Waridi wa BBC: ‘Nimewafunda wanawake 700, sitaki yeyote akosee maishani’

mm

Chanzo cha picha, Iren Mbowe

    • Author, Na Esther Namuhisa
    • Nafasi, BBC Dar es Salaam

“Utaratibu wa kurudi nyumbani ilikuwa saa 12 jioni ndiyo mwisho, ila siku moja nilichelewa na kufika nyumbani saa moja na nusu usiku, baba yangu aliniambia nirudi huko nilipotoka na ndoa yangu ilianzia hapo. Siku iliyofuata, mchumba wangu na familia yake waliamua kupeleka salamu za posa nyumbani ili aweze kunichumbia na nikafunga ndoa ya kimila…”

Hiyo ni sehemu ya maelezo ya Irene Mbowe, aliyeolewa mwanzoni kabisa mwa ujana na sasa ni maarufu katika mitandao ya kijamii kwa mafunzo ya ndoa na familia yakiwemo yanayoonekana kwa baadhi ya watu kukosa uhalisia. Katika mazungumzo yake na Esther Namuhisa wa BBC, Irene anaelezea pia umuhimu wa kutunza siri za watu anaowashauri, kiasi kwamba simu yake ikiharibika huitumbukiza chooni ili kuepusha siri kuvuja. Amefichua kuwa tangu mumewe kufariki dunia mwaka 2020 ametongozwa na wanaume takribani 90 lakini hakuna aliyefikia vigezo vyake…

…Niliolewa nikiwa na miaka 19 huku mume wangu akiwa na miaka 26 nikiwa sina mashaka wakati nnaolewa kwa kuwa mama yangu alikuwa ameniandaa tayari kuingia kwenye ndoa.

Mama yangu alipinga sana utoaji wa mimba, alisema kabla ya kuingia kwenye mahusiano, ni muhimu kujipima kwanza. Mama yangu alianza kunifundisha kwa wakati kuwa kuolewa katika umri huo ni sahihi ingawa kwa sasa idadi ya mabinti wa miaka 30 ambao hawajaolewa imekuwa kubwa.

Kuolewa katika umri mdogo, si jambo ninalojutia kwa kuwa sasa ninaona kuwa mtu ukifika miaka 35, ni ngumu kuolewa, wengi wanaangukia katika ndoa za watu au kuwa na mahusiano na vijana wadogo.

Hivyo, ninadhani ni vyema kama mtu hana vikwazo vya kusubiri kumaliza elimu bora aolewe. Ninashukuru kuwa nimekaa kwenye ndoa kwa miaka 23, na nimeona thamani ya maisha ya ndoa.

nn

Chanzo cha picha, bbc

Kwa nini uliamua kuwa mwalimu kwa wanawake wengine kuhusu masuala ya ndoa?

Napenda kumuhudumia mwanaume. Huyu mwanaume akiwa mume, akiwa kaka, mwajiri au mtoto. Siwezi kubishana na thamani ya mwanaume.

Mimi ni kungwi ambaye nimepata umaarufu mtandaoni kwa sababu nimekuwa sawa na mtetezi wa wanaume kwa kubeba mtazamo chanya ambao ni muhimu katika jamiii.

Baada ya kuishi kwenye ndoa kwa muda, na mitandao ya kijamii ilipoingia nilifungua akaunti ya Facebook na marafiki zangu walikuwa wanashangaa kuwa nimeolewa maana nilikuwa mtundu mtundu kidogo hawakuamini kuwa ningeweza kuwa mke wa mtu.

Lakini niliwastaajabisha zaidi marafiki zangu kwa kuanza kuwapa elimu juu ya ndoa. Ninajulikana kwa jina la bembeleza, na jina langu nimeliishi katika ndoa kwa kuwa mbembelezaji. Muonekano wangu tu, umekaa kikungwi!

Nilitamani kuwa mwalimu wa kuwafundisha wanafunzi darasani ila namshukuru Mungu kuwa nimekuwa mwalimu wa wanawake.

mm

Chanzo cha picha, Iren Mbowe

Je, Machapisho ya mtandaoni yanahakisi uhalisia?

‘Baba Nema samahani mume wangu umeme umeisha….Baba Nema nimekutumia laki tatu ufurahi na marafiki…lugha laini kwa mwenza wako ni muhimu. Kila unachokifanya ni muhimu kushirikishana na mume wako.

Tumia lugha laini, maana huwezi kujua mapambano gani mwenza wako anapigania iwe katika ujenzi, ada na kutafuta kipato kwa ujumla.’

Machapisho yangu yamekuwa yakiwashangaza wengi maana nimekuwa nabembeleza hata pasipohitaji kubembeleza. Video fupi ninazochapisha ni namna ya kupeleka ujumbe kwa jamii. Nikimaanisha kuwa Mwanamke ukiwa umechaguliwa kuolewa basi ujue kuwa hiyo ni thamani kubwa sana, ni sawa na kupata ajira.

Kuolewa ni sawa na kupita usahili, ndiyo ukaajiriwa vivyo hivyo kwenye upande wa ndoa.Mume na mke ni marafiki, hivyo kuongea kiurafiki ni muhimu, lugha laini ni muhimu.

mm

Chanzo cha picha, Irene Mbowe

Udhalilishaji katika mitandao kijamiii

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuna wakati nilijikuta kuwa mimi ni barua ambayo wengine walikuwa wanaisoma. Ninapenda kukosolewa, kuna wakati nilikuwa ninatumia mkorogo mkali ila kuna dada alikuja kunishauri kwa kunisihi kwanza na kuniambia niache hivyo vipodozi vinaharibu ngozi yangu. Kipindi natumia nilikuwa naamini kuwa mweupe ni urembo. Jambo ambalo najuta katika maisha yangu, ni vipako yaani mkorogo, ilinichukua muda kukabiliana na unyanyasaji huo.

Na jambo ambalo watu wa mtandaoni wananinyanyasia zaidi, wanahoji ilikuwaje nilibadili rangi ya ngozi yangu. Kuna wanaopenda watakusifia ila wengine ndiyo wanatumia fimbo ya kunipigia. Mtandaoni kuna udhalilishaji mwingi sana ila nilijiambia kuwa sitakasirika.

Nitajali lugha inayotumika, kwa kuondoa maoni ya udhalilishaji wa matusi na kutumia lugha chanya. Mitandao ya kijamii kuna wakati unaandika ujumbe, lakini wao wanatumia kashfa, udhalilishaji na kadhalika na hilo nimeweza kulipokea kwa kuwa ninajua mtandaoni ninakutana na watu ambao wana changamoto mbalimbali pia.

Mume wangu aliwahi kunipa angalizo pia nifanye yote ila isije kutokea udhalilishaji wa mtandaoni ukayumbisha mahusiano yetu. Ninakumbuka kuna wakati nilikuwa ninajiandaa kwa warsha kubwa, kabla sijapanda jukwaani nilitumiwa picha za mume wangu akiwa amelewa sana na ujumbe ukisema;

‘Angalia kungwi wenu mume wake yuko kwenye ulevi uliopitiliza, ilinibidi

nizime simu siku 3 ili nipate utulivu’

Watu wa mitandao wanapaswa kuelewa sisi ni binadamu kama watu wengine na tuna familia licha ya kuwa kioo cha jamii, ni vyema kujali hisia zetu.

mm

Chanzo cha picha, Irene Mbowe

Umuhimu wa elimu ya ndoa kuanzia umri mdogo

Kuna umuhimu mkubwa kutoa elimu kwa mwanamke maana wanawake ndiyo wanatoa mafunzo ya awali kuanzia kwa watoto wa kike na wa kiume. Mwanamke anapaswa kuwa na elimu yenye maarifa zaidi kwa kumtengeneza mama au baba wa baadaye.

Mwanamke atengeneze watoto bora, ambao ni mume au mke wa baadaye. Si rahisi kumfundisha mtu aliyekuwa mtu mzima tayari, bora elimu itolewe kwa ajili ya watoto.

Hata hivyo, mitazamo ya wataalamu kadhaa wa masuala mahusiano, ndoa na familia ni kuwa changamoto kubwa inayowakabili wanandoa ama wenza wa kiume kwa sasa ni kukosa uelewa na maarifa kuhusu namna bora ya kuishi na weza wao wa kike na kutunza familia, hivyo kuwepo umuhimu wa kuwafunda pia wanaume ili wazilee familia vizuri zaidi.

mm

Chanzo cha picha, Irene Mbowe

Nilibahatika kuishi ndoa kwa miaka 23, ndoa isiyo na doa mpaka mume wangu alipofariki, changamoto zilizokuwepo niliziweza…hakuna kitu kisicho na gharama, machozi yakitoka ni ya furaha tu. Nilikuwa namkumbusha pia mume wangu aende kufurahi na wenzake, ukitaka kumla bata usimchunguze sana.

Mpaka sasa nimewafunda wanawake 769, na nina uwezo wa kuwakumbuka kila mmoja kwa jambo ambalo nilifanya wakati wa kumfunda. Kati ya wote hao, hakuna ndoa iliyovunjika na zote zimebarikiwa kupata watoto, hivyo namshukuru Mungu sana. Jambo muhimu katika shughuli zangu ni usalama wa siri za mtu, simu yangu ikiharibika ninaitupa chooni. Sifichi cheni zangu kama ninavyoficha simu yangu. Jamii imenipokea kwa heshima kwa kile ninachokitoa kwa jamii, ninajivunia sana.

Kifo cha mume kilinifundisha kuwa mapenzi ni maisha

Nilisikitika sana kumpoteza mume wangu, Ila kikubwa nilikuwa ninampenda sana mume wangu. Mume wangu alifariki ghafla ingawa alikuwa ana changamoto za kiafya.Nilipata misiba minne;

Msiba wa mume, mume aliyenijali na kunipenda, mume aliyekuwa ananihudumia kwa asilimia 90 na kupotelewa na rafiki kipenzi ‘Bonge la bwana’

Maisha yangu yalibadilika ghafla.. na ilinichukua muda kubadili mfumo wangu wa maisha. Maisha yangu yalibadilika sana, nikajaribu taratibu kurudisha maisha yangu kusimama mwenyewe. Kwa sasa nina mjukuu mmoja na aliniacha na watoto watatu.

Baada msiba, nilikaa nikajitathmini mapenzi ninayapenda na ninayaweza lakini sijapata anayekidhi vigezo vyangu mpaka sasa ingawa tangu mume wangu afariki nimetongozwa na wanaume 87 mpaka sasa.

nn

Chanzo cha picha, Iren Mbowe

Ninatamani kuwa mama bora, na sitaki kujeruhi watu wengine. Suala la kuolewa tena bado, mapenzi na mahusiano ni maisha hivyo si jambo la kukurupuka. Nina Watoto ambao napaswa kuwatambulisha, maana watoto wa miaka 20 kuwatambulisha si jambo rahisi. Kwangu, utu ndiyo jambo la msingi, si rahisi kupata ndoa. Mimi ni mrembo sana, mimi ni mjanja na mimi ni ‘piece kali’ (mrembo haswa).

Ndoa ni maisha yenye thamani kubwa hivyo napaswa kufanya maamuzi sahihi. Familia ni kitu cha thamani sana, tutafute fedha na elimu lakini tusisahau kuwa familia ni kitu cha thamani sana. Nimejiwekea ratiba, kwa ajili ya familia, jamii, masuala ya kipato pia nina ratiba. Siku hizi wazazi wengi wamekuwa wanajisahau kwenye ratiba ya kazi zaidi ya familia, wengi wanakimbizana kutafuta fedha zaidi ya malezi.

mm

Chanzo cha picha, Irene Mbowe

Unaweza pia kusoma

Nilipokosea staki mwanamke mwingine akosee, nilipopatia nataka mwanamke mwingine apatie zaidi.

Mtu anayepita kwenye changamoto anaweza kumfundisha mwingine vizuri zaidi.Binafsi, ninapenda sana kujifunza ili kukusanya maarifa. Tusitumie maneno ya kashfa bali lugha nzuri kama ninavyotumia lugha nzuri kueleza wanaume ni wazuri si wabaya.

Ni muhimu kumfunda, mwanamke kuanzia urembo, uongozi, kuishi na mume, ujasiriamali. Kundi kubwa la wanawake wanaolewa si kwa sababu ya mapenzi bali wanataka kufanya maisha, ndiyo maana tatizo kidogo likirudia mara tatu, mtu anataka talaka yake. Kila mmoja akisimama katika nafasi yake kama mume, mke, mzazi na mtoto, Maisha yatakuwa bora sana tu.

Baada ya jamii kunikubali niliamua kuigusa jamii kwa kuanzisha kituo cha watoto ambao walikuwa wanaishi katika mazingira magumu. Watoto wengi wanaoishi katika mazingira magumu wamefikia hapo kutokana na migogoro ya ndoa. Wazazi wakipendana, tunazalisha jamii yenye afya bora ya akili, mwili mpaka ya rohoni.

Unaweza Pia Kusoma

Imehaririwa na Florian Kaijage