Afrika Kusini: Kumkamata Putin ni kutangaza vita dhidi ya Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Jaribio lolote la kumkamata Vladimir Putin atakapozuru Afrika Kusini litakuwa tangazo la vita dhidi ya Urusi, rais wa nchi hiyo anasema.
Cyril Ramaphosa alitoa onyo hilo zikiwa zimesalia wiki kadhaa kabla ya mkutano wa kimataifa kufanyika Johannesburg, ambapo rais wa Urusi anaalikwa.
Lakini iwapo Bw Putin ataondoka katika ardhi ya Urusi, atakabiliwa na hati ya kukamatwa iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Afrika Kusini ni mtia saini wa ICC na kwa hivyo inapaswa kusaidia katika kukamatwa kwake.
Hata hivyo imekataa kuheshimu wajibu huo siku za nyuma, kuruhusu kupita kwa usalama mwaka 2015 kwa Rais wa wakati huo wa Sudan Omar al-Bashir ambaye alikuwa akisakwa kwa uhalifu wa kivita dhidi ya watu wake.
Bw Putin amealikwa Afrika Kusini mwezi Agosti, wakati nchi hiyo itakapoandaa mkutano wa kilele wa wanachama wa nchi za Brics kifupi cha Brazil, Urusi, India, China na Afrika Kusini. Jumuiya hii ya uchumi unaokua kwa kasi inaonekana na wengine kama mbadala kwa kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiuchumi.
Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini, Democratic Alliance, kimeenda mahakamani kujaribu kulazimisha mamlaka kumkamata Bw Putin iwapo ataingia nchini humo.
Nyaraka za mahakama zinafichua kwamba Rais Ramaphosa anapinga vikali hatua hiyo, akieleza kuwa usalama wa taifa uko hatarini.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
"Afrika Kusini ina matatizo ya wazi katika kutekeleza ombi la kumkamata na kumsalimisha Rais Putin," alisema katika hati ya kiapo.
"Urusi imeweka wazi kuwa kumkamata rais wake aliyepo madarakani kutakuwa ni tangazo la vita. Itakuwa haiendani na katiba yetu kuhatarisha kujiingiza katika vita na Urusi."
Rais Ramaphosa aliongeza kuwa Afrika Kusini ni mojawapo ya mataifa kadhaa ya Afrika yanayofanya mazungumzo na Urusi na Ukraine "kwa lengo la kumaliza vita kabisa", na kwamba kujaribu kumkamata Bw Putin hakutakuwa na tija.
Mwezi uliopita ulishuhudia ujumbe wa amani kwa mataifa ya Ulaya, ambapo marais wa Afrika walitarajia wangeweza kuleta Ukraine na Urusi kwenye meza pamoja lakini hatimaye walishindwa.
Mengi yametolewa kuhusu mataifa ya Afrika kusita kuunga mkono maazimio ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa kulaani vita vya Urusi nchini Ukraine.
Waandishi wa habari wanasema sababu zinatofautiana kulingana na taifa hilo - iwe ni uhusiano wa Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na Umoja wa Kisovieti, au utegemezi wa sasa wa Mali kwa mamluki wa Urusi Wagner kupambana na wanajihadi.
Kuna uhusiano wa kiuchumi kati ya Urusi na mataifa ya Kiafrika pia, si haba nchini Afrika Kusini.
Mfanya biashara mkubwa wa Urusi aliyeidhinishwa, Viktor Vekselberg, anasemekana kuwa mmoja wa wafadhili wakubwa wa chama tawala cha Afrika Kusini, African National Congress (ANC).















