Waridi wa BBC : Nilikimbia ‘dogoli na okuleya’ kutimiza ndoto yangu ya kuwa sauti ya jamii

Chanzo cha picha, Annastazia Rugaba
- Author, Esther Namuhisa
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Kipande cha gazeti kilichofungia sabuni kilivyonipa taarifa ya thamani
- Bosi wangu alivyochana barua na kuifuta ajira yangu
Kutoka katika kisiwa cha Ukerewe kinachopatikana katika ziwa Victoria kaskazini magharibi mwa Tanzania ndipo alikozaliwa na kukulia Annastazia Rugaba, 40 ambaye simulizi ya safari ya kuifikia ndoto yake kuwa sauti ya jamii imejaa vizingiti vingi alivyokabiliana navyo akiwa mtoto wa kike.
Annastazia ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Idara ya utetezi katika taasisi ya kiraia ya Afrika mashariki TWAWEZA, amezungumza na Esther Namuhisa namna mila potofu, unyanyasaji wa kijinsia na fikra hasi vilivyompa ari ya kupigania hatma yake kupitia elimu.

Chanzo cha picha, Anna Rugaba
Alizaliwa katika mazingira ya mapambano. Mara tu baada ya baba yake kufariki na mama yake kubaki mjane aliyepoteza urithi kwa wakwe zake bila usaidizi wa malezi kwa watoto.
Akiwa mtoto wa tano, aliyekosa malezi ya baba tangu akiwa na umri wa miaka mitatu, hakutarajiwa kuwa angefika katika hatua aliyofikia sasa.
“Kwa sasa naweza kusema nimejipata lakini natamani vijana waanze kujitafuta mapema na si wakiwa na miaka 40 kama mimi”
Annastazia anasema amekuwa katika hali ya ukiwa baada ya mama yake kudhulumiwa na wakwe zake baada ya baba yake kufariki dunia, na haikuwezekana kupambana na baba mkwe wake ambaye alikuwa na uongozi wa uchifu pamoja na utajiri mkubwa.

Chanzo cha picha, Anna Rugaba
Alibahatika kuanza shule akiwa na umri mdogo tofauti na wasichana wengine, Watoto wengi kisiwani hapo kipaumbele kilikuwa ni kucheza dogoli, ambayo ilikuwa inathaminiwa sana zaidi ya masomo na ilikuwa inachezwa jioni katika soko au kituo cha burudani.
Ukerewe, mtoto wa kike akivunja ungo haruhusiwi kulala nyumba moja na wazazi wake halikadhalika kwa watoto wa kiume wakibalehe wanapaswa kujenga kibanda nje maana wana uwezo wa kuoa au kuolewa.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ilikuwa ni kawaida kwa mtoto wa kike kuagizwa na mzazi wake kwenda kutafuta sabuni, bila kupewa ela.
Ukisikia kutafuta sabuni, kwa lugha nyepesi ina maana uende ukajiuze ili uweze kupata fedha za kutafuta sabuni.
Ilikuwa ni aibu kwa mtoto wa kike kumuomba baba sabuni au mafuta, ilikuwa, lazima ukajitafutie fedha mwenyewe.
Na njia halali ya kujitafutia fedha ilikuwa ni kwenda mwaloni (ufukweni) kubadilishana bidhaa na wavuvi. Unakwenda na unga kwenye beseni unapewa Samaki, au kuni alafu unapewa samaki ambao unaweza kwenda kuwauza sokoni au kwenye sehemu mbalimbali, ingawa kuuza pombe ndiyo ilikuwa njia rahisi zaidi.
Wasichana wengi hawakuweza kumaliza shule ya msingi, waliishia darasa la pili au la nne.
“Nadhani Kitu kilichonisaidia, sikuwa mwenyeji wa jamii ile, wazazi wangu walihamia kwa ajili ya kazi.
Nyumbani kwa asili kulikuwa Kagera, baba angu asili yake ilikuwa msubi kutoka Biharamulo na mama muhaya kutoka Bukoba”.
Hivyo sikuwahi kwenda kwenye dogoli lakini mwaloni na sokoni nilikuwa nakwenda maana ilikuwa ndiyo njia ya sisi kupata kipato pia.

Chanzo cha picha, Anna Rugaba
Jinsi mkono wa kushoto ulivyosababisha kukata tamaa ya kusoma
Tangu akiwa mdogo, alikuwa na changamoto ya kutumia mkono wa kushoto. Mwalimu wake mmoja alikuwa akimchapa sana akikuta anaandika kwa mkono wa kushoto na alikuwa anawaambia wanafunzi wenzake wamzomee kwa kosa la kuandika kwa kutumia ‘mkono wa mavi’
“Hali hiyo ilininyima raha sana yaani hadi sasa huwa nikimkumbuka ninaumia sana kwani ilinitesa na kuniua ujasiri wangu.
Ukiandika vibaya pia ilikuwa ni tatizo lakini baadaye niliweza kutumia mikono yote miwili.
Na nilibaini kuwa kutumia mkono wa kushoto si kosa bali ulikua mtazamo tu.

Chanzo cha picha, Annastazia Rugaba
Tiba za waganga wa kienyeji na maradhi ya kudondoka
Annastazia anasema alipata magonjwa ambayo hayakueleweka aliyapata vipi, “nilikuwa nadondoka kila wakati, Hospitali walisema si kifafa maana sitoi povu na nilikuwa nikianguka nakuwa sina fahamu kwa muda wa nusu saa na kuanza kuugua.
Kuanzia darasa la nne niliugua sana ugonjwa huo wa kuanguka na tiba kubwa katika eneo hilo ilikuwa kwenda kwa waganga wa kienyeji.
Mama yangu alikuwa haamini masuala ya uganga wa kienyeji ila kwa kuwa niliugua sana alilazimika kunipeleka, kwa hiyo nilipelekwa kwa waganga wa kienyeji wa kila namna.
Nilipitia mateso makubwa yasiyoelezeka, mifumo ya matibabu ya kuchanjwa au kuogeshwa na kutishiwa vitu vya ajabu, kuwekwa kwenye nyumba za kutisha.
Nilikwenda kwa waganga wa kila kabila waliokuwa katika kisiwa hicho.
Sikupona mpaka namaliza darasa la saba, na shule niliudhuria siku chache sana, yaani ilikuwa hadi mara mbili kwa wiki.
Mpaka leo ukiniuliza ilikuwaje, nilifaulu katika maziingira yale.. sina jibu maana katika darasa la watoto zaidi ya sitini, tulifaulu saba tu.

Chanzo cha picha, Annastazia
Ukiongea lugha ya Kiingereza unatishiwa kurogwa
Nilisoma katika shule niliyochaguliwa kwa kipindi cha mwaka mmoja tu, shule ilikuwa na walimu wawili tu, Agricultural Science (Sayansi ya Kilimo) na Book Keeping (Utunzaji vitabu ya mahesabu) na walikuwa wanafundisha kwa Kiswahili.
Kwa bahati nzuri, dada yangu alifanikiwa kupata shule Mwanza nikahamia.
Ilikuwa shule ya kuzungumza lugha ya Kiingereza, wakati mimi nimetoka Ukerewe ambako ukizungumza Kiingereza unatishiwa kurogwa na iliaminika ukiongea Kiingereza ni kuwa unaringa.
Hata walimu iliwalazimu kuongea Kiswahili tu.
Kwa hiyo ilikuwa ni jambo gumu kwangu, adhabu za kutoongea Kiingereza nilipata nyingi sana kutokana na imani ya huko nilipotoka.
Na ilikuwa ngumu kwangu kusoma masomo 12 badala ya masomo mawili niliyosoma kidato cha kwanza.

Chanzo cha picha, Anna Rugaba
Kipande cha gazeti kilivyobadili dira ya maisha
Nilipomaliza kidato cha nne, uchaguzi wa kidato cha tano sikuupata mapema, hivyo nilikata tamaa na kutaka kwenda kusomea ualimu. Niliona ndoto zangu zimeishia hapo.
Lakini bila kutarajia, mtoto wa jirani alikuja na kipande cha gazeti, alichofungia sabuni kikiwa na jina langu, Annastazia Rugaba, ingawa nyumbani walikuwa wamenizoea kwa jina la Neema hivyo hakujua kama ni mimi.
Na karatasi hiyo ilikuwa imeandikwa nimepangiwa shule ya sekondari Kibiti, mkoa wa Pwani. Hata nilikuwa nimechelewa shule, hivyo mama yangu alipambana kuuza ng’ombe wawili ili niende shule.
Chupuchupu ndoa ya lazima-‘Okuleya’
Wakati wa kipindi cha likizo ya kusubiri majibu ya kidato cha nne, Annastazia alinusurika masaibu ya kuolewa kwa lazima, kijijini kwao Bukoka maarufu ‘okuleya’
Okuleya ni utamaduni wa jamii ya Wahaya mkoani Kagera ambapo kijana wa kiume hufanya njama kwa kushirikiana na vijana wenzake na kumvizia msichana hususani nyakati za jioni na kukamata kwa lazima. Wasichana wengi hushindwa kuondoka kwenye ndoa hizo kwa sababu ya mtazamo wa jamii kuwa kitendo cha kulala kwa kijana hata usiku mmoja anakuwa si msichan tena bali mwanamke.
Binti ukiolewa kwa namna hiyo katika tamaduni za kihaya, wanasema ukirudi nyumbani kizazi cha kiume kitakufa hivyo huchukuliwa ndiyo ndoa halali. Hata hivyo katika miaka ya karibinu ndoa za namna hiyo zimepungua kwa kiwango kikubwa.
Annastazia anasema aliwekewa mtego muda ambao alizoea kupita barabara fulani lakini siku hiyo alibadili njia na ndiyo ikawa pona yake. Ukichukuliwa hupaswi kurudi nyumbani.
Nilikuwa na ndoto kubwa sana ya kuwa mwanasheria ili kutetea wanawake wajane.
Ile ni mila ambayo imeathiri wasichana wengi sana, inaaminika kuwa kama ukichukuliwa alafu ukarudi kwenu basi kila kiumbe cha kiume kitakufa nyumbani kwenu, kama baba yupo atakufa, kaka au hata mbuzi dume au jogoo atakufa.
Kwa hiyo mabinti wengi wakishakwenda huko hawarudi nyumbani na hata wadogo zangu waliolewa kwa namna hiyo ila mimi nilinusurika kwa kwenda kusoma Rufiji.
Ambapo nilisoma na kufaulu kidato cha sita kwa kupata daraja la kwanza la alama tisa.
Ila nilipofika chuoni, nilikatishwa tena tamaa kuwa siwezi kusoma sheria kwa kuwa sina daraja la kwanza la alama saba.
Niliamua kuchagua masomo ambayo ilikuwa ndiyo kwanza yanaanza, na wengi walinishangaa ninatoka familia maskini alafu ninachukua riskya kusoma programu mpya.
Nilikuwa na maisha magumu sana, hata kupata chakula ilikuwa shida.
Mwaka wa kwanza sikuwa na mkopo lakini mwaka wa pili nilipambana na kugombea uongozi katika serikali ya wanafunzi na nikapata, nikawa makamu wa rais wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kwa neema nikapata mkopo na nikaweza kusaidia wanafunzi maskini kupata mikopo.
Shahada ya Mawasiliano ya Umma imenisaidia kupaza sauti kwa wasiokuwa na sauti licha ya kuwa sikuweza kuwa mwanasheria.
Hapo awali nilipofika darasa la saba sikio langu lilikufa, hivyo mimi ninasikia kwa kutumia sikio moja tu. Mwanzoni tulijua kaka yangu alinipga kofi ndiyo nikapata hali hiyo lakini la hasha…nilipokwenda kusoma Uingereza niliweza kwenda kuangalia vipimo vikubwa katika sikio langu, daktari huko aliniuliza nilipokuwa mdogo sikuugua ugonjwa unaitwa ‘mums’ kwa kikerewe tunaita ‘matuyuyu’ lakini sisi tulikuwa tunaamini ni kulogwa
Nilivimba pande zote mbili, na sikupata tiba, sasa kumbe ugonjwa huo ndiyo ulisababisha nisisikie na siwezi kutibika.
Wataalamu walisema kupigwa kofi kusingesababisha athari ya namna ile maana neva zilikuwa zimekufa.
Lakini Maisha yangu yanaendelea vizuri tu, hata ni ngumu kwa watu kugundua kuwa sisikii sikio moja na wengine ndiyo watafahamu leo.
Lakini nilipokuwa mwaka wa kwanza, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilikuwa ninapenda sana kutangaza.
Kiu yangu ya kuwa na kipindi cha wanawake na watoto lakini siku ya usaili ile naanza kujitambulisha sijamaliza hata, mwalimu akaniambia sauti kama nimemeza chura, siwezi kutangaza…
Iliniuma sana kwa kuwa wenzangu waliokuwa wanatangaza walikuwa wanapata posho na mimi hali yangu ilikuwa ngumu sana.
Wakati huo maji yaliyokuwa yakifungwa kwenye mifuko ya plastiki yakiwa yamepanda bei, siwezi kukunua maji ya chupa, nauli pia shida.
Nilivunjika moyo, kwa hiyo nikaachana na utangazaji.

Chanzo cha picha, Annastazia
Je anachokifanya sasa anakipenda?
Kiukweli katika miaka hii ya 40, ninaweza kusema kuwa nimejipata.
Kwa maana kwamba ninafanya kitu ninachokipenda mno.
Ingawa kuna wakati niliwahi kuwania nafasi ya kuwa mwanasiasa, lakini mwalimu wangu mmoja aliniita na kunishauri kuwa mimi si mwanasiasa, jambo ambalo ninamshukuru mpaka leo.
Aliniambia niende kwenye NGO nitaitumikia jamii vizuri zaidi.
Kuna wakati nilikuwa nafanya kazi Mufindi, Iringa, nilipokea barua kuwa nimechaguliwa kuwa mwalimu msaidizi katika chuo kikuu ila nilipofika, makamu mkuu wa chuo hakutaka kuniona na nikaambiwa barua yangu ya ajira aliichana.
Licha ya kwamba nakala ninayo, ila waliniambia ni ngumu sana kunipokea kwa sababu wakati nikiwa kiongozi wa serikali ya wanafunzi niliongoza mgomo wa kudai vifaa, jambo ambalo liliathiri kazi yake.
Iringa mpaka leo kuna kina Annastazia wengi kwa kuwa nimewalea vizuri.
Kwa kweli mambo makubwa, nimepata wigo mpana sana kwa kufanya tafiti nyingi, nmetembea nchi nyingi sana duniani, mpaka hati yangu ya kusafiria ilikuwa inajaa.
Nimesoma Uingereza mimi ambaye nilikuwa sijui Kiingereza nilijikuta kuwa mwanafunzi bora.
Nimepata uzoefu mkubwa katika jamii ya Tanzania, na pia kusimamia idara ya Afrika mashariki.
Mawasiliano ya umma ni masomo mazuri maana imekuwa kama bomba, maana naweza kutuma ujumbe na ninaweza kutoa ujumbe ueleweke na kila mtu
Ni stadi ambayo, ninathubutu kusema kuwani mtu niliyefanikiwa sana haswa nikiangalia mapito niliyopita.
Ninatamani jamii zetu ziendelee kutoa fursa kwa watoto wa kike maana mimi mpaka leo familia yangu haiamini kuwa niko hatua hii.
Maana safari ya kuugua ugonjwa wa kudondokadondoka, kutosikia, kuandikia mashoto mpaka nimefika kuwa mkurugenzi.
Hata nilipotangazwa kuwa naibu rais wa chuo watu walishangaa, hata dada yangu aliuliza hivi hicho chuo walikosa mtu kabisa?.
Nataka kusaidia jamii yangu, sitamani wajitafute wakiwa na umri mdogo si mzee kama mimi.
Nimeanzisha programu binafsi ya kuwasaidia vijana wanaomaliza kidato cha sita ili kusaidia kufanya maamuzi ya masomo gani kijana anaweza kuchagua akiingia chou kikuu.
Niliolewa mapema na niliingia katika majukumu ya mke na mama katika jamii ambayo inamtaka mwanamke kuwa mnyonge na asifukuzie ndoto zake.
Ukiolewa yaani kila kitu kimeisha, ilikuwa ni vigumu sana kupita hayo yote ili ukubalike katika hiyo jamii
Ila changamoto zote ndiyo zimenipa misuli ya kuitwa Annastazia wa leo.
Imehaririwa na Florian Kaijage












