Je, Israel ilimpataje Nasrallah, operesheni hii ilifanyikaje?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Shirika la itikadi kali la Lebanon la Hezbollah limepata hasara kubwa tangu katikati ya mwezi Septemba.

vifaa vya mawasiliano na simu za upepo zinazotumiwa na Hezbollah. Kulikuwa na milipuko tarehe 17 na 18 Septemba, na kujeruhi zaidi ya wapiganaji 1,500, huku wengine kadhaa wakiaga dunia.

Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa Lebanon Beirut siku ya Ijumaa, na kumuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah.

Swali ni kwa namna gani vikosi vya usalama vya Israel vilimsaka Nasrallah na kufanikiwa kuwalenga makamanda wakuu wa Hezbollah.

Unaweza kusoma

Kushindwa kwa mfumo wa usalama wa Hezbollah

Kulingana na mwandishi wa usalama wa BBC Frank Gardner, kumlenga Nasrallah ulikuwa uamuzi wa kimkakati wa Israel. Kwa miaka kadhaa iliyopita walikuwa wakiishi mafichoni na Israel walikuwa wakiwaangalia.

Kulingana na Garder, "Maelfu ya vifaa vya mawasiliano vya Hezbollah na Simu za upepo vililipuliwa hivi karibuni. Inaaminika kuwa shirika la kijasusi la Israel linahusika."

"Kutokana na kila kitu kilichotokea tangu wakati huo, ni wazi kuwa Israel imejikita sana katika muundo wa Hezbollah."

"Wakati jeshi la Israel linasema limewaondoa makamanda wakuu wote wa Hezbollah, swali ni jinsi lilivyovizuia kwa ufanisi vyombo vya usalama vya Hezbollah."

Nasrallah alipatikana vipi?

Kulingana na ripoti maalum ya shirika la habari la Reuters, Nasrallah alizungumza na vyanzo kadhaa vya Lebanon, Iran na Syria kabla ya kifo chake.

Shirika la habari la Reuters, likinukuu chanzo, lilidai kuwa Israel ilikuwa ikifanya ujasusi dhidi ya Nasrallah na Hezbollah kwa miaka 20 kabla ya kushambulia makao yao makuu.

Maafisa wawili wa Israel waliiambia Reuters kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kamati maalumu ya mawaziri waliidhinisha shambulio hilo siku ya Jumatano. Wakati huo, Netanyahu alikuwa akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Matthew Saville ni Mkurugenzi wa Huduma za Kijeshi katika Taasisi ya Royal United Services. Kulingana na yeye, inaonekana kuwa mpango huo umekuwa ukifanya kazi kwa miaka mingi na unaweza kuwa umetekelezwa katika viwango kadhaa.

"Inaonekana kulikuwa na utekaji nyara wa mawasiliano (usikilizwaji wa maagizo ya siri au mazungumzo au kupata habari). Huenda pia kulikuwa na 'uchambuzi wa picha' za satelaiti au picha zilizopigwa kwa siri. Hii ni pamoja na 'human int' (taarifa za siri zinazotolewa na wanadamu."

Kwa maneno mengine, wapelelezi walio chini wanaweza kuwa na jukumu kubwa pia.

Baada ya vita vya 2006 kati ya Israel na Hezbollah, Nasrallah aliacha kusafiri hadharani.

Chanzo kilicho karibu na usalama wa Nasrallah kiliambia shirika la habari la Reuters kwamba Nasrallah yuko katika hali ya tahadhari. Aliweka vikwazo vikubwa. Yaani mpaka kukutana na watu wachache sana.

Jinsi Israel ilivyoshambulia kwa mabomu

Maafisa watatu waandamizi wa jeshi la Israel waliliambia gazeti la Marekani la 'The New York Times' siku ya Jumamosi kwamba walikuwa na taarifa kuhusu mahali alipo Hassan Nasrallah kwa miezi kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti za Israel, uamuzi wa kumlenga Nasrallah ulifanywa mara moja na bila ya kuifahamisha Marekani, ili wasipoteze muda.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, Nasrallah alikuwa katika hali ya tahadhari baada ya milipuko ya vifaa vya mawasiliano, kwani haikuwa siri kuwa Israel ilitaka kumuua.

Nasrallah hakujumuishwa hata katika msafara wa mazishi ya makamanda wa Hezbollah, na hotuba zake zilizorekodiwa kabla kuchezwa siku chache baadaye.

Israel inasema makao makuu ya Hezbollah yalikuwa chini ya jengo la makazi kusini mwa Beirut, ambapo bomu lilimlenga Nasrallah.

Jeshi la Israel linasema kuwa limewaua makamanda tisa wa jeshi la Hezbollah akiwemo Nasrallah katika muda wa wiki moja.

Magnus Ranstort wa Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Uswidi ni mtaalam anayefuatilia masuala ya Hezbollah. Kulingana na yeye, maendeleo haya ni kikwazo kikubwa kwa Hezbollah, ambayo inafichua kushindwa kwa intelijensia yake.

Kulingana na Magnus, "Wao (Waisraeli) walijua kwamba Nasrallah alikuwa akifanya mikutano. Alikuwa akikutana na makamanda wengine aliposhambuliwa."

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumamosi, msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Nadav Sheshani alisema kuwa alikuwa na taarifa za 'muda halisi' kuhusu mkutano kati ya Nasrallah na viongozi wengine.

Hata hivyo, Seshani hakufafanua jinsi taarifa hizo zilivyokuwa zikipatikana. Sheshani alisema wanakwenda kukutana ili kushambulia Israel.

Brigedia Jenerali Amichai Levin, kamanda wa jeshi la anga la Hatjerim la Israel aliwaambia waandishi wa habari kwamba makumi ya mabomu yalirushwa ndani ya sekunde.

Kulingana na yeye, "Hii ilikuwa operesheni ngumu sana na ilikuwa imepangwa kwa muda mrefu."

Kwa mujibu wa Saville, "ndege za kivita za Jeshi la Anga la Israel F-15 zimeripotiwa kudondosha mabomu takribani 80, yenye uwezo wa kuharibu ngome hiyo, baada ya kupata taarifa thabiti kuhusu eneo la Nasrallah."

"Mabomu yalirushwa yakilenga vyumba vya chini ya ardhi huko Beirut Kusini na Dahiya. Hapa ndipo Nasrallah alipokuwa akikutana na makamanda wengine."

"Kutokana na hayo yote ni wazi kwamba mashirika ya kijasusi ya Israel yalifanikiwa kupenya vyombo vya usalama vya Hezbollah.

Nafasi ya Nasrallah hivi karibuni itachukuliwa na mtu mwenye sifa zinazofanana na hizo za kidini. Lakini itamchukua miaka kiongozi huyo mpya kupata wafuasi.

Unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Yusuf Jumah