WARIDI WA BBC 'Niliamini nikinywa mkojo wangu ningepona HIV'

Na Anne Ngugi

BBC Swahili

TH

Chanzo cha picha, Dorothy Onyango

Dorothy Onyango mwaka huu ana miaka 66 ,ameishi na VVU kwa miaka 33 sasa , kwa simulizi yake mwenyewe anasema kuwa hakutumai kuwa wakati kama huu, miongo mitatu baadaye angekuwa hai hasa baada ya kuambukizwa virusi vinavyosababisha Ukimwi , kipindi ambacho mtu angepatikana na HIV alionekana kama msinzi mkubwa ,kulingana na anavyosimulia .

'Ninaona kama muujiza kuwa mimi ni mama ambaye ametimiza miaka ya kuitwa mzee na ningali hai , unajua kuwa mimi niliambukizwa HIV nikiwa bado kijana wa miaka 33 , nimepitia mengi baada ya kuambukizwa virusi lakini namshukuru mwenyezi mungu kuwa niko hai hii leo' anasema Dorothy

Alivyoambukizwa HIV

TH

Chanzo cha picha, Dorothy Onyango

Maelezo ya picha, Dorothy ameshinda tuzo kadhaa kupitia shirika lake la WOFAK .

Wakati Ulimwengu ukiadhimisha siku ya Ukimwi duniani siku ya ijumaa wikii hii , Dorothy ni mwingi wa tabasamu hasa akifikiria pandashuka alizozipitia .

Mwaka wa 1990 ndio mwaka ambao mama huyu alifahamishwa kuwa alikuwa ameambukizwa virusi vya HIV ,wakati huo anasema kuwa ilikuwa vigumu kwa mtu kujitokeza waziwazi kuzungumzia hali yake .

Dorothy anakumbuka miaka hiyo ikiwa na unyanyapaa na chuki dhidi ya watu kama yeye .

Mama huyu anakiri kuwa hadi wakati alipopewa majibu ya kuwa na Virusi vya HIV wakati wote alikuwa na dhana kuwa HIV ni ya watu washerati asijue kuwa atakuwa mwathiriwa .

Wakati alipopewa taarifa za hali yake ya Ukimwi akilini mwake alikuwa na picha ya kutamausha ya jinsi mwili wake ungedhoofika na hatimaye afariki kabla ya kutimiza ndoto zake .

Hii dhana hasa ilitokana na matangazo ya hapo awali ambayo ilionesha picha za waathiriwa wa HIV wakiwa wamembamba na bila afya .

Jaribio la kunywa mkojo

TH

Chanzo cha picha, Dorothy Onyango

Maelezo ya picha, Dorothy alikunywa mkojo wake akiamiani atapona HIV , ila hakuona mabadiliko .
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

“Miaka 33 iliyopita hukuweza kuzungumza hadharani kuhusu VVU. Tulikuwa tunakutana kwa siri kama wanawake wenye VVU ili kuzungumza juu ya changamoto zinazotukabili, hakukuwa na dawa wakati huo, na zile zilizokuja zilikuwa za gharama kubwa' Anasema Dorothy

Kisa cha kwanza cha VVU kiliripotiwa nchini Kenya mwaka wa 1984. Kwa wale waliopimwa, siku zao zilihesabiwa. Wengi walilazimika kubeba mzigo mkubwa wa unyanyapaa, na kutengwa na familia na marafiki. Watoto wengi wakawa mayatima, na wanawake wakawa wajane,anasimulia Dorothy.

Dorothy akiwa miongoni mwa kundi la watu ambao waligunduliwa na ugonjwa huo mapema miaka ya 90, waliishi na changamoto na sasa wamezeeka wakiwa na virusi , mama huyu anasema kuwa ilichukua muda wa miaka mitano kwa yeye kupata ujasiri wa kuzungumzia hali yake hadharani.

Mama huyu anakumbuka mengi aliyojaribu kuyafanya wakati huo kama njia ya kuondoa virusi kutoka kwa mwili wake.

"Kwa kukata tamaa, nilitumia chochote nilichoambiwa kinaweza kutibu VVU. Nilikunywa kwa mfano Kemron, Palm Omega, na wakati fulani, nilikunywa mkojo wangu. Nilihudhuria mkutano huko Japan na mmoja wa watu waliokuwa huko kutoka Asia alisema kwamba anapokojoa mara ya kwanza asubuhi,alitumia mkojo wake - baada ya kurudi nyumbani nilijaribu kunywa mkojo mara mbili au tatu lakini sikuweza'.

Mwanga mkubwa umekuwa katika shirika lisilo la kiserikali alilounda miaka ya tisini , ili kuleta wanawake waliokua na VVU wakati huo pamoja kama njia ya kuendeleza uhamasisho na pia kuwapa moyo wakati huo mgumu kwa waliokuwa wakiishi na maambukizi ya HIV .

Kuishi na HIV uzeeni

TH

Chanzo cha picha, Dorothy Onyango

Akiwa na miaka 66 amasema amekuwa ni mwanamke mwangalifu zaidi kuhusu maisha yake ya kila siku na mitindo wake wa kuishi , kwa mfano anachagua sana aina ya chakula anachotumia au lishe yake kwa jumla na kujali sana afya yake ya kiakili.

Dorothy pia hufanya mazoezi kila mara .

Mama huyu ni mwanzilishi wa shirika la WOFAK (Women fighting Aids in Kenya ) kupitia shirika hili anasema kuwa amelenga kuhakikisha kuwa kila mwanamke licha ya umri wake ,ambaye ana HIV anajukubali na kuendelea na maisha yake kwa njia bora .

Dorothy ameandika kitabu kinachohusu maisha yake na hali ya kupambana na virusi ya HIV . Kitabu chake amekipa jina 'Beyond Public Confesion' , ambapo amelenga sana jinsi yeye na maisha ya wanawake wengi wanavyopambana kila kuchao hasa wanaoishi na virusi vya HIV

Dorothy ni mama ya watoto watatu na wajukuu wawili na anajivunia msaada ambao ameupata sasa kutoka kwa jamii yake.

Imehaririwa na Yusuf Jumah