuwafyatulia risasi moja kwa moja. Alipigwa risasi tumboni, pamoja na wengine sita, aliliambia shirika la habari la AFP.
Yasser anasema alitaka kurudi ili kuchukua unga na vitu vyake vingine kutoka nyumbani kwake, “nataka kuchukua nguo kwa ajili yangu na mke wangu kwa sababu tunaishi katika shule,” anasema akiwa ndani ya hospitali alikokuwa akitibiwa.
Jeshi la Israel liliwaonya Wapalestina wasirudi maeneo ya kaskazini na katikati mwa mji wa Gaza wakati wa mapatano hayo ya siku nne. Ndege za Israel zilidondosha vipeperushi vya kuwaonya watu. Vipeperushi vinasema: “Vita bado havijaisha na kurudi kaskazini ni marufuku na ni hatari sana.”
Ripoti zinaeleza Wapalestina 15 walijeruhiwa kwa risasi na jeshi la Israel walipokuwa wakijaribu kuvuka kuelekea kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, wakati wa siku ya kwanza ya mapatano hayo.
Licha ya hayo, mitaa kadhaa ya Gaza ilishuhudia harakati za magari na mikokoteni ya punda iliyosheheni watu waliokimbia makazi yao na mali zao wakisisitiza kurejea makwao.
Kijana wa Kipalestina Ahmed, aliyekimbia kutoka kitongoji cha Al-Zaytoun kaskazini mwa Gaza, anasema usitishaji vita unapaswa kujumuisha maeneo yote ya Gaza, vikiwemo vitongoji vya kaskazini. "Hawapaswi kutupiga risasi, kuna usitishaji wa mapigano," aliliambia shirika la habari la Associated Press.
Ahmed anaongeza kuwa yeye na familia yake wanataka kurejea nyumbani kwao ili kukagua mali zao na nyumba yao."Tunataka kujua nini kilitokea nyumbani kwetu. Hatujui kilichotokea. Tuko hapa hatujafanikiwa kufika."
Saleh Al-Shawaf anasema akiwa njiani kuelekea nyumbani kwake kaskazini mwa Gaza, "ninarudi peke yangu. Nimeiacha familia yangu na kurudi ili kujua nini kilitokea. Siku 48 za vita hatukujua chochote kuhusu nyumba yetu.”
Raia wengine waliokimbia makazi yao kutoka kaskazini hadi kusini wanasema hawakufaidika na usitishaji huo kwa sababu hawakuweza kurudi makwao.
Mmoja wao alisema bila kutaja jina lake, "tuliondoka Beit Lahia upande wa kaskazini. Hatukuchukua chochote. Tulichukua nguo zetu tu. Tunataka tuishi. Sifaidiki na makubaliano haya. Natumai nitaweza kurudi nyumbani kwangu nikiwa mzima."
Makubaliano yanasemaje?
Kwa mujibu wa masharti ya makubaliano hayo yaliyochapishwa na Hamas, kupitia akaunti yake ya Telegram, mapatano yanajumuisha usitishaji vita kutoka pande zote mbili katika eneo lote la Ukanda wa Gaza, na kuhakikisha uhuru wa kutembea kwa wakaazi kutoka kaskazini hadi kusini.
Pia kuna saa sita ambapo ndege za Israel haziruhusiwi kupaa katika anga ya Gaza kwa madhumuni ya ujasusi. Lakini mamia ya malori ya misaada na mafuta yanaruhusiwa kuingia katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza.
Waliokwama Misri warejea
Ubalozi wa Palestina mjini Cairo uliwafahamisha raia wa Palestina waliokwama Kaskazini mwa Sinai wanaotaka kurejea kwa hiari katika Ukanda wa Gaza wataruhusiwa kuingia Gaza kwa mara ya kwanza tangu kuzuka kwa vita tarehe 7 Oktoba.
Mamlaka ya Misri pia ilithibitisha Wapalestina wote waliokwama mjini Cairo na majimbo mengine ya Misri wataruhusiwa kurejea, kuanzia Jumamosi.
Mamlaka ya Misri ilifunga kivuko cha Rafah kufuatia mashambulizi ya Israel katika kituo hicho mwanzoni mwa vita - yalisababisha hasara kwa pande zote za Misri na Palestina.
Wengi wa wale waliokwama upande wa Misri wanasisitiza kurejea Gaza, kwa nia ya kukaa na familia zao na kuzuia jaribio la kuwaondoa wakaazi wa Ukanda huo.
Ammar Abed aliambia BBC alikwenda Misri kwa likizo kabla ya vita. Anasema, ''kuna mipango ya kuwaondoa watu wa Ukanda wa Gaza, lakini tunarejea kwa dhamira ya kuzuia hilo. Ulimwengu ujue kwamba tunarudi Gaza licha ya uharibifu na mzingiro. Kufa ukiwa na familia haiumizi sana kuliko kutazama vifo katika televisheni.”
Jamal Attiya, Mpalestina anayeishi Algeria, anasema anarejea Ukanda wa Gaza ili kuthibitisha kwamba Wapalestina wataendelea kubaki nchini mwao. “Licha ya vita, tunarejea nchini kwetu. Watu hawaondoki Ukanda wa Gaza, wanatarudi.”
Bakr Abu Reda anasema alikwama kwenye kivuko upande wa Misri kwa siku 48. "Tunafuata habari kuhusu familia zetu kwa shida. Hatuna mawasiliano yoyote na wanafamilia. Familia yangu inaishi Gaza katika mazingira magumu. Hakuna utulivu, hakuna faraja. Tulikuwa na wasiwasi kila wakati. Hakuna mahali pakukaa - isipokuwa kuwa na familia zetu huko Gaza."
Basil Helles, ambaye amengoja kurudi Gaza kwa siku 46, anasema furaha yake haielezeki. "Tumezipeza familia zetu na wapendwa wetu. Tuliahidi tutakuwa pamoja kwa matumaini kwamba vita vitakwisha."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah