Afya: Faida za shelisheli kwa afya

Chanzo cha picha, GETTY IMAGES
Shelisheli ni chakula maarufu nchini Jamaica. Kilifika huko kutoka Visiwa vya Pasifiki na meli ya kibiashara ya Uingereza mwaka 1794.
Shelisheli lilikuwa chakula cha bei nafuu na chenye lishe kwa Waafrika waliokuwa watumwa wakifanya kazi katika mashamba ya sukari yanayomilikiwa na Uingereza.
Miti yake hukua haraka na kuzaa matunda ndani ya mwaka mmoja baada ya kupandwa, na kutoa matunda 200 hadi 400 kwa mwaka.
"Shelisheli ni kama viazi au muhogo, linaweza kuchomwa, kuchemshwa au kukaangwa. Tunaweza hata kutengeneza unga na kutengeneza keki," anaeleza Caroline de Lisser mmiliki wa mgahawa huko Portland Parish, Jamaica.
Shelisheli linapatikana zaidi katika maeneo ya kitropiki (katikati ya dunia) na Visiwa vya Pasifiki, Karibea, na Kusini-mashariki mwa Asia – katika maeneo kama Indonesia, Ufilipino, Sri Lanka, na Kusini mwa India.
Katika maeneno ya pwani ya Arika Mashariki, shelisheli pia ni maarufu. Upishi wake hautofautiani sana na ule wa Jamaica.
“Unaweza kulipika shelisheli na nazi baada ya kulikata vipande vidogovidogo, au kulichemsha ama kulikaanga na unaweza kula ukiwa na samaki, nyama ama dagaa,” anasema Khadija Zahor, mpishi kutokea jiji la Dar es Salaam, Tanzania.
Afya ya Moyo
Shelisheli lina utajiri wa maadini ya potasiamu. Potasiamu husaidia katika mtiririko mzuri wa damu kupitia mishipa. Na kudhibiti misuli kukaza katika moyo. Potasiamu inadhibiti shinikizo la damu.
Viwango vya juu vya mafuta husababisha magonjwa mengi ya moyo na mishipa. Magonjwa haya ni pamoja na mshtuko wa moyo na kiharusi.
Utafiti wa Kituo cha Taifa cha Teknolojia kwenye Bilojia, Marekani, unaonyesha kuwa nyuzinyuzi ambazo pia zinapatikana katika shelisheli husaidia kupunguza mafuta.
Kudhibiti Kisukari
Shelisheli ni chakula bora kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari. Kwa kuwa lina nyuzi nyingi na protini na uhaba wa sukari.
Utafiti unaeleza kuwa unga wa shelisheli husaidia kudhibiti viwango vya sukari ya damu kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari.
Nyuzinyuzi hupitia kwenye utumbo polepole. Matokeo yake, chakula huchukua muda ili kumeng'enywa. Kwa hivyo, viwango vya sukari ya damu haviongezeki baada ya kula.
Usagaji chakula

Chanzo cha picha, Mike Goldwater/Alamy
Nyuzinyuzi husaidia kuboresha usagaji. Nyuzinyuzi huchukua maji ndani ya tumbo na kulainisha kinyesi. Matokeo yake, kinyesi hupita kwa urahisi.
Kwa hivyo, vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi kama vile shelisheli huleta choo kwa urahisi na kufanya usagaji mzuri wa chakula.
Pia huboresha afya ya utumbo kwa kukuza bakteria wazuri mwilini. Kwa kuongezea, tafiti zinasema huzuia maambukizi na kuvimba kwa kuboresha kinga.
Huboresha Utendaji wa Ubongo
Shelisheli ni chanzo cha madini ya chuma, vitamini C na virutubisho vingine vingi. Chuma ni muhimu kwa utendaji mzuri wa seli za damu.
Huchukua jukumu kubwa katika kusafirisha oksijeni kwenda viungo vyote. Kiwango cha chini cha madini ya chuma, kinaweza kusababisha upungufu wa damu. Pia, usambazaji wa oksijeni kwenda kwenye ubongo hupungua.
Vitamini C, vitamini E, asidi ya omega-3 vinavyo patikana katika shelisheli ni kinga. Uchunguzi unaonyesha kinga hizo hupunguza hatari ya magonjwa ya ubongo.
Fauka ya hilo, hulinda seli za ubongo na tishu. Pia hupunguza kasi ya maendeleo ya magonjwa ya ubongo, kama kupoteza kumbukumbu au uwezo wa kufikiri.
Afya ya Uzazi
Shelisheli lina asidi ya mafuta ya Omega 3 na 6. Kwa hiyo, inaboresha afya ya uazazi kwa wanaume na wanawake. Utafiti wa Kituo cha Taifa cha Teknolojia kwenye Bilojia, nchini Marekani unaonyesha, asidi ya mafuta ya omega-3 huboresha mwendo wa mbegu za kiume.
Uchunguzi pia unaonyesha asidi ya mafuta ya omega-3 hupambana na mvurugiko wa homoni kwa wanawake. Pia huongeza upinzani wa insulini. Kwa kuongezea, asidi hiyo husaidia kuzuia saratani ya kibofu na ovari.
Huzuia Saratani

Chanzo cha picha, DR. Ken Banks
Vitamini vya kinga kama vile vitamini A, vitamini C, na asidi ya mafuta ya omega-3 huzuia saratani. Kawaida, saratani hutokea kwa sababu ya ukuaji usioweza kudhibitiwa wa seli, unaotokana na uharibifu wa muda mrefu wa seli.
Kama ilivyoelezwa tayari, vitamini hivyo husaidia kupunguza seli kukua bila mpangilio katika mwili. Kwa hivyo, vitamini vya kinga huzuia ukuaji na maendeleo ya saratani.
Kwa kuongezea, utafiti wa kituo hicho pia unaonyesha vitamini vya kinga husaidia kuharibu seli za saratani.
Kudhibiti Uzito
Shelisheli linafaa katika kupunguza uzito. Shelisheli limejaa nyuzi muhimu za kudhibiti uzito. Nyuzinyuzi humfanya mtu ashibe kwa muda mrefu zaidi.
Matokeo yake, hamu ya kula vyakula visivyo na afya hupungua. Kwa hiyo, husaidia kuzuia kupata uzito usiofaa.
Kwa kuongezea, shelisheli ni chanzo cha protini. Lina idadi kubwa ya protini zote muhimu. Zikiwemo zile za kujenga misuli.
Protini husaidia katika ujenzi na uvunjaji wa kemikali mwilini. Kwa hivyo, kula shelisheli kunaweza kukusaidia kupunguza uzito.
Huboresha Afya ya Ngozi
Vitamini C huboresha ngozi. Pia hutengeneza upya seli mpya za ngozi. Utafiti wa Kituo hicho unaonyesha vitamini C hulinda ngozi kutokana na uharibifu wa jua.
Inasaidia kupunguza athari za miale hatari, ulegevu wa ngozi na dalili za kuzeeka. Hivyo, kula shelisheli hukulinda na mabadiliko ya ngozi yanayohusiana na kuzeeka.
Afya ya Mifupa
Shelisheli lina madini mengi sana, ikiwa ni pamoja na kalsiamu, fosforasi, manganese, na magnesiamu. Kalsiamu na fosforasi ni muhimu kwa mifupa yenye afya.
Huifanya mifupa kuwa imara, kuboresha uzito wa mifupa na kuzuia kuvunjika. Hivyo hupunguza hatari ya magonjwa ya mifupa.
Vitamin K katika shelisheli pia hupunguza hatari ya matatizo ya mifupa.
Tahadhari na Faida Nyingine

Chanzo cha picha, Caroline de Lisser
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Shelisheli linaweza kusababisha kushuka kwa shinikizo la damu ikiwa una shinikizo la chini la damu. Hata hivyo, huathiri watu ambao tayari wana shinikizo la chini la damu.
Linapanua mishipa yako ya damu. Matokeo yake, inawezesha mtiririko wa damu kwa urahisi, na kupunguza shinikizo lako la damu.
Shelisheli lina kiasi kikubwa cha potasiamu. Uchunguzi unaonyesha kuwa hii ni hatari kwa watu walio na magonjwa ya figo. Figo linapokuwa na matatizo, hufanya kazi kubwa ili kupunguza potasiamu.
Hilo linaweza kusababisha hali kuwa mbaya kwa mgonjwa. Katika hali kama hizo, inashauriwa kuacha kula mashelisheli. Zungumza na daktari wako au mtaalamu wa lishe kabla ya kutumia.
Maua ya shelisheli ni dawa yenye ufanisi. Maua hayo yana kemikali ambazo hufukuza mbu na wadudu wengine.
Shelisheli ni katika chakula cha mifugo. Majani na matunda yaliyoanguka huongezwa kwenye mlo, na kuufanya kuwa na virutubisho vingi kwa wanyama.
Mbao za mshelisheli ni nyepesi na imara. Kwa hivyo, matumizi ya mbao kwa useremala yameenea. Hutumika kutengeneza samani.
Imetafsiriwa na Rashid Abdalla












