Kuanguka kwa Assad kunavyothibitisha 2024 umekuwa mwaka mbaya zaidi kwa Iran

Picha za Bashar al Assad (kulia) na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei.

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 7

Siku chache zilizopita Kiongozi Mkuu wa Iran alimuelezea Bashar al-Assad kama "shujaa wa ulimwengu wa Kiarabu," kupitia yeye Jamhuri ya Kiislamu imepata makumi ya mabilioni ya dola.

Lakini katika usiku mrefu zaidi wa Assad, mshirika wake wa karibu amemwacha.

Huenda huu ukawa mwaka mbaya zaidi kwa maslahi ya Iran tangu vita vyake vya umwagaji damu na Iraq katika miaka ya 1980.

Wanamgambo washirika wake huko Gaza na Lebanon - Hamas na Hezbollah - wameangamizwa baada ya vita vya zaidi ya mwaka mmoja na Israel, adui yake mkuu Donald Trump amerejea katika Ikulu ya White House huku utawala wa Syria, lango la ushawishi wake kwa ulimwengu wa kiaarabu likiporomoka.

Baada ya miongo kadhaa ya uungwaji mkono usiotetereka kwa utawala ambao ulitoa msaada wa kijeshi, kiuchumi na kisiasa, Iran imeshuhudia hali ya mambo ikibadilika nchini Syria na imeanza mazungumzo na makundi ya waasi ambayo yamefanikiwa kumshinda Al Assad, katika kujaribu kuepusha makabiliano kati ya mataifa hayo jirani.

"Ni watu wa Syria ambao wanapaswa kuamua juu ya mustakabali wa nchi yao na mfumo wake wa kisiasa na kiserikali," Rais wa Iran Masud Pezeshkian alisema Jumapili.

Ameongeza kuwa Wasyria lazima wawe huru kufanya hivyo bila kuingiliwa na mataifa ya kigeni.

Ujumbe huo ni wa kitendawili kidogo ukitoka katika nchi ambayo imechangia pakubwa kuifikisha Damascus hapo, jambo ambalo waasi nao hawajasahau.

Siku ya Jumapili, baada ya kuwasili kwa shangwe za ushindi huko Damascus, kiongozi wa kundi la wanamgambo ambalo limekuwa na jukumu muhimu katika kumpindua al-Assad, Abu Mohammed al-Jolani, alifyatua risasi kutoka msikiti wa Umayyad mjini Tehran akisema;

"Ushindi huu mpya, ndugu zangu, unaashiria taswira mpya katika historia ya eneo hili, historia iliyojaa hatari (ambazo ziliifanya) Syria kuwa kama uwanja wa Iran kuchezea, kueneza madhehebu, kuchochea ufisadi."

Ahmed al Sharaa, anayejulikana kwa jina la Abu Mohammed al-Jolani.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Wana wasiwasi sana mjini Tehran hivi sasa," Roxane Farmanfarmaian, profesa wa Siasa za Kimataifa za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Chuo Kikuu cha Cambridge, aliiambia BBC Mundo. "Inakanganya sana hasa kile Iran imefanya kufikia hatua hii."

Kwa kuanzia, mabadiliko ya utawala, wana hatari ya kupoteza daraja la ardhini walilokuwa nalo ili kuunga mkono Hezbollah nchini Lebanon, "lile daraja la ardhini ambalo walikuwa wamejitahidi sana kulitunza," anaeleza mtaalamu huyo wa Iran.

Eneo la Syria limeiruhusu Tehran kutuma silaha, watu na pesa kwa uhuru kwa wanamgambo wa Kiislamu wa Lebanon, mmoja wa washirika wake wakuu. Kuacha njia hizo wazi sasa itakuwa ngumu sana.

Syria ilikuwa sehemu muhimu ya kile kinachoitwa "mhimili wa upinzani," muungano uliokuzwa na Iran ili kukabiliana na Israel, ambayo pia inajumuisha Hezbollah, Wahouthi wa Yemen na wanamgambo wa Kishia wa Iraq, ambao sasa wamedhoofika sana.

Kuanguka kwa Assad pia kunaonyesha, kulingana na Farmanfarmaian, "udhaifu mkubwa katika uwezo wa Iran kuleta matokeo, na pia kutetea washirika wake na maslahi yake."

Ingawa bado haijawa wazi "ni kwa kiwango gani wameumizwa na vita vya Lebanon na mashambulizi ya Israel," anabainisha, inaonekana kwamba matukio haya mawili "yamelidhoofisha sana jeshi la Iran na kupunguza ufikiaji wake wa kimkakati."

Bashar al Assad na Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei.

Chanzo cha picha, Getty Images

Madhara kwa Iran

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza baada ya utawala wa Assad kutumia nguvu kukandamiza maandamano ya amani ambayo yalizuka nchini Syria mwaka 2011, na kuiweka Damascus kwenye hatihati.

Vikosi vya Kikurdi, Jeshi Huru la Syria linaloungwa mkono na Uturuki, Vikosi vya Kidemokrasia vya Syria vinavyoungwa mkono na nchi za Magharibi, wanajihadi kutoka Al Qaeda na Dola ya Kiislamu, na makumi ya makundi ya waasi wa ndani wamekuwa wakipigana wao kwa wao na jeshi la Syria kwa miaka 13.

Katika machafuko haya, Iran na Hezbollah, pamoja na Urusi, zimekuwa muhimu katika kuuunga mkono utawala huo.

Lakini katika miaka ya hivi karibuni, wakati mapigano yamepungua, Tehran kwa kiasi kikubwa iliondoa vikosi vyake vya kijeshi nchini Syria, ikiamini kuwa hali inaweza kudhibitiwa, kwa mujibu wa Ray Takeyh, mtaalamu kutoka Mashariki ya Kati katika Baraza la Mahusiano ya Kigeni.

Tangu kuuawa kwa Jenerali Qassim Suleimani, mmoja wa makamanda wakuu wa jeshi la Mapinduzi, katika shambulio la Marekani la Januari 2020, Iran imeacha kutetea maslahi yake nchini Syria, Takeyh anaeleza katika uchambuzi uliochapishwa na taasisi ya Marekani.

Ubalozi wa Iran mjini Damascus ulivamiwa baada ya makundi ya waasi kuwasili katika mji mkuu wa Syria.

Chanzo cha picha, Getty Images

Kasi ambayo makundi ya waasi yalifanikiwa kusonga mbele katika muda wa wiki moja tu kutoka mkoa wa kaskazini wa Idlib na kutoka kusini hadi mji mkuu imeiacha Iran njia panda.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mwenyewe, Abbas Araghchi, alikiri katika mahojiano ya televisheni kwamba, ingawa walipata taarifa kwamba makundi ya waasi yanapanga uasi kaskazini, "kilichotushtua ni, kwa upande mmoja, kushindwa kwa jeshi la Syria kukabiliana mapema na, kwa upande mwingine, kasi ya matukio hayo."

Kuchoshwa na Al Assad

Matamshi yaliyotolewa katika siku za hivi karibuni na maafisa wakuu wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu pia yanadhihirisha kuuchoka utawala wa Tehran na mshirika wake aliyeondolewa madarakani.

Araghachi alisema kwenye televisheni kwamba sababu ya kuanguka kwa Bashar al-Assad ni kukosekana kwa mazungumzo na waandamanaji na ukosefu wa juhudi za kufikia suluhu la kisiasa ili kupata makubaliano na upinzani, kwa mujibu wa idhaa ya Persian ya BBC.

Hiki ni kitendawili kwa serikali ambayo imekuwa ikishutumiwa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kukandamiza haki za binadamu, haki ya kuandamana na kuwafunga mamia ya wapinzani nchini Iran.

Kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Iran, Tehran, Ankara na Moscow zilikubaliana wakati wa kile kinachoitwa Mchakato wa Astana (mazungumzo yaliyoanzishwa mwaka 2017 na washirika hao watatu wa Syria kutafuta suluhu la kidiplomasia kwa vita ili kudhibiti kutoridhika kwa watu wengi nchini Syria.

Lakini "kasi ndogo ya mabadiliko" kwa serikali ya Assad katika mabadiliko na kufikia suluhisho la kisiasa kulisababisha kusambaratika kwake, Araghachi alisema.

Assad amekuwa "mwajibikaji zaidi kuliko mshirika, ikimaanisha kuwa wakati wake ulikuwa umepita," Saeed Laylaz, mchambuzi wa karibu wa serikali ya Iran, aliambia Financial Times. Kuendelea kumtetea hakukuwa na uhalali tena na kungekuwa na gharama zisizokubalika, chanzo kilisema.

Si rahisi kubainisha imeugharimu utawala wa Iran kiasi gani.

Nchi hizo mbili ziliimarisha uhusiano wao wakati wa vita vya Iran na Iraq, ambapo Syria, tofauti na nchi nyingi za Kiarabu, iliegemea upande wa taifa la Uajemi.

Katika kipindi hiki, Damascus iliisaidia Iran kukwepa vikwazo vya kimataifa kwa kupeleka mauzo ya silaha kutoka kambi ya Mashariki hadi Tehran kupitia eneo lake, anaeleza Ali Ramzanian wa idhaa ya BBC ya Persian.

Zaidi ya dola bilioni 30 za Marekani

Misaada ya kijeshi ilitolewa kuanzia 2011 na kuendelea, awali kwa kisingizio cha kupigana na Islamic State.

Vyombo vya habari vya Iran vinakadiria msaada huo kuwa kati ya dola bilioni 30 na 50, ingawa unaweza kuwa mkubwa zaidi, kwa mujibu wa Ramzanian.

Ukweli kwamba kundi kuu la waasi linaloongoza Syria ni wanamgambo wa Kiislamu wenye mizizi ya al-Qaeda - ingawa walijitenga na kundi hilo miaka kadhaa iliyopita - ni kutokana na hali ya wasiwasi kwa majirani wa Syria, ikiwa ni pamoja na Iran.

Hayat Tahrir al-Sham ina mizizi yake katika Al Qaeda, ingawa ilijitenga na kundi hilo mwaka 2016 na kutekeleza serikali ya msimamo wa "wastani" ya Kiislamu katika jimbo la Idlib, ambalo limedhibiti kwa miaka mingi.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Hakuna kiongozi wa Kiarabu, haswa katika Ghuba, ambaye anaridhishwa sana na hatua hizi na nadhani Iran na Waarabu wako katika makubaliano mapana juu ya hili," profesa wa Cambridge alisema.

Serikali za Kiarabu zinahofia kwamba kuibuka kwa vuguvugu la Kiislamu nchini Syria kunaweza kutoa mwanya kwa makundi ya wenyeji yenye msimamo mkali.

Kwa sasa, Hayat Tahrir al Shams (HTS) imehakikisha kwamba inakusudia kushirikiana na makundi yote ya Syria na imewahakikisha ulinzi walio wachache.

Lakini chochote wanachosema, wao ni kundi la Kiislamu ambalo lina mitazamo mikali sana juu ya Washia, kama vile Taliban.

Walisema walifanya ujumuishaji na wa kisasa zaidi kwa kuangalia kile kilichotokea Afghanistan.

Kwa hivyo kuna wasiwasi mkubwa (nchini Iran) kwamba kuna pengo kati ya kile wanachosema na kile watakachofanya," anasema Roxane Farmanfarmaian.

Kama Kayvan Hosseini wa Idhaa ya BBC ya Kiajemi anavyoeleza, idadi kubwa ya watu wa Syria, 75%, ni Sunni, wakati Shiia, ikiwa ni pamoja na Alawites, Ismailis na Maimamu, ni 10% tu.

"Wakati mustakabali wa Syria haujafahamika, kilicho wazi ni kwamba Iran ina nafasi ndogo sana ya kurudia matukio ya Lebanon, Iraq na hata Yemen ili kupata ushawishi na mamlaka," Hosseini alisema.

Je Iran inaweza kufanya uchaguzi gani?

Kwa mujibu wa Ray Takeyh, hali ya sasa inaiacha Iran na chaguzi mbili: kuongeza kizuizi cha nyuklia au kuanza mazungumzo.

Tehran haina silaha za nyuklia, lakini ina mpango wa nyuklia na, kulingana na shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, imeharakisha mchakato wa kurutubisha uranium hadi viwango vya kusababisha wasiwasi.

Iran imekuwa ikidai kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa malengo ya amani pekee.

"Kadiri nguzo zingine za kuzuia zinavyoporomoka, umuhimu wa silaha unaongezeka," mtaalam wa CFR anabainisha.

Katika muktadha huu, "Iran huenda ikakubali fursa za kidiplomasia za Marekani na Ulaya, ikiwezekana hata kutoka kwa utawala ujao wa Trump."

Roxane Farmanfarmaian hafikirii kama Tehran itaanzisha mazungumzo na mataifa ya Magharibi, lakini labda itafungua na majirani zake.

"Iran hivi karibuni imeanza mchakato wa mawasiliano na majirani zake wa Saudi ambao umekuwa wa taratibu, lakini unaelekea upande mmoja. Na (kuanguka kwa Bashar al-Assad) kutaimarisha hili," anasema profesa.

Imetafsiriwa na Martha Saranga