Waridi wa BBC: 'Nilipomwambia mama nilikuwa na ujauzito alinizimia simu'

Chanzo cha picha, Rosina Sharon
Rosina Sharon ni mzaliwa wa kijiji kidogo kinachofahamika kama kalokol Kaunti ya Turkana nchini Kenya .
Kaunti ya Turkana ni mojawapo ya maeneo ambayo yako mbali sana na maendeleo ya kawaida ambayo unaweza kupata katika miji mikubwa nchini Kenya , kwa mfano miundo mbinu kama barabara za kisasa .
Ila Rosina Sharon amejijengea jina kubwa katika mtandao wa youtube hasa kwa upande wa Ulimbwende na vipodozi .Yeye huwafunza watu jinsi ya kujipodoa , na jinsi mtu hasa wanawake wanaweza kutumia vipodozi kupata muonekano ambao wanaupenda .
Ila mwanadada huyu hakuanzia hapo na anapotizama nyuma na kuona hatua alizopiga licha ya changamoto nyingi alizopitia anatumia fursa yeyote kuwarai hasa vijana kutopoteza muda wao na mambo ya anasa na badala yake kujiboresha maishani .
Kuwa mwanafunzi bora kaunti ya Turkana
Rosina Sharon alizaliwa na kusomea Kalokol, wakati alikamilisha masomo ya shule ya msingi aliibuka mwanafunzi bora kutoka Turkana nchini Kenya na kujipata amechaguliwa kujiunga na mojawapo ya shule maarufu za kitaifa nchini humo, kama anavyosimulia yeye alikuwa ni mwanafunzi mwerevu na kwa hivyo wazazi wake na kila aliyemfahamu walimuona kama ambaye angepeperusha bedera ya kijiji chao hata juu zaidi kimasomo na kitaaluma
Baada ya kukamilisha shule ya sekondari alijiunga na chuo kikuu kimoja nchini Kenya na kuanza masomo ya taaluma ya kuwa mwanasheria. Kwa miaka alipambana na katika pilkapilka hizo aliteuliwa kama katibu mkuu wa chama cha wanafunzi mawakili nchini Kenya .
”Nilikuwa ni mwanafunzi maarufu sana nikiwa chuo kikuu , pia nilikuwa machachari na kiongozi mwanafunzi ambaye aliwatia wengi moyo kwa kila jambo ambalo nilikusudia kulifanya. Nilikuwa na ndoto kubwa za kufikia , kwa mfano kuwa wakili mashuhuri nchini Kenya ”anasema Sharon
Habari za kupata kifua kikuu na Ujauzito

Chanzo cha picha, Sharon
Sharon anasimulia kuwa mwaka wa mwisho katika masomo yake ya kuwa wakili , ndio mwaka ambao alikuwa aandike mitihani yake ya mwisho kabla ya kufuzu . Ni mwaka ambao hawezi kuusahau kwani ndipo majaribio yake mengi yalianza .
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huo anakumbuka alianza kuwa mgonjwa na mnyonge, kila wakati alikuwa anakohoa kikohozi cha damu asijue ni kipi kilichokuwa kikimsibu.
Mwanadada huyu anasema kuwa alianza kuwa na wasiwasi kuhusu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua .
”Mwanzo nilihisi kana kwamba nilikuwa nina saratani , wakati mwingine nilikuwa nashuku ni kwa nini mwili wangu ulianza kudhoofika kwa kasi kile , na ndipo nikaamua kufika hospitalini kupata vipimo ” anakumbuka Sharon
Baada ya vipimo Sharon anasema kuwa aligundulika alikuwa na ugonjwa wa Kifua kikuu hali kadhalika alikuwa na ujauzito wa miezi 3 .
Taarifa hizo zilikua za ghafla na hakujua afanye nini wala amgeukie nani kwani wakati huo alikuwa anajitayarisha kufanya mtihani wake wa mwisho kukamilisha chuo kikuu .
Ni kama dunia yake ilikuwa imefika mwisho aghalab kama ambavyo anasema kwani kwa kupatikana na ugonjwa wa TB ilimaanisha kuwa angekuwa karantini kwa miezi 6 hivi kuwa chini ya matibabu sugu na hali kadhalika kuepuka kuwaambukiza watu wengine .
Mwanadada huyu anasema kuwa chuoni alishauriwa asifanya mtihani wake hadi mwaka mmoja baadaye. Ilimbidi awe hospitalini pekee yake kwa siku nyingi .
Anakiri kuwa alipatwa na sonona na hali ya wasiwasi mwingi kwani chuoni alipokuwa mwanafunzi tetesi zilienea kuwa alikuwa na Virusi vya HIV vinavyosababisha Ukimwi , ila anasema kuwa haikuwa hali halisi ni kutokana na kuwekwa karantini na ugonjwa wa kifua kikuu ndiposa baadhi ya maswahiba wake wa karibu walianza kumsema vibaya
“Nilisikitika sana kwa uvumi ambao ulikuweko kwamba nilikuwa na HIV, japo nilifanyiwa vipimo vingi na vinavyohusu HIV hakuna wakati vipimo viliashiria kuwa nilikuwa nao , ila uvumi ulienea chuoni na hapo nilijihisi vibaya na mpweke ”anasema Sharon

Chanzo cha picha, Sharon
Kutelekezwa na familia
Baada ya ugunduzi kuwa Sharon alikuwa na ujauzito alikuwa anapambana na ugonjwa wa kifua kikuu, hatua ya mwanadada huyu kuzungumza na wazazi wake iliambulia patupu na akajipata ametekelezwa kwa siku nyingi , anasema kuwa alipojaribu kumpigia mama yake mzazi katikati ya mazungumzo mama alikata simu ghafla na kumueleza kuwa apambane na hali yake .
Vile vile baba yake mzazi hakutaka hata kumsikia wala kumuona
Wakati Sharon anakaribia kujifungua ni dada yake aliyemsitiri , siku aliyojifungua mtoto ndio ilikuwa siku ya mwisho yake kumeza dawa za kifua kikuu .
Kujifungua mtoto kulimaanisha kuwa mwanamke huyu angepambana kutafuta ajira kwa haraka, ila halikuwa jambo rahisi .Baada ya muda hata dada yake alianza kuchoka kuishi naye , na Sharon alijipata akiishi katika chumba kimoja pekee yake bila mbele wala nyuma
Ndoto ya kuwa Youtuber

Chanzo cha picha, Sharon
Ule muda wa upweke wake aliutumia kutizama video katika mtandao wa youtube, hasa alijikuta amependezwa sana na video zilizohusu vipodozi na ulimbwende .
Hatua kwa hatua alijiwekea imani kuwa hata yeye angekuwa mzalishaji katika mtandao wa youtube. Wakati mmoja anasema aliamua kuzalisha video moja kupitia simu yake ambayo alitumai ingewafundisha watu jinsi ya kujipodoa sehemu ya macho . Hapo hapo anasema video zake kwenye youtube zilianza kutizamwa .
Wakati huo anasema alikuwa anaishi nyumba ambayo ilikuwa haina vyombo isipokuwa mto wa kulalia .
Akiendelea kuunda vídeo za mtandao wa youtube, alianza kupata umaarufu ambao ulimaanisha kuwa angepokea malipo kupitia video zake za mafunzo ya urembo na vipodozi.
Na miaka mingi baadaye Rosina Sharon ni mmoja wa wanawake nchini Kenya ambao video zao zinatizamwa mno na hilo limemuwezesha kutengeneza biashara kupitia mtandao wake .
Kwa hivi sasa ni mmiliku wa chuo cha vipodozi na yuko katika mpango wa kufungua studio inayohusu urembo na vipodozi .
Mara kwa mara mwanadada huyu huzungumza sana kwa umma kuhusu safari yake , pandashuka za maisha na mabadiliko katika maisha yake ambayo yalitoa fursa ya kujitafuta upya na njia ya kuishi bila kutegemea yeyote .












