Waridi wa BBC: ‘Nilipoteza uwezo wa kuona nikiwa mwaka wa mwisho chuo kikuu’

- Author, Martha Saranga
- Nafasi, BBC Dar es Salaam
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Akiwa na umri wa miaka 23 ndani mwaka wa mwisho wa masomo katika chuo kikuu akisomea shahada ya kwanza ya Usimamizi wa rasilimali watu, aliugua kichwa na macho ghafla na baadaye kuanza safari za matibabu hospitalini kwa takribani miezi miwili, baada ya hapo maisha yake yalibadilika kabisa.
Binti Kipepeo, ama Bernadetha Msigwa, ni mwandishi wa kitabu cha ‘’kipenga cha mwisho’’, alipata msukumo wa kuandika kitabu kutokana na kuwa mlemavu wa macho akikaribia kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania mwaka 2014.
Alizaliwa mwaka 1991 na kulelewa katika familia ya kipato cha kawaida akiwa na ndoto za kumaliza elimu ya chuo kikuu ili kuweza kupata sughuli ya kiuchumi itakayomuwezesha kuisaidia familia yake.
‘’Mara ya mwisho nilimuona mama yangu tukiwa hospitali’’anasimulia Bernadetha.
‘’Nakumbuka nilianza kuumwa kichwa na mishipa ya macho, hadi baadaye nilianza kuona giza na hatimaye sikuona tena’’

Chanzo cha picha, Bernadetha Msigwa
Wazazi walinihangaikia sana kutafuta matibabu kwa muda mrefu lakini haikuweza kusaidia.
Akiwa na umri wa miaka 33 sasa, Bernadetha anasema hatasahau katika maisha yake kwani haikuwa rahisi kujikubali lakini alijikaza na kuamua kwamba sasa maisha hayana budi kuendelea.
‘’Baada ya kukutana na watu wasioona walinitia moyo sana, kwamba maisha yanaweza kuendelea vizuri tu licha ya kutoona, waliniambia ninaweza kutoka nyumbani na kufanya safari kutoka eneo moja hadi lingine bila tatizo.’’
Anamkumbuka rafiki yake aitwaye Faraja ambaye alipoteza uwezo wa kuona akiwa chuo kikuu, alimtia moyo sana kumfanya kwa mara ya kwanza aweze kutoka nyumbani peke yake.
Mara ya kwanza hata família ilipata wasiwasi ikamuhoji Faraja ambaye alimuhakikishia mama mdogo aliyekuwa akiishi na Benadetha, kwamba inawezekana kabisa kufanya safari na kufika salama.
‘’Watanzania ni watu wema sana, mara zote nikiwa na fimbo nyeupe hawaachi kunisaidia’’

Chanzo cha picha, Bernadetha Msigwa
Ndoto ya elimu

Chanzo cha picha, Bernadetha Msigwa
”Baada ya kupoteza uwezo wa kuona na kukaa nyumbani kwa takriban miaka miwili, nilishauriwa kwenda kujifunza maandishi ya walemavu wa macho ama Nukta nundu.
Ilinichukua miezi kadhaa kufahamu lugha hiyo na baadaye kurejea chuoni kumalizia masomo yangu ambayo nilifaulu vizuri tu.
Ninashukuru kwamba nilikutana na walimu na wanafunzi wa ngazi mbalimbali za kielimu ambao wamepitia changamoto kama yangu na zaidi” anakumbuka.
Anazfafanua: Nilipata moyo sana na baadaye kuamua kufanya ‘’stashahada ya uzamili ya elimu maalumu’’ katika chuo kikuu huria ambayo nayo nilifaulu vizuri.
Nimepata ajira ya kujishikiza mahali, nashukuru si haba nayamudu mahitaji yangu binafsi na ninajitegemea kimaisha.
Changamoto ya ulemavu wa macho
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
‘’Maisha yalibadilika hasa kuishi katika hali ya kutoona wakati ulikuwa mzima na unaona, iliniumiza sana. Watu katika jamii wana mitazamo mbalimbali kuhusu watu wasioona”, anaeleza Bernadetha.
Anasema kuna wakati ilikuwa vigumu kuvaa mavazi bila usaidizi kwani alishangaa tu watu wakimshangaa kuwa amegeuza nguo, au watu walipomsalimia kwa kumpa mkono walimsema ana kiburi hataki kutoa mkono wasielewe kuwa haoni kama kapewa mkono.
Anaeleza kuwa wapo wanaodhani watu wasioona ni watu wanaohitaji kusaidiwa kila kitu, ama ‘’hatuwezi kufanya chochote’’ kitu ambacho si kweli.
Anasema wapo watu wema pia ambao wakati mwingine ukikutana nao kwenye usafiri wa umma wanauliza kwa nini uko peke yako?
kwanini ndugu hawakusindikizi,na unajaribu kumueleza kwamba wakati mwingine hata wanaotusaidia wanahitaji kuendelea na ratiba zao za maisha nasi kufanya majukumu yetu peke yetu.
Anaweka bayana kuwa ujasiri alio nao umemsaidia kufanya mambo mengi na kutokuwa tegemezi.
Heri kufa macho kuliko moyo
Kwa mtu mwenye changamoto kama yangu asikate tamaa, kila kitu Mungu ndiye mpangaji.
Kile ambacho mtu anadhani anaweza kukifanya akifanye kwa ujasiri akiamini kuwa kinawezekana.
”Kwa wazazi wenye watoto wenye ulemavu tafadhali msiwafungie ndani. Ninajivunia ujasiri ambao Mungu amenipa kuweza kuendelea na maisha. Ninaweza kufanya kazi na kumudu maisha yangu. Sijawa tegemezi sana kusubiri kufanyiwa kila kitu”.
Uandishi wa vitabu na matarajio ya baadaye

Chanzo cha picha, Bernadetha Msigwa
Kitabu cha “Kipyenga cha mwisho” ni simulizi ya maisha yake Bernadetha baada ya kujikubali hali yake.
“Wazo la kuandika kitabu cha Kipenga cha mwisho nililipata kupitia maisha yangu mwenyewe baada ya kupoteza uwezo wa kuona”.
Ninaamini kwamba kwa kuwa bado niko hai nina kila sababu ya kufurahia maisha na kupambana nayo hadi pumzi ya mwisho.
Ninapenda kila mmoja akisome ili aweze kupata tumaini juu ya jambo lolote analodhani linamkatisha tamaa na kumruddisha nyuma”. Anaeleza kwa uso wa bashasha na wa kutia matumaini.
Anaelza zaidi kuwa kama yeye ameweza kujikubali na kuwa na matumaini tena kuhusu maisha basi kila mtu anaweza.
”Hakuna kukata tamaa hadi mwisho wa maisha yako.Kitabu hiki kwa sasa kinapatikana kwangu, nilitoa nakala chache kwanza, ninataraji kuandika vitabu zaidi ili kuwapa moyo walemavu kama mimi na jamii kwa ujumla ili wasikate tamaa katika maisha yao”.
Vipi kuhusu mahusiano?
Nina rafiki ambaye Mungu akijaalia huko mbeleni anaweza kuja kuwa mume wangu. Tulikutana kwenye daladala tukabadilishana na namba za simu na kuanza kuwasiliana.
Amekuwa ni rafiki mzuri ananichukulia vizuri hasa kuniamini katika uwezo wangu wa kufanya vitu mbalimbali, aliweka wazi.
Ana ombi moja kwa serikali: Kutoa kipaumbele pia kwa wasioona na hata wenye ulemavu wote, yaani kupata kazi inapokuwa shida, inawakatisha tamaa walemavu walioko shuleni.
Lakini wakiona fursa sawa kwa walemavu na wao wanastawi itawatia moyo kusonga mbele.
Pia kuna wale ambao hawakupata fursa ya kusoma sana, mamlaka za serikali zinaweza kutengeneza mifumo ya kuwainua kiuchumi na kuwafanya wasiwe tegemezi na ombaomba barabarani.
Imehaririwa na Florian Kaijage












