Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Dosari katika mkakati wa Israel" – gazeti la The Independent
Tunaangazia tahariri katika gazeti la Uingereza la The Independent, ikiwa na kichwa cha habari: "Dosari mbaya katika mkakati wa Israel: Vita kamili havitaifanya kuwa salama zaidi."
Gazeti hilo linasema, "matokeo pekee, ikiwa Rafah itashambuliwa, bila shaka itakuwa ni hasara nyingine kubwa ya maisha. Kwa hiyo, uvamizi haupaswi kuendelea."
Gazeti hilo linarejelea onyo la hivi karibuni lililotolewa na Waziri wa Baraza la Mawaziri la Vita la Israel, Benny Gantz kwa Hamas akisema “ikiwa haitawaachilia Waisraeli na mateka wengine kufikia mwezi wa Ramadhani, mashambulizi ya ardhini dhidi ya Rafah yataendelea.”
Anasema Netanyahu, ambaye anataka "kumaliza kazi," hatapinga hilo. Lakini Je, Marekani, mdhamini mkuu wa usalama wa Israel, itakubali hilo?
Gazeti hilo linaamini kuendelea na mashambulizi maanake ni kurusha maguruneti, mizinga, vifaru, tingatinga zenye silaha, na vikosi vya askari waendao kwa miguu dhidi ya hospitali ya walemavu na kambi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani katika eneo lenye wakazi wapatao milioni 1.4.
Miongoni mwao, kama gazeti linavyosema, "raia walio kwenye njaa, karibu nusu yao ni watoto."
Tahariri hiyo inaangazia baadhi ya hatari, ikiwa ni pamoja na kwamba Jeshi la Israel litawauwa mateka wao, ambao wanatafuta kuwaokoa - au Hamas itawaua kwa kulipiza kisasi.
Israel itahakikishaje haifanyi maelfu ya watu wapya kuwa na msimamo mkali? Gazeti hilo linasema: Hii ndiyo kasoro katika mkakati wa Israel.
Tahariri hiyo inaamini moja ya hatari za mgogoro huu ni “kuwatenganisha marafiki wa zamani na kutengeneza maadui wapya.”
Marekani, Umoja wa Ulaya, na Uingereza zimeanza kusema kwa sauti kubwa zaidi kuliko hapo awali, na pia kumeanza kuwepo mazungumzo kuhusu kuitambua Palestina kama taifa huru, na sauti kama ya Afrika Kusini na Brazil, zinavyoituhumu Israel kutenda uhalifu wa kivita.
Mkakati wa kuivamia Rafah "utafanya juhudi za Israel kwa majira zake, kama vile Jordan, Misri, na Saudi Arabia, kudumisha uhusiano wa kawaida, kutowezekana.
Gazeti hilo linamalizia kwa kutoa wito wa "kusitishwa mapigano, Israel lazima itafute njia bora ya kuendeleza vita, au bora zaidi nikutafuta njia ya kupata amani."
Mgongano wa Israel na Misri juu ya Rafah
Tunageukia gazeti la Israel la The Jerusalem Post, ambapo Eli Budeh aliandika makala akiangazia athari za kushambulia Rafah kwa uhusiano kati ya Israel na Misri.
Mwandishi anasema mahusiano haya hadi sasa yameshinda changamoto za mzozo, ingawa kwa shida.
Mwanzoni mwa makala hiyo, mwandishi anawasilisha maoni Israel na Misri zinashirikina katika malengo kadhaa ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na kuwashinda Hamas au kupunguza kwa kiasi kikubwa mamlaka yake ya kisiasa na kijeshi.
Misri inaiona Hamas kama tawi la Muslim Brotherhood, ambalo Rais Sisi alilipiga marufuku. Nchi zote mbili zinataka kurejesha utulivu katika Ukanda wa Gaza na eneo zima.
Mwandishi anaamini, Israel na Misri zinataka kuundwa kwa ushawishi mpya wa kikanda unaoongozwa na Sunni kwa msaada wa Marekani, ili kuondosha ushawishi wa Iran na washirika wake.
Lakini anasema wakati huo huo kuna mgongano wa masilahi kati ya Israel na Misri.
Kutoelewana kuhusu "nini kifanyike baada ya vita. Wakati Misri inaunga mkono kurejeshwa kwa Mamlaka ya Palestina kutawala Gaza, Israel inapinga.
Mustakabali wa Ukingo wa Magharibi. Misri inaunga mkono kuunganishwa kwa Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza na kuanzishwa kwa taifa la Palestina, Israel inapinga.
Mwandishi haoni kuwa migongano hiyo ni tishio kwa uhusiano wa Misri na Israe. Lakini operesheni ya kijeshi ya Israel huko Rafah ina uwezekano wa kweli wa kuharibu uhusiano kwa mtazamo wa Misri.
Mwandishi anasema, Misri inajaribu kutatua tatizo hilo kwa kuitishia Hamas na Israel. Misri iliwajulisha Hamas kwamba Israel itashambulia Rafah ikiwa haitakubali makubaliano ndani ya wiki mbili. Wakati huo huo, pia iliionya Israel kuhusu matokeo mabaya ya operesheni ya kijeshi huko Rafah.
Msimamo wa dunia kuhusu vita unabadilika kwa maneno lakini si kwa vitendo
Tunamalizia na mwandishi Talal Okal aliandika makala katika gazeti la Palestina "Al-Ayyam" chini ya kichwa: "Hivi ndivyo Netanyahu na timu yake wanavyotaka."
Mwandishi anasema maoni ya umma duniani yameanza kubadilika kuhusiana na mwenendo na matokeo ya vita vya Israel dhidi ya watu wa Palestina, lakini msimamo wa Israel haubadiliki.
Ingawa mabadiliko ya misimamo ya nchi, haswa za Magharibi, "bado ni ya kinadharia, ni ngumu kutabiri, na bado haijabadilika na kuwa hatua za kuwalazimisha wababe wa kivita wa Israel kusitisha vita vyao dhidi ya watu wa Palestina.
Mwandishi anaeleza kuwa Netanyahu anaamini kuacha kuendelea na mashambulizi huko Rafah ni kushindwa kusikokubalika.
Netanyahu anatambua kwamba upinzani wowote dhidi ya kuivamia Rafah ni onyo na wasiwasi tu. Kwa hiyo, utawala wa Marekani bado haujaondoa uungaji mkono wake kwa vita vya Netanyahu, ikiwa ni pamoja na kampeni yake inayotarajiwa dhidi ya Rafah.
Lakini inatka tu kupunguzwa idadi ya raia ambao watauawa ili kupunguza madhara kwa Israel, ambayo inakabiliwa na tuhuma za kufanya mauaji ya kimbari.
Mwandishi hatarajii "misimamo ya utawala wa Marekani kubadilika, hasa kwa vile unafanya kazi kwa niaba ya Netanyahu.
Mwandishi anahitimisha makala yake kwa kutaka watu waamini kile anachosema Netanyahu kuhusu kukataa kwake kuanzishwa kwa taifa la Palestina, na kwamba atapigana vita hadi mwisho, ili kufikia udhibiti kamili wa ardhi ambayo iko kati ya mto na bahari, katika ramani aliyoiwasilisha katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Septemba iliyopita.
Inatarajiwa kuwa "Israel itaendeleza vita vyake, kwa ajili ya simulizi na madai yake ya kibiblia na kihistoria. Viongozi wa vita wa Israel wanashinikiza kupanua vita katika eneo hilo kinyume na matakwa ya washirika wake ambao hujikuta wakihusika mahali ambapo hawataki, na kwa njia ambayo inadhuru maslahi yao.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah